Biblia, Quran yatumika kuokoa mpasuko CCM

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa amesema mkutano wa Halmashauri Kuu wa chama hicho (Nec) ulilazimika kutumia mistari ya Biblia na Quran kuyapatanisha makundi yaliyoibuka baada ya sakata la Richmond kuibuliwa, hivyo kutishia uhai wa chama.

CCM iliingia kwenye mtafaruku uliotengeneza makundi mawili makubwa mwaka 2008 baada ya sakata la Richmond kutinga bungeni na kisha kuwakumba baadhi ya makada wa juu wa chama hicho, waliotuhumiwa kuhusika na kashfa hiyo ya kifisadi iliyotokana na zabuni tata ya uzalishaji umeme wa dharura iliyoipa ushindi kampuni hiyo(Richmond).

Baadhi ya makada wa chama ngazi za juu katika chama na serikali, akiwemo aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na mawaziri wawili walioitumikia Wizara ya Nishati na Madini kwa nyakati tofauti wakati wa mchakato wa zabuni hiyo, Dk Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi walilazimika kujizulu kutokana na kudaiwa kuhusika katika sakata hilo, huku maofisa wengine wa umma wakitakiwa kuchukuliwa hatua na serikali.

Kutokana na hali hiyo kukaibuka makundi yaliyojulikana kuwa ya mafisadi na ya wapiganaji ambayo yote yanawapambe wengi. Makundi hayo yalijionyesha wazi kuwa hayapikiki chungu kimoja, hivyo kukiweka chama njia panda, huku baadhi wakibashiri kwamba, sasa CCM inaelekea kupasuka.

Akizungunza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Msekwa alieleza mambo ambayo kamati ya rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, iliyoundwa na Nec mwaka jana kuchunguza chanzo cha makundi hayo na jinsi Nec ilivyomaliza mpasuko huo.

Msekwa ambaye ni miongoni mwa wajumbe watatu katika kamati hiyo, alisema kupatikana kwa amani katika mgogoro huo, kulitokana na wapatanishi kutumia vitabu vya Biblia Takatifu na Quran Tukufu.

Wajumbe wengine wa kamati hiyo iliyoundwa na Nec ni Abdulrahman Kinana na mwenyekiti, rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi.

"Mzee Mwinyi alitumia zaidi Quran na mimi nilitumia Biblia. Nilitumia neno la Mungu kutoka Injili ya Mathayo Mtakatifu kifungu kinachosema: "Heri wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu" na Mzee Mwinyi alitumia maneno yanayosema: "Ikiwa kuna makundi mawili yanagombana basi ni heri yasuluhishwe na ikiwa moja litakataa basi waandamwe," alifahamisha Msekwa.

Mbali na kutoa siri hiyo, Msekwa alimmwagia sifa Spika wa Bunge Samuel Sitta kwa kile alichoeleza kuwa amefanikiwa kumaliza sakata la Richmond kwa busara kubwa.

Akielezea sababu ya uhasama wa wabunge wa CCM, Msekwa alisema yalitokana na sakata lililoibuliwa mwanzoni mwa mwaka 2007 na kusababisha mtikisiko mkubwa ndani ya serikali ya awamu ya nne.

Alisema baada ya sakata hilo kulipuka kulitokea mgawanyiko mkubwa katika chama uliozaa makundi mawili. Alitaja vinara wa makundi hayo kuwa ni mbunge wa Monduli Edward Lowassa na Spika wa Bunge, Samuel Sitta.

Kwa mujibu wa Msekwa makundi hayo kila moja lilikuwa likituhumu kundi jingine kuwa lina nia ya kuwang'oa wenzao madarakani, jambo hilo lilileta mtafaruku mkubwa.

"Tumewaita vinara wa makundi hayo na kukaa nao meza moja. Lakini hatukuwa na nia ya kutaka kuwatoa kafara kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari, bali tulitaka amani idumu jambo linaloonyesha kuwa tumefaulu," alisema Msekwa na kuongeza:

"Pamoja na kukaa nao kwa muda wa saa nne katika moja ya kumbi za pale bungeni, kila mmoja alikuwa na kero zake jambo tulilogundua kuwa kila mtu alikuwa akifagilia kitumbua chake kisiingie mchanga".

Katika kile kinachoweza kutafsiriwa kama ni kumtonesha kidonda jana Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, Msekwa alimfagilia spika Sitta kwa kumaliza sakata la Richmond na kisha kuonya kuwa watakaoliendeleza watachukuliwa hatua.

Alisema kauli ya Sitta wakati wa kumaliza suala la Richmond, ilionyesha jinsi spika alivyo makini na kwamba, alimemaliza hasira zake zote na alikuwa na nia ya kuijenga nchi na kuimarisha chama.

"Yule Spika sisi tunaamini kuwa alimaliza hasira zake kabisa na kwa kweli ni mtu wa kupongezwa kwani alimaliza sakata la Richmond na kutoa onyo kwa wale wanaotaka kuendeleza.

Hilo ni jambo ambalo kiongozi makini anatakiwa kulifanya, pale inaonyesha kuwa amefungua ukurasa mpya kabisa."

Siku mbili kabla ya mkutano wa 18 wa Bunge kufunga hoja ya Richmond, lilijadiliwa kufungwa na kisha Spika Sitta alimwonya Rostam kuacha kuendeleza malumbano na badala yake akubali yaishe.

Hata hivyo mbunge huyo alikuja juu na kusema kuwa Sitta hakuwatendea haki Watanzania kwa namna alivyomaliza suala hilo, kwani bado kuna mambo mengi yangeweza kuwekwa wazi endapo ingeundwa kamati maalumu ya majaji kuchunguza suala hilo.

Wakati huohuo, CCM imepitisha kwa kauli moja kuwa siku ya Desemba 31 kila mwaka kwa Watanzania kuadhimisha Siku ya Kawawa kwa ajili ya kumkumbuka mkongwe huyo wa siasa nchini.

Katika taarifa yao kwa vyombo vya habari, wamewataka Watanzania kutumia jina la Kawawa katika maeneo muhumu ikiwemo viwanja vya ndege kwa ajili ya kumuenzi na wakasema wanaandaa utaratibu kumpa nishani ya juu ya heshima kutokana na uongozi wake uliotukuka.
 
Back
Top Bottom