CCM sawa na gari bovu, halitufikishi mbali | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

CCM sawa na gari bovu, halitufikishi mbali

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Magezi, Jun 24, 2010.

 1. M

  Magezi JF-Expert Member

  #1
  Jun 24, 2010
  Joined: Oct 26, 2008
  Messages: 2,827
  Likes Received: 87
  Trophy Points: 145
  CCM sawa na gari bovu, halitufikishi mbali


  • Dawa ni kurekebisha injini na kubadilisha dereva

  MNAMO Novemba 2002, waziri wa zamani na mbunge wa miaka mingi, Jackson Makwetta, wakati akihutubia mkutano wa hadhara mkoani Iringa alisema: "CCM ni chama chenye nguvu sana hapa nchini. Kina wanachama na watu wengi wanakipigia kura...huu ni wakati mwafaka kwa CCM kufanya kila kinachotakiwa ili kuondoa umasikini vinginevyo tusitafute mchawi."

  Ujumbe huu mzito ulitolewa karibu miaka 10 iliyopita na juzi tu Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alipokuwa kwenye mkutano kuhusu kilimo, mjini Arusha, alionekana kweli anamtafuta mchawi alipohoji; “sijui Watanzania tumelogwa na nani?”

  Na vilevile mkuu wake, Rais Kikwete akiwa katika moja ya safari zake nchini Uingereza, alipata kuulizwa na mwandishi wa gazeti la Financial Times ; "ni kwanini Tanzania inaendelea kuwa masikini kwa zaidi ya miaka arobaini na mitano sasa hata baada ya kupata Uhuru pamoja na utitiri wa raslimali ilionao". Kikwete alionyesha vile vile mshangao! Majibu yake yakawa tu ni sawa na ya Pinda.

  Bila kupoteza muda, ni vyema sasa tuzingatie maneno ya Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair katika kitabu chake cha falsafa cha 1997 kinachoitwa "Njia ya Tatu: Siasa Mpya kwa ajili ya Karne Mpya" (tafsiri ni yangu).

  Blair ameandika: "Nimekuwa nikiamini siku zote ya kwamba siasa, awali ya yote, ni kuhusu mawazo. Bila ya kuwa na nia madhubuti ya kusimamia malengo na kanuni, serikali zinakuwa hazina mwelekeo wala mafanikio, ijapokuwa wana wingi wa wabunge. Zaidi ya hapo mawazo yanahitaji utambulisho ili yapate umaarufu na kueleweka kwa mapana" (tafsiri ni yangu).


  Hili la siasa ni kuhusu mawazo. Kwetu Watanzania, kwa kweli, hatupaswi kushangaa sana kutokana na kuwa na Rais wa kwanza, Mwalimu Nyerere, aliyeamini kwa dhati kuhusu Ujamaa na aliitolea siasa hiyo maelezo ya kutosha ili kuifanya ieleweke na jamii kwa kuandika hata vitabu kadhaa.

  Binafsi, nikiwa nachukua masomo yangu ya chuo kikuu nje ya nchi - kipindi cha awamu ya tatu chini ya Rais Mkapa, kitu kimoja kilichokuwa kinanisumbua wakati wa mazungumzo ya kawaida na wanafunzi wenzangu na hata wasio wanafunzi juu ya masuala mbalimbali duniani, ni pale hasa wanapouliza juu ya hali ya Tanzania.

  Ukweli ni kwamba baadhi yao wanamfahamu Mwalimu Nyerere na itikadi yake ya siasa ya Ujamaa na Kujitegemea; hivyo walipenda kujua tumefikia wapi.

  Nilijikuta napata taabu sana kuwaelezea hali ya nchi yetu; kwa maana ya kitu cha kujivunia. Haitoshi kusema tu nchi yetu ni ya amani na utulivu! Kuna masuala muhimu kama ya mawazo na falsafa.

  Nikitafakari zaidi haya matatizo ya kisiasa tuliyonayo, naweza kusema kwamba nchi yetu sasa hivi ni kama tumeweza kuwa na viongozi wa kutosha baada yake Mwalimu kiasi kwamba tunapaswa kuelewa tunachotaka ili kukabili changamoto za wakati huu. Niseme tu kwa bahati mbaya Mwalimu alichangia kudhoofika kwa mawazo mchanganuo kwa vile aliacha wafuasi wengi wasio makini, na vile vile kushindwa kuacha viongozi bora. Kwa maneno mengine, aliacha bora viongozi wa kutosha!

  Nikiwahesabu marais wastaafu - Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, na hata Rais Kikwete ni katika kundi hilo la bora viongozi. Kwa haraka, Mwinyi kwa jinsi Mwalimu alivyolazimika kuingilia masuala mbalimbali kwenye urais wake, huwezi kusema alikuwa mfano wa kiongozi wa kuiga.

  Nikimtafakari Mkapa, kuna mambo mawili. Kwanza kabisa kitendo cha yeye kulivalia njuga rushwa katika kampeni ya urais 1995, huku akiwa ametumikia kama waziri katika Serikali ya Mwinyi iliyotawaliwa na rushwa na yeye kutojipambanua kama mtu aliyechukia rushwa kwa kuwakemea wanaojihusisha au hata kujiuzulu kwenye baraza la mawaziri ilikuwa ni jambo la kusikitisha na la aibu.

