Bunduki walizokamata Polisi ni `mwanasesere`
Na Waandishi wetu
7th July 2010
Hii ni moja ya bunduki `mwanasesere` kati ya 1,656 ambazo Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ilizikamata kwa madai kuwa ni hatari kwa maisha ya binadamu na wanyama.Mkononi ni baadhi ya zilizodaiwa kuwa ni risasi (gololi) ambazo ni za plastiki na ndogo kama shanga.
Bunduki ambazo Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema ni hatari na kwamba limezikamata 1,656 katika viwanja vya maonyesho vya Julius Nyerere, zimebainika kuwa ni matoi ya kuchezea watoto.
Uchunguzi wetu umebaini kuwa matoi hayo yametengenezwa kwa plastiki sawa na matoi mengine mengi ya aina hiyo ambayo yamezagaa mitaani nchini.
Aidha, risasi zake ni za plastiki zenye ukubwa kama shanga, hali inayoacha shaka kama kweli ni hatari kwa usalama wa binadamu na wanyama.
Jeshi la Polisi linasema kuwa bunduki hizo ambazo zinaonyesha zimetengenezwa China, zina uwezo wa kupiga mita 30.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Charles Kenyela, aliliambia gazeti hili jana kuwa, bunduki hizo ambazo kwa sasa wanaendelea na uchunguzi zinaonyesha zina uwezo wa kuua kwa mujibu wa maelezo yaliyoandikwa kwenye silaha hizo.
Kamanda Kenyela alisema maelezo ya bunduki hizo yanasema kuwa, Do Not shoot at any human or animal (usimpige binadamu yeyote au mnyama).
Alisema kwa mujibu wa maelezo hayo, inaonyesha wazi kuwa na uwezo wa kumjeruhi au kuua mtu.
"Tunaomba wananchi waendelee kuzirudisha zile ambazo wameshazinunua kwani ni hatari kwao na kwa watoto wao," alisema.
Alisema kwa sasa bunduki hizo zinaendelea kufanyiwa uchunguzi wa kina ikiwa ni pamoja na kujua ziliingiaje hapa nchini na kwenye viwanja hivyo.
"Binafsi sifahamu pale uwanjani ziliingiaje, sifahamu kama kuna utaratibu wa kukagua bidhaa, ndio maana tumeamua kufanya uchunguzi," alisema.
Silaha hizo ambazo zilikutwa zikiwa na namba AF 133, polisi wanasema zina uwezo wa kubeba gololi ndogo (kama shanga) 20, zilikamatwa Jumapili iliyopita huku vijana kadhaa wakiwa wamekwisha kuzinunua.
Vijana hao ni Isaya Afidh (18) na Growin Mhagama (28) ambao baada ya kuhojiwa na polisi walieleza kuwa walizinunua kwenye banda la maonyesho ambalo linamilikiwa na Fatuma Abdallah (53), mkazi wa Magomeni Zanzibar.
Alisema polisi baada ya kufika hapo, mmiliki huyo alithibitisha kuwauzia watu hao bunduki hizo ambazo polisi wanaziita za bandia.
Alieleza kuwa tayari alishauza katoni mbili ambazo kila moja ina bunduki 72.
Kufuatia tukio hilo, mmiliki huyo alikamatwa siku hiyo na anaendelea kuhojiwa wakati silaha hizo zikiwa zimehifadhiwa kituo cha Polisi cha Kilwa Road kwa uchunguzi zaidi.
Wakati huo huo, mmiliki wa katoni hizo, Fatma Salum Abdalah kutoka Zanzibar, jana aliiambia Nipashe kuwa aliagiza bidhaa hizo kutoka China Mei mwaka huu na zilipitia bandari ya Zanzibar.
Alisema matoi hayo ambayo yana mfano wa bunduki ni ya plastiki na hata risasi zake ni plastiki na haziwezi kusababisha madhara kwa binadamu kama ilivyodaiwa na polisi.
Alisema aliposhusha mzigo huo Zanzibar, alitoa baadhi ya matoi hayo kama zawadi kwa wanafunzi wa shule yake ya Sufa Schools Comp Ltd waliofanya vizuri katika masomo kama zawadi.
Fatma alisema kila bunduki moja walikuwa wakiiuza kwa Sh. 2,500 na waliagiza kutoka China katoni 27 kwa gharama ya Sh. milioni 16.
Alisema wamepata hasara ya kiasi hicho cha fedha, baada ya polisi kuwavamia usiku wa kuamkia juzi na kuwachukulia mzigo wote na kwamba walishauza katoni mbili tu kati ya hizo.
"Polisi walichukua katoni 25, lakini katika maelezo yao wameandika kuwa wamechukua 23. Ina maana hizo mbili zimekwenda wapi?" alihoji.
Alisema watu walikuwa wakienda kwenye banda lao na kununua bidhaa hizo kwa jumla na kwenda kuziuza kwa bei ya reja reja.
Alisema baada ya mkasa huo, hivi sasa hawapati wateja kwa kuwa watu wamekuwa wakiwatazama kama wahalifu.
"Hapa tunanyooshewa vidole tu, kila mara utaona watu wanatunyooshea vidole kana kwamba ni majambazi na hata bidhaa nyingine tulizonazo hazinunuliwi kwa kuwa watu wanaogopa kuja hapa," alisema Fatma.
Alikanusha taarifa zilizotolewa kuwa anashikiliwa na polisi na kusema kwamba alikwenda kuhojiwa na kuachiwa mara moja bila kupata bugudha yoyote.
"Sijashikiliwa na mtu, niko huru salama salimini
Kuhusu maandishi yalioandikwa pembeni ya ‘bunduki' hizo kuwa usiitumie kumlenga binadamu au mnyama, Fatma alisema hayo ni maandishi ya kawaida na hayamaanishi kuwa inaweza kuwaua binadamu na wanyama.
"Hata sigara mbona imeandikwa ni hatari kwa afya ya binadamu, lakini inauzwa? ..Mapanga ni silaha watu wanapita nayo barabarani wanauza, lakini hawakamatwi," alisema na kuhoji: "Sasa haya matoi ndio limekuwa jambo kubwa kiasi hicho?"
Alisema alikodi banda hilo kwa walemavu ambao mwisho wa siku amekuwa akiwapa posho kama malipo ya pango.
Nipashe ilipata moja ya ‘bunduki' hizo na kubaini kuwa ni plastiki na hata ‘kisu' ambacho kiko pembeni yake ni plastiki.
CHANZO: NIPASHE