Wangapi mnaikumbuka barua ya Papii Kocha aliyoiandika kwa Rais Kikwete mwaka 2013 kuomba msamaha? Nakumbuka kaka Evarist Chahali aliichukua barua hii na kuiwasilisha kwa Waziri Lazaro Nyalandu aliyeahidi kuifikisha kwa Rais Kikwete. Kuanzia hapo sijui nini kiliendelea. Labda Chahali anaweza kutueleza what happened. Rais alijibu ile barua au aliipuuza?
Nimekumbuka barua hiyo kwa sababu June 25 mwaka huu, Papii Kocha na baba yake Nguza Vicking walitimiza miaka 12 gerezani. Nimeikumbuka barua hiyo kwa sababu kumekuwepo na sintofahamu nyingi kuhusu kesi hii. Nimeikumbuka barua hiyo kwa sababu baadhi ya watu wanaamini familia ya Babu Seya ilionewa. Nimeikumbuka barua hiyo kwa sababu inadaiwa kuna watoto waliowahi kukiri kwamba walifundishwa kutoa ushahidi wa uongo mahakamani.
Anyway mimi sio Hakimu, shahidi sala wakili wa kesi hii, lakini leo nimeipitia upya barua ya Papii Kocha na ikanigusa sana. Nimeipitia nikaona kama ni ya jana japo iliandikwa miaka mitatu iliyopita. Hebu na wewe isome tena:
____________________________________________________
Mfungwa NO:836'04
Gereza Ukonga,
S.L.P 9091
Dar es Salaam,
Mh.Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania,
YAH: MAOMBI YA KUPEWA MSAADA (MSAMAHA) WA KUFUTIWA ADHABU YA KIFUNGO NILIYOPEWA NA MAHAKAMA YA HAKIMU MKAZI KISUTU.
Husika na somo hilo hapo juu.
Mimi ni mfungwa katika gereza kuu la Ukonga. Kwa heshma na taadhima na kwa kutambua utu na huruma yako ya ki-MUNGU ulionayo dhidi ya binadamu wenzako pamoja na mamlaka uliokabidhiwa na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Naanguka na kushika miguu yako mitukufu muheshimiwa rais.
Nakuomba msaada (msamaha) kwako muheshimiwa rais, kwa njia hii ya maandishi kusudi niweze kuondolewa adhabu ya kifungo cha maisha gerezani,niliyohukumiwa na mahakama tajwa hapo juu.
Mh.Rais mimi nimefungwa nikiwa bado kijana mwenye umri mdogo, na ukweli kutoka moyoni sikufanya kosa hilo. Si mimi, baba yangu Nguza wala ndugu yangu yeyote aliyefanya kitendo kile. Lakini wenye mamlaka wakatuona tuna hatia na kuamua kuteketeza kizazi chetu gerezani.
Natamani kiama ifike ili mwenyezi Mungu aweke wazi ukweli wote uliojificha nyuma ya pazia. Mpaka sasa natambua wazi hatima pamoja na dhamana ya maisha yangu ipo katika mikono yako mitukufu Mh. Rais Naomba huruma yako muheshimiwa Rais maana mimi ni mtoto wako ninaehitaji huruma yako wewe mzazi.
Lakini pia sisi ni binadamu wenye nafsi na miili kama wengine. Waliotumia mamlaka yao kutuweka gerezani nao ni binadamu pia, wenye miili na nafsi. Ipo siku nafsi zetu zitapaswa kutoa hesabu ya tuliyoyafanya hapa duniani. wakati huo miili yetu tunayoitumia
kunyanyasa wanyonge itakuwa imeoza mavumbini.
Natumaini kauli yako ya mwisho ndio itakayoleta pumzi ya uhai nafsini mwangu. Nakutakia kazi njema, afya njema na maisha marefu.
Mungu akubariki.
Wako mtiifu
Mfungwa NO:836'04
JOHNSON NGUZA (PAPII KOCHA)
[HASHTAG]#MyTake[/HASHTAG]:
Kama barua hii haikumfikia JK naomba Chahali afanye mpango imfikie JPM. Inaonekana kuna mengi tusiyoyajua nyuma ya pazia. Inawezekana wanaokwenda jela sio wote wana hatia. Hakimu wa haki anabaki kuwa MUNGU peke yake. Brother Chahali plz work on it the way u did last time na Mungu atakubariki.!