  Ni aibu; hasa ukizingatia ile kanuni ya uwajibikaji wa pamoja ambapo mjumbe katika baraza la mawaziri anakuwa ni sehemu ama ya mafanikio au kushindwa kwa serikali.


  Nitoe mfano wa waziri wa iliyokuwa serikali ya Moi wa Kenya, Kenneth Matiba ambaye alijiuzulu kufuatia masuala mbalimbali ya wakati huo na haikushangaza wiki moja baadaye kufukuzwa kwenye chama tawala cha KANU (wakati huo chama hicho kilikuwa baba na mama kweli kweli).

  Lingine la kutia aibu ni wakati wa kipindi cha kwanza cha urais wake Mkapa. Alipoulizwa kuhusu malalamiko juu ya mageuzi ya kiuchumi alijibu kwamba ni wale tu waliokuwa wanafaidika na "uchumi holela" kabla yake; yaani utawala wa Mwinyi ndio waliokuwa wakilalamika. Hivi kweli mtu aliyekaa miaka mingi tu kama waziri katika Serikali ya Mwinyi na ambaye hakuwahi kukemea maovu dhidi ya uchumi aliwezaje kutoa kauli hiyo?

  Kwa hili la uwajibikaji wa pamoja, napenda kumtaja waziri mwingine wa Moi, Simeon Nyachae aliyejitahidi sana kunyoosha mambo mbalimbali. Nyachae, kwa kifupi, aliwahi kushika wizara mbalimbali pamoja na Kilimo na Maendeleo ya Mifugo na Fedha. Kipindi akiwa Kilimo alitoa agizo la kuzuia uingizwaji wa sukari kutoka nje ya Kenya, lakini katika hali ya kusikitisha kesho yake Moi alibatilisha agizo hilo.

  Lakini, hata hivyo, haikuishia hapo; kwani akiwa Fedha alifikia hatua ya kutangaza kwenye mkutano wa wabunge na wadau wengine kwamba uchumi wa Kenya ulikuwa katika chumba mahututi (ICU); na kupendekeza hatua kali kadhaa zichukuliwe kuokoa uchumi wa Kenya.

  Haikuchukua muda Nyachae alishushwa cheo na kuhamishiwa Wizara ya Maendeleo ya Viwanda lakini akaamua kujiuzulu serikalini. Kufuatia hapo, mizengwe na hali ya kuandamwa kwake, ilishika kasi!

  Zaidi ya hapo, ni imani yangu kwamba kama Mkapa angekuwa ni mtu wa kanuni bora, kwa jinsi alivyokuwa anasisitiza mageuzi ya kiuchumi chini ya mwamvuli wa utandawazi akiwa Rais, naamini angekuwa ametupa picha ya fikra yake juu ya uchumi huo kupitia maandishi yake mbalimbali (sio hotuba), hasa kabla au hata akiwa waziri.

  Ni juzi tu, katika kupitia vitabu mbalimbali nyumbani, nilikuta kitabu fulani ambacho kiliandikwa Septemba 2002 na Dk.
  Vincent Cable ambaye sasa hivi ni Waziri wa Biashara wa Uingereza. Kipindi anaandika kitabu hicho alikuwa Waziri kivuli wa Biashara na Viwanda wa chama cha Liberal Democrats.

  Kitabu hicho kilikuwa kinaangalia namna ya kurekebisha ubepari wa kisasa. Na leo hii naamini mheshimiwa huyo akibanwa kuhusu mawazo yake juu ya kitabu hicho cha karibu miaka kumi iliyopita, hatababaika.

  Suala hili la viongozi kuweza kuandika mawazo yao juu ya jambo lolote la kitaifa ni la kusisitiza sana na ndio maana ya 'siasa ni kuhusu mawazo' alichokuwa anazungumzia Blair. Lazima kuwe na maono au dira zinazoshindana.

  Na kiongozi anapostaafu vile vile awe anaweza kuandika kitabu kinachochambulika na chenye ukweli kuelezea kipindi cha utumishi wake na mambo mengine ili vizazi vijavyo viweze kunufaika! Niongeze tu kusema kuwa ni jambo la faraja kwamba angalau aliyekuwa Gavana na Waziri wa Fedha wa zamani na mwanzilishi wa CHADEMA, Mzee Edwin Mtei, aliweza kuandika kitabu kuhusu maisha yake na utumishi wake serikalini.

  Ni jambo la kusikitisha kwamba mchakato ulikuwa umeanza wa Mwalimu kuandika kitabu kuhusu uongozi wake lakini ugonjwa ulimkuta tena. Na waliomfuatia, Mwinyi na Mkapa sijui hata wangeweza kuanzia wapi kuandika kutokana na kuonyesha udhaifu mkubwa wa kiuongozi!

  Isingekuwa hivyo, naamini Mkapa angekuwa ameshajinyakulia zawadi nono ya Taasisi ya Mo Ibrahim inayofuatilia utawala bora barani Afrika, ambayo Dk. Salim Ahmed Salim ni mjumbe na ambayo kwa mwaka wa pili sasa wameshindwa kumpata anayestahili tuzo hiyo barani Afrika.


