Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,318
- 33,125
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamshi Vuai Nahodha
Ziara ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamshi Vuai Nahodha, imekumbwa na vurugu mjini hapa Wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya kufuatia vijana wanaosadikika kuwa ni wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuupokea msafara wake kwa bendera za chama hicho huku wakionyesha alama ya vidole viwili.
Kutokana na hali hiyo, vijana wa Cham Cha Mapinduzi (CCM) (mabaunsa) waliamua kujibu mapigo kwa kuanza kutembeza mkongoto wa nguvu kwa vijana wa Chadema hivyo kusababisha amani kutoweka kwa muda mfupi katika eneo hilo.
Tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 3:45 asubuhi katika eneo la njia panda ya kuingia forodhani na barabara kuu iendayo Sumbawanga wakati msafara wa waziri huyo ukielekea katika hoteli ya Al-Noor ambako alikwenda kwa ajili ya kusomewa taarifa ya Wilaya ya Mbozi.
Baada ya msafara wa magari ya viongozi wa CCM, Polisi na Uhamiaji waliofuatana na waziri huyo kuingia mjini Tunduma vijana waliokuwa wamejipanga pembeni mwa barabara walianza kuzomea huku wakionyesha alama ya vidole viwili inayotumiwa na Chadema, mmoja wa vijana hao alikuwa na bendera moja ya chama hicho akipeperusha juu.
Kufuatia hali hiyo, vijana wa CCM ambao waliokuwa wamevalia fulana nyeupe zilizoandikwa mgongoni CCM Imara waliwavamia vijana wa Chadema waliokuwa wakizomea msafara huo na kumkamata kijana mmoja aliyekuwa na bendera hiyo na kuanza kumpa kipigo.
Baada ya vurugu hizo ambazo zilidumu kwa takribani dakika kumi, polisi waliokuwa wakilinda usalama wa msafara wa Waziri huyo waliingilia kati kwa kumtia nguvuni kijana aliyekuwa akipewa kipigo na vijana wa CCM ili kuokoa maisha yake ambayo yalikuwa hatarini na kumpeleka katika Kituo cha Polisi Tunduma.
Kijana huyo ambaye jina lake halikuweza kujulikana mara moja wakati akipigwa na mabaunsa wa CCM, alichaniwa nguo zake huku akibebwa juu juu. Baada ya kufikishwa kituo cha polisi vurugu hizo zilisimama na polisi kutanda barabara yote kuanzia hoteli ya Al-Noor hadi ofisi za CCM kata ya Tunduma.
Waziri Nahodha akizungumza na wananchi katika viwanja vya CCM Kata ya Tunduma, alisema hajafurahishwa na vurugu zilizotokea na kuwaagiza askari chini ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi, kuimarisha ulinzi katika mji wa Tunduma.
Alisema wafanyabiashara wa soko mjini Tunduma wafanye biashara zao kwa amani kwa sababu biashara inayofanywa kwa amani inakuwa na tija.
Lipo jambo ambalo sikulipendelea sana leo (jana) wakati napita niliona hali ya utulivu siyo nzuri, nikiwa kama waziri mwenye dhamana siwezi kuona hali hii ikiendelea, naomba askari chini ya RPC (kamanda wa polisi mkoa) imarisheni ulinzi haraka, alisema Nahodha.
Alisema mji huo unatakiwa kuimarishwa ulinzi kwani zinafanyika biashara za aina mbalimbali za halali na haramu na kuna mkusanyiko wa watu kutoka nchi mbalimbali.
Alisema wale wanaofanya biashara haramu watambue kuwa sasa likizo imekwisha, hivyo polisi wachukue hatua haraka kuanzia jana kwa kuimarisha ulinzi.
Aliongeza kuwa wale wanaofanya biashara halali wasibughudhiwe waachwe waendelee kufanya kazi zao kwa utulivu na wale wanaofanya biashara ya kubadilisha fedha Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iwawekee utaratibu mzuri ili kusitokee wizi wa watu kuibiwa fedha zao.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Tunduma, Daniel Mwashuya, alisema mji huo ulishikandikana kuwa na amani, lakini sasa imewezekana kwani ndani ya chama wamejipanga kusaidia kuiimarisha.
Tunduma sasa ni safi, wana Tunduma wanataka amani, hawa wanaoleta vurugu katika mji wetu tutawaminya kwa ukucha, tunawaweza na kwa tukio la leo wengine wametimkia mabondeni, alisema Mwashuya.
Mji huo ambao upo mpakani kwa mara kadhaa umekuwa ukikubwa na vurugu zisizoisha hali ambayo imekuwa ikiharatisha usalama wa wakazi wake. Mara kadhaa wanaofanya vurugu hizo wamekuwa wakikimbilia upande wa pili wa nchi jirani ya Zambia.
Akizungumzia kijana wa Chadema aliyekamatwa, Kamanda Nyombi alisema kuwa alipelekwa katika kituo cha Polisi cha Tunduma, ingawa hakueleza sababu za kukamatwa kwake.
CHANZO: NIPASHE