Bomoa bomoa ya kikatili Magomeni | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Bomoa bomoa ya kikatili Magomeni

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by BAK, Sep 22, 2008.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Sep 22, 2008
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,688
  Likes Received: 82,540
  Trophy Points: 280
  Date::9/22/2008
  Bomoa bomoa ya kikatili Magomeni

  Na Salim Said
  Mwananchi

  FAMILIA sita zimekosa sehemu ya kuishi baada ya watu wanaodai kununua nyumba ya urithi ya watoto zaidi ya 10 wa marehemu, Yussuf Mbonde iliyopo Magomeni Mwembechai, kubomoa nyumba hiyo kwa kutumia greda huku wakilindwa na vijana wa kukodi maarufu kama mabaunsa pamoja na usimamizi wa polisi waliokuwa na silaha.

  Bomoabomoa hiyo ilitokea jana majira ya saa 9:00 alasiri baada ya uvamizi huo kutokea na kusambaratisha nyumba na vitu vyote vilivyokuwemo ndani.

  Kwa mujibu wa wanafamilia, waliohusika na uvunjaji huo ambao wamedai kuinunua nyumba hiyo kutoka kwa Ayasi Mbonde ambaye ni mjomba wa wanafamilia hao, ni Sabahi Chondoma na Abdallah Chondoma.

  “Nyumba ni ya kwetu na hatujauza, Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni ilisema haina uwezo wa kusikiliza kesi hii na kutuambia twende mahakama ya ardhi na kesho (leo) ndio ilikuwa tunaenda mahakamani,” alisema Ayoub Yussuf.

  Alisema rasharasha za bomoabomoa hiyo zilianza juzi wakati watu hao walipoenda na kuvunja milango ya maduka na ya uani huku wakitoa maneno ya vitisho kwamba lazima wahame la sivyo watauawa.

  “Sabahi anatuambia tutahama lazima kwa sababu yeye ana fedha na polisi ni watu wake hivyo hawawezi kumfanya lolote,” alisema mwanafamilia huyo kwa machungu.

  Yussuf alifafanua kwamba baada ya vitisho hivyo walienda kwa mwenyekiti wa mtaa na Kituo cha Polisi Magomeni kutoa taarifa, lakini hawakupewa ushirikiano.

  “Polisi ndio waliosimamia tena walikuwa na silaha, halafu hakuwa na hata namba katika sare zao,” alisema Rajabu Yussuf.

  "Wametuvamia kwa marungu na mawe mimi mwenyewe mkono huu wamenijeruhi; wamenipiga mawe ya kifua na mdogo wangu wamempiga mawe usoni; watoto wetu wengine walikuwamo ndani hatuwaoni," alisema.

  Miongoni mwa mali zilizoharibiwa ndani ya nyumba hiyo ni vitu vyote vilivyokuwemo ikiwa ni pamoja na fedha taslimu ambazo watu hao waliobomolewa walidai kuwa ni Sh20 milioni.

  Juhudi za kumpata mwenyekiti wa serikali ya mtaa wala watu wanaodai kununua nyumba hiyo pamoja na mjomba wao, hazikufanikiwa, huku polisi waliokuwepo eneo la tukio wakikataa kuzungumza na mwandishi kwa madai kwamba si wazungumzaji wa jeshi hilo .

  Wanafamilia hao walisema hawana mahali pa kwenda baada ya nyumba yao kubomolewa na watabakia hapohapo kwa kuwa wao ni masikini hawana fedha ya kuhonga kwenye vyombo vya sheria.

  Wanaodai kuwa ni warithi halali wa nyumba hiyo ni Zuwena, Riziki, Ayoub, Sharifa, Abdalla, Juma, Bakari, Fatuma na Rajabu ambao wote ni watoto wa marehemu mzee Yussuf Mbonde.

  Kwa ujumla watu waliokuwa wanaishi humo pamoja na watoto ni watu 15.
   
Loading...