CCM, NRM na hadithi ya pacha wasiofanana

mr mkiki

JF-Expert Member
Sep 22, 2016
5,322
2,000
Kuvielewa vyama viwili tawala vya CCM nchini Tanzania na NRM cha Uganda, ni kuelewa tabia za jumla za wananchi wa nchi hizo mbili.

Inaonekana kama waasisi wa vyama hivyo walijua tabia hizo na ndiyo sababu wakavisuka katika namna inayoendana na tabia za watu wao. Ni tabia zipi hizo za watu wa nchi hizi mbili?

Tabia ya kwanza ni ile ya wananchi wa kawaida. Wengi wao hufurahi pale tu wanapoona mmoja wao au mwenzao kutoka katika kundi lao; iwe kabila, kanda, dini au jinsia- akiwa anawawakilisha katika vyombo vikubwa vya maamuzi. Tabia ya pili ni ile ya watu wa daraja la kati (middle class) ambao wao wanaridhika na kuwa na maisha mazuri, kupewa vyeo na kufurahi nguvu za kimamlaka.

Kundi hili la pili ni la watu ambao ili mradi wana vyeo na wanaendesha au kuendeshwa na magari mazuri, hawatakuwa na tatizo na yeyote aliye madarakani.

NRM na CCM ndiyo vyama vikongwe zaidi vilivyo madarakani katika ukanda huu wa Afrika Mashariki. Kwa kutumia mbinu zinazokaribia kufanana lakini kutofautiana katika utekelezaji wake, vyama hivi vimebaki madarakani kwa muda mrefu kuliko vyama vingine vya siasa katika eneo hili.

Ni kwa vipi vyama hivi vinafanana na kutofautiana? Na ni kwa vipi wametumia tabia hizo za wananchi wao kubaki madarakani muda mrefu kuliko vyama vingine vya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara?

Mahali pazuri pa kuanzia ni kwenye mwanzo wa vyama hivi viwili.

Mwanzo wa NRM

Chama cha NRM kilianza June 9, mwaka 1981. Mwanzoni, kilikuwa ni sehemu ya kundi la kijeshi la Popular Resistance Army (PRA) kilichoanzishwa na Yoweri Museveni na wenzake.

Wakati kinaanzishwa, chama hicho kilikuwa kinaundwa na watu wenye sifa tatu zinazofanana; wa asili ya Bahima, Waanglikana na wakimbizi wa Kitutsi kutoka Rwanda. Nchini Uganda, kabila lenye watu wengi zaidi ni Baganda na dini yenye wafuasi wengi ni Wakristo Wakatoliki.

Ili kuondoa kasoro hiyo, Museveni kwanza aliungana na Profesa Yusuf Lule na chama chake cha Uganda Freedom Fighters (UFF) kwa ajili ya kuondoa nakisi hiyo kwake na wapiganaji wake wa PRA. Muunganiko huo wa PRA na UFF ndiyo uliounda NRM.

Hata hivyo, akiandika katika jarida la kila mwezi la The Dispatch, mwandishi mwandamizi wa Uganda, Timothy Kalyegira, alieleza kwamba wananchi waliokutana na majeshi ya Museveni walimwuliza maswali makubwa mawili tu; ni lini atawarejeshea Baganda utawala "wao" wa kifalme wa Baganda uliovunjwa na utawala wa Milton Obote mwaka 1967 na kwanini majeshi hayo yanaundwa na watu wa jamii ya Wahima zaidi?

Kwa kusikiliza na kuelewa matakwa hayo ya wananchi, Museveni akaamua kuungana na majeshi ya chama cha Uganda Freedom Movement (UFM) kilichokuwa kinaongozwa na Andrew Kayira, wa kabila la Baganda aliyekuwa akiungwa mkono sana na wananchi wa kabila lake hilo kwenye mapambano hayo ya kumng'oa Obote.

Inaonekana Museveni alijifunza mengi wakati akiwa msituni kuhusu tabia na matakwa ya Waganda kiasi kwamba mara baada ya kuingia madarakani Januari 26, 1986, kazi yake ya kwanza ilikuwa ni kuunganisha makundi mbalimbali ya watu ndani ya NRM.

