Barua kwa Mwalimu J.K Nyerere

josefredy

Member
Oct 24, 2019
7
2
BARUA KWA MWALIMU.
Anuani: mahala pema, mahali peponi.
Ndugu Mwalimu,

Heri ya miaka 98 ya kuzaliwa, Mbuya muhandiri! Na imani unakumbuka kizanaki kwakua uliishi uafrika na kufa mwafrika.
Wakati wino huu ukimwagikia karatasi hii nyeupe, mke wako kipenzi Maria ametembea safari ndefu ya miaka zaidi ya 20 bila hata kusindikizwa na kivuli chako anachojivunia ni maneno yale ya kichungaji aliyosikia siku ya mwisho kabla hujasafiri kwamba "kimwili hauko nasi ila kiroho uko nasi", mwanao kipenzi Makangoro anajianda kusherekea miaka 61 bila ya kua na nafasi ya kusikia soga na nasaha zako kama ulivyomzoesha, muungano ulioupigania uliuacha na umri wa kijana sasa una umri karibu na uzee.

Natumaini wakati na saa hii nikiandika barua hii upo na ndugu Benjamini mkapa, Rashid kawawa, Sam sitta na marafiki zenu mkinywa mvinyo wa sifa wenye radha ya utawala bora na uongozi uluotukuka wenye ugwadu kwa mbali wa makosa watu waliyokataa kuwasameheni, najua wanakwambia na kukusimulia mengi kwakua ulitangulia kusafiri, wanakusimulia kwamba bado mpangaji wa ofisi kuu mnazi mmoja Zanzibar anachaguliwa Dodoma, na sasa viongozi hawapangi tena magogoni ulipopanga wewe kwa miaka 24 sasa wanapanga chamwino.

Tanzania na Africa tumetembea safari ndefu bila kupata kusikia nasaha zako ndo maana nikaamua nikusalimie kwa barua hii. Hatukujua namna ya kukutumia wewe kama bunduki kupambana vita dhidi ya ukabila, utengano na ubaguzi, umaskini, na ujinga, tangu umeondoka tumeshindwa kupata hata mfano wa bunduki inayotoa mlio kama wako, nyingine zina sauti nyepesi nyingine zina sauti nzito lakini haziui.

Nakumbuka ulisema "maendeleao hayana budi yahusiane na maisha ya watu, yamefanya nini kwa watu" naomba nikuhakikishie mwalimu tuliyaacha maneno yako nje ya nyumba yako ya milele mwilongo.

Mwalimu vyama ulivyovishauri visishiriki uchaguzi 1995 visubiri vikue na kuviita vyama vya ruzuku, vimezidi kumea katikati ya miiba, mawe na ukame. Mabomu vizuizi na kubezwa kinguvu vimekua haki zao za kuzaliwa lakini nikutoe hofu mwalimu kwamba wamefungwa miguu lakini wanatembea, wamefungwa vinywa lakini wanaongea.

Ulitumia miaka 24 magogoni ukipigania misingi ya elimu ya kujitegemea, nasikitika kukwambia tumesahahu mwalimu, siku hizi kuna michuano ya nani mwenye shahada nyingi? Wasomi wakizunguka na bahasha zilizojaa maoni ya walimu juu ya uwezo wao wa kukumbuka na baada ya mizunguko ya siku hurudi nyumbani na swali TUTAKULA NINI? Nadhani hatukukuelewa au tulisinzia wakati ukielekeza kwamba "elimu si njia ya kuepukana na umaskini, ni njia ya kupambana nao" wasomi wakipata shahada hulewa na kupayuka kwa sauti kwaheri umasikini.

Nadhani kitu pekee vijana wa dot.com wanakumbuka kuhusu wewe ni kwamba kuna nyakati za utoto wao walibebwa na kufunikwa khanga zenye taswira ya uso wako, wamesahau na kuuzika ujamaa wako, hawataki kuitukuza elimu uliyoihusudu yaani elimu ya kujitegemea na zaidi linalosikitisha vijana wa dot.com wanataka uhuru tu lakini kufanya kazi kwao mwiko nakuhakikishia tulikuzika nayo hapo mwitongo sera yako ya uhuru na kazi.

