Bila CCM madhubuti upinzani imara nchi yetu itayumba...

BongoTz

JF-Expert Member
Nov 3, 2006
272
0
Ingawa sikubaliani na baadhi ya sera zake za kijamaa, ukweli ni kwamba huyu Nyerere alikuwa anaona mbali sana! Na I think kila mwanasiasa wa Tanzania regadless kama ni kutoka CUF, CCM, Chadema, TLP ama DP, anatakiwa kusoma hii speech, aitafakari, na kuielewa. Hususani wanasiasa chipukizi wa kizazi hiki cha BongoFlava kama January Makamba na Zitto Kabwe (maybe Kikwete pia). P.S. Maneno yaliyofungwa [i.e. Upinzani imara], nimeyaongeza mimi: Enjoy...

AGOSTI 16,1990--Diamond Jubilee, Dar es Salaam

Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu,
Waheshimiwa wageni wetu na rafiki zetu,
Kidumu Chama cha Mapinduzi.

Tumekusanyika katika Mkutano huu hasa kwa kazi moja kubwa: kumteua mwenzetu mmoja atakayesimamishwa na Chama ili achaguliwe kushika kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano. Lakini vile vile nafasi hii itatumiwa kuwaomba wajumbe kufanya mabadiliko machache katika Katiba ya Chama, na kumchagua Mwenyekiti mpya, pamoja na kufanya uchaguzi mwingine wowote utakaotokana na kitendo hicho.

Kuhusu mgombea kiti cha Rais, Halmashauri Kuu ya Taifa itampendekeza ALI HASSAN MWINYI kwa mara ya pili. Hatukuwa na shaka yoyote juu ya uamuzi wetu huo. Rais Mwinyi amewafanyia watu wetu na Taifa letu kazi kubwa sana katika kipindi cha matatizo mengi kabisa. Matatizo hayo, hasa ya uchumi, bado hayajaisha; mijadala ya namna ya kupambana nayo bado inaendelea, na lazima iendelee; na hatua za kuyatatua nazo ziendelee kuchukuliwa. Maana wakati wa matatizo kutofanya lo lote nako ni kitendo, na katika hali kama yetu ni kitendo cha kujiangamiza! Mabadiliko makubwa ya Katiba yanayopendekezwa kwa wajumbe ni kurudishwa kwa "kofia mbili" kulingana na utaratibu wetu wa awali, yaani kuunganisha majukumu ya Chama na ya Serikali katika ngazi fulani za uongozi. Sababu kubwa za pendekezo hilo ni, kuimarisha uongozi katika ngazi zinazohusika, na kupunguza gharama za uendeshaji. Zote zitaelezwa baadaye.

Tatu, nimeelewana na wenzangu katika Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa kwamba sasa wakati wangu umefika wa kuacha kiti cha Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi. Hii ni ngazi moja ya uongozi ambayo tangu awali tulipendelea kuwa Mwenyekiti wa Chama chetu, na Rais wa Jamhuri ya Muungano awe ni mtu yule yule. Sababu kubwa zilizotufanya tukubali kuyatenga majukumu haya kwa muda, zilitokana na hofu na mashaka ya kipindi cha mpito.

Mabadiliko ya uongozi kutoka Awamu ya Kwanza kwenda Awamu ya Pili yamemalizika kwa utulivu mkubwa sana. Hatuna sababu tena ya kuendelea kuyatenga madaraka haya. Sasa ni vizuri turejee kwenye uamuzi wetu wa awali na wa msingi kwamba Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi awe pia ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunamshukuru sana mwenzetu, Ndugu Ali Hassan Mwinyi, kwamba uongozi wake wa busara katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, umetufikisha hapa. Ndugu Rais, Asante sana.

Chama Kimoja na Vyama vingi.

Ndugu Wajumbe: Uchaguzi wa sasa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, na Wabunge, utaendeshwa kwa kufuata Katiba yetu ya sasa ya Chama kimoja. Hatukusudii kubadili utaratibu huu kwa sasa.

Lakini mjadala juu ya utaratibu utakaoiongoza Tanzania katika siku za mbele umeanza, na ni matumaini yangu kwamba utaendelea. Sheria hutungwa kusimamia vitendo; na katika nchi yetu hivi sasa ni kinyume cha Sheria kuanzisha chama kingine cha siasa. Wote hatuna budi tuitii sheria hii mpaka hapo itakapobadilika. Lakini nchi hii inajitahidi kuwa nchi ya kidemokrasia ya Chama Kimoja; na taratibu za mtu kutoa maoni juu ya mabadiliko ama ya Sheria iliyopo au ya Katiba wakati anafuata Sheria zilizopo lazima ziruhusiwe katika mfumo wo wote unaoitwa wa kidemokrasia. Kwa kweli sifa moja ya demokrasia ya kweli ni kwamba inawapa wachache nafasi ya kisheria ya kujaribu kuwashawishi wengi waone ubora wa maoni yao. Hii ndiyo njia pekee ya kuleta mawazo mapya na tabia mpya katika jamii kwa amani na utulivu. Ni demokrasia gani hiyo inayozuia wananchi kuihoji katiba yake, au sheria nyingine yo yote ya nchi? Demokrasia ikichukua sura ya udikiteta, udikiteta wenyewe utakuwa na sura gani?

Suala hili halimo katika ajenda yamMkutano wetu; bado hatujaelewa vizuri uzito wa matokeo ya mabadiliko, na bado mjadala wenyewe haujafikia hatua ya kutuwezesha kufanya uamuzi sasa, au hata kuweka tarehe ya uamuzi. Maoni yangu binafsi ni kwamba si vizuri jambo kubwa kama hili likaamuliwa kwa pupa. Ni vizuri tujipe muda wa kutosha kuelewa maana ya uamuzi wowote tutakaoufanya. Tukiamua kuendelea na chama kimoja, basi tuwe tumeelewa sababu zake, na tukiamua kuanzisha mfumo wa vyama vingi, basi tuwe pia tumeelewa sababu zake. Na kwa hiyo ni wajibu wetu kupima kwa makini sana hoja zinazotolewa na pande zote mbili za mjadala. Ndiyo maana ni vizuri mjadala upate muda wa kutosha, na uendeshwe kwa makini.

Lakini baada ya kusema hayo ni lazima nisisitize yafuatayo:

kwanza, jambo kubwa kwa maendeleo ya nchi yetu ni kuendeleza demokrasi yenyewe, na siyo muundo unaoiendesha. Na pili, suala hili litakapoletwa ili liamuliwe na Mkutano wa Chama, hoja zitakazoongoza uamuzi huo lazima ziwe na uhusiano na hali halisi na mahitaji ya Tanzania ya wakati huo.

Tanzania ilianza uhuru wake ikiwa na vyama vingi; lakini haikuwa na demokrasia. Katika uchaguzi mkuu wa Tanganyika wa 1960, kabla ya uhuru wetu, TANU ilishindana na vyama vingine. Katika viti 71 vya kuchaguliwa, TANU ilichukua viti 70 na kupoteza kiti kimoja. Kile tulichopoteza tulikuwa tumepingwa na mwanachama wa TANU ambaye hakukubali mjumbe aliyeteuliwa rasmi na TANU kugombea kiti hicho. Alijisimamisha mwenyewe, akapingana na TANU, akatushinda! Katika jimbo hilo la uchaguzi ndipo peke yake palipotokea uchaguzi wa kweli; lakini katika majimbo mengine yote 70 yaliyobaki ama hapakuwa na uchaguzi kabisa - katika majimbo 58 - ama palikuwa na uchaguzi wa bandia,- katika majimbo 12 - kati ya Chama cha kweli, TANU, na vyama jina tu.

Katika uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Tanganyika uliofanyika Oktoba, 1962, mgombea wa TANU alipingwa na mgombea wa chama kingine. Lakini huu nao ulikuwa ni uchaguzi wa kushindanisha Chama cha kweli na Chama cha upuuzi kidogo. Chama cha upinzani kilipata kura 21,276 na TANU ilipata karibu kura 1,128,000. Vyama vilivyokuwa vikipinga TANU ama vilikufa au vilianza kufa vifo vya kawaida.

