CCM maslahi na vitisho vya Chui wa karatasi

abdulahsaf

JF-Expert Member
Aug 31, 2010
858
130
July 28, 2012 by zanzibaryetu

Na Abdallah Vuai

Wiki hii kuna kituko cha aina yake kimetokea ndani ya Chama cha Mapinduzi upande wa Zanzibar kwa wanachama wachache wa Chama hicho Wilaya ya Mjini kuasi dhidi ya mamlaka halali ya CCM. Ni kisa,. Kituko kinachoweza kuvunja mbavu pale baadhi ya Wana CCM walipotoa tamko la kuwatuma viongozi wao wa Wilaya kuwataka Makamu Mwemyekiti wa CCM Zanzibar na Rais mstaafu wa Zanzibar,Amani Abeid Karume kunyanganywa kadi kwa madai wamekwenda kinyume na msimamo wa CCM juu ya Muungano.

Viongozi wale waliobariki uasi ndani ya CCM nawawafanisha na aliyekuwa Rais wa Umoja wa Vijana wa African National Congress(ANC) Julius Malema. Katika mkutano huo ambao mbali ya kutaka Makamu Mwenyekiti wao Karume afukuzwe CCM,lakini pia walitaka wanachama wengine kama Mweka Hazina wa Chama hicho Zanzibar,Mansoor Yussuf Himid nae kunyanganywa kadi!

Kisa na mkasa; ni msimamo wa Hamza Hassan Juma, Mshimba Mbarouk, Thuwayba Edington Kisasi, Omar Yussuf Mzee, Mahmoud Mohammed Mussa, Haroun Ali Suleiman, Asha Bakar Makame, Salmin Awadh Salmin, Othman Masoud Othman, Nassor Salim, Mansoor Yussuf Himid katika muundo wa Muungano wakiukosoa hadharani kuwa hauna tija kwa kuwa umeshindwa kufikia kile Wazanzibari walichokuwa wakikitaka baada ya Mapinduzi ya Januari 12,1964 na matumaoni yao katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kwa Karume wanamtuhumu kuunga mkono mabadiliko ya muundo wa Muungano, ingawa Karume hajapata kusema aina gani ya mfumo wa muundo wa Muungano anaupendelea.

Wanachama wale wanamvumishia Makamu Mwenyekiti wao jambo ambalo hakulisema, uvumi wao ni sawa na abrakadabra inayotaka kuzuka ndani ya CCM. Mambo ya uzushi, fitna na pengine kutaka kukigawa Chama chao kikongwe katika Bara la Afrika.

Kuwepo kwa mawazo tofauti ndani ya CCM au kwenye jamii sio kosa kwani muda mfupi baada ya NEC ya CCM kukutana Dodoma mwezi Mei mwaka huu ilitoa taarifa ya kuelezea msimamo wake kuhusu muundo wa Muungano kuendelea na mfumo wa sasa.

Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti Bara, Pius Msekwa akihojiwa na Shirika la Utangazaji la Ujerumani idhaa ya Kiswahili alisema pamoja na msimamo huo wa CCM wanachama wake hawajafungika kuwa na mawazo au kutoa fikra tofauti na ule wa Chama chao kwenye kutoa maoni katika Tume ya Mabadiliko ya katiba.

Rais Jakaya Kikwete akizindua Tume ya Jaji Warioba nae aliweka mkazo haki ya kutoa maoni na kila mtu kuheshimu mawazo ya mwengine. Ibara ya 18(a) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema; kila mtu anao uhuru wa maoni na kueleza fikra zake.

Msimamo huo unatiliwa mkazo na Rais wa Zanzibar,Dk. Ali Mohammed Shein alipowahakikishia Wazanzibari kwamba wako huru kutoa maoni wayatakayo, hakuna atakayeingilia.

Kitabu cha Cycles of American kilichotungwa na Arthum Schelesinger Jr anasema kutokufungwa na mawazo ya kale katika mazingira yanayobadilika kunampa kiongozi wa kidemokrasia nafasi ya kutengeneza maonjo matamu ili apendwe na kufurahiwa na wengi.

Je, viongozi wale wa CCM Wilaya ya Mjini wanadhani watapendwa kwa kukandamiza uhuru wa maoni, kuishi mazingira ya kisiasa ya kibabaishaji ambayo kwanza hayakisaidii Chama hicho,lakini pia kinaweza kukimbiwa na wanachama kwani mfumo wa vyama vingi sera na uwazi ndani ya vyama ndio kigezo cha watu kujiunga na Chama husika.

Sheria inampa mtu kuwa mwenye haki mbele ya mtu mwingine na papo hapo kuwa mwenye haki mbele ya jamii kwa ujumla hivyo, wanachama wa CCM na hasa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanayo haki ya kijamii Social justice katika suala zima la mustakabali wa mfumo wa muundo wa Muungano wanaouona unafaa.