Sijui kama mzee mkapa kakwambia chama chako kilivyokua mpaka kinafikia hatua kushiriki uchaguzi peke yake, sijui kama ameshakwambia kwamba miaka 5 sahivi ni midogo kuleta maendeleo yenye tija. Nadhani Kabla hajaondoka alisikia kuna watu wamekikatia tiketi chama chako wanataka kisafiri kama KANU ya rafiki yako Kenyatta, CPA ya rafiki yako Nkurumah na UPC ya nduguyo Obote lakini anafahamu wanakula na kunywa meza moja na waamuzi wa safari yao na kikubwa zaidi wanawalipa.

Mwalimu tumevaa na kubeba mabomu mwili mzima kupambana na rushwa lakini mwalimu tunapigana usiku hatupigani mchana kama ulivyopigana wewe na Sokoine. Ulitukataza kutangatanga kwenye mitaa ya magharibi na mashariki za mbali tukiwa na mabakuri ya shida na njaa tuweze kuishi, nakuhakikishia bado sisi ni wabeba mabakuri maarufu.

Ule udongo mliochanganya na kaka yako Abeid kuna upande wanahitaji udongo wao maana wanafinywa wakitaka kulia wanafinywa tena, yale makaratasi mliyosaini wanauliza uliyaweka droo lipi hapa magogoni wanataka wayaone, na bado wanauliza ni mambo mangapi mlikubaliana kushirikiana na Abeid maana hawaelewi wanaona wanakaliwa mpaka kichwani na kwasababu yetu wanakosa kutambulika, kwasababu yetu hawajulikani. Ukipata nafasi nidadavulie ulimaanisha nini uliposema kuifufua Tanganyika ni kuua muungano?

Mwalimu wanasema wanafanya vizuri lakini wanajipigia ngoma wenyewe, wanacheza wenyewe na kujishangilia wenyewe wakijiimbia tenzi za sifa zenye vichwa vya habari maendeleo je wanaimba na kucheza na wananchi ? Mwalimu naomba nikuhakikishie viatu vyako vinawapwaya wengi lakini hujaza marakatasi na kujifanya vinawatosha, wengine huvalishwa majoho juu ya utendaji wako nikuhakikishie mwalimu majoho yote hupwaya na kuburuzika chini.

Baba makongoro kuna kundi siku hizi wakishika peni na karatasi wanafananishwa na magaidi waliobeba silaha za moto wakati kazi yao ni kutujuza tu wala sio kutuvuruga Ila wanatikiswa kwasababu kila wakiandika maneno yao yanatoa mwanga mkali na mweupe na wenye nguvu hawapendi mwanga ule.

Mwalimu maandishi uliyotuachia tumeyazika kwenye maktaba tunazojazana kusoma hali za hewa za ulaya, mapinduzi ya amerika na ufugaji wa ng'ombe Denmark, Uongozi wetu na hatma ya Tanzania, ujamaa, crusade for liberation, Uhuru na maendeleo na vingine vingi vinapambana na vumbi makabatini.Ule umati uliokupokea kutoka uingereza oktoba 1999 ukiwa husemi, huoni, na hutembei bila kubebwa, nawaza umati ule ulikua unalia kwanini ? walijawa na majonzi kwanini? Au kisa ulikua maarufu? Mshangao wangu unatokana na kuzifukia na kuharibu kaburi la nasaha zako, tunakutaja mara moja tu, oktoba 14 kila mwaka sidhani kama.unastahili kukumbukwa kwa aina hii.

Najua bado kichwani kwako unakumbukumbu ya mashtaka ya uchochezi juu yako 1958, wakati huu naandika fimbo iliyokuchapa wewe bado inachapa mpaka sasa na wakati huu imeongezewa miiba na pilipili, mwalimu je ungependa fimbo iliyokuchapa wewe ichape na wengine kisa tu wanatoa sauti zinazochoma wenye nguvu masikio?

Ile sheria mama aliyotuachia Turnbull bado tunaipiga viraka kila palipo na tundu, imefikia hatua matundu mengi haizibiki tena lakini hawataki kuichana sijui kwasababu inalala na kuamkia upande wao? Sijasahau ulituonya kwamba sheria mama ya Turnbull inaweza kutupa mikono ya chuma katika ofisi nyeti za taifa hili.

