Bunge la 12: Bunge lapitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kwa Kura 373 sawa na asilimia 98.7

Bunge la 12: Bunge lapitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kwa Kura 373 sawa na asilimia 98.7

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
4,783
Reaction score
14,975
Wakati mkutano wa 19 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukiendelea jijini Dodoma, leo Juni 24, 2025 pamoja na mambo mengine wabunge watapiga kura kupitisha bajeti kuu ya Serikali ya shilingi trilioni 56.49 kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Bajeti hiyo inajumuisha stahiki za watumishi na michango ya pensheni (Serikali Kuu) shilingi trilioni 9.17 pamoja na ununuzi wa bidhaa na huduma shilingi trilioni 5.58.

Bajeti hiyo inatarajiwa kugharamiwa na mapato ya ndani ya shilingi trilioni 40.47, misaada shilingi trilioni 1.07 na mikopo ya shilingi trilioni 14.95.

Kati ya mapato ya ndani yanayotarajiwa, mapato ya kodi ni shilingi trilioni 32.31, mapato yasiyo ya kodi shilingi trilioni 6.48, na mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa shilingi trilioni 1.68.

Aidha, mikopo inajumuisha shilingi trilioni 6.27 kutoka vyanzo vya ndani na shilingi trilioni 8.68 kutoka vyanzo vya nje.


Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya, akijibu swali la Mbunge wa Kibaha Vijijini, Michael Mwakamo, bungeni jijini Dodoma.
"Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), imepanga kutekeleza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Mlandizi hadi Ruvu kwenye Stesheni ya SGR kwa awamu, ambapo mkataba wa ujenzi sehemu ya Mlandizi hadi makutano ya Stesheni ya SGR ya Ruvu (Km 15) ulisainiwa Mei 2, 2025 na mkandarasi yupo kwenye hatua za awali za kuanza kazi."

"Kwa sehemu ya makutano ya Ruvu hadi Stesheni ya SGR (Km 8), maandalizi ya usanifu yanaendelea na kazi hiyo inatarajiwa kuchukua miezi mitatu kabla ya kutangazwa kwa zabuni za ujenzi."

Profesa Kitila Mkumbo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, akihitimisha hoja kuhusu Hali ya Uchumi wa Taifa 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2025/2026, bungeni jijini Dodoma.

"Serikali imeamua kuanza kutekeleza mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, na bajeti kuu ya mwaka wa fedha 2025/2026 imeainisha hivyo. Huu ni utekelezaji wa kihistoria, kwani tangu tamko la kwanza litolewe na Rais wa Awamu ya Pili, Hayati Ali Hassan Mwinyi mwaka 1993/1994, hatujawahi kufikia hatua hii.

"Tunaweza kuona jambo hili limetekelezwa miaka 30 baadaye chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambapo Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba ameweka vyanzo maalumu kwa ajili ya kutekeleza mpango huo."

Geofrey Pinda, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Maryam Mwinyi.

"Serikali imeanzisha Programu maalumu ya uendelezaji upya wa maeneo chakavu katika miji inayokabiliwa na changamoto kama ukosefu wa huduma za msingi. Kupitia programu hiyo, jumla ya maeneo 111 yenye ukubwa wa hekta 24,309.35 yameainishwa katika mikoa 24 kwa ajili ya kuendelezwa upya ili kuongeza tija kiuchumi na kijamii."

"Tunatoa wito kwa wabunge kuwahimiza wananchi na wadau kushirikiana katika maeneo yatakayoguswa ili kurahisisha zoezi la kuondoa makazi chakavu na kuboresha maisha ya wananchi. Vile vile, Serikali inaendelea kubadili taswira ya miji kupitia miradi ya ujenzi inayotekelezwa na NHC, TBA, Watumishi Housing Investment na mifuko ya hifadhi ya jamii."

Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha

"Wananchi hawahitaji kushtuka kuhusu habari ya deni la Taifa, sababu sehemu kubwa ya deni hilo inaenda kwenye upande wa makampuni binafsi na si Serikali inayotakiwa kulipa. Kuna tofauti kati ya deni la Taifa na deni la Serikali — ambapo deni la Taifa linajumuisha pia mikopo ya kampuni binafsi ambazo hukopa kwa sababu ya ukosefu wa mitaji."

"Kwa upande wa deni la Serikali, hilo linaangaliwa kwa kuhusianisha na mapato ya Serikali. Tunakopa ili kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, na kinachotutofautisha Tanzania na nchi nyingine ni nidhamu yetu ya matumizi ya fedha hizo, ambayo huwafanya wakopeshaji waendelee kutuamini."


Bunge kukubali na kupitisha Hali ya Uchumi wa Taifa 2024 na kupiga kura kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali ya TSh 56.49 trilioni kwa mwaka wa fedha 2025/2026

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha bajeti kuu ya Serikali ya shilingi trilioni 56.49 kwa mwaka wa fedha wa 2025/2026 baada ya bajeti hiyo kujadiliwa na wabunge kwa muda wa siku saba.

Akisoma idadi ya kura za wabunge waliopitisha bajeti hiyo, Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson amesema idadi ya wabunge waliopiga Kura ni 378, waliosema Ndio ni 373, hakuna waliosema Hapana na ambao Hawakuamua (abstain) ni 5 ambapo idadi ya wabunge waliosema ndio wameifanya bajeti hiyo kupita kwa asilimia 98.7.
 
Back
Top Bottom