Hali hiyo ndiyo iliyotufanya tuunde tume ya kutusaidia kupata maoni ya wananchi ya kutuwezesha kuanzisha mfumo wa demokrasia ya Chama Kimoja. Katika uchaguzi wa Bunge wa 1965 tulitumia mfumo uliopendekezwa na tume hiyo. Tuliamua kushindanisha wanachama wawili wa Chama cha TANU, na kuwapa nafasi wapigakura kumchagua mmojawapo. Matokeo yake yalikuwa ya demokrasia ya kweli kweli. Kwa mara ya kwanza kabisa kulikuwa na uchaguzi katika nchi nzima; na wabunge wa zamani, pamoja na mawaziri, waliweza kushindwa na wagombea wapya. Huo ndio utaratibu tunaoendelea nao hadi leo. Hatukuanzisha mfumo wa Chama Kimoja ili kuondoa demokrasia, bali tulianzisha mfumo wa Chama Kimoja ili kuanzisha na kuendeleza demokrasia.

Uchaguzi wa Zanzibar wa mwaka 1963 ulikuwa wa vyama vingi. Lakini wakoloni Waingereza na wateja wao walifanya mbinu ili Waafrika, ambao ndio wengi, wasishinde katika uchaguzi huo na kuunda Serikali ya Zanzibar huru. Kwa hiyo Serikali ya Zanzibar "huru" iliundwa na wapenzi wa Sultani. Utaratibu wo wote unaowanyima wengi haki yao hauwezi ukaitwa demokrasia. Zanzibar ya Desemba, 1963, ilikuwa ina vyama vingi, lakini haikuwa demokrasia.

Na Waswahili wamesema: Wengi wape, usipowapa, watanyakua wenyewe. Tarehe 12, Januari, 1964, wengi, waliokuwa wamenyimwa haki yao kwa mbinu za kipumbavu, wao wenyewe wakajichukulia haki yao. Serikali ya Mapinduzi haikuwa Serikali ya kuchaguliwa kwa kupiga kura; lakini ilikuwa ni Serikali ya wengi ambayo waliipata kwa kukubali kujitolea mhanga. Vyama vilivyopinga Mapinduzi vilivunjwa, Chama kimoja kilichoyakubali mapinduzi kilijiunga na ASP.

Hiyo ndiyo historia fupi ya jinsi tulivyoanzisha mfumo wa Demokrasia ya Chama Kimoja. Mpaka 1977 Tanzania ilikuwa na Vyama Viwili, lakini mfumo wa Chama Kimoja. Mwaka huo CCM ikazaliwa na kuwa mrithi wa Vyama hivyo na mfumo huo.

Ndugu wajumbe, inawezekana kwamba bado ziko sababu nzito za leo za kuendelea kuwa na mfumo wa Chama Kimoja. Ni vizuri sababu hizo zikajadiliwa na zikaeleweka. Haitatosha kurudia hoja zile zile za mwanzo wa uhai wa uhuru wetu. Kwa mfano, wakati ule sheria ilikuwa inaruhusu vyama vingi, lakini hatukuwa na vyama vya maana; sasa sheria hairuhusu kuanzishwa kwa Chama kingine cha siasa. Lakini mimi siamini kuwa sheria ikiruhusu vyama vingine vianzishwe hatutaweza kupata Chama cho chote cha maana.

Naamini kuwa sasa uko uwezekano wa kupata Chama au vyama ambavyo ni vizuri au angalau ni afadhali-fadhali kidogo. Lakini pamoja na hayo, tukiridhika kwamba ziko sababu za kutosha za kuendelea na mfumo wa Chama Kimoja basi na tuendelee na Chama Kimoja bila ya kuona haya na bila ya kumwomba radhi mtu ye yote. Kipimo cha kiatu mpime mvaaji.

Na endapo tutaamua kuwa na mfumo wa Vyama Vingi, basi ni vizuri pia sababu za kufanya hivyo zitokane na hali na mahitaji halisi ya Tanzania ya leo. Halitakuwa jambo la busara, wala la heshima, kuacha mfumo wetu wenyewe ambao tumeuzoea, tukajaribu mfumo ambao hatuna mazoea nao, kwa sababu tu ya kufuata upepo unaovuma kutoka nje ya nchi yetu; au kwa sababu tu ya kutaka kuwapendeza mabeberu-mabepari ili watupe misaada.

Nimewahi kusema kwamba mimi binafsi naamini kuwa endapo tutaamua kuendelea na mfumo wa Demokrasia ya Chama Kimoja uamuzi huo hauwezi ukawa uamuzi wa kudumu; kwamba siku moja Watanzania wataamua kuwa na mfumo wa Vyama Vingi. Lakini ni vizuri nikasema pia kwamba kwa maoni yangu hatuwezi tukaamua kuacha mfumo wa demokrasia ya Chama Kimoja, tukajaribu mfumo wa demokrasia ya Vyama Vingi, kwa matumaini ya kwamba tukikuta kuwa mfumo huo hautufai, basi tutarudia tena Demokrasia ya Chama Kimoja. Tutajidanganya; haiwezekani na ni vigumu kabisa.

Ukimwacha mkeo ukaoa mwingine, na ukagundua kuwa huyu wa pili ni balaa, ni vigumu kumrudia mkeo wa kwanza. Demokrasia ya Vyama Vingi ikitushinda, mfumo ambao ni rahisi kufuatia utakuwa ni udikteta wa mtu mmoja au utawala wa kijeshi. Hiyo ni sababu nyingine muhimu ya kutofanya uamuzi kwa pupa. Inafaa tukajipa muda wa kutosha kuelewa athari zinazoweza kutokana na uamuzi wo wote tutakaoufanya. Si vema kuruka bila kuwa na hakika utaangukia wapi!

Mpaka sasa katika mjadala huu, wasi wasi unaoelezwa ni hatari inayoweza kutokea kwa umoja wetu kama tukiwa na utaratibu wa Vyama Vingi. Tusiipuuze hoja hiyo; umoja wa watu wetu ndiyo nguvu yetu kubwa kuliko zote. Hatari za mifarakano inayoweza kuzuka kwa misingi ya dini au ukabila lazima ziepukwe; na wakati wo wote itakapotokea mipango ya kuanzisha vyama vingi ni lazima kujitahadhari sana na hatari hizo na ikiwezekana kuzikinga kabisa.

Mgawanyiko kati ya Sisi na Wao.

Lakini kwa sasa hivi hatari iliyoanza kujitokeza kwa wazi wazi ni mgawanyiko wa "Sisi" na "Wao" wa tabaka za kiuchumi na kijamii.

Katika jitihada ya kuongeza ufanisi na ari ya kufanya kazi, kama utawaruhusu watu wajipatie mali kiasi wanachoweza maadamu hawavunji Sheria, tofauti za mapato na hatimaye za hadhi katika jamii zitaongezeka. Hali hiyo itatokea hata kama viwanda vikubwa vikubwa na huduma muhimu vinamilikiwa na umma.

Tofauti kati ya watu maskini na watu matajiri zinaongezeka Tanzania
. Inafaa tuwe macho. Ni lazima tuendelee kutumia Sheria za nchi, na mipango mbali mbali ya Serikali, kuona kuwa tofauti hizi hazifikii kiasi cha kuhatarisha umoja na amani katika nchi yetu. Na hasa hasa ni lazima tuendelee kuhakikisha kwamba mahitaji ya msingi ya watu wote yanapatikana na yanalindwa. Lengo letu lazima liendelee kuwa kuinua hali ya maisha ya kila mtu, na kila mtu aweze kupata huduma za msingi za elimu na matibabu. Kama watu wachache wanaishi maisha ya fahari fahari, na watu walio wengi hawapati hata mahitaji yao ya lazima, hatutaweza kudumisha amani na utulivu nchini mwetu. Ni muhimu sana kwa Chama chetu na Serikali zake kulizingatia jambo hili kwa makini.

