RIWAYA; BOMU
imeandikwa na Halfani Sudy
Simu 0652 212391
Sehemu ya Kumi na Tano
"Unataka kufanya nini David?" Daniel aliuliza swali huku akitabasamu.
"Fuata maelekezo yangu Daniel!! Mimi sitanii nitakupasua kweli na risasi!!" David alionya.
"Tatizo nini David?" Adrian naye aliuliza kule nyuma.
"Nawe tulia! Usijione upo salama, angalia nyuma yako huko!" David alisema kwa hasira.
Adrian aligeuka nyuma. Ile sehemu ya ndani wanapowekea mizigo. Pua yake iligusana na mdomo mweusi wa bastola.
"Tumetekwa" Adrian alisema akiwa amekata tamaa.
"David, wamekulipa shilingi ngapi hawa watu kiasi ukaamua kuisaliti nchi yako namna hii?" Daniel aliuliza huku tabasamu lake likiwa vilevile.
"Adrian! Ruka katika usukani hapa. Utafuata maelekezo yangu. We Daniel ruka nyuma kule. Ukakutane na muhuni.." David alisema kwa amri.
Daniel Mwaseba na Adrian Kaanan walifanya kama walivyoagizwa.
"Adrian tunaenda Tegeta. Ukileta ujanja wowote ule sitaki kurudia tena kukwambia nitakufanya nini!" David alionya tena.
"Sifiki Tegeta mimi" Daniel alimjibu kimoyomoyo.
Taa ziliruhusu. Gari la kina Daniel ambalo kwasasa lilikuwa linaendeshwa na Adrian lilikata kulia likiifuta barabara ya Sam Nujoma.
Ndani ya gari kulikuwa na utulivu mkubwa. Kila mmoja akiwaza lake moyoni.
Walipita Mlimani city, Daniel alichungulia kwa nje dirishani lakini hakumuona Martin Hisia.
"Tutaonana soon brother" Daniel alisema kwa sauti ndogo.
Gari lilishika kasi. Adrian alikuwa analiendesha bila wasiwasi wowote ule. Hakutishwa na mdomo wa bastola uliokuwa unamgusagusa shingoni. Zilikuwa ni kazi zao kugusana na bastola.
Walifika Mwenge, gari lilikata kushoto kuelekea Tegeta. Adrian na Daniel mara kwa mara walikuwa wanaangaliana kwa kutumia kioo cha kati. Walikuwa wanawasiliana kwa alama zao.
Na walielewana.
Gari liliendelea kusonga mbele.
Kuelekea Tegeta.
Adrian pia aliangalia nyuma yao kwa kutumia vioo vya pembeni. Lile gari aliloliona tangu wakiwa kule Ubungo ambalo alihisi kuwa linawafatilia bado lilikuwa nyuma yao.
"Hawa watu ni kina nani? Kwanini wamemteka Dr Luis? Siamini, na David naye ni miongoni mwao? Kajuana nao lini hawa watu wakati muda mwingi alikuwa msituni? Nina maswali mengi sana ambayo yanipasa niyapate majibu. Na nitayapata kutoka kwa David mwenyewe" Daniel aliwaza.
Daniel alikiangalia tena kioo cha kati, na Adrian naye alikiangalia.
Waliangaliana.
Macho yao yaliongea tena.
Walielewana.
Safari iliendelea huku ukimya wa kifo ukiwa umetawala ndani ya garu. Mateka walikuwa kimya, watekaji nao walikuwa kimya.
"Hannan alinipa taarifa kwamba simu ya meneja Fadhili ilionekana imewashwa na kisha kuzimwa Tegeta. Niliamini taarifa ile, na nilitaka kwenda kweli Tegeta. Lakini mwishoni kabisa aliniambia 'Do did'. Najua aliyekuwa nao huko hawakumuekewa. Hilo neno tunalitumia mimi na yeye tu endapo mmoja wetu atakapokamatwa na kulazimishwa kumleta mwenzie mtegoni. 'Do did' leo imetusaidia.
Ila hawa jamaa wana roho mbaya. Unamtoaje mgonjwa katika hali hospitali na kumteka. Lakini lazima watalipa kwa haya mambo wayafanyayo" Daniel aliwaza.