Kwa sababu wa ustadi wa Museveni wa kuunganisha watu wa makundi mbalimbali ndani ya serikali; mara nyingi serikali yake ikiwa na baraza la mawaziri kubwa kuliko nchini nyingine yoyote ya Afrika Mashariki na washauri wa Rais wengi - wakati mmoja wakizidi 100, NRM kikageuka kuwa chama pekee cha Uganda kinachoweza kujidai kuwakilisha nchi nzima.

Chama cha Obote cha UPC kilikuwa kikidaiwa kuwa na wafuasi wengi kutoka Kaskazini mwa Uganda, Democratic Party (DP) kikionekana kuwa na wafuasi wengi zaidi katikati ya Uganda na vyama vingine vikiwa vinachukua wafuasi hapa na pale.

Mwanzo wa CCM

Kwa upande wake, CCM kimetokana na muunganiko wa vyama viwili vilivyohusika katika kutafuta Uhuru wa Tanganyika na Zanzibar. Kutoka Tanganyika, TANU ndiyo iliyokuwa kinara huku Afro Shirazi (ASP) kikiwakilisha Zanzibar. TANU ilikuwa muunganiko wa watu wa makabila, imani na rangi zote huku ASP awali kikisimamia maslahi ya watu wa asili ya Afrika na Washirazi.

Muunganiko wa ASP na TANU kuunda CCM ulikuwa na faida kubwa mbili; mosi kumeza ubaguzi wa ASP dhidi ya watu wa rangi na asili nyingine na kufanya chama hicho kuwa hasa cha kitaifa.

Katika baraza la kwanza la mawaziri tangu kuundwa kwa CCM; ilihakikishwa kwamba watu wa rangi, kanda, dini na walau mikoa mbalimbali ya Tanzania waliwakilishwa ndani yake.

Na tangu kuundwa kwake, CCM imekuwa ikihakikisha kwamba marais wake wote wanawakilisha watu wa dini zote kuu za Tanzania; Waislamu kwa Wakristo, na wakati huohuo nafasi mbalimbali za uteuzi zikienda kwa watu wa makabila yote - bila ya kuonyesha upendeleo wa wazi kwa eneo au dini moja.

Matokeo yake ni kwamba CCM ndicho chama pekee nchini Tanzania kinachoweza kujigamba kuwa na wafuasi karibu katika kona zote za taifa hilo kubwa kupita yote miongoni mwa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kama walivyo wananchi wa Uganda, wananchi wa Tanzania pia si aina ya watu ambao wanataka madaraka au mamlaka kwa gharama yoyote - ali mradi waone kwamba kuna wenzao wanawawakilisha au wale wa kipato cha kati wakiona wanafaidika na mfumo uliopo.

Kufanana katika itikadi na mikakati

CCM na NRM ni vyama vinavyoweza kujiita vyama vya kikada. Wakati wa uanzishwaji wake vilikuwa na viongozi waliokuwa na itikadi za kisoshalisti na vyama vyenyewe vikawa vya kikada kwa maana ya kuunganisha jeshi na itikadi za kisiasa.

Katika zama za chama kimoja, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (TPDF) lilikuwa likichukuliwa kama mkoa miongoni mwa mikoa ya Tanzania na ilikuwa ikiwakilishwa hadi ndani ya Bunge la Tanzania.

CCM pia imekuwa na viongozi wa juu waliopikwa katika misingi ya kikada; kwa maana ya watu waliohitimu mafunzo ya kiitikadi na kijeshi pia. Watu kama Jakaya Kikwete, Abdulrahman Kinana, Moses Nnauye na sasa Ngemela Lubinga walikuwa askari wakati wakifanya kazi zao za kisiasa kabla ya kuvua magwanda na kuingia moja kwa moja katika siasa kama raia.

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF) nalo lilikuwa na uwakilishi ndani ya Bunge la Uganda na ndiko wanasiasa mashuhuri kama Noble Mayombo, Aronda Nyakairima wengine walikojijengea umaarufu kabla ya kupanda vyeo na kuwa wanasiasa mashuhuri.

Ni muhimu pia kusema kwamba wengi wa waliokuja kuwa maofisa wa ngazi za juu wa UPDF ama walifundishwa na makamanda wa TPDF au kupata mafunzo yao ya kijeshi katika vyuo za Tanzania. Miongoni mwa maofisa hao ni kama Ivan Koretta, David Tinyefuza, Elly Tumwine, Jim Muhwezi na wengine wengi. Ni sahihi kusema UPDF ni mtoto wa TPDF.

