CCM kusuka au kunyoa kwenye maridhiano

CCM kusuka au kunyoa kwenye maridhiano

Parabolic

JF-Expert Member
Joined
Dec 3, 2013
Posts
2,743
Reaction score
2,601
123942341_2709278242657781_3738074267151149893_n.jpg


Wakati Tume ya Kuchunguza Uvunjifu wa Amani kabla na baada ya uchaguzi Mkuu ikiendelea kukamilisha kazi yake ya miezi mitatu, picha inayojionyesha kwa sasa, CCM ina machaguo mawili tu, ama kuiendesha nchi kidikteta au kukubali kuachilia mabavu yake na kuwapa nafasi wapinzani.

Kuna kila dalili kwamba CCM imepoteza mvuto miongoni mwa Watanzania na ndio sababu ya kutokea vurugu za Oktoba 29, 2025. Ni kutokana na kushindwa kukidhi matarajio ya Watanzania walio wengi, ikiwa pamoja na kushindwa kutoa ajira kwa vijana, ongezeko la umasikini na kuminywa kwa uhuru wa maoni.

Mambo yanakuwa magumu kutokana na ongezeko la idadi ya watu ambao kimsingi ndio wanaohitaji hali bora za maisha na CCM ndio chama kinachoongoza Serikali kinapaswa kukidhi matarajio yao.

Akiwasilisha taarifa ya Hali ya Taifa ya Uchumi ya Mwaka 2023, Bungeni mjini Dodoma, Juni 13, 2024, Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo alisema idada ya Watanzania ilikadiriwa kufikia 63,670,531 mwaka 2023 ikiwa ni ongezeko la asilimia 3.1 ukilinganisha na idadi ya watu milioni 61.74 waliotajwa katika matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Alisema Tanzania Bara ilikuwa na watu milioni 61.7 sawa na asilimia 96.9 huku Tanzania Zanzibar ikiwa na watu milioni 1.9.

Ukuaji wa uchumi hauko vibaya, kwani pato halisi la Taifa (GDP) lilifikia Shilingi trilioni 156.6 mwaka 2024, ikilinganishwa na Shilingi trilioni 148.5 mwaka 2023. Hii inawakilisha ukuaji wa asilimia 5.5, ikiongezeka kutoka asilimia 5.1 mwaka uliopita.

Hata hivyo, kwa kasi ya ongezeko la idadi ya watu, CCM inapaswa kufikiria upya mikakati ya ukuaji wa uchumi kukidhi mahitaji ya wananchi.

Yaliyotokea katika uchaguzi wa Oktoba 29, 2025 ni jibu tosha kwamba CCM kama chama cha siasa imepoteza mwelekeo na pia imepoteza matumaini ya wananchi ndio maana walikuwa tayari kujitokeza barabarani kuandamana bila kujali vitisho vya polisi wenye silaha za moto.

Yaliyotokea Oktoba 29 yalikuw ani mafuriko ya hasira za wananchi na yameonyesha kwamba wakiamua wanaweza kutekeleza wanachofanya.

Chanzo

Kwa muda mrefu CCM imekuwa ikipuuza kilio cha kupatikana kwa Katiba mpya. Katika uchaguzi mkuu, kulikuwa na madai ya mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi, lakini nacho hakikusikilizwa.

Kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, wadau mbalimbali wa kisiasa hasa chama cha upinzani cha CHADEMA waliibua hadharani wasiwasi kuhusu kile walichokitaja kuwa udhaifu wa kimfumo na dosari zilizoweza kuathiri uhalali na uaminifu wa uchaguzi.

Wadau hao waliwasilisha hoja zao kupitia mikutano na waandishi wa habari, matamko ya umma, barua kwa mamlaka za uchaguzi, hatua za kisheria mahakamani, pamoja na majukwaa ya kiraia.

Kwa ujumla, hoja hizo zilihusu masuala kadhaa, ikiwemo uhuru na mwenendo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Walisema kuwa mamlaka ya utendaji yalikuwa na ushawishi mkubwa katika mchakato wa uteuzi wa makamishna na kwamba maamuzi ya NEC ikiwemo uthibitishaji wa wagombea na ushughulikiaji wa migogoro yalionekana kuipendelea chama tawala.

Pia walieleza wasiwasi kuhusu usajili wa wapiga kura na daftari la wapiga kura, ambapo CHADEMA ilitoa tahadhari mara kwa mara kuhusu ubora na uadilifu wa daftari hilo. Walidai kuwapo kwa ucheleweshaji na dosari katika zoezi la usajili na uhakiki wa wapiga kura, madai ya kunyimwa haki wapiga kura wanaostahili, pamoja na taarifa za majina yanayojirudia na majina ya watu waliokwisha kufariki kuonekana kwenye daftari.

