Bernard Membe alitimiza nguzo zote sita za ujasiri

DaveSave

JF-Expert Member
Nov 20, 2010
440
634
MANENO ya Kiingereza yenye kubeba tafsiri ya ujasiri ni mengi. Hapa nitatumia mawili, “valorous" na “plucky”, kueleza wasifu wa Bernard Kamillius Membe. Mwanasiasa, mwanadiplomasia na kachero aliyebobea.

Valorous, mwenye kuonesha ujasiri hata mbele ya hatari. Plucky, asiyeyumba katikati ya nyakati ngumu. Tafsiri zote hizo zinamgusa Membe, mbunge wa Mtama kwa miaka 15, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa miaka nane.

Miaka mitano ya utawala wa Rais wa Tano, John Magufuli, ulimdhihirisha zaidi Membe. Si mwoga, hapendi kushindwa, anaweza kupambana mpaka pumzi ya mwisho. Kunyanyua mikono na kusalimu amri, hiyo kwake ni mwiko.

Fanya marejeo; wakati wa Magufuli kulitokea fukuto la kisiasa ndani ya CCM. Hesabu mmoja baada ya mwingine ambao walituhumiwa kumhujumu Magufuli ambaye alikuwa Mwenyekiti wa CCM. Utaona kuwa wote, hata wale ambao walionesha mwanzoni kwamba ni wagumu, hatimaye walisalimu amri, isipokuwa Membe.

Kituo kimoja baada ya kingine, Membe alibaki yuleyule. Na njia ambazo alizichagua katika mgogoro wa kisiasa ndani ya CCM, uliohusisha wengi, tena watu wazito, Membe alikuwa na namna ya peke yake ya kuushughulikia.

Alikwenda mahakamani kumshitaki Cyprian Musiba, kada wa CCM, aliyejitambulisha kuwa ni mwanaharakati mtetezi wa Magufuli. Ni baada ya Musiba kumtaja Membe kuwa anamhujumu Magufuli.

Wengi walitajwa na Musiba, ikiwemo kutamkwa isivyofaa. Wapo waliokaa kimya. Walikuwepo waliolaumu na kutishia kuchukua hatua lakini hawakufanya kitu. Membe, Wakili Fatma Karume na Waziri wa Ardhi wa zamani, Prof Anna Tibaijuka, walishinda kesi na Mahakama iliamuru walipwe fidia.

Agosti 11, 2021, Mahakama Kuu Zanzibar ilimhukumu Musiba kumlipa Fatma, Sh7.5 bilioni kwa kumdhalilisha. Agosti 13, 2021, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, ilimwamuru Musiba kumlipa Prof Tibaijuka Sh80 milioni kwa kumchafua.

Oktoba 28, 2021, Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, ilimwamuru Musiba kumlipa Membe, Sh6 bilioni. Fatma na Tibaijuka wamekuwa wakijivuta kukazia hukumu, lakini Membe alishatangulia mbele na tayari wajibu wa kudai upo kwa dalali wa Mahakama, kampuni ya Yono.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Moravian Uamsho Tanzania, Bandekila Mwamakula, alimwandikia barua Membe, kumwombea msamaha Musiba. Hata hivyo, Membe alijibu kuwa asingemsamehe abadan!

Bora kutoeleweka lakini sharti usimamie kile unachoona ni sahihi kwa ajili ya kulinda na kuhifadhi utu wako. Hicho ndicho Membe alikisimamia. Na ndio kinaitwa “ujasiri wa kiroho" – “spiritual courage".

Huyo ndiye Membe. Watu aina yake ndio wale husemwa waliumbwa na “moyo wa simba” – “lionhearted". Anapotaka lake lazima alipiganie. Akianzisha vita sharti ifike mwisho. Kuonewa kwake mwiko. Kumvunjia heshima usijaribu, mtamalizana.

WATANZANIA WALICHELEWA KUMJUA

Msimamo wa Membe wa kukataa kuburuzwa kipindi cha uongozi wa Magufuli, ulifanya watu wengi wamfahamu Membe halisi. Kwamba alijitoshekeza kwa ujasiri wa kijamii (social courage) na ujasiri wa kimwili (physical courage).

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally, alitangaza kusudio lake la kukutana na Membe ili amhoji ni kwa nini anatajwa kumhujumu Magufuli. Haukupita muda, Membe alijibu kuwa alikuwa tayari wakati wowote kuitikia wito. Alipoona anachelewa kuitwa, alihoji: “Nasubiri wito, mbona siitwi?”

Kamati ya Maadili ya CCM, iliwaita Membe na makatibu wakuu wastaafu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana na Yusuf Mamba. Membe alikuwa wa kwanza kujibu kuwa angeitikia wito.

Membe alihudhuria kikao, na alipotoka, alizungumza kwa kujiamini: “Tulikuwa na mkutano wa saa tano, wa mijadala mizuri, mikubwa ya kitaifa, inayohusu Chama Cha Mapinduzi na nchi yetu. Nina furaha kubwa ajabu. Nimepata nafasi nzuri ya kufafanua mambo ambayo chama changu kilitaka kuyajua.”