Muunganiko huu wa jeshi na vyama vya siasa ni jambo muhimu sana katika muktadha wa kisiasa wa Tanzania na Uganda. Uhusiano huu, pamoja na sababu nyingine, umesaidia kufanya vyama hivyo kubaki madarakani pasipo kupinduliwa kama ilivyotokea kwa nchi za Afrika.

Itikadi pia ni jambo muhimu katika uendelevu wa vyama hivyo. Ingawa vyama hivyo viwili vimebadilika sana katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, walau awali vilikuwa vinaunganishwa kiitikadi katika masuala muhimu kama vile ujamaa wa kiafrika, Umajumui wa Afrika na Ukombozi wa Mwafrika. Ni rahisi zaidi kuunganisha watu wakati mkiwa angalau mnaelewana katika baadhi ya misingi.

CCM inajulikana kwa bendera yake yenye rangi za njano na kijani lakini ikiwa na alama ya jembe na nyundo ikimaanisha chama cha wakulima na wafanyakazi. NRM wana rangi za njano na kijani lakini pia ina nyekundu kwa sababu ya damu iliyomwagwa kwenye kuikomboa Uganda. Kuna alama pia za kitabu na basi, ikimaanisha dhamira ya awali ya NRM ya kuondoa ujinga kwa Waganda na kuwapeleka katika safari ya maendeleo.

Tofauti zao

Tofauti kubwa kati ya CCM na NRM inaelezwa zaidi na tofauti za waasisi wawili wa vyama hivyo - Museveni na Julius Nyerere. Waliokuwa wasaidizi wa Mwalimu Nyerere huwa wanasimulia namna alivyofadhaika alipoona askari mwenye bunduki akiwa analinda jengo la benki hiyo.

Mwalimu aliamini bunduki si kitu ambacho raia wanatakiwa kukiona mara kwa mara. Hakuamini katika matumizi ya bunduki labda kama ingebidi sana. Katika makuzi yake kama Mkatoliki, Nyerere aliamini sana katika kulinda uhai.

Kwa upande mwingine, Museveni alimhusudu Nyerere. Hata hivyo, kitabia, Museveni ni muumini wa bunduki na matumizi ya mabavu. Mmoja wa waandishi nguli wa Uganda, Andrew Mwenda, aliandika mwezi uliopita kwamba Museveni ni mtaalamu linapokuja suala la matumizi ya mabavu na matumizi ya nguvu zilizopitiliza.

Kwa sababu hii, wanajeshi wa Tanzania kama Kikwete, Kinana na Edward Lowassa, walijitosa katika siasa na kupanda juu huku wakiwa wamejitofautisha kabisa na jeshi. Wengi wa Watanzania waliozaliwa kuanzia mwaka 2000 pengine hata hawajui kama Kikwete au Lowassa waliwahi kuwa askari.

Nyerere aliitengeneza CCM kuwa chama halisi cha siasa chenye misingi ambapo chama ni kikubwa kuliko mtu binafsi au taasisi nyingine yoyote. Museveni, awali alifuata njia ya Nyerere, lakini baadaye inaonekana alibadili uelekeo na sasa yeye pengine ni mkubwa kuliko chama chenyewe.

Kwa hiyo, kuwa mwanasiasa mwenye nguvu na ushawishi Tanzania kunahitaji kuwa na nguvu ndani ya CCM na si jeshi. Makundi yote yenye maslahi yako ndani ya CCM na jeshi halina ushawishi mkubwa. Nchini Uganda, inaonekana kwamba kuwa mwanajeshi au kuwa na kete jeshini ni muhimu kuliko kuwa na ushawishi ndani ya NRM bila msuli wa UPDF.

Ndiyo sababu, mtu anayepewa nafasi ya kumrithi Museveni wakati atakapoondoka madarakani - kama ataondoka, ni mtoto wake, Muhoozi Kainerugaba; jenerali katika UPDF na si Moses Kigongo ambaye amekuwa Makamu Mwenyekiti wa NRM kwa miaka takribani 40 sasa.

Mmoja wa mawaziri waandamizi wa Museveni, Jenerali Kahinda Otafiire, tayari ametangaza kwamba jeshi halitaweza kukubali mgombea urais wa Uganda katika uchaguzi wa Januari 14 mwakani kupitia upinzani, Bobi Wine, ashinde kwenye urais kwa sababu wao hawakwenda msituni kupigana vita ili waje kuongozwa na mwanamuziki. Bobi ni mmoja wa wanamuzi maarufu wa Uganda.