Ndugu Wanachama: Mimi nang'atuka; naivua kofia ya Mwenyekiti wa Chama chetu. Lakini bado naendelea kuamini kuwa bila CCM madhubuti nchi yetu itayumba. Hatuna kiongozi mwingine. Napenda Chama chetu, CCM, kiendelee kuwa Chama cha watu, na hasa watu maskini. Napenda Chama chetu kiendelee kushika uongozi kwa kukubalika na umma wa wananchi, hata kama huko baadaye utaratibu wa demokrasia utabadilika ukawa wa Vyama Vingi. Lakini kama sote tunataka kweli Chama chetu kikubalike kwa wananchi na kiendelee kuongoza nchi yetu, basi yako masharti fulani ambayo ni lazima yatimizwe; na wanachama wote, kwa nafasi mbali mbali, tunapaswa kuona kuwa masharti hayo yanatimizwa.

Naamini kuwa masharti haya yanahitaji CCM ijichunguze yenyewe kwa makini sana hivi sasa. Hata kama dalili za sasa zingeonyesha kuwa utaratibu wa Vyama Vingi hauungwi mkono na watu wengi, haifai hata kidogo sisi Viongozi na Wanachama wa CCM tukatosheka tu na hali ya Chama chetu bila kujichunguza kwa makini.

Kazi ya Chama

Msingi wa kujichunguza huko lazima uanze kwa kuelewa vizuri shabaha yenyewe ya kuwa na chama cha siasa. Uchunguzi huo ufuatiwe na uchambuzi wa kuona ni wapi tumefaulu, na ni wapi tumeshindwa, tukitumia kipimo hicho cha shabaha tulizojiwekea. Na mwisho lazima Chama kijiunde upya pale ambapo ni lazima ili kutekeleza shabaha zake kwa ufanisi zaidi.

Chama cha siasa ni chombo kinachowaunganisha kwa hiari watu wenye itikadi moja na shabaha moja. Na katika utaratibu wo wote ule, Chama kinahitaji kuzitambua wazi wazi hizo shabaha zake: kinataka kufanya nini na kwa nini? Na kwa kuwa kila chama hudai kuwa kinaitakia nchi yao kila lililo jema, na mema yote hayawezi yakafanywa kwa wakati ule ule, basi ni vizuri kiwe na hakika pia juu ya mpangilio wa umuhimu wa shabaha zake. Ni lazima baadhi ya shabaha zitekelezwe kabla ya nyingine; na hii -angalau kwa muda- inaweza ikaleta uwiano mbaya baina ya shabaha moja na shabaha nyingine. Kwa hiyo, ingawa wote tunataka maendeleo, na wote tunataka ufanisi, katika hali halisi inawezekana mikoa yote isipate maendeleo kwa usawa, na mapato ya wananchi yatapitana. Umoja na utulivu wa Taifa unataka wote tukubali shabaha zetu, na tukiri pia kwamba kwa kuwa hatuwezi kuzitekeleza zote kwa pamoja, ni lazima wakati wa safari baadhi ya wananchi wajitoe mhanga zaidi kuliko wenzao. Lakini la maana ni kudhamiria kwa makini kutekeleza shabaha zake zote hatua kwa hatua, na hivyo hatimaye kuleta uwiano ambao umekusudiwa.

Baada ya kuamua juu ya shabaha zake na mpango wa utekelezaji wa shabaha hizo, itabidi vile vile Chama kichague mikakati na taratibu ambazo kinaamini kuwa ndizo zinazofaa kwa kufikia shabaha zilizowekwa. Katika kufikiria uamuzi huo, Chama kitahitaji kuzingatia mambo mawili. Kwanza kiwango cha teknolojia na rasilmali zilizoko au zinazotarajiwa kupatikana nchini na nje ya nchi; na pili mazingira na mahitaji yaliyopo ndani ya nchi na duniani.

Kama nilivyokwisha kusema, chama cha siasa ni chombo kinachowaunganisha kwa hiari watu wenye itikadi moja na shabaha moja. Shabaha zake na sera zake lazima zitokane na kukubaliwa na wanachama wake. Na kama moja ya shabaha kubwa za chama hicho ni demokrasia ya Taifa zima - maana kuna vyama ambavyo demokrasia si shabaha yake - basi lazima chama hicho chenyewe kiwe cha kidemokrasia katika muundo wake na katika vitendo vyake. Lazima wakati wote wanachama wake wawe ndio wanaoamua juu ya sera za Chama chao, na ndio watakaoamua wakati wa kubadili utekelezaji wa mipango yao, kama hapana budi.

Vile vile Chama cha Siasa lazima kiwe na taratibu za kutenda kazi zake. Lazima kifanye jitihada na mbinu za kuufanya umma uunge mkono sera zake, na lazima wanachama wajizatiti katika uchaguzi, ama wa Chama kimoja au wa vyama vingi, ili chama chao kiweze kuunda Serikali itakayoendeshwa na wanachama wake. Pia, lazima kiwe kimejiandaa kiasi cha kutosha kuweza kuelekeza sera za Serikali iliyoundwa na kuwa na kiasi cha kauli juu ya sera hizo.

Lakini Chama ni chama; Chama si Serikali. Chama kisijaribu kufanya mambo kana kwamba ndicho Serikali. Kazi za Chama ni tofauti na za Serikali, na tofauti hiyo ni muhimu kwa uhai na mafanikio ya vyote viwili, Chama na Serikali yake. Jambo hili ni muhimu; lakini ni vigumu sana kuidumisha tofauti hii, hasa katika utaratibu wa Chama Kimoja. Maana ya Chama kushika hatamu huweza ikageuzwa ikawa Chama ndiyo Serikali.

Chama cha Siasa lazima kijitegemee: kwa fedha na katika mambo mengine. Lazima chama kiwe ni huru kabisa; na hakina bwana mwingine ila wanachama wake. Katika utaratibu wa Chama Kimoja ni jambo la kawaida kwa Chama kupokea ruzuku kutoka serikalini.

Na kwa kweli hata katika nchi za Vyama Vingi, vyama vyote vilivyoko hupokea ruzuku kwa ajili ya kazi maalum, bora tu vyama hivyo vithibitishe matumizi ya fedha zilizopokewa. Nami naamini kuwa ili kuwa na Chama cha maana, hata katika utaratibu wa Chama Kimoja, ruzuku inayotolewa lazima iwe ni kwa kazi maalum, na matumizi yake yanapaswa kukaguliwa na kuthibitishwa kwa utaratibu unaokubalika.

Na mwisho chama kizuri katika utaratibu wo wote ule lazima kiweze kuwakilisha mawazo ya wananchi serikalini. Kina wajibu kwa wanachama wake, lakini vile vile kina wajibu kwa Taifa zima. Chama cha Siasa katika nchi ambayo haina utulivu ni chama jina tu, na sera zake wakati wo wote zinaweza zikafutiliwa mbali ama kwa kuangusha Serikali, au kwa ghasia na machafuko ya kisiasa nchini.

Jukumu hili la Chama kwa Taifa na wananchi wake ni muhimu zaidi katika nchi ya Chama Kimoja, kwa sababu katika nchi hiyo Chama ndicho kiungo peke yake kati ya umma na Serikali. Lazima kiwe kimejiunda katika namna ambayo shida, matarajio na mawazo ya wananchi wakati wote yanafikishwa mbele ya Serikali; na vile vile kiweze kuwaeleza wananchi mafanikio, matatizo, mapendekezo na maamuzi ya Serikali.

Je, CCM itayakabili vipi majukumu haya?


Je, kwa vipimo hivyo CCM ina sura gani?


