CCM endeleeni kukata Dawa ya kiungo kilichooza mwilini ni kukatwa! Kukiacha ni kujichulia kifo!

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,531
HATIMAYE CCM imekata kilichosema hakikatiki! Lakini tunapaswa, na hasa CCM, inapaswa kujiuliza, je, imemaliza kibarua cha kukata? Binafsi naamini kazi ya kukata ndiyo kwanza imeanza labda mwenye kikatio aingie uvivu!
Lakini kabla ya kuonyesha wakati wapi niwapongeze sana CCM angalau kwa kuthubutu kukata gogo lililojidai halikatiki! Hakika huu ulikuwa mtihani mkubwa sana kwa CCM.

Haijapata kutokea kiongozi au mwanachama akaitisha CCM kiasi hiki! Wengi walidhani kweli hili hogo halikatwi! CCM ingejitakia balaa huko mbele ya safari kama isingekata! Tena kwa mkato mkali! Hongereni sana! Dawa ya kiungo kilichooza mwilini ni kukatwa! Kukiacha ni kujichulia kifo!

Sasa tuone kuna viungo vingine vya kukata? Naam, vimejaa tele! Viungo vilivyoambukizwa ugonjwa mbaya wa kukataa kukatwa! Lazima vikatwe la sivyo vitaharibika hadi navyo vidai HATUKATWI. CCM lazima ikumbuke ililea tabia hii ya viungo kukataa kukatwa.
Ndiyo! Ni pale ilipokuja na falsafa ya kukata gamba na ikaambiwa gambi halivuliki litaishia kiunoni na yenyewe ikatishika! Ikaacha kukata! Viungo vigonjwa vikaamini ukisema SIKATWI watanywea! Sasa CCM isizembee tena, ikate!

MKATO NAMBA 1: Kuna mzee mtu mzima huyu anakielewa chama na taratibu zake vyema. Anajua wazee ndio watuliza fujo hivyo hawapaswi kushiriki fujo.Lakini mzee huyu akatoka chana kweupe akashiriki fujo! Tena kwa kiwango cha hadi kutishia CCM. Eti anayemtaka asipochaguliwa nchi itaingia kwenye machafuko!

Mzee huyu kwa umri wake na nyadhifa alizowahi kushika serikalini na katika chama alipaswa kujua KUKUBALIKA na KUSTAHIKI ni vitu viwili tofauti. Unaweza kukubalika lakini hustahiki! Lakini mbaya zaidi mzee huyu aliona kukubalika huku kukinunuliwa. CCM lazima ikate! Tena ikate bila soni maana hapa baba atakuwa mhusika! Wasijali kilio cha kizee, WAKATE!

MKATO NAMBA 2: Kuna kiongozi amekulia CCM toka TANU hadi CCM. Amekuwa waziri. Huyu angepaswa kujua vyema dhana ya uongozi wa pamoja. Mrema alikiuka dhana hii AKAKATWA! Huyu ametoka kwenye kikao wala hakukisusia lakini akaita waandishi wa habariakatangaza uamuzi wake yeye na wenzake wawili! Huyunaye ni lazima AKATWE!

Ni hatari kuacha kiungo cha aina hii mwilini! Kifaa kitakachomkata kitumike pia kuwakatia alioandamana nao! Mmoja waziri, mwingine mtu mzito tu chamani! Hawa nao walipaswa kuelewa uwajibikaji wa pamoja; Waziri ambaye anatoka kwenye kikao ambacho mkuu wake wa kazi ndiye mwenyekiti na kutangaza hakubaliani na maamuzi hafai! Na WAKATWE. Kutoadhibu tabia hii ipo siku waziri atatoka kikao cha baraza la mawaziri na kudai hakubaliani na maamuzi kwa kuitisha kikao pale Habari Maelezo.

MKATO NAMBA 3: Kuna wabunge wa chama ambao wote walishiriki maamuzi ya bunge yaliyofanya kiongizi kujiuzulu lakini wabunge haohao wamehudhuria mikutano iliyoitishwa na mtu waliyemuadhibu bungeni. Hii ilijenga taswira kuwa kule bungeni alionewa! Hawa bila soni wamesikika wakimpigia debe huku wakijua fika muda wa kampeni bado na kuwa mhusika anakiuka taratibu za chama kilichowapa tiketi ya kuingia bungeni.IItakuwa ajabu sana chama kikirudia kuwapa leseni ya kugombea ubunge. Hawa nao na WAKATWE bila huruma.