Akanyanyua tena sura yake katika kioo cha kati. Adrian naye alifanya vivo hivo. Akamkonyeza kwa jicho lake la kushoto.
"Its the time" Daniel alisema kwa sauti ndogo aliyoisikia mwenyewe.
Sekunde hiyohiyo, Adrian aliliyumbisha gari kwa nguvu na kwenda kulikwaruza gari la pembeni. Gari lao liliyumba vibaya huku likielekea kugongana uso kwa uso na roli, likilotokea Tegeta. Adrian alikata kona kwa haraka na ustadi mkubwa na kurudi upande wake. Walihitaji mstuko mdogo tu kutoka kwa wale watu.
Na waliopata.
Daniel Mwaseba alikuwa ameshafanya kitu....
Wakati yule jamaa aliyumbishwa na ule myumbo wa kwanza wa gari, Daniel aliitumia nafasi ile kupiga kwa nguvu kiganja cha yule jamaa, na bastola ilidondoka chini. Jamaa alitoa yowe dogo la hofu lisilo na mwendelezo, kwani alikutana na mkono wa kiume wa Daniel ulioizungusha shingo yangu kwa nguvu kuelekea kushoto. Ulisikika mlio kama kijiti kikavu kimevunja. Jamaa alienda katika sayari nyingine palepale. Wakati gari lilkikaa sawa barabarani, Daniel Mwaseba alikuwa ameimaliza kazi.
David alikuwa anatetemeka huku akiwa bado kamuelekea bastola yake Adrian. Hakuna aliyemsemesha.
"Hawa wajinga wanaotufuata watatutambua leo!!" Daniel alisema kwa jazba.
Adrian alifanya alitulia katika usukani. Safari ya kuelekea Tegeta iliendelea..
David akiwa vilevile, na mtetemo wake wa haja huku bastola yake ikiwa imeelekezwa kichwani kwa Adrian Kaanan.
***
Imma Ogbo aliingia katika chumba ambacho alikuwa amewekwa Dr Luis. Safari hii ndio alipanga kwenda kumwambia Dr Luis lengo lao kuu la kumteka. Alimkuta Dr Luis amekaa katika kiti akiwa mwingi wa mawazo.
"Tumekutana tena rafiki yangu.." Imma Ogbo alisema huku akitabasamu.
Dr Luis alimwangalia tu.
"Dr Luis, ni wewe pekee ndiye unayeweza kupigania maisha yako. Huko nje hakuna harakati zozote za kukutafuta. Rafiki yako mheshimiwa rais hana habari na wewe. Hapa ni wewe na wewe tu ndio wenye nafasi ya kujiokoa" Imma Ogbo alisema.
"Kwani mnataka nini kwangu ninyi watu? Kama mnataka kiasi chochote cha pesa mimi nitawapa. Naomba niachieni nirudi kwetu. Mmeniteka bila sababu, maswali yenu yote nimeyajibu sasa mnataka nini tena kutoka kwangu?" Dr Luis alisema.
"Sikiliza Dr Luis. Huu si wakati wa kulalamika. Hapa si mahali sahihi pa kulalamika. Hakuna atakayekuonea huruma kwa malalamiko yako. Sikiliza tutachokwambia, nawe utekekeze. Huo ndio usalama wako"
Dr Luis alibaki kimya.
"Tunataka ututengenezee kirusi cha DH+...." Imma Ogbo alisema kwa sauti ndogo.
"Unasemaje!!!?" Mshangao mkubwa ulionekana katika macho ya Dr Luis.
Hakuamini maneno yale kutoka kwa yule mtu. Kabla ya dakika hii aliamini ni yeye pekee ndiye anayejua kuhusu kirusi cha siri cha DH+ hapa duniani.
Kumbe katu haikuwa hivyo.
Moyoni akahisi, hata siri yake na rais Mgaya sasa itakuwa hadharani kwa hawa watu.
Hili lilikuwa ni Bomu kwake!!!
Je nini kitatokea? Tukutane hapahapa keshokutwa.