Chama cha Mapinduzi ni Chama cha wakulima na wafanyakazi; misingi yake iko wazi wazi kuhusu shabaha na shughuli za Taifa na sera za Serikali. Misingi hiyo imetamkwa katika Azimio la Arusha na katika Katiba ya Chama. Chama chetu kimedhamiria kufuata misingi ya heshima na usawa wa binadamu; na kwa mujibu wa misingi hiyo, CCM ni Chama cha Kijamaa, na kwa hiyo kinasimamia misingi ya demokrasia. Shabaha zake ni kulinda uhuru na heshima ya nchi yetu, kudumisha umoja wa Taifa letu, na kutafuta maendeleo yaliyo
sawa ya uchumi na ya jamii kwa watu wote na kwa taifa zima.

CCM imekwishachagua mipango, mikakati na sera zinazofaa katika kuendeleza misingi na shabaha hizo. Inajitahidi kusimamia na kuendesha uchumi kwa njia ya kidemokrasia na kuleta maendeleo sawa katika Taifa, na inajaribu kufanya hivyo kwa kushika sehemu kubwa ya milki ya umma au kutawala sehemu kubwa ya njia kuu za uchumi wa nchi yetu. Lakini CCM inatazama hali halisi, na inatambua kwamba mabadiliko yanayotokea ya teknolojia na matukio ya kimataifa yanaweza yakalazimu kurekebisha njia zitakazotumiwa ili kufanikisha hiyo shabaha ya kusimamia uchumi kwa njia ya kidemokrasia. Mjadala unaoendelea sasa unajaribu kujibu matatizo ya jinsi ya kuoanisha jitihada na utundu wa mtu binafsi na maendeleo ya uzalishaji wa mali ya umma, na huku misingi ya heshima ya usawa na heshima ya binadamu ikilindwa. Katika mambo yote hayo, CCM inashika nafasi yake ya uongozi kwa ufanisi wa kutosha katika ngazi ya Taifa. Katika ngazi ya mkoa na ngazi za chini zaidi, pengine CCM haina ufanisi mkubwa katika lengo hilo.

Uanachama wa CCM ni jambo la hiari. Kwa sehemu kubwa Chama kimefanikiwa kuzuia vishawishi vya kudai kadi ya CCM kuwa ni sharti la kupatia kazi au kupata huduma nyingine za umma. Ni dhahiri kwamba uongozi wa Chama chetu lazima ushikwe na wanachama wa CCM. Tunachoweza kukosolewa ni kwamba wakati mwingine tunachagua viongozi wasiostahili. Lakini ni vigumu katika utaratibu wo wote wa demokrasia kuzuia mgombea mwenye haki kwa mujibu wa sheria asichaguliwe na wapiga kura. Vile vile tunawataka askari wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuwa wanachama wa CCM.

Naamini kuwa uamuzi huu ulikuwa sahihi kabisa wakati tulipounda Jeshi la Wananchi wa Tanzania mwaka 1964, wakati ambapo TANU na ASP ndivyo kwa kweli vilivyokuwa "Chama Kimoja'', kila kimo- ja katika upande wake wa Muungano, hata kama haikuwako Sheria au Katiba ya kusema hivyo.

Ni vema kuueleza uamuzi huo. Mazoea ya kila nchi yanatokana na historia yake. Wakoloni, kutokana na uzoefu wao, walitushauri kuwa si jambo jema jeshi kujiingiza katika mambo ya siasa. Tunakubali kwamba Jeshi si Chama cha Siasa. Lakini Jeshi la nchi yo yote kama ni jeshi la kizalendo kweli, na si jeshi la mamluki, halina budi likubali Katiba ya Nchi hiyo na shabaha zake za msingi. Kama nchi ina mfumo wa Vyama Vingi, Jeshi halina budi likubali mfumo huo na kuulinda; na kama nchi ina mfumo wa Chama Kimoja, Jeshi halina budi likubali mfumo huo na kuulinda.

Mfumo wa Chama Kimoja ulitokana na hali halisi na historia ya Nchi yetu. Baada ya maasi ya jeshi tulilorithi, na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, tulilazimika kuunda Jeshi jipya litakalolingana na hali halisi na historia ya Nchi yetu. Kwa hiyo tulilazimika kuchukua vijana wazalendo waliokubali shabaha za Vyama Vyetu.

Uamuzi huu ulikuwa ni uamuzi sahihi kabisa. Tulikataa kabisa utaratibu wa kufanya Jeshi la Wazalendo kuwa maamuma, au watazamaji tu, katika mambo ya siasa ya Nchi yetu. Kwa hiyo Jeshi letu ni Jeshi la Wanachama wa CCM; limefunzwa sana mambo ya siasa; lina mwamko mkubwa sana wa kisiasa, na linashiriki kikamilifu katika mambo yote ya siasa. Hapa tuna mikoa 26 - mmojawapo ni wa Jeshi. Jeshi letu linakubali Katiba ya Nchi yetu, na Shabaha Kuu za Nchi yetu kama zilivyoelezwa katika Azimio la Arusha. Na kwa kuwa shabaha hizi zina manufaa ya msingi kwa Taifa zima, na siyo kwa Wanachama wa CCM tu, mimi nalitazamia Jeshi la Wananchi wa Tanzania kuendelea kulinda maslahi ya Wananchi wa Tanzania. Jeshi letu lazima liendelee kuwa Jeshi la kizalendo na kisiasa. Haliwezi kuwa Jeshi la mamluki.

Faida za Jeshi letu kuwa ni Jeshi la Kizalendo na Kisiasa zimeonekana wazi wazi kabisa. Nimewahi kusema, na leo nitarudia, kwamba vitu vitatu vimelisaidia Taifa letu kuwa na hali ya umoja na utulivu tulio nao: Kiswahili, Azimio la Arusha na mfumo wa Chama Kimoja. Labda ningeongeza cha nne: Jeshi la kizalendo na Kisiasa.

Kama tungekubali kujenga Jeshi maamuma na la watazamaji tu kisiasa, mimi sina hakika kama tungeweza kujenga demokrasia na kudumisha hali ya umoja na utulivu tulio nao katika Nchi yetu. Kwa hiyo kama gharama moja ya kubadili mfumo wetu wa demokrasia ya Chama Kimoja na kujaribu demokrasia ya Vyama Vingi, ni kulitoa Jeshi katika siasa, hiyo peke yake, kwa maoni yangu, ni sababu ya kutosha kuendelea na mfumo wetu wa sasa.

Jeshi letu haliwezi likafanywa kuwa Jeshi maamuma katika mambo ya siasa. Jeshi letu ni Chuo safi cha siasa kuliko Chuo kingine cho chote katika nchi nzima. Jeshi haliwezi kuwa Jeshi la mamluki, ni Jeshi la Kizalendo. Sijui kama Jeshi letu linaweza kutazamiwa kujenga ubepari. Hiyo haikuwa shabaha yetu. Tulijitahidi kulifanya Jeshi letu kuwa Chuo cha Ujamaa. Matumaini yangu ni kwamba tumefaulu kiasi cha kutosha; na kwamba Jeshi letu litaendelea kulinda na kutetea misingi mikuu ya Azimio la Arusha.

Na wala huu si msimamo wa kuonea haya au kuombea radhi. Marekani wana vyama viwili, vyote vya kibeberu na kibepari. Vyama hivyo ndivyo vinavyoitawala Marekani kwa zamu. Vyote vinalinda ubepari. Lakini hata siku moja hutasikia kuwa Rais ye yote wa Marekani amemteua Mkomunisti, au Msoshalisti kuwa Mkuu wa Majeshi ya Kimarekani! Mungu akiwapa ushauri huo wataukataa! Mimi binafsi nitafurahi sana Tanzania nayo ikiwa na Vyama Viwili vya Kijamaa; na ikakataa kabisa kabisa kuweka Vyombo vyake vya ulinzi na usalama mikononi mwa wapingaji wa siasa hiyo.

Nilikuwa nikieleza kwamba uanachama wa CCM ni wa hiari. Ukiacha maeneo machache niliyoyaeleza, kuwa na kadi ya CCM si sharti la kupatia kazi, au huduma ya umma au leseni ya biashara au haki yoyote ya raia wa Tanzania.

Pia, CCM imefanikiwa kwa kiasi cha kutosha kushika nafasi yake ya uongozi nchini mwetu katika shughuli za kidemokrasia za uchaguzi katika ngazi za Taifa na za chini zaidi. CCM inaweka taratibu za kuwapata wagombea kwa mujibu wa Sheria, na hivyo shughuli hizo huwa sehemu ya demokrasia ya Chama. CCM inasimamia, na kwa kiasi kikubwa inaendesha, kampeni za uchaguzi katika ngazi zote. Zaidi ya hapo, Chama kinaisaidia Tume ya Uchaguzi katika kuhimiza uandikishaji wa wapigakura, na usimamizi mzuri na wa haki katika vituo vya wapigakura na kuhesabu kura [tatizo hili bado halijapatiwa ufumbuzi ingawa mfumo wa chama kimoja ulikoma mwaka 1992].

Katika hatua zote hizo, CCM inajishughulisha sana. Lakini ufanisi wake katika shughuli hizo bado haujawa wa kuridhisha hasa. Mara nyingi, pamoja na safari hii, tumelazimika kuongeza siku za kuandikisha wapigakura, au katika uchaguzi wa madiwani, hata kuahirisha uchaguzi wenyewe! Haya yasingeweza kutokea kama taratibu za Chama zingekuwa nzuri kila mahali, na kama taratibu hizo na muundo wa Chama vingetumika vizuri. Chama kinahitaji kujichunguza chenyewe na taratibu zake katika suala hili.

Na ingawa kwa nadharia muundo wa Chama chetu ni wa kidemokrasia, lakini katika vitendo hatuonyeshi demokrasia wakati wote na kwa shughuli zetu zote. Hata kama Chama chetu kingekuwa ni Chombo cha uchaguzi tu, na hakina shughuli nyingine, ungetazamia kwamba kati ya uchaguzi na uchaguzi mwingine, wale waliochaguliwa na wale ambao wangependa kusimama katika uchaguzi ujao, watafanya juhudi wakati wote kudai mikutano ya wanachama kwa mujibu wa Katiba, ili kujadili mambo yanayowahusu! Hawa wakati wote wangekuwa ni makada wazuri sana wa Chama. Lakini hatuna tabia hii. Kati ya uchaguzi na uchaguzi mwingine wagombea wengi husahau Chama, na hawajali sana mikutano ya wanachama. Huanza kukikumbuka Chama uchaguzi unapokaribia. Lakini ukweli ni kwamba demokrasia si kitu ambacho unaweza ukakiwasha wakati unapotaka kukitumia, na kukizima wakati ambapo hukitaki. Wanachama wa CCM wanaweza tu kuwa na nafasi ya kuchagua vizuri mjumbe wanayemtaka kama wakati wote wamekuwa wakikutana, na wamekuwa wanaelewa matatizo yanayobadilika katika maeneo yao na katika Taifa lao, na wanayaelewa masuala yanayotakiwa kuamuliwa katika vikao vya ngazi mbali mbali. Shughuli za kidemokrasia lazima ziwe kazi ya kudumu katika Chama cha kidemokrasia na katika Taifa la kidemokrasia, vinginevyo Chama hicho wakati wote kitakuwa katika hatari ya kutumiwa na wakorofi wachache tu.

Vilevile, pamoja na kanuni zilizo wazi zilizoandikwa katika Katiba ya Chama, si matawi yote yanayofanya Mikutano ya Wanachama wote kila baada ya miezi mitatu. Mwaka 1987 na '88 nilipozungukia baadhi ya matawi yetu katika sehemu mbali mbali za Tanzania Bara na Zanzibar, ilikuwa ni wazi kabisa kwamba hata mikutano ya kikatiba mara nyingi haifanyiki; mikutano michache hufanyika kama kiongozi wa Chama wa ngazi ya juu zaidi amepangiwa kuhutubia! Maana yake ni kwamba mawazo ya Wanachama kuhusu matatizo ya mahali pao, au juu ya masuala mengine ya wakati huo, hayawezi kufikishwa katika ngazi ya Wilaya, ya Mkoa au ya Taifa; kwa kifupi mawazo ya wananchi hayaifikii Serikali. Mikutano ya Wanachama na Jumuiya za Wananchi ndiyo inayokisaidia Chama kupata maoni ya Wananchi wakati wote. Kama mikutano hiyo haifanyiki, Wananchi hawana chombo cha kufikisha maoni yao katika vikao vya juu vya Chama na Serikali.

Na sijui ni mara ngapi makatibu wa matawi na Wenyeviti wa Matawi hufanya mikutano na viongozi wa mashina, kusikiliza mawazo ya shina, kuzungumzia kazi za kufanya katika kipindi kinachokuja, au kupendekeza ajenda za Mkutano wa Tawi, au hata kueleza maamuzi yaliyotolewa katika ngazi za juu za Chama, na jinsi uamuzi huo utakavyowahusu wao. Kwa kweli watu wengi wanaoitwa viongozi wa Chama siku hizi si viongozi hata kidogo; ni watu wa ofisini tu. Tuna viongozi wachache sana kwa maana halisi ya neno "kiongozi", yaani "Mwonyesha njia". Huwezi kuonyesha njia kwa kung'ang'ania ofisini.

Hiyo ni kasoro kubwa sana ya CCM hivi sasa. Jitihada zimefanywa angalau kuipunguza kasoro hiyo, lakini jitihada hizo hazikuendelezwa kwa kutumia taratibu za kudumu za kutoa taarifa na maoni kati ya Matawi, Wilaya, Mikoa na Makao Makuu. Shida zinazotokana na matatizo ya usafiri, upungufu wa fedha na kadhalika zinajulikana, lakini ni vigumu kuamini kuwa tusingeweza kufanya kazi za Chama vizuri zaidi kuliko tunavyozifanya sasa, hasa katika Matawi ya mijini. Mara nyingi hali ya matawi haya nayo ni mbaya tu kama ile ya Wilaya na Mikoa iliyo mbali sana. Huko nyuma, wakati wa Vyama vyetu vya awali matatizo haya ya usafiri na upungufu wa fedha yalikuwa makubwa zaidi, na idadi ya viongozi na wafanyakazi wa Chama ilikuwa ndogo zaidi, lakini kazi hizi za mikutano ya Chama na kuwa karibu na wananchi, zilikuwa zinafanywa vizuri zaidi. Watu wa kuwajibika kwa kasoro hii hatimaye ni Halmashauri Kuu ya Taifa na Mwenyekiti wake wa zamani. Halmashauri Kuu ya Taifa ingepaswa kuhakikisha kuwa Kamati Kuu Sekretarieti yake inafuatilia shughuli za Mikoani, na kupitia kwao kuhakikisha kwamba Wilaya na Matawi nayo yanafanya kazi kama inavyotakiwa. Bado juhudi zaidi zinatakiwa katika suala hili.

Kipimo kingine cha upungufu wa CCM ni kwamba hatujaweza kujitegemea kwa fedha.
CCM inapata ruzuku kubwa kutoka Serikalini, na maana yake ni kwamba inachukua kodi za wananchi wote, wanachama na wasiokuwa wanachama. Nimesema mapema kwamba hata katika nchi yenye vyama vingi si jambo la ajabu kwa chama cha siasa kupokea fedha kutoka Serikalini kwa shughuli maalum. Na katika nchi ya Chama Kimoja ni haki kabisa iwe hivyo kwa kuwa Chama ndicho chombo peke yake nchini kinachoweza kuisaidia Serikali katika utekelezaji wa sera zake, hasa pale ambapo utekelezaji huo unahitaji kuwahamasisha watu. Lakini kama Chama kinataka kubaki kuwa chenye nguvu na cha hiari kabisa, basi ruzuku hiyo lazima iwe ya kazi maalum tu. Si vizuri hata kidogo Chama chetu kitegemee ruzuku ya Serikali kwa kuendesha shughuli zake za kawaida. Tukifanya hivyo tutaacha kuwa Chama; tutakuwa ni Idara tu ya Serikali.