Tofauti nyingine ipo katika kubadilishana nafasi za juu. Tangu Museveni aingie madarakani, CCM imetoa marais wanne tofauti - Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na John Magufuli; wote wa dini, makabila na maeneo tofauti ya Tanzania. Museveni hajaondoka madarakani kwa miaka 36 sasa.

Museveni anatumia mbinu ya kugawa vyeo na mali kwa makabila tofauti na maeneo tofauti mara kwa mara huku msingi wa viongozi ukiwa ni uleule - wakati CCM ikitumia utaratibu wa nyoka wa kujivua ngozi na kuvaa nyingine kila baada ya miaka 10; ikihakikisha watu tofauti wanaingia madarakani na kufaidisha kundi maslahi tofauti kabisa na lililoshika hatamu kwa miaka 10 nyuma.

Kwa sababu hii, ni vigumu kuiona NRM ikidumu kwa muda mrefu pasipo Museveni - hata kama kitabaki madarakani kwa sababu yeye pekee ndiye mwenye nguvu ya kudhibiti makundi maslahi ndani ya chama hicho.

Hali ni tofauti na CCM ambayo inaonekana itaendelea kuwepo miaka mingi, ali mradi kiendelee kubaki madarakani. Pasipo madaraka, inaweza kuwa vigumu kwa kiongozi atakayekuwepo kudhibiti makundi maslahi yaliyopo.

Chanzo; BBC NA Ezekiel Kamwaga.

Mjinga lazima aseme hii post ni ndefu kusoma lakini ndio jamii ambayo mtawala utumia pia. Acha majibu mepesi katika nchi yako.
 

mr yamoto

JF-Expert Member
Oct 2, 2016
922
1,000
Natamani watu wangesoma kwa makini hii habari ila naona wengi tumekariri jina la BBC badala ya habari yenyewe. Kuna mambo mwandishi kaandika ni mazuri tu kwa nchi yetu.
 

Odhiambo cairo

JF-Expert Member
Jul 11, 2015
15,339
2,000
Mada kama hivi watu wanakimbia kwenye hoja
Ukweli ni kuwa , vyama hivyo vimebaki madarakani , si kwa sababu vina sera nzuri au kukubalika miongoni mwa jamii kuliko washindani wao. Bali ni kwa sababu ya bunduki na hazina ya taifa . Lakini pili vyombo vya dola na vya maamuzi vimeingizwa ndani ya vyama hivyo.

Mtu kama M7 aliingia msitufungie kwa madai ya kuibiwa kura. Leo yeye hayupo tayari kushindwa hata kama uwezo wake umefika mwisho !! (UAFRIKA).

Kwa upande wa Ccm miaka ya Nyerere tulikuwa tunayakemea mataifa yaliokandamiza raia wake !!. Ajabu na kweli tunakemewa sisi leo !!. Mbaya zaidi Ccm na wafuasi wake , wamekuwa washabiki na wafuasi wa ma dictator ulimwenguni na mifano ipo.

Kwa ujumla nyani hajaona la kwake .
 

mr mkiki

JF-Expert Member
Sep 22, 2016
5,322
2,000
Ukweli ni kuwa , vyama hivyo vimebaki madarakani , si kwa sababu vina sera nzuri au kukubalika miongoni mwa jamii kuliko washindani wao. Bali ni kwa sababu ya bunduki na hazina ya taifa . Lakini pili vyombo vya dola na vya maamuzi vimeingizwa ndani ya vyama hivyo.

Mtu kama M7 aliingia msitufungie kwa madai ya kuibiwa kura. Leo yeye hayupo tayari kushindwa hata kama uwezo wake umefika mwisho !! (UAFRIKA).

Kwa upande wa Ccm miaka ya Nyerere tulikuwa tunayakemea mataifa yaliokandamiza raia wake !!. Ajabu na kweli tunakemewa sisi leo !!. Mbaya zaidi Ccm na wafuasi wake , wamekuwa washabiki na wafuasi wa ma dictator ulimwenguni na mifano ipo.

Kwa ujumla nyani hajaona la kwake .
Nini kifanyike?
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom