BRELA yaishangaa Benki Kuu
2008-03-04 10:20:15
Na Gaudensia Mngumi
Wakala wa Serikali wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), umeishangaa Benki Kuu (BoT) kulipa mabilioni ya fedha kwa makampuni ambayo haikuyafanyia uhakiki.
Kadhalika, umesisitiza kuwa, haujawahi kusajili kampuni ya Richmond Development Company LLC, iliyopewa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura.
Akizungumza na Nipashe jana jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw. Esteriano Mahingila, alisema BoT ilifanya malipo kwa makampuni kadhaa kupitia akaunti ya madeni ya nje (EPA) lakini hata siku moja haikuwahi kuuliza taarifa za usajili wa wateja hao iliyokuwa inawalipa.
Alitoa maelezo hayo alipoulizwa juu ya madai kuwa yapo makampuni yaliyolipwa kupitia EPA lakini nyaraka zake za usajili hazipo au ziliyeyuka kutoka BRELA.
``Kwa upande wa EPA kulikuwa na mpango uliokuwa unafanyika kwa vile hawakuhakiki usajili wa kampuni hizo. Hata siku moja BRELA haikushirikishwa katika kubainisha rekodi, haikuwahi kuulizwa kama yapo au ni hewa,`` alishangaa Bw. Mahingila.
Alisema iwapo BoT ingehakiki kampuni hizo 22 zilizodaiwa kulipwa kinyume cha sheria, udanganyifu wa zaidi ya Sh. bilioni 133 pengine usingetokea.
Ripoti ya ukaguzi wa EPA ilisema kuwa kampuni za M/S Rastash na G&T zilidaiwa kuwa pamoja na kulipwa fedha taarifa za usajili wake hazikupatikana kwa wakala huyo.
Akitoa ufafanuzi alisema taarifa za G&T zilipatikana na ilisajiliwa na wakala huo, hata hivyo BoT ilikosea kuwasilisha namba ya kampuni hiyo kwa msajili ndiyo maana awali rekodi zake hazikuonekana.
``Kampuni ya M/S Rastash hiyo haipo. Tuliyoisajili ni Rashhazi Tanzania yenye namba 46913 ya Septemba 2003.``
Alisema na kuongeza kuwa wakati mwingine kukosea taarifa za kampuni hizo kunasababisha kushindwa kupatikana rekodi zake.
Akizungumzia madai ya kuihusisha BRELA na kupoteza nyaraka za usajiliwa Richmond alisema``nataka ieleweke kuwa BRELA haijawahi kusajili kampuni ya Richomond Development Company LLC iliyoingia mkataba wa kuzalisha umeme na TANESCO.``
Alisema kilichosajiliwa na wakala huyo ni kampuni ya Richmond Development Company (T) Limited.
Mtendaji huyo Mkuu alisema kampuni hiyo inayozalisha umeme wa dharura haijasajiliwa.
Moja ya viambatanishi vilivyowasilishwa bungeni na Kamati ya Kuchunguza Zabuni ya Richmond zilidai kuwa BRELA iliharibu ushahidi wa wamiliki wa kampuni hiyo. Sehemu ya barua hiyo iliyonukuliwa na ripoti ya kamati inasema.
``Tume ya kuchunguza kampuni ya Richmond haikuundwa mapema kwa vile kulikuwepo na mkakati wa kuharibu ushahidi.
Kwanza Richmond ilisajiliwa BRELA na majina ya wana hisa yalikuwa ya viongozi wasiopungua watano akiwemo Waziri Mkuu ili kupoteza ushahidi, wapo maofisa walitumwa BRELA na kuhakikisha nyaraka za usajili zinachukuliwa na kisha kutengenezwa nyingine zikiwa na majina tofauti.
``Pili yupo ofisa mmoja wa BRELA aliyesaidia kutoa mafaili hayo na kupokea nyaraka mpya za kuficha huo ufisadi. Yeye amepewa nyumba ya serikali eneo la Chang`ombe na imekarabatiwa kwa gharama za serikali na kuwekewa fenicha za kisasa.``
Akijibu madai hayo Mtendaji Mkuu alisema ``milango iko wazi kila anayetaka kuhakiki taarifa za usajali wa kampuni ya Richmond Development Company (T) Limited kufika BRELA kujionea.``
Aliongeza kuwa ilisajiliwa Julai 12, 2006 na kupewa hati namba 57014.
``Kampuni husajiliwa na kufunguliwa jalada kisha huandikishwa kwenye daftari la usajili wa makampuni ambalo taarifa zake huwekwa kwa mpangilio maalumu wenye mfuatano wa kinamba.``
Alisema taarifa za Richomond Development Company (T) zilizoko BRELA hazijawahi kubadilika na maelezo yaliyoko kwenye daftari ndiyo yaliyomo kwenye jalada.
Bw. Mahingila alilionyesha gazeti hili taarifa za usajili wa kampuni hiyo zilizoandikwa kwenye daftari la makampuni namba 56687-57642 la kuanzia Juni 6, 2006 hadi Septemba 11, 2006.
Katika taarifa hizo wakurugenzi wa Richmond wanatajwa kuwa ni Naeem Gire na Mohamed Gire. Naeem ana hisa 250,000 wakati kampuni nayo ina hisa 750,000 na kampuni hiyo siyo ile iliyoingia mkataba na TANESCO.
SOURCE: Nipashe