Tukifikia hali hiyo Serikali itaongoza Chama; Chama hakitaweza tena kuongoza Serikali. Nautaja upungufu huu nikijua kuwa Uongozi wa Chama chetu ulikwisha kuuzingatia na ukateua kamati maalum ya kukishauri Chama jinsi ya kuushughulikia. Mapendekezo ya Kamati hiyo yamo katika kutekelezwa.

Kasoro nyingine mbili za CCM ni kubwa zaidi, katika mfumo wo wote. Nimesema mapema kwamba Chama chetu si Chombo cha Uchaguzi kinachowashwa wakati wa uchaguzi, na kuzimwa baada ya uchaguzi. Chama chetu ni Chama cha uongozi wa kila siku na wakati wote. Ili Chama cha siasa kiwe mwakilishi wa wananchi katika Serikali, na kiaminike na umma, lazima Chama hicho kiwe karibu nao kila siku. Lazima Chama kiwasaidie wananchi kujiendeleza na kupanua mawazo yao kwa kuwaelimisha, kwa kuwaunganisha kwa hiari katika shughuli zao za kujitegemea, na kadhalika. Na hasa Chama lazima kiwasaidie wananchi wanapopatikana na matatizo ya aina yoyote, yawe yanatokana na kudura ya Mungu, au ni maafa tu ya kijijini au hata nyumbani mwa mtu. Lazima Chama kiwe mtetezi wa watu wote, wake kwa waume - na watoto - kuhusu vitendo vya dhuluma au maonevu vinavyofanywa na mtu ye yote, awe bepari mwajiri, au mwenye nyumba, au hata watendaji wa Chama wanaotumia vibaya madaraka yao. Katika matatizo ya wananchi yanayohusu vyombo vya Serikali, Wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, na Madiwani, wana wajibu maalum.

Ukiacha matukio machache sana, viongozi wa CCM hawana tabia hiyo ya kujali shida za watu. Hatuna utaratibu wala tabia ya kusikiliza watu wenye shida za kweli na kujaribu kuwasaidia. Kama Viongozi wetu wote wa ngazi mbali mbali wangekuwa na taratibu na tabia ya kuwasaidia wananchi tusingefikishwa hapa tulipofikishwa.

Wananchi wenye shida za kweli kweli hutapatapa mno siku hizi kutafuta msaada. Na sasa tumefikia hali ya ovyo kabisa kwamba Rais wa nchi yetu analazimika kutatua matatizo madogo madogo katika sehemu mbali mbali za nchi kumsaidia raia mmoja mmoja. Hali hii ni hali ya aibu kwetu wote, na inadhihirisha tu jinsi vyombo vya Chama na ya Serikali vinavyofanya kazi vibaya. Iko faida kubwa inayotokana na kazi hizo anazozifanya Rais wetu, lakini vile vile ni kupoteza muda na nguvu za Rais wetu anazozihitaji kutimiza majukumu yake maalum ambayo ni magumu na yanadai muda wake wote.

Na mwisho, katika aina yo yote ya utawala wa kidemokrasia, Chama kinachoshika Serikali hakitakiwi kufanya kazi za Serikali, na haifai kifanye vitendo kana kwamba ndicho Serikali. Maelekezo hayo yametolewa mara nyingi, yametolewa na mimi mwenyewe, na Halmashauri Kuu ya Taifa, na viongozi wengine wa Chama na Serikali.

Maagizo ya Chama chetu kwa Serikali kwa desturi ni maagizo ya jumla na hutolewa na vikao vinavyohusika. Maelekezo ya Chama hayawezi yakatolewa na mtu kwa mtu, na katika mambo ya utendaji wa kila siku. Lakini baadhi ya viongozi wa CCM hawaachi tabia ya kujichukulia madaraka ya Serikali kwa njia mbali mbali. Bado maagizo yanatolewa kwa mtendaji wa Serikali ili mtu fulani apewe leseni, au apewe kazi, au kikundi fulani kipewe ruzuku au upendeleo fulani.

Na mtendaji huyo maskini, mwenyewe akiwa mwanachama safi wa CCM, huona vigumu sana kukataa, hata kama anajua kwamba si vizuri kufanya hivyo. Katika hali hiyo mtendaji huyu anamtarajia kiongozi yule wa Chama amtazame vizuri. Hayo ni makosa; lazima tuyaache. Mtu anayekuja kwenye Chama na tatizo lake, anaweza kupelekwa kwa mtendaji wa Serikali anayehusika, hata pamoja na barua ya kumwomba mtendaji huyo afikirie shida yake. Lakini lazima mtendaji huyo aachiwe kufanya kazi yake bila ya hofu ya kuwaudhi wakubwa au matumaini ya kutazamwa vizuri kesho na kesho-kutwa

Tumekemea sana, kwa mfano, tabia ya kuwatoza Wananchi michango ya aina ya kodi. Ingawa baadhi ya viongozi wa Chama wa ngazi za juu wamefukuzwa au wamelazimishwa kujiuzulu kwa kosa hili hili, lakini matawi, Ofisi za Wilaya na hata Mikoa inaendelea kuwatoza wananchi michango ya aina hiyo. Hilo si kosa tu; kwa Chama chetu ni dhambi; ni haramu! Watendaji na Kamati zinazohusika lazima waadhibiwe vikali na Chama kila wanapofanya hivyo, na udhibiti huo uendelee wakati wote. Mimi si mwanasheria, lakini nadhani kwamba wanaochangisha michango ya aina ya kodi wangeweza, au wangepaswa, kupelekwa mahakamani na kushtakiwa kwa makosa ya kujipatia fedha kwa njia haramu.

Chama kinaweza kuwatoza wanachama wake ada. Kwa mujibu wa Katiba ya Chama, Kamati inayohusika katika ngazi yoyote inaweza kuamua kwamba wanachama wake wote katika eneo hilo watoe mchango maalum kwa shughuli fulani, ingawa tena litakuwa kosa kujaribu kumlazimisha kila mwanachama kufanya hivyo. Chama, katika ngazi zote, kinaweza kuwaomba watu wasiokuwa wanachama kutoa michango, mradi tu maombi yenyewe hayatolewi kwa namna ya vitisho, na michango haiombwi kwa ahadi za kumpa msaada au upendeleo fulani huyo anayetoa.

Matembezi ya Mshikamano ya kila mwaka yanayoongozwa na CCM, ambayo sasa yanafanikiwa sana, yanadhihirisha jinsi watu wetu walio wengi walivyo radhi kuchangia shughuli za Chama kwa hiari zao kama wakiendewa kwa taratibu zinazofaa. Shughuli nyingine za kutafuta fedha zinaweza kupangwa ambapo wanachama na wasio wanachama wanaweza kushiriki, wakipenda. Lakini kamwe Chama kisijaribu kutoza kodi, au ushuru, au malipo mengine yoyote ya nguvu-nguvu kwa mtu ye yote, awe mwanachama au si mwanachama. Michango yoyote ya fedha inayotolewa kwa Chama kwa ajili ya shughuli za Chama lazima itokane na ridhaa ya mtoaji mwenyewe.

Ndugu Wanachama: Makosa niliyoyataja si makosa yasiyoepukika katika utaratibu wa Chama Kimoja. Inawezekana kwamba ni rahisi zaidi kuyafanya katika utaratibu wa Chama Kimoja, lakini si kwamba hayawezi kuepukwa. Kama wananchi wetu bado hawajatukasirikia sana kwa makosa hayo, na hivyo ndivyo inavyoonekana mpaka sasa, basi tukidhamiria tunaweza kuyafuta kabisa katika Chama chetu. Na lazima tufanye hivyo.

Kwanza kasoro hizo hazikuwako wakati wa mapambano ya kupigania Uhuru yaliyoendeshwa na Vyama vyetu vya awali. Kwa mfano, tusingeweza kujaribu kumtoza kodi mtu ye yote. Michango yetu ilikuwa ni ya hiari kabisa. Chama kilijitahidi sana kujitegemea na kazi nyingi za Chama zilifanywa kwa kujitolea. Uongozi wa Chama wakati ule haukuwa unahesabika kama ni nafasi ya kushika madaraka au ya kujipatia fedha. Ilikuwa nafasi tu ya kutoa mchango mkubwa zaidi katika mapambano ya kudai Uhuru wa Nchi yetu na wa wananchi wake. Kushika uongozi wakati ule kulikuwa kujitoa mhanga, na kwa kawaida mtu alikuwa hapati kitu cho chote isipokuwa kujitolea hali na mali na kuridhika tu moyoni mwake kuwa amepigania jambo analoliamini. Lakini siku hizi mambo ni tofauti.

Si jambo la aibu kugombea nafasi za uongozi katika Chama na Serikali zetu. Halmashauri Kuu ya Taifa, na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa; Bunge, na Baraza la Mawaziri la Serikali ya Muungano; Baraza la Wawakilishi, na Baraza la mapinduzi: hivi vyote ni vikao vya Chama na Serikali vinavyofanya maamuzi muhimu ya Nchi yetu. Ni jambo jema na muhimu sana wanachama wetu watake kuwa katika vikao hivyo ili washiriki katika maamuzi hayo. Taratibu zetu zote za uchaguzi zina shabaha ya kuwawezesha wanachama wetu kufanya hivyo kwa njia za uhuru na usawa. Na wakisha kuchaguliwa katika nafasi hizo ni wajibu wa Chama na Serikali kuwalipa mishahara au posho za vikao, au - kwa baadhi yao - mishahara pamoja na posho za vikao, na marupurupu mengine ya kazi. Hili si jambo la ajabu, wala la kuonea haya.

Viongozi wetu si matajiri, hata tuseme kuwa hawahitaji kulipwa; na wala si watawa. Lakini hata watawa nao lazima wale, wavae na walale mahali. Viongozi wetu wana familia zao au wanatarajia kuwa na familia. Kwa hiyo ni haki kabisa kuwalipa viongozi na wafanyakazi wa Chama chetu. Na wala malipo yao si makubwa sana isipokuwa kwa kulinganisha na pato la wastani la nchi maskini kama yetu. Na hicho ni kipimo cha maana cha kuzingatia. Lakini hakuna kiongozi mwaminifu wa Chama chetu ambaye ataweza kutajirika kwa mapato anayolipwa na Chama. Wote mnazijua hali za viongozi wetu waliokwisha kuacha kazi. Mara nyingi hali za maisha yao ni duni kiasi cha kuaibisha.

Lakini baada ya kusema hayo lazima niseme pia kwamba siku hizi kuna watu wengi mno ambao huingia katika Chama na kugombea nafasi za uongozi kwa matumaini ya kupata fedha na vyeo kwa faida zao wenyewe. Siku hizi watu wanatazamia kulipwa posho na ujira kwa karibu kila shughuli ya Chama au ya uongozi. Ni shughuli chache mno zinazofanyika kwa misingi ya kujitolea kutokana na imani katika shabaha za Chama. Moyo wa kujitolea umefifia mno. Katika hali kama hiyo ni vigumu sana kuwapata viongozi wenye moyo wa kuwatumikia wenzao.

Lakini Chama cho chote, hata chama cha michezo tu, lazima kiendeshwe na washabiki wake kwa njia za kujitolea. Moyo wa kujitolea ukifa, chama hakiwi chama tena; kinakuwa ni chaka tu la mawindo ya kujitafutia mali. Uongozi na kazi katika Chama unahitaji ushahidi kidogo wa kutaka kutumikia Chama chetu na Wananchi wenzetu.

Ujamaa

Mwisho Ujamaa. Ndugu Wajumbe; Kwa mujibu wa Katiba, na natumaini hata imani za watu, CCM ni Chama cha kijamaa. Chama chenyewe, wanachama wake wote na hasa viongozi wake wote wanapaswa kufanya vitendo vinavyolingana na maelekezo ya kijamaa yaliyomo ndani ya Katiba. Chama chenyewe pamoja na wanachama wake wote lazima waitekeleze na kuidumisha misingi na shabaha zilizomo katika ibara ya 4 hadi ya 19 ya Katiba ya CCM ya mwaka 1987, na zilizomo katika Azimio la Arusha.

Ili kufanya hivyo kila kiongozi na kila mwanachama anapaswa kuishi kwa kuheshimu taratibu za kijamaa: amheshimu kila binadamu, na ajitahidi kusikiliza shida za kweli za kila Mtanzania. Na Chama chenyewe, lazima kiwe tayari na kiwe na uwezo wa kumdhibiti mwanachama wake yeyote anayetenda vitendo kinyume cha misingi ya maendeleo ya kijamaa.

Kama Chama chetu kitapuuza misingi ya ujamaa, basi kitakuwa kinapuuza msingi mmoja muhimu wa amani na utulivu katika Taifa hili. Tutavuruga amani; maana tutakuwa tumeondoa matumaini ya kuleta maendeleo yanayoheshimu utu na usawa.

Pamoja na kasoro zake zote, Chama chetu kimeitumikia vema nchi yetu kwa kujitahidi kuzingatia misingi yake ya kijamaa. Mafanikio yetu makubwa yametokana na kuiheshimu misingi ya kijamaa. Baadhi ya makosa yetu makubwa yametokana na hapo tulipoipuuza misingi hiyo. Kama wanachama wetu wote wataizingatia misingi hiyo kwa makini zaidi tutaweza kufanya kazi nzuri zaidi. Lakini mpaka sasa, kwa uongozi wa CCM, nchi imedumisha umoja wake na utulivu wake. CCM imepata mafanikio hayo, ingawa nchi imekuwa na matatizo makubwa sana ya uchumi, pamoja na mabadiliko yaliyokuwa ya lazima na ya mara kwa mara ya watumishi, ya miundo na ya vyombo vya utekelezaji. Pia, CCM imepata mafanikio ingawa mazingira ya uchumi wa Tanzania katika uwanja wa kimataifa yalivurugika sana.

Narudia kusema kwamba Kiswahili, Chama Kimoja na Azimio la Arusha vimetusaidia sana kujenga na kuimarisha amani na utulivunchini mwetu. Kutumia Kiswahili kuwa lugha ya Taifa la Tanzania kumesaidia sana katika kufanikisha mapambano dhidi ya ukabila. Kama kila Mtanzania angekuwa anatumia lugha ya kabila lake, au kama tungejaribu kufanya Kiingereza ndicho kiwe lugha rasmi ya Tanzania, nina hakika kabisa kwamba tusingekuwa tumefikia umoja wa Taifa ambao tumekwisha kuufikia. Pamoja na kwamba mimi binafsi napenda tuendelee kufundisha Kiingereza katika shule zetu, kwa sababu Kiingereza ndicho Kiswahili cha dunia, tuna wajibu mkubwa kuzidi kukiendeleza na kukiimarisha Kiswahili: Ni silaha kubwa ya umoja wa Taifa letu.

Sina hakika kama tungefanikiwa kuzuia migogoro ya ukabila na dini bila mfumo wa demokrasia ya Chama Kimoja ambacho hakina kabila wala dini. Katika nchi yetu changa, vyama vingi vingeweza kuchukua sura ya dini au ukabila. Msimamo wa Tanzania kuhusu uhuru wa kuabudu kwa watu wote nchini, pamoja na msimamo wa uongozi kwamba Chama hakina dini rasmi na wala Dola haina dini rasmi, vimesaidia sana kujenga umoja na utulivu wa nchi yetu. Ikitokea kukazuka waumini wa dini yo yote, wanaotaka kuingiza nchini mwetu siasa ya udini, basi usalama wa Taifa letu utategemea sana msimamo usioyumba katika nchi nzima juu ya kuwa na Dola isiyokuwa na dini rasmi na Chama au Vyama visivyokuwa na dini. Badiliko lo lote katika msimamo huo litaleta hatari kwa umoja na utulivu wa Tanzania. Uhasama wa dini na ukabila utatuangamiza; ni hatari zaidi kuliko ukimwi.