Kitendo cha Membe kuitikia wito wa mamlaka za CCM, kwenda kuzungumza bila hofu katikati ya vitisho vingi vilivyokuwepo, hicho ndicho huitwa ujasiri wa kisomi (intellectual courage).

Misimamo ya Membe ilifanya watu wajiulize nini kilimbadilisha. Hapana, nyakati zilimdhihirisha. Hakuna wakati wowote Membe hakuwa Membe.

Akiwa Waziri wa Mambo ya Nje, aliyekuwa Waziri Mkuu wa UK, David Cameron, alipotoa sharti kuwa kila nchi inayoendelea na ambayo inapokea misaada kutoka kwao, lazima itunge sheria ya kuruhusu ndoa za jinsia moja, Membe alijibu:

“Tupo tayari kwa lolote, hatuwezi kuvunja utaifa na utamaduni wetu kwa nchi yoyote tajiri inayotoa masharti ya kipuuzi ili tushibe matumbo yetu. Kama wanadhani misaada ndio silaha yao wakae nayo.” Jibu hilo la Membe ndio mantiki ya “ujasiri wa kimaadili" – “moral courage".

Kusimama kilicho sahihi kwa gharama yoyote. Balozi wa UK Tanzania, alimjibu Membe kuwa sharti alilotoa Cameron halikuihusu Tanzania.

Chokochoko za kikundi cha waasi M23, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kuitisha Tanzania, ziliifanya Afrika itambue kuwa Tanzania ilikuwa na Membe, Waziri wa Mambo ya Nje, mwenye misimamo mikali na ambaye msamiati wa woga haupo kichwani kwake. Membe akawaahidi M23 kichapo. M23 walikiona cha moto.

Ni Membe aliyeifanya Tanzania iwe nchi pekee Afrika iliyotoa msimamo wa kulaani mataifa makubwa ya Marekani na washirika wake, walipoivamia Libya mwaka 2011 na kumuua aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi. Membe alisema, dhamira haikuwa kumwondoa madarakani Gaddafi, bali kumuua. Membe alikuwa na moral courage!

Mwaka 2008, Membe alikuwa kiongozi pekee wa Kiafrika mwenye kuhusika na mashauri ya kigeni, aliyeisema Zimbabwe, iliyokuwa ikiongozwa na Robert Mugabe, kwamba ilikuwa haioneshi kwenda kwenye uchaguzi huru na haki. Na baada ya uchaguzi, Membe alisema Zimbabwe haikuwa na jinsi zaidi ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Kauli za Membe zilikichukiza chama tawala Zimbabwe, ZanuPF. Membe hakupindisha kauli. Wapo wanachama waandamizi wa ZanuPF, walitoa maneno makali mno kumshambulia Membe. Mwisho, Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliundwa Zimbabwe. Mugabe akawa Rais, mpinzani wake, Morgan Tsvangirai, akawa Waziri Mkuu.

Wakati wa Membe akiwa Waziri wa Mambo ya Nje, Tanzania haikukosa kauli kwenye masuala ya kimataifa. Anzia mgogoro wa Mashariki ya Kati, Wapalestina na Waisrael mpaka Sahrawi (Sahara Magharibi) na kilio chao cha kutawaliwa kimabavu na Morocco.

Membe alikuwa mchungu katika sakata la ufisadi wa ununuzi wa rada nchini. Kampuni ya BAE System ya Uingereza, ni kubwa na kongwe ulimwenguni kwa utengenezaji wa vifaa vya ulinzi, usalama na sayansi ya anga. BAE System iliiuzia Tanzania rada na baadaye Waingereza walibaini bei ya rada ambayo Tanzania iliuziwa ilikuwa kubwa mno.

Bunge la Uingereza, chemba ya chini (House of Commons), mjadala ulikuwa wa moto mno kuhusu BAE kuipiga Tanzania. Kisha Taasisi ya Uchunguzi wa Rushwa Kubwa Uingereza (SFO), ilithibitisha kuwa kulikuwa na mazingira ya rushwa kwenye biashara ya rada ambayo BAE iliiuzia Tanzania.

Baada ya BAE kubanwa, ilitaka irejeshe Tanzania pauni 29.5 milioni (Sh70 bilioni) ambayo ilipewa jina la “chenji ya rada”, kwa njia ya msaada. Membe alikataa fedha hizo. Alisema, BAE walitaka waonekane hawakuwahi kufanya kitu kibaya kwa Serikali ya Tanzania.

Msimamo wa Membe ukawa ni lazima BAE wakiri kuwa waliiuzia Tanzania rada kwa bei ya juu kuliko uhalisia na warejeshe fedha ambazo walitambua zilikuwa za ziada. Membe alisema, kupokea fedha kwa njia ya msaada kungeipaka matope nchi, na hilo hakuliataka.