Nafahamu mwaka 1955 ulimwandikia barua padri Lynch kumweleza juu ya uamuzi wako wakuachana na ualimu ili kuikomboa Tanganyika, vijana wengi sasa wanaishi maamuzi yako ya mwaka 1955 kwakua bunge na ofisi nyeti za taifa hili zina sura na taswira ya pesa, nguvu na umaarufu.

Mwalimu hukumuacha makongoro wala madaraka malangoni pa ofisi yako wala dodoma, uliwaacha butiama wapambane na hali zao, wenzako wanakukosoa kwa vitendo wanapandisha vijana wao mabasi ya kijani kuelekea dodoma na wengine wanawabebesha mabegi vijana wao kuwarudisha maofisini hasa ofisi kuu uliizomkataza madaraka kucheza kwenye viunga vyake wakati wa likizo, kwa vigezo wao waliwahi kupanga.

Mwaka 1962 uliandika kijarida ukisema tujisahihishe nakuhakikishia bado hatujaanza kujisahihisha na mbaya zaidi bado tunakosea sana, tumekua tukioshwa na mapambio na tenzi za sifa kutoka vinywani mwa wanaotuzunguka wanaotupa ujasiri ya kua hatukosei.
Sio kwamba sifahamu kwamba unalia machozi ya damu, unatetemeka kwa hofu na kutiririka jasho woga juu ya hatma ya taifa lisilofutika moyoni mwako, juu ya kupuuzwa kwa nasaha zako na mwenendo wa taifa lako.

Nikipata nafasi saa na wakati mwingine nitatuma ujumbe umpe Mandela ila kwa leo mwambie ANC yake inajichimbia kaburi na kujizika kwa udongo wa rushwa, upendeleo na kukosa maadili pia mwambie wana wake aliokaa gerezani Rhoden island kwajiri yao wanawachinja na kuwafukuza waliokupa hifadhi,mchango wa mawazo na hata kupayuka kwa niaba yenu wakati mkifurukuta muwe huru.

Nikipata nafasi ntakutumia ujumbe umpatie Nkurumah mwambie ndoto yake ya Africa kua moja bado tunaiota katikati ya usingizi mzito hatujui lini tutaamka na lini itaisha muhakikishie hatujui? Mwambie heshima yake iliyozikwa na Joseph Arthur sasa imefufuliwa na kuoshwa lakini mwambie bado haijavalishwa nguo inazostahili.

Mwambie baba wa Libya kiboko ya idris 1 kwamba bado damu yake inawaandama waliomuua na walioweka chumvi kwenye mchuzi wa kifo chake sasa wanapakua, kula na mpaka kuvimbiwa, wanatamani wamuombe msamaha Ila hata alilala hawajui mwambie wanatamani kufika nyumbani kwake kwa milele ila hawajui anakaa mtaa gani kitongoji gani wala rangi ya paa la nyumba yake. Waambie Mandela, Nkurumah, Gaddafi wasijisikie wanyonge nikinunua karamu mpya na nikipata ruhusa nitawasimulia ya kwao. Patrice Emely Lumumba usimsemeshe kitu maana sitaki kumuongezea kasi ya kulia nitamtafuta kwa wakati wangu muda ukiniruhusu.

Mwambie mzee Nyalali vile vipeperushi vya ushauri juu ya mambo ya mzee Lincoln tumevichanachana nakuwashia moto, ushauri wake unatucheleweshea maendeleo kwaio hatutaki kusikia lakini mtie moyo mwambie kuna watu wanatafuta majivu ya vipeperushi vile japo majivu yamefichwa kwa mbawa za nguvu.

Mugendi jina lako la utotoni, shina la karamu yangu limeanza kukauka wino na karatasi yangu haina tena nafasi ya kubeba ujumbe wangu,nikipata nauli nitakuja Mwitongo Butiama kukusalimia lakini sitaingia ndani nitaongea na wewe nikiwa nje nikimaliza kuyaishi maono yako nitakufata ndani.

" umoja hautufanyi tuwe matajiri lakini itafanya iwe vigumu kwa Afrika na Waafrika kupuuzwa"

IMG_20200911_131339.jpg
12654532_1256032691090562_3388564133783555438_n.jpg
 
Back
Top Bottom