Jambo la tatu ambalo lina umuhimu mkubwa vile vile ni jinsi tulivyojitahidi kufuata misingi ya Ujamaa kama ilivyoainishwa katika Azimio la Arusha. Mara kwa mara itatubidi tufanye marekebisho fulani ya mikakati, na sera na mbinu ili kuleta maendeleo tunayoyatarajia. Lakini wakati yanapofanywa marekebisho hayo, Tanzania isikosee ikaacha msimamo wake wa kuhakikisha kwamba uko usawa wa binadamu, kuna usawa wa msingi katika hali ya maisha ya kila mtu, na kwamba kuna heshima ya binadamu kwa kila raia wa Tanzania.

Tukifanya kosa kama hilo tutavuruga msingi wote wa utulivu na amani katika nchi yetu. Maana yake ni kwamba tutaruhusu na kuimarisha tabaka na fikira za "Sisi" na "Wao". Tutaacha watu wachache wawe na mali na nguvu, na fidhuli ya kuwa na mali na nguvu; na watu wengi wawe ni maskini na wanyonge; na wana manung'uniko, na ghadhabu za umaskini na unyonge. Mgawanyiko wa namna hiyo ni hatari sana. Utaratibu wa Vyama Vingi katika mazingira na hali fulani unaweza usiathiri utulivu. Lakini tofauti kubwa sana za mapato au za hali ya maisha au hata za matumaini tu ya maisha mema ya baadaye haziwezi kuzaa utulivu. Mimi siamini hata kidogo kwamba mnaweza kujenga amani na utulivu wa kudumu katika nchi maskini bila kuheshimu misingi ya haki na usawa. Na "unyang'au" kwa hulka yake hauheshimu misingi ya haki na usawa.

Ndugu Wanachama: Nitaacha kuwa Mwenyekiti mwisho wa kikao hiki. Lakini sitaacha kuwa mwanachama, na mwanachama mkereketwa wa CCM. Na kama mwanachama mwingine ye yote mzuri nitakuwa tayari kutoa ushauri wangu kama ushauri huo utatakiwa na vikao vyake vya Taifa. Shabaha ya hotuba hii ya mwisho ni kujaribu kukisaidia Chama chetu kiendelee kuliongoza Taifa letu, na kuliwezesha kukabiliana na matatizo ya kesho na kuleta maendeleo tunayoyataka.

Nia yangu ni kutaka Chama chetu kijizatiti upya ili kiweze kuendelea kuiongoza nchi yetu katika mfumo wo wote ule: wa Chama Kimoja, au wa Vyama Vingi. Ukombozi wa Afrika haujakamilika. Awamu ya kwanza karibu inakwisha; Awamu ya pili ndiyo inaanza. Nia yangu ni kutaka CCM imara, itakayoisaidia Nchi yetu iendelee kushiriki kwa ukamilifu katika harakati za ukombozi wa Bara letu, Afrika.

Kidumu Chama cha Mapinduzi!
Idumu Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea!
 

kmp

Member
Jun 18, 2009
39
0
Mi nadhani elimu ya uraia bado kabisa haijafika mahali kunakostahili zaidi ya kuongelewa mjini na kwenye makongamamo tu. Tazama watu hao mi pia nafikiri maeneo kama hayo ndiko hara REDET wanafanyia research zao.

Taarifa muhimu za mwenendo wa nchi hii na alama za nyakati hazijawafikia kabisa watu kama hao.

Hii inasikitisha sana, watu hao tizama hawana elimu, maisha bora kwao bado ni ndoto. Hii inadhihirisha ule usemi kwamba ukitaka kuendelea kutawala basi mnyime mtu elimu ili aendelee kuwa mjinga.

baba wa Taifa mwalimu Nyerere katika moja ya hotuba zake alisema- The best way to help the poor is to give them good education.

lakini kwa hali halisi inaonesha viongozi wetu wamesahau hilo ili waendelee kutawala milele.

Mimi natoa wito kwa asasi zisizo za kiserikali, wadau mbalimbali wa JF,vyombo vya habari, wasanii ingawa si kama wale waliovalisha T-shirts za SISIEM pamoja na mdau mmoja mmoja kujitahidi kuwasaidia watu wapate taarifa na elimu stahili juu ya nchi hii.

Pia nadhani TZ bado ipo chini sana katika statistics za awareness inayohusiana na civil rights, democracy, participation katika mambo mbalimbali katika jamii etc. Mwenye statistics hizo atuwekee hapa jamvini tuzione.

Ni hayo tu!
 

nickname

JF-Expert Member
Dec 20, 2009
544
250
Motto wa serikali ya awamu ya nne ya TZ katika ngwe ya miaka mitano ya mwisho na jinsi utekelezaji wake unavyoonekana ni ''Ari zaidi nguvu zaidi na kasi zaidi kuelekea umaskini''.&lt;br /&gt;<br />
Kidumu Chama Cha Majambazi kidumuuuu
 

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
125,012
2,000
Motto wa awamu ya nne katika ngwe ya miaka mitano ya mwisho na jinsi utekelezaji wake unavyoonekana ni ''Ari zaidi nguvu zaidi na kasi zaidi kuelekea umaskini''.
Kidumu Chama Cha Mafisadi kidumuuuu

Dah! ukistaajabu ya Mussa......yote hayo katika kuendelea kuifilisi Tanzania, wameyaona ya Misri na Tunisia nadhani wanaweweseka na kuingiwa woga mkubwa sana
 

tzjamani

JF-Expert Member
Oct 9, 2010
995
0
Motto wa awamu ya nne katika ngwe ya miaka mitano ya mwisho na jinsi utekelezaji wake unavyoonekana ni ''Ari zaidi nguvu zaidi na kasi zaidi kuelekea umaskini''.
Kidumu Chama Cha Mafisadi kidumuuuu

Hapa umekosea mkuu ni Majambazi.
 

Zinduna

JF-Expert Member
Nov 6, 2011
2,379
1,500
Mungu atuepushie mbali........!!!!

IMGP0398.JPG
 

Akili Kichwani

JF-Expert Member
Jan 7, 2010
1,509
1,250
uwongo huo.............. mbona ccm ipo na bado nchi inayumba??.................. au "kuyumba maana yake nini??..................
 

LiverpoolFC

JF-Expert Member
Apr 12, 2011
11,103
2,000
Iyumbe kiasi ya hapa? Ama mpk mwone vilindi vya damu ya Watanzania ndio mjuwe Nchi inayumba? Kawaambie waliku2ma humu jamvini wenyeji wameshajuaga mbinu wa sisiem kitambo. Mbona ya mwenyekiti wa chichiem hajawaita vijana na akawaita wazee tu?
 

KAKA A TAIFA

JF-Expert Member
Apr 27, 2011
567
225
Kweli manake kobe ukimvua gamba bila ridhaa yake ina maaana gamba halijakomaa.sasajipya mpaka liote likomae lazima ayumbe sana kwa jua na mvua.ila nasema hivi kila uhai unataka maji ,na hewa
 

pat john

JF-Expert Member
Mar 31, 2009
245
0
Iyumbe kiasi ya hapa? Ama mpk mwone vilindi vya damu ya Watanzania ndio mjuwe Nchi inayumba? Kawaambie waliku2ma humu jamvini wenyeji wameshajuaga mbinu wa sisiem kitambo. Mbona ya mwenyekiti wa chichiem hajawaita vijana na akawaita wazee tu?
Ni ajabu mbona anaongea kupitia wazee tu. Wazee siku zao CCM imeshazimaliza wanasubiriwa makaburini. Kwa nini asiwaite vijana bila kujali vyama halafu aongee na Taifa kupitia kwao. Vijana ndio wanaokipata cha moto kutokana na uozo wa serikali ya Chama Cha Mafisadi akina Jairo. Vijana ndio watateseka kwa miaka mingi ijayo wao na watoto wao.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom