Chama chetu hakikuwa na haja.Haja ya kuzunguka nchi nzima na 'kukitangaza' chama sasa. Haikuwa na haja ya hadi kumkodi Balozi wa China kunogeshga mikutano ya chama inayoongozwa na Katibu Mkuu Kanali Mstaafu Abdurahman Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi
Nape Nnauye. Haja haikuwepo.Tulikuwa wapi miaka yote ya utawala wetu wa miaka 52 sasa?
CCM yetu haikuwa na haja ya kushangilia kupokea makada toka vyama vingine.Watanzania walioongozwa na CCM tangu 1977 (ikichukua mikoba ya TANU-Tanganyika na ASP-Zanzibar) hawawezi kuielewa CCM sasa. Hawadanganyiki na mikutano ya sasa ya CCM,iwe ya hadhara au ya siri. CCM imechezea bahati yake.Bahati ya kuaminiwa.Ya kuonwa kama chama kisicho na mbadala. Bahati ya kuganda mioyoni mwa watanzania maskini wengi wakiwa wakulima na wafanyakazi.
CCM haikuwahi kuwa na upinzani wa maana kwa miaka mingi.Kama chama kikabweteka.Sasa kinatapatapa.Hakukuwa na haja hiyo sasa kama chama kingejiandaa kabla. Watanzania wa sasa hawafuatilii mikutano ya CCM na kuiona kama sehemu ya maisha yao-kama zamani. Mambo yamebadilika. CCM haina haja ya kujaa hasira,visa na hujuma. Ni muda wa kufunzwa na watanzania.Kufunzwa siasa za ushindani.
Watanzania sasa wanazidi kuungana juu ya uandikaji wa Katiba mpya.CCM haikuwa na haja ya kuwapinga.Ilipaswa au inapaswa kuungana nao na kuyaishi maamuzi ya watanzania. Suala hili la Katiba mpya halina haja ya kulipuuza na kuliletea propaganda. Hakuna haja kung'ang'ania hoja zinazosadifu 'u-conservative' wa chama.Mazoea. Kunoga kwa madaraka. Uandikaji wa Katiba mpya Tanzania ni upepo mkali wa kisiasa usiozuilika na CCM. Kuuzuia ni kupeperushwa nao. Hakuna haja ya kutafuta makuu.
Mzee Tupatupa wa Lumumba,Dar es Salaam