Mara nyingi haki ya kijamii ndio kilele cha demokrasia ambapo maamuzi ya nchi yapo mikononi mwa wananchi wenyewe na yafaa kutambua kuwa pasipo haki hakuna amani, Tulitegemea wakati huu ambapo Tume ya Mabadiliko ya Katiba inaendelea kukusanya maoni kungekuwa na uhamasishaji wa CCM Mjini kuwahimiza wanachama wao kwenda kutoa maoni.

Kama kosa la akina Hamza Hassan Juma, Mshimba Mbarouk, Thuwayba Edington Kisasi, Omar Yussuf Mzee, Mahmoud Mohammed Mussa, Haroun Ali Suleiman, Asha Bakar Makame, Mohamed Raza Daramsi,Salmin Awadh Salmin, Othman Masoud Othman, Nassor Salim, Mansoor Yussuf Himid, na wengineo ambao wanawajibika kuitetea Zanzibar ni kosa na dhambi kwa CCM Wilaya Mjini basi historia itawahukumu kwa uzalendo wao, vyenginevyo, CCM maslahi watalia na kusaga meno kwa vigae.

CCM maslahi wanataka kuwapitisha Wazanzibari katika njia yenye miba,kiza kinene iliyokuwa na mashaka mengi huku tope za Uhafidhina zikiwanasa miguuni na kuchelewesha safari katika kufikia Muungano wenye maslahi kwa kila upande, Tanganyika na Zanzibar.

Kwa kutaka kuwanasua Wazanzibari na tope la Muhafidhina, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman akitoa mada katika semina kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuhusu katiba mpya, aliukosoa Muungano kwa kiwango ambacho kiliwaridhisha Wawakilishi.

Katika kuthibitisha udhaifu wa muundo wa Muungano, Mwanasheria Mkuu anauliza mambo kadhaa ikiwemo uhalali wa Rais wa Muungano kuchaguliwa kwa wingi wa kura kwa kuzingatia tofauti ya idadi ya watu baina ya Zanzibar na Tanzania Bara;
Uhalali wa Rais wa Zanzibar kuwa Mjumbe tu wa Baraza la Mawaziri na sio Mwakilishi wa Zanzibar ndani ya Baraza la Mawaziri ili kuepuka kubanwa na Kanuni ya Baraza la Mawaziri ya Uwajibikaji wa pamoja.

Nini wajibu wa kikatiba wa Makamu wa Rais katika uendeshaji wa Serikali, Makamu wa Rais ni Msaidizi Mkuu wa Rais wa Muungano kuhusiana na Zanzibar kama ilivyokusudiwa na Mapatano ya Muungano? Jee ni Msaidizi Mkuu wa Rais wa Muungano kwa Mambo ya Muungano au Msaidizi Mkuu ni Waziri Mkuu? Hoja nyengine aliyowahi kuieleza Mwanasheria Mkuu ni pamoja na Makamu wa Rais hana urithi akimaanisha katika Serikali ya Muungano hana Mamlaka wala haiwakilishi Zanzibar na kwa mujibu wa katiba na sheria Rais wa Jamhuri ya Muungano anaweza akitaka tu,halazimiki.

Jee Mawaziri wanaotoka Zanzibar waliomo katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya Muungano wanaiwakilisha Zanzibar au ni watumishi wa Rais wa Muungano kama walivyo Mawaziri wengine?

Jee kuna chombo chochote cha Kikatiba au kisheria kinacholazimisha Serikali mbili za Jamhuri ya Muungano kukutana, kushauriana na kufanya maamuzi ya pamoja kama Mamlaka mbili za kuendesha Jamhuri ya Muungano?

Katika mfumo wa sasa wa Serikali mbili upo uwezekano wa Serikali mbili zinazoongozwa na vyama viwili tofauti kufanya kazi kwa maelewano, Jee kipo chombo cha kutatua mizozo inayoweza kujitokeza baina ya Serikali mbili?

Maswali haya sio yangu, ni ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar katika mada yake kwa Wawakilishi ambayo yanatuthibitishia haja ya mabadiliko ya muundo wa Muungano ingawa wapo watu wengine kwa ulevi wa madaraka wanayafumbia macho kwa tama ya vyeo na pesa.

Msanii maarufu kule Msumbiji ,Marcelino Dos Santos katika moja ya tungo zake alisema " We Must Plant". Tafsiri ya haraka haraka ni kwamba tuna lazima ya kupanda, kupanda nini, mawazo ya mabadiliko katika muundo wa Muungano ambao wengi wanataka uwe wa Serikali mbili,lakini wa mkataba sio wa kikatiba.

Wazanzibari wengi wanaotumikia Serikali ya Muungano aghalab wamekuwa wakisahau kule walikotoka, wakifika Tanganyika wanageuka na kuwaona Wazanzibari wakorofi na baadhi ya wakati hata kuwabeza.