Vyama vya upinzani, vikiongozwa na CHADEMA, pia vilipinga kile walichokitaja kuwa kuwavua wagombea sifa kiholela, hususan katika ngazi za serikali za mitaa na bunge, huku wagombea wa chama tawala cha CCM wakiachwa bila kuchukuliwa hatua kama hizo.

Wadau wa kisiasa waliituhumu serikali na chama tawala kwa matumizi mabaya ya rasilimali za umma wakati wa kampeni, ikiwemo viongozi wakuu wa serikali kufanya kampeni wakitumia magari ya umma, ulinzi wa serikali, na majukwaa ya shughuli za umma.

Hoja nyingine kubwa ilikuwa nafasi ya polisi na vyombo vya usalama. Viongozi wa upinzani walidai kuwa vyombo vya dola vilifanya kazi kwa upendeleo, vikichukua hatua kali zaidi dhidi ya shughuli za upinzani.

Kutokana na changamoto hizo, CHADEMA na wadau walioungana nayo walitoa wito mara kwa mara wa kufanyika kwa marekebisho ya sheria za uchaguzi na taasisi husika ili kuhakikisha uchaguzi huru, wa haki na wenye uaminifu.

Lakini maoni haya hayakusikilizwa, badala yake CCM ilijielekeza kwenye vitisho na matumizi ya nguvu za kijeshi kwa waliopanga kuupinga uchaguzi huo. Kwanza waliidhibiti CHADEMA kwa kumkamata mwenyekiti wao, Tundu Lissu na kumfungulia kesi ya uhaini na kesi za uchochezi. Pia chama hicho kilifunguliwa kesi za mgawanyo wa mali na hivyo kikazuiwa kufanya kazi zake.

Kwa upande mwingine viongozi wa Serikali akiwamo Rais Samia Suluhu Hassan, alisikika mara kadhaa akiwaonya watu waliopanga kuupinga uchaguzi huo.

Akihutubia mamia ya wakazi wa Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam Oktoba 21, 2025, wakati wa mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu wa Rais Samia alisema, yeye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa nchi hii, hivyo hakutakuwa na maandamano bali watu kwenda vituoni kupiga kura.

Akihutubia maelfu ya wananchi kwenye Viwanja vya Gombani ya Kale Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba leo Septemba 20, 2025, Rais Samia alisisitiza kuwa serikali yake itahakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa salama.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali imejitahidi sana kusimamia utulivu wa kisiasa, usalama na amani ndani ya nchi.

"Napenda kuongeza sauti yangu kwenye masuala ya ulinzi na usalama. Ndani ya miaka mitano yote hamjasikia pepepe, mkisikia basi ni ajali imetokea wamekufa wangapi na labda mtu mwenyewe atakwenda kuchokoza na kuvunja amani, lakini hamjasikia vurugu ndani ya nchi hii. Hata wale waliovuka mipaka na kuleta vurugu ndani ya nchi yetu tuliwashughulikia na hawajathubutu kurudi tena," alisema Rais Samia.

Aliendelea: “Niwaeleze kwamba, tarehe zile za kupiga kura, hakutakuwa na vurugu zozote, tokeni kwa wingi mkapige kura, vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga vyema kuilinda nchi yetu, na mimi ndiyo amiri jeshi mkuu ninayesema hapa.

“Tumejioanga vyema kuilinda nchi yetu, kwa hiyo hakutakuwa na nywinywi wala nywinywinywi.”

Matokeo ya uchaguzi

Matokeo yake siku ya uchaguzi mambo yaligeuka, ghafa maandamano yakaibuka kuanzia saa 5 asubuhi jijini Dar es Salaam na kusambaa katika miko ya Arusha, Mwanza, Mbeya, Njombe, Iringa na Kilimanjaro.

Licha ya vurugu zilizotokea Oktoba 29, 2025, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ilimtangaza Rais Samia Suluhu Hassan kushinda kwa kupata kura milioni 31.91 sawa na asilimia 97.6, akifuatiwa kwa mbali na wagombea wa vyama vingine 17 vilivyoshiriki.

Ripoti za waangalizi wa uchaguzi

Muhtasari wa taarifa ya awali ya waangalizi wa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania 2025 kutoka SADC (SEOM), uliowasilishwa na Richard Msowoya, Spika wa zamani wa Bunge la Malawi na Mkuu wa Ujumbe wa Waangalizi wa SADC alisema pamoja na mengine, kulikuwa na idadi ndogo ya wapiga kura iliripotiwa, na katika baadhi ya vituo hakukuwa na wapiga kura kabisa.

Pia alisema kulikuwa na tuhuma za udanganyifu wa kura kutokana na kura za mafungu zilizokuwa zimepangiliwa vizuri kwenye masanduku ya kura zikiashiria watu walipiga kura nyingi kwa wakati mmoja, pamoja na ukosefu wa waangalizi wa ndani katika vituo vingi.