  Sasa nikimtazama Kikwete vizuri, pamoja na yeye kutumikia kwa miaka kumi nafasi kubwa ya Waziri wa Mambo ya Nje, sijawahi kabisa kusoma ameandika kitu chenye uzito kuhusu Tanzania au hata bara la Afrika. Na sote tanafahamu kwamba bara letu linakabiliwa na changamoto kubwa mno!

  Kwa kweli kitendo cha yeye kuonyesha mshangao juu ya hali ya umaskini wetu karibu miaka hamsini baada ya uhuru, isingekuwapo endapo angekuwa ni mtu makini katika nafasi zake za utumishi wa nchi.

  Na ndio maana Mwalimu Nyerere alitoa tahadhari hii kwenye sherehe za Mei Mosi mkoani Mbeya 1995 aliposema: "Je, wanaotaka kutuongoza wanaweza, kwanza, kuelezea tulikuwa wapi, tuko wapi, tunataka kwenda wapi? Pili, je wanao uwezo wa kutupeleka kule tunakotaka kwenda? Tatu, watatushirikishaje kule ili na sisi tusaidiane kwenda huko? Hiyo ndiyo kazi iliyobaki. Pimeni Sana!"


  Pengine kwa namna fulani mtu unaweza kusema Kikwete ni matokeo au matunda ya kukaa kwa kipindi kirefu sana kwenye serikali za Mwinyi na hasa Mkapa. Kuonyesha hili vizuri, ni kitendo cha hivi karibuni cha kuwaita eti "wazee" kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, ambao kazi yao ilikuwa ni kushangilia tu wakati akizungumzia suala nyeti la madai ya wafanyakazi.

  Na hiyo ilifanana kabisa na wakati Mkapa alipowaita wazee hao hao Diamond Jubilee na kuishambulia vikali kamati ya katiba ya Jaji Robert Kisanga. Matukio haya mawili kwa kweli yalinifanya nikumbuke msemo wa Kingereza kwamba "na viongozi wa aina hii, nani anahitaji madikteta?"

  Na kweli, tabia hii ya kutaka kudhibiti ukuaji wa demokrasia tunaiona kwenye suala muhimu la mgombea binafsi na hata suala la Chama Cha Jamii (CCJ) kuwekewa mizengwe kupata usajili wa kudumu mpaka sasa. Tusisahau pia kwamba kauli mbiu ya CCM ya uchaguzi ni 'Ushindi ni Lazima 2010'.

  Pamoja na hayo yote ya kuweza kukatisha tamaa, kuna matukio mengine ya kutia moyo. Ni jambo ambalo halijapata kutokea kwa waziri wa zamani kuweza kutamka waziwazi kwamba endapo Kikwete hawezi kuchukua maamuzi magumu ya kuwachukulia hatua watuhumiwa wakubwa katika mambo mbalimbali, basi ni vizuri achukue maamuzi magumu kwa kutogombea tena kipindi cha pili.

  Waziri huyo haoni sababu yoyote ya kupewa kipindi kingine. Jambo la pili ni kitendo cha wafanyakazi kutomwalika Rais kwenye sherehe zao za Mei mosi mwaka 2010. Hili la pili pia ni historia katika nchi yetu na inawezekana hii ilichangia kumpandisha hasira sana Kikwete kwenye hotuba yake Daimond Jubilee.

  Kwa kuhitimisha, tulipofikishwa, hali ya Tanzania chini ya CCM naifananisha na gari ambayo injini yote inahitaji kufanyiwa matengenezo makubwa pamoja na kubadilisha dereva.

  Si vyema kuifanyia matengenezo injini ya gari hiyo na kumwacha dereva huyo huyo aiendeshe kwa sifa yake; maana ataiharibu kabisa! Afadhali gari isitengenezwe kabisa lakini ipatiwe dereva makini, itaendelea na safari vizuri. Vinginevyo dereva na injini vyote viondolewe na kuwekwa vipya ili safari inoge zaidi.


  Tukiwa tunaelekea kuadhimisha nusu karne ya Uhuru Desemba 9, 2011, kwa nini basi angalau tusijivunie hata kwa kitu kimoja: Kwa kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika kwa kuleta mabadiliko ya kisiasa katika hali ya amani na utulivu? Je, huu si wakati mwafaka wa kuweka Serikali ya Mpito itakayorejesha matumaini ya Watanzania?

  Tusikubali mawazo na maneno ya kale ya kulogwa kwamba atakayejitokeza na mwenye sifa zaidi kumpinga Kikwete (sio kama Shibuda) atapatwa na kifo cha ghafla! Tunataka nchi inayoendeshwa kwa siasa makini. Wale waumini wa amani na hasa wafuasi wa Mwalimu wafahamu historia inawatazama!

  Zingatieni maneno ya Waziri Mkuu mwingine wa Uingereza, Harold Wilson, aliyesema "katika siasa, wiki ni muda mrefu".

  Chanzo: Raia Mwema
   
Loading...