Februari 2020, Membe alifukuzwa uanachama wa CCM. Uamuzi huo, aliujibu kuwa sababu ni yeye kuiambia Kamati ya Maadili CCM kwamba alitaka kugombea urais. Alisema alitaka kumkabili Magufuli ndani ya chama hicho.

Baada ya kutimuliwa CCM, Membe alijiunga na Chama cha ACT-Wazalendo, akateuliwa kuwa mgombea urais. Baadaye uongozi wa chama chake ulibadili gia angani na kumuunga mkono aliyekuwa mgombea wa Chadema, Tundu Lissu.

Badala ya Membe kukubali kumuunga mkono Lissu, yeye alitamba bado mgombea. Hakufanya kampeni. Kuna wakati alijigamba kuwa angeingia uwanjani dakika ya 89 kutokea benchi na kufunga goli la ushindi dakika ya 90 na mchezo kuisha.

Danadana zote za kugoma kujitoa, na kunadi ahadi kemkemu kuwa angeibua kishindo kikubwa kwenye kampeni, ikiwemo kufunga goli la dakika ya 90, lakini hakufanya chochote, hicho huitwa “ujasiri wa hisia" – “emotional courage”. Membe aliona kutangaza kujitoa kungemaanisha hana nguvu, hakubaliki. Alikomaa na hisia zake.

MEMBE MTOTO WA RONDO

Novemba 9, 1953 katika tarafa cha Rondo, jimbo la Mtama, Lindi, ndipo Membe alizaliwa. Elimu ya msingi alisoma Shule ya Rondo-Chipond kati ya mwaka 1962 na 1968, kisha akajiunga Shule ya Seminari ya Namupa, Lindi, kwa masomo ya sekondari kuanzia mwaka 1969 na alihitimu kidato cha nne mwaka 1973.

Kidato cha tano na sita, Membe alisoma Shule ya Seminari ya Itaga, iliyopo Uyui, Tabora mwaka 1973 na 1974. Mwaka 1980 mpaka 1984, Membe alisoma shahada ya kwanza ya Sayansi ya Siasa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Na mwaka 1990 mpaka 1992, Membe alisoma shahada ya uzamili ya Uhusiano wa Kimataifa, Chuo Kikuu cha John Hopkins, Washington DC, Marekani.

Mwaka 1978, Membe akiwa na umri wa miaka 25 tu, alikuwa mchambuzi wa usalama wa taifa, akifanya kazi Ofisi ya Rais, Idara ya Ulinzi na Usalama wa Taifa. Kazi hiyo aliifanya kwa miaka 11. Mwaka 1992, baada ya kumaliza shahada yake ya uzamili ya Uhusiano wa Kimataifa, Membe aliteuliwa kuwa mshauri wa Balozi wa Tanzania nchini Canada, ofisi yake ikiwa Ottawa. Na alifanya kazi hiyo kwa miaka nane.

Mwaka 2000, Membe alishinda ubunge jimbo la Mtama na aliwakilisha vipindi vitatu mpaka mwaka 2015 alipoamua kustaafu ubunge. Januari 2006, Membe aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani. Oktoba 2006, alihamishwa wizara na kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, kisha Januari 2007, Membe akawa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, nafasi ambayo alidumu nayo miaka nane, mpaka Novemba 2015.

Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015, majina mawili yalitajwa sana katika urais wa Muungano ndani ya CCM; ni Bernard Kamillius Membe na Edward Ngoyai Lowassa. Chinjio la CCM likamnyofoa Lowassa mapema, kisha Membe aliingia tano bora lakini kura za Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) CCM, zilipopigwa, alitoa wa tano.

Membe alishindwa na January Makamba, Dk Asha Rose Migiro, Balozi Amina Salum Ali na Dk Magufuli. Migiro, Amina na Magufuli walipenya tatu bora kwenda Mkutano Mkuu ambako Magufuli alishinda na kuteuliwa kuwa mgombea urais CCM, kisha akawa Rais.

Huyo ndiye Membe, maisha yake yamebeba tafsiri ya nguzo zote sita za ujasiri; ujasiri wa kisomi, kijamii, kimaadili, kihisia, kimwili na kiroho. Mei 12, 2023, ilimpendeza Mungu, Membe avute pumzi ya mwisho.

Mungu alimleta Membe duniani kama zawadi, na amemtwaa kama ahadi. Kila nafsi itaonja mauti.

Ndimi Luqman MALOTO
FB_IMG_16840807491348143.jpg
 
Hivi ubalozi alivuliwa naona maandishi yako yoote hujamtambulisha kama ni balozi.?
 
Baba yetu mkubwa alikataa kutoa msamaha kwa jamaa fulani enzi zake za uongozi kwa kashfa fulani ila askofu alipomwendea msamaha akatoa sababu alimuheshimu sasa kiongozi wake wa dini...jamaa akapewa na viboko juu.. sasa hapa unasema askofu alimwendea mwanadiplomasia akakataa kutoa msamaha..unataka kujaribu kusema nini mtoa mada...
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom