Biashara na mashetani hadi lini? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Biashara na mashetani hadi lini?

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Pdidy, Nov 18, 2009.

 1. Pdidy

  Pdidy JF-Expert Member

  #1
  Nov 18, 2009
  Joined: Nov 22, 2007
  Messages: 33,466
  Likes Received: 5,708
  Trophy Points: 280
  Biashara na mashetani hadi lini?  [​IMG]
  KWA sasa nchi imo kwenye mgawo wa umeme kwa mara nyingine tena katika sehemu zote zinazopata nishati hiyo kutoka kwenye gridi ya taifa. Hili ni tatizo ambalo limegeuka donda ndugu hapa nchini, tangu lilipojitokeza kwa mara ya kwanza yapata miaka 17 iliyopita.
  Ni tatizo ambalo mpaka sasa limeonyesha kwamba limeshindikana kupatiwa ufumbuzi wa kudumu mbali na ule unaoonekana kama dawa ya kutuliza maumivu tu wakati ugonjwa ukibaki palepale. Ila kushindikana huko kupatiwa ufumbuzi hakujiweki wazi kama kunatokana na kuwa nje ya uwezo wa nchi wa kulikabili tatizo husika au kunalelewa kama tatizo lenyewe la nishati ya umeme lisivyoonyesha sura halisi ili kueleweka kama ni tatizo pori au tatizo la kufugwa.
  Nasema hivyo baada ya kuona majaribio yote ambayo yamekwishafanyika katika kukabiliana na tatizo hilo la nishati ya umeme hapa nchini kuonekana yameegemea zaidi katika usemi wa Kiswahili wa “kufa kufaana” kuliko kuonekana yamelenga kulitatua tatizo husika.
  Tatizo hili la umeme linaonekana kwa upande mwingine kugeuka neema kwa baadhi ya watu na hivyo kuleta hisia za kwamba pengine ndiyo maana limeamua kuweka makazi ya kudumu hapa nchini kwa vile huenda linao wenyeji wanaolikirimu.
  Hisia hizi zinajiweka katika ukweli kutokana na kuwepo kwa watu wanaoonekana kuzipokea kwa bashasha taarifa za kuwepo kwa mgawo wa umeme hapa nchini.
  Mfano taarifa za mgawo huu unaoendelea zilipotolewa, baadhi ya vyombo vya habari viliandika taarifa hizo kwa mbwembwe zilizoshindwa kuficha furaha zao kufuatia kutolewa kwa taarifa hiyo ambayo si tu kwamba ni mbaya bali yenye kuleta maumivu yenye uchungu kwa kila mwananchi.
  Vyombo hivyo vya habari vimeandika vikiushadidia, vinaouita utabiri, ambao binafsi naweza kuuita utabiri wa kishetani, utabiri wa mambo machafu, vikiandika kwa wino uliokolezwa kwamba “utabiri umetimia”.
  Tatizo hili la nishati ya umeme hapa nchini naliona kama lisilopaswa kuwepo kwa namna yoyote, ila linakuja tu kwa vile wapo wanaotaka liwepo, wale wanaoneemeka kutokana na tatizo hilo. Ni vigumu kuamini kwamba watu wanaosukumwa na tatizo fulani kufanya uwekezaji unaowapatia neema wangependa tatizo hilo lenye neema kwao litoweke.
  Ni lazima tujenge imani kuwa, uwekezaji wa aina hiyo kwa vyovyote vile utalifanya tatizo husika liwe la kudumu. Ndiyo maana tunaona uwekezaji huo unaosukumwa na matatizo ya dharura, unalazimisha kujifunga kwenye makubaliano magumu na ya ajabu, kama yale ya kwamba ‘naweka mitambo yangu ya kuzalisha umeme, uwe unatumika au hautumiki malipo yangu yanabaki yaleyale kwa muda wote wa mkataba’. Tena mkataba wenyewe unapewa muda mrefu ili uweze kuvinufaisha hata vitukuu vya wawekezaji.
  Bila shaka makubaliano hayo yanakuwa yameweka kinga ya kuilinda neema ya hao wawekezaji isije ikatetereka iwapo tatizo la umeme linapungua au kuisha kabisa.
  Nashawishika kuamini kuwa, katika hali ya aina hiyo, upo uwezekano wa tatizo la umeme kufufuliwa kama linakuwa linaelekea kufa, kutoweka, au kuumbwa jipya kabisa kwa uwezeshwaji wa wanaoneemeka nalo.
  Kwa mfano, tumeshuhudia watu wakiunda kampuni hewani isiyojulikana kokote wala kueleweka inamilikiwa na nani, na kampuni hiyo kuleta mitambo chakavu ikidai ni ya kuzalisha umeme wa kuiuzia TANESCO.
  Kampuni hiyo iliyoshindwa kuzalisha umeme huo huku ikionyesha inataka ilipwe pamoja na kushindwa kutimiza lengo lake, tumeona jinsi ilivyoleta utata mkubwa kiasi cha kulilazimu Bunge kuunda kamati teule kuchunguza mwenendo wake.
  Baada ya kazi ya uchunguzi, kamati hiyo ikajiridhisha kuwa kampuni hiyo ni ya kitapeli. Tena uchunguzi huo ukaonyesha kuwa utapeli uliofanyika ulijulikana hata ndani ya serikali ila ukaachwa uendelee kupata baraka, jambo lililomfanya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa pamoja na mawaziri wengine wawili kujiuzulu. Hilo ni jambo kubwa.
  Baada ya hapo likafuata shinikizo kuwa mitambo ile chakavu ya kampuni ya kitapeli inunuliwe na serikali kupitia kampuni yake ya kufua na kusambaza umeme nchini, TANESCO. Yaani bila aibu wala haya baadhi ya wananchi wakawa wanayatumia matatizo yanayoonekana kuikabili nchi yetu kuishauri serikali kufanya biashara na kampuni ambayo tayari wawakilishi wetu, wabunge, wameishahakikisha kuwa ni ya kitapeli. Yaani nchi ikubali kuubariki utapeli kwa kisingizio cha nishati ya umeme!
  Hapo ndipo ulipojitokeza utabiri unaoshangiliwa na baadhi ya vyombo vya habari, kwamba umetimia, utabiri wa kwamba kama mitambo hiyo chakavu isingenunuliwa nchi ilikuwa katika hatari ya kuingia gizani, ambao naweza kuufananisha na utabiri wa kusema kwamba usipokubali kuwa mwizi usalama wako utakuwa hatarini.
  Nisingekuwa na matatizo na utabiri huo iwapo ushauri ungekuwa unasema kwamba kufuatia mitambo hiyo kuonekana haina mwenyewe, basi serikali iitaifishe kama njia mojawapo ya kukabiliana na tatizo la nishati ya umeme.
  Mtu mwenye akili timamu ni lazima ajiulize ni kwa nini utabiri huo ulio mchafu, hata kama ni wa kweli, ushangiliwe kutimia kwake? Ni kwamba wanaoshangilia hawashangilii ujuzi uliotumika katika utabiri wala kumshangilia aliyetabiri, hawa wanalo lao jambo na wala tusiwachukulie kama wendawazimu kwa kuyashangilia maafa ambayo pia yanawaathiri.
  Kwangu mimi, ninaloliona ni lile la kufa kufaana. Hawa lazima ni kati ya wale waliokuwa wanaishinikiza serikali ikubali kununua mitambo ya Dowans iliyokuja kwa jina la Richmond, mitambo ambayo mpaka sasa haijulikani mmiliki wake ni nani kutokana na kila mtu kuikana. Maajabu hata wanaotaka inunuliwe hawako tayari kusema inunuliwe kutoka kwa nani! Kisingizio ni kwamba inunuliwe ili kuinusuru nchi kuingia gizani. Yaani nchi ilazimike kuingia kwenye biashara na maruhani kwa kisingizio cha kuogopa giza! Tunasahau kujiuliza, nchi zote zisizokuwa gizani zina Richmond na Dowans?
  Katika mazingira ya aina hiyo, tunaweza tukaamini vipi kwamba si maruhani hayo tunayorubuniwa tukafanye nayo biashara yanayosababisha hali hii ya msukosuko wa nishati ya umeme hapa nchini ili yenyewe yapate uhalali wa kufanya biashara na nchi yetu?
  Tuelewe kwamba biashara zenye utata wa aina hii zinategemea zaidi mahitaji (demand) hata kama ni ya kulazimisha, ili ziweze kuwa kwenye soko. Kwahiyo mbinu za kila aina ni lazima zifanywe hata kama ni za kuyatengeneza mahitaji bandia, maana kinachofanywa si kumjali mteja bali kujali maslahi yanayopatikana kutokana na biashara hiyo haramu. Hicho ndicho kinachoshangiliwa na mawakala wa maruhani.
  Mfano, kuna kauli zinazotolewa na baadhi ya wanaoyaunga mkono maruhani yanayojifanya kuzalisha umeme, kauli za kwamba suala la umeme lilipaswa kuendeshwa kitaalamu kuliko kulipeleka kisiasa ijapokuwa siasa ndiyo inayosiamia mambo yote yakiwemo ya kitaalamu. Sawa, tuwaulize hao wataalamu wa masuala ya umeme. Nini kusudi la kuchimba mabwawa ya kuhifadhi maji ya kuzalisha umeme.
  Neno kuhifadhi tafsiri yake ni kuweka kitu kwa matumizi ya hata baadaye. Sasa inawezekanaje mabwawa hayo yatumike kuhifadhi maji ya kutumika wakati wa msimu wa mvua tu na zikiacha mabwawa nayo yawe yamekauka? Lengo la kuchimba mabwawa ni kwamba walau yaweze kuhifadhi maji kwa kipindi cha mwaka mzima hata kama mvua hazikunyesha.
  Sasa ili tuache kulaumiana kwa mambo yaliyo nje ya uelewa wetu, ingebidi wataalamu wawaeleze wananchi hayo mabwawa kila moja lina uwezo wa kuhifadhi kiasi gani cha maji na kwa muda gani kusudi linapotokea tatizo kama hili waelewe ni nani anapaswa kuwajibika. Maana majuzi tu wakati wa masika mabwawa yalijaa tukawa tunaambiwa kuwa ilibidi maji yafunguliwe ili kubakiza tu kiasi kinachohitajika kwa usalama wa mabwawa, leo hii tunaambiwa yamekauka!
  Au yalifunguliwa ili yaondoke yote? Inabidi tuelewe kama tatizo ni maji kusudi tuelewe kuwa liko nje ya uwezo wetu, la sivyo tujue kuwa tatizo linaletwa na hawa maruhani ambao naamini wako ndani ya uwezo wetu hata kama hawaonekani.
  Tusikubali kumkufuru Mungu kwa madai ya kwamba yanayotupata sasa yametokana na mapenzi yake wakati kumbe wanaoyasababisha tunao miongoni mwetu.
  Hawa maruhani wanataka kufanya biashara kwa kutumia jasho letu, na kama wana uwezo wa kufanya hivyo bila kuonekana wala kujulikana, tuelewe uwezo wao ni mkubwa. Sasa kwa nini tumkufuru Mungu kuwa katunyima mvua badala ya kuyakemea haya mashetani yenye uwezo wa kuyakausha maji yetu tunayokuwa tumeyahifadhi?
  Yale mabwawa yametengenezwa kiasi kwamba yakijaa sana maji yafunguliwe ili yabaki kiasi kinachohitajika, na ndivyo ilivyokuwa miezi michache iliyopita wakati wa mvua za masika. Sasa kwa nini tusihisi kuwa haya maruhani yameingilia mifumo ya mabwawa yetu ili maji yakauke kwa kipindi kifupi katika kuhalalisha hizi biashara haramu? Je, kweli hapa kuna utabiri wowote wa kuushangilia kwa wale tunaowaona wanafanya hivyo? Nani asiyeelewa kuwa shetani ana nguvu nyingi? Hapa kuna utabiri wowote wa kitaalamu? Mbona sisi tulishayatabiri haya kuwa yangeweza kutokea kulingana na mwenendo wa mambo ulivyo hapa nchini mwetu? Ili kuzima nguvu za maruhani hawa na kuondoa uwezekano wa nchi yetu kupatwa na majanga ya mara kwa mara, ni bora serikali ikahakikisha inafanikisha kwa haraka matumizi ya vyanzo mbadala vya nishati ya umeme badala ya kukimbilia kampuni za kufua umeme wa dharura kama inavyofanyika hivi sasa.
   
Loading...