Tumeshangazwa na matamshi ya Waziri wa Ulinzi,Shamsi Vuai Nahodha katika michango yake katika semina ile akionekana kutetea sana mfumo huu mbovu na dhaifu wa muundo wa Muungano.

Nahodha anaeleza namna kero za Muungano zinavyoshughulikiwa katika Kamati isiyokuwa na meno ya Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais, tumuulize Nahodha, miaka 48 kipi kimesababisha kushindwa kutatuliwa kwa kero hizo na sababu za kuzuka kwake?

Alipokuwa Waziri Kiongozi, Nahodha aliandika barua kumwandikia Waziri Mkuu juu ya maamuzi ya Baraza la Wawakilishi kuliondoa suala la mafuta na gesi asilia katika mambo ya Muungano, barua hiyo hadi hivi leo yeye anakuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Waziri Mkuu hajaijibu, tuseme haijafika pale Magogoni, imepotea Posta, au ndio wapo mbioni kuijibu?

Ndipo mwasisi wa Muungano, Hassan Nassor Moyo alipohoji kama kuna dhamira ya dhati ya kutatua kero hizo maana ni kipindi kirefu kimepita na pia alitoa angalizo kwamba wao enzi zao walifanya makosa,lakini makosa hayo lazima yasawazishwe na kizazi hichi.

Mwanafalsafa wa Ugiriki Socrates aliyeishi baina ya mwaka 469 BC – 399 BC siku moja aliwashangaza Wagiriki alipokwenda sokoni mkononi ameshika tochi akimulika mulika, wachuuzi walianza kumdadisi, imekuwaje leo? Akawaambia "kwenye nuru hii , kuna walio gizani."

Kweli kuna walio gizani na ndio maana wameanza kutoa vitisho kwa wengine wakiwatishia kuwafukuza katika CCM,hapa nataka kukumbusha jambo moja,wakati fulani,Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema "CCM sio baba yake wala mama yake" akafafanua "ikiwa kitapoteza sera na mwelekeo sina sababu ya kubaki ndani ya Chama hicho"

Sitaki kuamini kwamba CCM imepoteza sera, bali kuna watu ndani ya Chama hicho husasan Zanzibar hawana dira, hawana sera, wala hawana mwelekeo wanaishi kwa fitna, chuki na hawatumii bidii yao kukigeuza Chama hicho kuwa kimbilio la wengi, hawa ni ‘mufilisi' kisiasa.

Mfumo wa muundo wa Muungano wa sasa hauwezi kusafishika kwa maji taka, lazima tutumie maji safi la salama na wala wale wanaojidanganya kuwa vitisho vinasaidia kulinda Muungano wanaota ndoto ya mchana sawa na ' Mfalme aliyetembea uchi' huku watu wake wakijipanga barabarani kusifia vazi jipya la mfalme wao na wakijifanya hawaoni ubovu wa vazi jipya la Mfalme lililomweka nusu uchi kweupeni.

Tunashukuru Mungu wapo watetezi wa kweli wa Zanzibar kama Mwanasheria Mkuu anayetoa kasoro za Muungano bila woga, kama pale alipoelezea kizungumkuti cha kukosekana mfumo rasmi wa lila Mamlaka kuitambua Mamlaka Nyengine.

Othman anasema Hiyo ni kasoro kubwa sana katika Muungano na ambayo kwa bahati mbaya imejificha. Miongoni mwa athari zake ni Kwanza, ingawa Rais wa Jamhuri ya Muungano ana mamlaka kwa mambo ya Muungano ndani ya Tanzania Bara na Zanzibar, masuala kama vile ya Sheria za jinai si suala la Muungano na hivyo kinga aliyonayo ya kutoshtakiwa ndani ya Katiba ya Muungano haiwezi kutumika Zanzibar kwa vile Zanzibar ina mamlaka na sheria zake za jinai.

Mwanasheria Mkuu anauliza Suala muhimu hapa ni jee Rais wa Muungano anaweza kushtakiwa kwa kosa la jinai ndani ya Zanzibar? .Suala hili kwa hali ya sasa linaweza kuonekana la kituko, lakini ni la muhimu sana" Anasema.

Hakuishia kwa Rais wa Muungano,pia aliuliza kwa Rais wa Zanzibar anapokwenda Tanzania Bara. "Pili, suala kama hili ni muhimu kujiuliza kwa Rais wa Zanzibar anapokuwa ndani ya Tanzania Bara. Tatu, Katiba haijaweka bayana masuala ya mashirikiano ya kimahkama hasa katika utekelezaji wa amri za Mahakama za pande mbili. Jambo pekee lililoelezwa ni upelekaji hati za Mahakama"

Kwa maswali hayo yasiyokuwa na majibu ndipo pale haja na ulazima wa kuwa na mfumo wa muundo wa Mungano wa mkataba unaposhika nafasi kwani kwa mazingira yalivyo njia pekee na bora ya kuweka sawa nyumba yetu ni kufanya mabadiliko ya muundo.
 
Back
Top Bottom