MKATO NAMBA 4: Kuna watumishi wa chama mikoani na ilayani walionyesha mapenzi yao dhahiri kwa wagombea haswa, mmoja wao. Hawa walitoa ushirikianotofauti kwa wagombea. Hawa ndio viongozi wa chama walio karibu na wanachama na wananchi. Uhai wa chama unawategemea wao kwa kiasi ikubwa. Na ndio watakaosimamia kampeni ya chaguo la chama chaguo ambalo halikuwa lao!

Si vyema wakaendelea kwenye nafasi zao hata kama kuna msemo kuwa makundi yavunjwe wote wawe kitu kimoja! Ama kwa hakika uundaji wa makundi na kushabikia makundi ni jambo halifai toka mwanzo. Ni uozo usiopona kirahisi. Si vema ndani ya chama watu wakaaminishwa wanaweza kuunda makundi halafu waje kuyavunja. Makundi ni sawa na kansa! Haiponi mpaka kiungo kichomwe mionzi au kikatwe! Hawa nao na WAKATWE.

MKATO NAMBA 5: Kuna wafanyabiashara matajiri walifadhili kampeni kinyume na utaratibu na utamaduni wa Taifa. Mbaya zaidi malengo yao ikiwa ni kujinufaisha ikiwa huyo anayemdhamini akipita. Taifa kuacha wafanyabiashara wajihisi fedha zao zinaweza kutuchagulia kiongozi ni hatari mno!

Nina hakika vyombo vyetu vya Usalama viliwabaini; si rahisi kuwa watu ambao sisi wananchi wa kawaida tuliwaona wakigawa fedha, wasibainike kwa vyombo hivi. Ama kwa hakika, kikundi hiki ni cha hatari mno kwa mustakabali wa usalama wa taifa letu.

Wahusika wanapaswa kuadabishwa ili wajue utajiri wao si paspoti ya kuingilia mchakato wa uteuzi wa wagombea wa nafasi yoyote ile nchini.

MKATO NAMBA 6: Kuna vyombo ambavyo kwa mamlaka waliyopewa wangepaswa kuwabaini, kuwakamata na kuwafikisha mbele ya sheria wote waliokuwa wakipokea au kutoa rushwa. Tumeshuhudia watangaza nia hasa mmoja wao na kikundi chake wakifanya mambo kama vile hatuna vyombo vya ulinzi, usalama au vya kupambana na rushwa.

Utadhani Nape Nnauye ndiye alikuwa na wajibu huo! Uzembe wao huu ulichochea vitendo vya rushwa! Ulifanya wengi waamini mgombea wao ameviweka mfukoni! Kama vyombo hivi vingetimiza wajibu wake Taifa lisingepitia vurugu zote tulizoona.

Utadhani walianza kazi vikao vya mwisho Dodoma! Hakika wangeanza kamatakamata mapema huenda hata vikao vya chama Dodoma vingekuwa vyepesi. Hawa nao waliozembea hivi inafaa wakuu wao WAKATWE!

MKATO NAMBA 7: Kuna viongozi wa kiroho, wengine waliojipachika unabii na utume ambao walitumia nafasi zao kuaminisha umma kiongozi wanayemuunga mkono ni chaguo la Mungu! Mazoea haya ya viongozi wa kiroho kushiriki siasa za kiushabiki ipo siku yataligharimu Taifa.

Tumeona mtu akifananishwa na Joshua na ilipoonekana haijakolea, akafananishwa na Mtume Mohamad! Tushukuru Mungu Waislam hawakukerwa! Au labda hawakupata muda wa kukerwa! Tumeona nchi za wenzetu kauli kama hizi zilivyoleta mauaji na ghasia!

Mimi sina uhakika kuwa huyu aliyefananishwa na Mtume na yule aliyemfananisha na Mtume wako salama kiasi gani machoni mwa waumini. CCM lazima IMKATE yule aliyetoa kauli ya hatari namna hii kwa malengo binafsi ya kisiasa na kimaslahi. Iweje kiongozi mzoefu kama yule asipime uzito wa kauli hii? Iweje aliyepachikwa utume asikanushe haraka kuwa yeye si Joshua wala si Mohamad!?
Hakujua uzito wa jambo hili?

Kama hakujua hivi angepata Ikulu tungekuwa salama? Angetambulika kamaAmiri Jeshi Mkuu, Mtume na Rais wa JMT?! Kwa viongozi wa kiroho (au uroho?) waliojihusisha na siasa za udanganyifu ni vyema chama kupitia serikali KIWAKATE.

Serikali ichunguze kwa makini vyanzo vyao vya mapato na biashara zao. Je, wanaendesha shughuli zao kitaasisi au ni mali binafsi? Ni kweli wao ni NOT FOR PROFIT institutions au ni wafanyabiashara kama makampuni mengine?! Tukichelewa wakaota mizizi kama wa huku Afrika Magharibi, ipo siku tutajuta.

MKATO NAMBA 8: Kuna watendaji serikalini wakiwamo mawaziri, makatibu wakuu na watumishi wengineo, walioonyesha mapenzi yao kwa wagombea kinyume cha utaratibu na bila kuzingatia maslahi mapana ya Taifa. Kuna wengine inasemekana walihusika katika ugawaji pesa za rushwa. Hawa nao wachunguzwe na watakaobainika na WAKATWE.

Tukiwa na watumishi serikalini na hasa mawaziri na makatibu wakuu waliojiunga na makundi ni hatari. Hawa wakibaki serikalini wanaweza kuendesha mgomo baridi kwa kuwa aliyepita si mtu wao. Hali kadhalika, mtu wao akipita watatekeleza majukumu yao watakavyo kwa kuwa watajua bwana mkubwa anajua walimlinda!

MKATO NAMBA 9: Kuna wajumbe wa NEC na Mkutano Mkuu ambao kwa kiburi cha kutisha, walifikia hatua ya kumdhalilisha Mwenyekiti kiti wa CCM, KAMATI KUU, KAMATI YA NIDHAMU NA MAADILI NA BARAZA LA WAZEE.

Hili ni jambo la kusikitisha mno na la hatari kwa chama.

Haijapata kutokea tokea enzi za TAA, ASP, TANU hadi CCM Mwenyekiti wa Chama kudharauliwa vile! Wale wote waliojigeuza mavuvuzela ya kuimba wana imani na aliyekatwa na wao WAKATWE! Tena hawa wakatwe kwelikweli. Hivi hawamwamini Mwenyekiti wao ambaye pia ni Rais na Amiri Jeshi Mkuu?

Hawajui Mwenyekiti wao ana 'macho' ya kuona wasivyoviona wao? Kwa kuwa kanda zipo basi yale mavuvuzela yote YAKATWE la sivyo ipo siku Mwenyekiti na Wazee wa Chama wataambulia aibu kuu ukumbini. Hawa hawafai kuwa wa NEC wala wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM!

Huenda wamezoea kiasi wanaona wao tu ndio wanaweza kuwa wa NEC au wajumbe wa Mkutano Mkuu. Chama kiwaonyeshde mlango wa kutokea waende huko utovu wao wa nidhamu utakakovumiliwa na si CCM ya Mwalimu Nyerere.
Lazima nidhamu kwenye vyombo hivi irejeshwe, ijengwe upya! Ilijengwa, isiachiwe ibomolewe na wachumia tumbo mavuvuzela! Hivi MNEC au mjumbe wa MkutanoMkuu ambao ndio chombo cha kuchuja wagombea iweje wajihusishe na kambi ya mgombea? Hawa walipaswa kutolewa nje! Chama kilikosea sana kuwaruhusu washiriki kupitisha majina! Walishajiondolea sifa wenyewe! Hawa ndio walikuwa viongozi wa ile kwaya ya TUNA IMANI! WAKATWE HARAKA! Wasipokatwa ipo hatari siku moja kwaya ikawa HATUNA IMANI NA MWENYEKITI!

Baada ya CCM ikisaidiwa na Serikali kuendesha zoezi la KATAKATA, inabidi CCM itafakari kwa kina ni mtaa gani ile nidhamu ya chama ilikimbilia! Nazungumza hivi kwa kuwa niliwahi kuwa mwanachama wa TYL, TANU na hatimaye mwanachama mwanzilishi CCM! Na kadi zote tangu TYL nimehifadhi! Enzi zile hatukuona vituko hivi.

CCM iteue jopo la watu watakaoisaidia kutafiti kwa kina mapungufu na namna ya kuziba mapengo yaliyojitokeza. Kuendelea kana kwamba mambo yalienda sawa itakuwa kujidanganya. Nimalizie kwa kuipongeza CCM! Pamoja na udhaifu wake imeinusuru nchi kwa kiwango cha kuridhisha. Sijui kama Watanzania wanaelewa kuwa nchi iliponea chupuchupu kuangukia mikononi mwa mafioso wa kitaifa na kimataifa?

Historia itakapoandikwa itathibitisha na kuwainua wale wote walionusuru nchi! Hongereni sana wazee wa chama (isipokuwa yule aliyekwenda Sheikh Amri Abeid), Sekretariati ya Maadili, Kamati Kuu (isipokuwa wale watatu waliopinga maamuzi) na Baraza la Wazee. Historia itawaandika kwa wino mzito! Binafsi nimpongeze Mwenyekiti kwa kufunika uso wakati nyani anauawa! Kweli akili za mwenzako changanya na za kwako!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom