CCM vipofu wa kusikia, wepesi wa kuota ndoto mchana

Elineema J Mosi

JF-Expert Member
May 17, 2013
808
148
JAHAZI likipoteza mwelekeo kinachofuatia ni kuyumba. Kibaya zaidi baada ya kuyumba ni chombo kuwa katika hatari ya kuzama..

Jahazi kupoteza mwelekeo na kuyumba si jambo la ajabu sana. Nahodha na wasaidizi wake bado
wanaweza kufanya bidii kukirudisha chombo kwenye mwelekeo wake. Hata hivyo, kuchelewa kufanya hivyo kunafanya kazi ya kulinusuru jahazi kuzama kuwa ngumu zaidi. Chama cha Mapinduzi (CCM) ni chama tawala. Ni chama kilichobeba dhamana kubwa ya uongozi wa nchi. Ni ukweli huo unaofanya yanayotokea ndani ya CCM yatuhusu sote hata tusio wafuasi wa itikadi za vyama vya siasa.

Aliyekuwa kada wa CCM na katibu mkuu wa chama hicho Horrace Kolimba (sasa marehemu) ndiye aliyeanza kusema ukweli juu ya mwelekeo wa CCM. Kolimba alisema ukweli wake akausimamia. Alitamka hadharani, kuwa CCM imepoteza dira. Hata wakati huo, uongozi wa CCM uliikana kauli ya Kolimba. Kolimba alikuwa na ujasiri wa kuisimamia kauli yake hadi kufa kwake. Atakumbukwa daima kwa kauli na msimamo ule aliouonyesha.

Miaka mingi imepita tangu Kolimba atamke kauli ile. Tumeanza kusikia sauti nyingi zaidi zikitamka mambo yenye kufanana na yale aliyosema Kolimba. Alianza Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Ikafika mahali Mwalimu hakuishia tu kuzungumza juu ya yanayotokea ndani ya chama chake. Mwalimu aliandika kitabu ili kuacha kumbukumbu ya kudumu juu ya alichotaka kusema. Hata baada ya Mwalimu tumeanza kuwasikia makada wengine wa CCM wenye kutamka hadharani yale yenye kufanana na ya Kolimba na Mwalimu.

Mfano mzuri ni wa hivi majuzi pale tulipomsikia Joseph Butiku wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere alipozungumza na Wanahabari. Idadi ya wanaojitokeza hadharani bado ni ndogo, wengi wanaishia kunong’ona tu. Kwamba wana- CCM wenyewe wameanza kujihoji ni jambo la heri kwa chama hicho tawala. Wenye kuhoji yanayotokea ndani ya CCM wanafanya hivyo kwa mapenzi na chama chao, hata kama wanajiweka katika hatari ya kupigwa mihuri ya “upinzani’ na kuhatarisha kutengwa kutoka kwenye kundi kuu. Tunapozungumzia dhana ya kuimarisha demokrasia ya ndani ya vyama ( intra-party democracy) si jambo la busara hata kidogo kujaribu kuzuia sauti zenye kuhoji, kudadisi na hata kupinga na kushutumu hata kama sauti hizo ni chache kiasi gani.

Kuzizima sauti hizo kunasaidia tu kuongeza manung’uniko na minongono ya chini chini. Zinachangia kuongezeka kwa harakati za chini kwa chini. Kunachochea kuongezeka na kuimarika kwa makundi ndani ya chama hata baada ya uchaguzi. Manung’uniko, minong’ono na makundi yanaimarika pale ambapo wenye fikra na mitazamo tofauti wanapobanwa sana ndani ya chama na hata kufikia kukosa majukwaa ya kusemea.

Wanapojisikia hofu ya kuchapwa bakora za chama ama kutengwa, huwafanya wawe na nidhamu ya woga na huanza kutoaminiana. Wanachohitaji CCM kwa sasa ni kurudi kwenye misingi yake iliyowezesha kuundwa kwa chama mama TANU na Afro-Shiraz na baadaye kuzaliwa kwa CCM. CCM irejee kwenye ahadi za mwanachama wa chama hicho kwa chama chake. Kati ya ahadi muhimu za mwana TANU na baadaye Mwana – CCM ni: ” Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko”. Leo tuna mifano ya wana- CCM walioingia chama hicho wakitokea kambi ya upinzani. Majuzi hapa mmoja wa wana- CCM hao aliyetokea kambi ya upinzani amesikika akitamka hadharani, kuwa walipokuwa upinzani kazi yao ilikuwa ni kutunga uongo.

Alichomaanisha mwana-CCM mpya huyu na aliyepewa dhamana ya uongozi, ni kuwa kama alikuwa ni mmoja wa watunga uongo kwenye kambi ya upinzani, basi, kuondoka kwake kutoka upinzani na kujiunga na CCM kutakuwa ni jambo la heri kwa aliowaacha huko kwenye upinzani.

Waliobaki huko watafurahia kwa kuondokewa na mtu mwongo. Lakini tafsiri nyingine juu ya kiongozi huyu anayetangaza hadharani alivyo mwongo ni ukweli kuwa huko CCM alikokimbilia, kuna wenye busara pia watakaomtilia shaka kutokana na tabia yake hiyo ya uongo. Si ajabu, kuwa wana- CCM hao wapya waliotokea upinzani kura walizopata hazikutosha kuwaingiza katika Halmashauri Kuu ya CCM katika uchaguzi wa CCM uliomalizika hivi karibuni. Imefika wakati kwa wana-CCM kuacha hofu ya kuambizana ukweli. Tulio nje tunakiona chama kikiyumba.

Rushwa na ufisadi ndani ya chama vinakiyumbisha. Ndani ya CCM kuna wanaoliona hilo pia. Baadhi yao kwa unafiki watamwambia nahodha; “kanyaga mafuta baba!” Huku wakijua kinakoelekea chombo siko. Na kila jahazi huwa na panya wake.Wenye kumsisitiza nahodha akanyage mafuta mara nyingi huwa na tabia za panya wa jahazini. Jahazi likianza kuzama, panya wale huwa wa kwanza kurukia majini na kukiacha chombo kikizama. Kuna umuhimu wa kusema yaliyo ya kweli. Na kuna aina tatu za wasema kweli. Kuna anayesema ukweli na kujificha.

Huyu anaweza kuwa na sababu za msingi za kutaka kusema ukweli na kujificha. Ndiyo huyu atakayekwambia ukweli juu ya jambo fulani kisha kukutamkia; ”Tafadhali jina langu lihifadhi”. Aina ya pili ya msema ukweli ni yule anayesema ukweli na kisha kuukimbia. Atasema ukweli, akibanwa sana na wenzake, basi, ghafla atakanusha ukweli aliosema hadharani. Atauruka ukweli wake mwenyewe. Atayakanusha maneno yake hata kama yamerekodiwa na kila mmoja akayasikia. Atang’aka, atakikimbia kivuli chake. Hii inatokana na woga unaozaa unafiki.

Lakini mwisho kuna huyu anayesema ukweli na kisha kuusimamia kwa lolote lile, inyeshe mvua, liwake jua. Ni watu wa aina ya akina Kolimba. Jamii yetu ilihitaji kuwa na watu wengi zaidi wenye kulikaribia kundi hili la tatu la wasema ukweli. Siku zote ukweli ni mzigo mzito, haupaswi kubebwa. Ukweli husambazwa. Tumeshuhudia, kuwa kabla ya kifo chake, Mwalimu Nyerere si tu aliamua kuusema ukweli juu ya chama chake, bali kwa maslahi ya taifa aliamua kuandika na kutuachia kitabu chenye ukweli huo ndani: Uongozi Wetu Na Hatma Ya Tanzania.

Alikifahamu chama chake. Aliona uchungu alipoona kinapoteza mwelekeo. Hakusubiri vikao vya chama, alizungumza hadharani na sote tukamsikia. Katika hilo la uchungu kwa chama chake, Mwalimu aliona maslahi mapana zaidi yaliyokuwa hatarini, maslahi ya taifa la Tanzania. Na labda ndiyo tafsiri ya alipotamka, kuwa ”CCM si Mama yangu”. Mwalimu aliiona nguvu ya chama iliyokuwa ikipotea. Ni nguvu kubwa ya kihistoria ya CCM iliyotokana na TANU na ASP. Vyama vilivyokuwa kimbilio la wanyonge. Viongozi wake walitokana na makabwela na waliwatumikia makabwela. Ni dhahiri kuwa leo CCM iko njia panda. Ukweli huu aliwahi kuutamka mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, Benjamin Mkapa. CCM ya leo haina hakika juu ya njia gani ya kufuata huku ikibaki kuwa kimbilio la wanyonge.

CCM imekubali kuwakumbatia au labda kukumbatiwa na matajiri. Ubia huu ni wa shaka kwa makabwela. Iweje leo CCM yenye kufuata itikadi ya kijamaa ikimbiliwe na wafanyabiashara mabepari? Tofauti na ilivyokuwa kwa TANU na CCM ya miaka hiyo ya nyuma. CCM ya leo imeshindwa kuweka bayana mipaka ya mahusiano yake na matajiri. Haliwezi kuwa jambo la heri kwa jahazi la CCM kukimbiliwa na matajiri. Hili ni kundi ambalo chama kililipaswa kulidhibiti. Wafanye biashara zao, wawatendee haki wafanyakazi wao na wakulima wenye kuzalisha malighafi.

Je, makabwela wa nchi hii watarajie nini, pale wanapoona matajiri si tu wameingia kwenye jahazi la chama, bali pia wanajaribu kusogea karibu kabisa na nahodha? Tuna lazima ya kufikiri kwa bidii na kushiriki kuchangia fikra zetu kwa kujadili kwa uwazi.
Nitasema kweli Daima.

BY
ELINEEMA J MOSI
ARUSHA-TANZANIA
 
Back
Top Bottom