Aligusia pia suala la kufungwa kwa mtandao wa intaneti kulizuia SEOM kupata takwimu kamili za upigaji kura na kuhesabu na waangalizi wengi hawakuweza kushuhudia kufungwa na kuhesabiwa kwa kura kutokana na matukio na vitisho vya vurugu katika baadhi ya maeneo.

Ripoti za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika, Mtandao wa Uangalizi wa Uchaguzi wa Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika (EHORN) na ile ya Chama cha African National Congress cha Afrika Kusini pia vilikosoa mwenendo wa uchaguzi huo.

Taasisi ya Thabo Mbeki ya nchini Afrika Kusini nayo ilitoa ripoti yake Novemba 23, 2025 ikikosoa uchaguzi huo.

Taasisi hiyo ilieleza kusikitishwa na uvunjifu wa amani uliojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu nchini humo, ikisema kuwa imekosa ‘serikali halali’.

Kulingana na taasisi ya Thabo Mbeki, matokeo ya urais na ubunge nchini Tanzania, hayaakisi matakwa ya Watanzania wenyewe.


Mbali na taasisi hiyo, Rais wa zamani wa Botswana, Ian Khama, akizungumza katika kongamano la African Renaissance lililofanyika Lukenya University nchini Kenya Novemba 10, 2025, alisema “hamtambui Rais Samia Suluhu Hassan kama kiongozi halali wa Tanzania.”

Alieleza kuwa uchaguzi wa mwaka 2025 ulitawaliwa na vitisho, vifo, na ukandamizaji wa wananchi waliopinga utawala, akisisitiza kuwa mazingira hayo hayakuruhusu demokrasia ya kweli.

Hata hivyo, mara kdhaa Rais Samia amesikika akitetea uchaguzi huo, akisema wanachi walijitokeza mapema kwenda kupiga kura kabla maandamano hayajatokea.

Akihutubia wakati wa kuzindua Bunge la Jamhuri ya Muungano, Jovemba 14, 2025, Rais Samia alisema, “Aidha, utaratibu wa kuongeza vituo vingi vya kupigia kura ulisaidia sana kupunguza msongamano katika vitu hivyo, kwa hakika upigaji kura kurahishwa sana na haukuchukua muda mwingi wa wananchi kama ilivyozoeleka.

“Jambo lililowafanya baadhi ya waangalizi wa uchaguzi kudhani wananchi hawakujitokeza kupiga kura.”

Pamoja na utetezi huo, ni wazi kwamba CCM ina wakati mgumu wa kujitetea mbele za wananchi na hata kwa jumuiya ya kimataifa.

Nini kifanyike?

Pamoja na kwamba CCM imeshaahidi kuunda Tume ya Maridhiano, bado ina wakati mgumu wa kuachilia madaraka yake ili igawane na wapinzani, kwani hilo ndilo suluhisho la kupunguza shinikizo la malalamiko ya wananchi.

Vinginevyo, CCM inaweza kuamua kuziba masikio na kuiendesha nchi kidikteta kabisa, jambo ambalo ni la hatari Zaidi, kwani linaweza kuibua mlipuko mwingine wa machafuko huko tuendako.

Kwa hali ilivyo sasa, huenda CCM ikakubali kushirikiana na vyama vya upinzani hasa CHADEMA, japo hakikushiriki uchaguzi. Ushirikiano huo unaweza kufanyika kwa kuanzisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama ilivyo kwa Zanzibar.

Kuna kila dalili kwamba, joto lililopo sasa halitakuja kupoa badala yake linaweza kuongezeka Zaidi, hivyo, usalama pekee wa CCM utategemea jinsi ilivyotengeneza mazingira ya kupumulia ili joto la madai ya wananchi lipungue.

Soma pia: Maridhiano yatakuwa useless kama Lissu atakataa kushiriki

Afueni hiyo itatokana na kuwashirikisha wapinzani kwenye Serikali, kwa kukubali mabadiliko waliyokuwa wakidai katika uchaguzi. Mabadiliko hayo ni pamoja na mchakato wa mabadiliko ya Katiba na mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi.

Japo, CCM inaweza isiachilie moja kwa moja, bali kinachotafutwa sasa ni kuendelea kubaki madarakani kwa kuachilia taratibu.

Suluhisho la kudumu ni kukamilisha mchakato wa mabadiliko ya Katiba uliokwama tangu mwaka 2014. Mchakato huo unapaswa kuwa shirikishi na wa uwazi ili kutoa fursa kwa makundi yote kutoa maoni yatakayoleta mwafaka wa kudumu.

Je, CHADEMA wattakubali kushiriki hayo maridhiano kwa kiasi gani?
 
Hizi pumba tupu. Hao wapinzani wa kuwaachia nchi wako wapi? Nani ana mfumo wa uongozi? Au una maanisha akina Heche bangi?
 
Back
Top Bottom