Cassius Clay 1964

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,925
30,273
CASSIUS CLAY 1964

Hii picha ilikuwa maarufu sana miaka ya 1960. Ilipigwa siku Cassius Clay alipomshinda Sony Liston na kuchukua mkanda wa uzito wa juu wa masumbwi.

Kwangu mimi picha hii inaniletea kumbukumbu nyingi za miaka hiyo. Kwanza nakumbuka kupokea simu kanipigia baba yangu niko nyumbani ananifahamisha kuwa Cassius Clay amempiga Sony Liston.

Kwa nini baba anipigie simu kunipa taarifa hizi? Alikuwa anajua ni kwa kiasi gani nikimpenda Cassius Clay. Wakati huo bado hajawa Muhammad Ali. Nyakati hizi zilikuwa za kipekee sana kwangu na kwa hakika watoto wengi wa umri wangu.

Hizi zilikuwa nyakati za The Beatles, Elvis Presley, Cliff Richard, Helen Shapiro, Ray Charles, Sam Cooke na wengineo. Nyimbo za hawa wanamuziki zilituchukua sana. Lakini kadri umri ulivyozidi kusogea na fikra zangu za utoto zikawa naziacha nyuma pamoja na hawa watu maarufu.

Lakini mara moja moja ninaposikia miziki yao wa nyakati zao narejea udogoni inakuwa kama jana. Nakumbuka siku nilipoiona senema ya Elvis Presley, "Blue Hawaii," Empire Cinema. Ilikuwa siku ya Eid Fitr. Nyimbo zake hadi leo zinajaza moyo wangu kumbukumbu nyingi.

Nimemuona Helen Shapiro katika "Play it Cool," anaimba "I don't Care."

Katika senema hii alikuwapo Billy Fury. Kijana wa Kiingereza akipiga mitindo ya Rock and Roll.

Siku moja niko Liverpool Coach Station, London stesheni ya mabasi kwenda "bara" ya Uingereza ukipenda.

Natoka Cardiff nakwenda Glasgow. Cardiff ukifananisha na London ni shamba mfano unatoka Kilwa unakuja Dar-es-Salaam upande basi kwenda labda Arusha.

Ukifika Dar es Salaam kituo cha mabasi Mnazi Mmoja na wewe huijui Dar-es-Salaam bila shaka utanyoosha miguu kuangalia mji kabla ya kwenda Arusha angalau upate cha kuhadithia ukirejea Kilwa.

Basi nanyoosha miguu kuangalia mitaa jirani na hapo Liverpool Coach Station. Nikakuta tangazo limebandikwa nje kwenye kioo cha mgawa mmoja mdogo mfano wa AK Tea Room.

Tangazo lile linamtangaza Helen Shapiro kama Born Again Christian na kueleza wapi atahubiri Injili. Zaidi ya miaka 30 sasa imepita. Nilipangiwa kusomesha darasa moja la undergraduates University of Iowa.

Wamarekani wana utamaduni na mila za kipekee sana. Wanafunzi wamekaa darasani utadhani wako kijiweni wana barizi. Wenyeji wameniekeza kabla vipi naweza ku-connect na darasa langu siku ya kwanza wakanielewa. Nikaweka kwenye projector poster ya Blue Hawaii nikawauliza kama wanamjua huyo kwenye poster.

"That's Elvis..."

Nikawaeleza kwa kifupi historia yangu na Elvis Presley nikiwa na miaka 12. Nikaweka picha yangu nyuma yangu wanesimama vijana wa umri wangu. Hii iliwamaliza kabisa. Darasa lilichangamka na lecture ilimalizika vyema kabisa. Wamarekani wanaamini dunia yote iko kwao kwengine Afrika ni mwitu.

Muhammad Ali hakupata kuwa mbali na mimi hadi kifo chake.

Kitabu chake, "Muhammad Ali My Own Story," ni katika vitabu ninavyovipenda sana. Nilipofika New York nilifika Guy Madison Garden ambako Muhammad Ali alipigana na Joe Frazier 1971 katika pambano lililoitwa, "Fight of the Century." Nilifika pia Central Park kuangalia John Lennon Memorial. Lennon alikuwa mmoja wa The Beatles.

Katika wenyeji wangu New York alikuwa Spiegel ambaye alikuwa rafiki wa karibu sana wa John Lennon. Jana yake alikuwa nyumbani kwa Lennon jirani sana na Central Park na siku ya pili ndiyo Lennon akauliwa kwa kupigwa risasi nje ya nyumbani kwake.

Mimi nilishangaa aliponieleza hili na yeye alishangaa nilipomwimbia nyimbo ya The Beatles, "Things We Said Today," na nikamwambia nikiipiga nyimbo hii kwenye guitar langu Hoffner.

Wakati huo nilikuwa na miaka 16.

333891835_578639200866660_5519900118419920962_n.jpg


335456423_1262469191049945_5850042891668838095_n.jpg

Cassius Clay v Sonny Liston, MIami Beach 1964

334438316_223424066856035_3380240507058261617_n.jpg

Muhammad Ali v Joe Frazier, Guy Madison Garden New York 1971

334419667_600345668798834_8513452081450922321_n.jpg

John Lennon Memorial, Central Park New York
 
Mzee wangu, mbona sijaona kiambatanisho cha picha ya Muhammad Ali (Cassius Clay) ulioanza kuizungumzia katika aya ya Juu? Au kuna tatizo katika kifaa changu.
 
Hongera sana,miaka hiyo nyumbani kwenu mnasimu ya mezani?? Dah hongereni sana
 
Hongera sana,miaka hiyo nyumbani kwenu mnasimu ya mezani?? Dah hongereni sana
Dagiii...
Mzee alikuwa pia na film projector tukiangalia senema.

Yeye ndiye aliyenifunza mimi kupiga picha.

Alinipa camera mbili aina ya Kodak nikiwa na miaka 12.

Babu yangu nyumba yake ilikuwa ya kwanza kuwa na umeme maji na shower bafuni.

Ziko stori nyingi sana nikiangalia nyuma hushangaa.

Siku moja baba yangu alichukua comic niliyokuwa nasoma akafungua kisha nikamsikia anasema, "Huyu Donald Duck bado yupo hadi leo?"

Sikuamini kuwa baba yangu katika udogo wake 1930s alikuwa akisoma comics.

Yako mengi.
 
Mzee miaka ya nyuma kulikuwa na Mwanamuziki Morogoro aliitwa Salum Abdallah, ulimfahamu, au ulikuwa mdogo mno
 
Back
Top Bottom