CCM, CDM vyatuhumiana

joseeY

Senior Member
Nov 4, 2010
108
17
Kiwewe cha uchaguzi Igunga kimezidi kutesa vyama vya CCM na Chadema, baada ya kuendelea kutuhumiana huku chama tawala kikidai kunasa kile ilichokiita mpango wa siri wa wapinzani wake hao wa kujitangazia ushindi kabla Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kufanya hivyo.

Chadema nacho kimekituhumu CCM kwamba kimeandaa mpango wa kupeleka wapigakura mamluki kutoka katika baadhi ya mikoa ukiwamo Dar es Salaam.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Steven Wassira aliwaambia waandishi wa habari mjini Igunga kwamba Chadema kimepanga mpango huo wenye lengo la kuwaandaa wanachama wake waone wameibiwa kura pindi CCM kitakapotangazwa mshindi.“Tunazo taarifa za uhakika kuwa wamepanga kutumia magari ya matangazo kutangaza kuwa Chadema imeshinda, hata kabla ya kura kuhesabiwa ili wapate leseni ya kuanzisha vurugu,” alisema Wassira.

Wassira ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano), alisema tayari CCM wameviarifu vyombo vya ulinzi na usalama ili kuchukua hatua na pia kuwaelimisha na kuwasihi wananchi kutoingia katika mtego huo.

“Lengo ni kuwaharibu vijana kisaikolojia kwamba yakitangazwa matokeo tofauti waone wamechakachuliwa kura zao na CCM. Tunawasihi Chadema na wanachama wao watulie wakati wananyolewa,” alisema Wassira.

Wassira alisema wanakusudia kutumia mikutano ya hadhara ya kampeni iliyobakia wiki hii ya lala salama, kuwaeleza wananchi juu ya mpango huo wa Chadema ambao alidai hauwatakii mema wananchi wa Igunga.

Hata hivyo, Mratibu wa Kampeni za Chadema Igunga, Mwita Waitara alikanusha vikali madai hayo akisema hawana sababu ya kufanya hivyo kwa kuwa wananchi wameshafanya uamuzi wa kuikataa CCM.“Wassira anafahamu utaratibu wa kutangaza matokeo ulivyo kwamba Chadema hatuna uwezo huo. Hivi kama tulikuwa na uwezo huo kulikuwa na sababu gani ya kufanya kampeni na kuteua hadi mawakala?,” alihoji.

Alikishutumu CCM akidai kuwa kina mpango wa kuingiza watu 1,050 kutoka Mikoa ya Dar es Salaam, Singida na Shinyanga ili watumie shahada bandia kukipigia kura chama hicho tawala.Waitara alidai kuwa watu 500 watatoka Dar es Salaam, 300 Singida na 250 Shinyanga lakini akasisitiza kuwa Chadema kina mtandao mpana na kitahakikisha kinazuia mpango huo usifanikiwe.

 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

0 Reactions
Reply
Top Bottom