Barua kutoka Bwiru Boys Sec School

Barua kutoka Bwiru Boys Sec School

Mohamed Ismail

JF-Expert Member
Joined
Mar 16, 2014
Posts
228
Reaction score
249
*BARUA*

Kwako
*Alumni wa Bwiru boys*
Salaams nyingi zikufikie popote ulipo zenye rehema na upendo juu yako. Natumai umzima wa afya na unaendelea vizuri na shughuli zako za kila siku za kulijenga taifa letu pendwa. Sina mashaka na wewe na katika utendaji wako wa kazi maana kila siku nilikuusia kuwa Forward ever.
Madhumuni ya barua ni kukutaka kukumbusha kuwa ni muda mrefu umepotezana na mimi. Ulikuwa mtoto mwema kwangu kwa kipindi ambacho nilikaa na wewe. Nilifanya kila juhudi ili uweze kutimiza ndoto yako. Ninaamini kipindi chote ambacho umekaa na mimi uliweza kujifunza vitu vingi mbali na kupata elimu lakini ulijifunza stadi nyingi za maisha. Ninajua ulipata kazi ngumu sana kuweza kuishi na ndugu zako ambao mmezaliwa na mama tofauti. Lakini yote ilikuwa ni kuwajenga muwe kitu kimoja muondoe na tofauti zenu kwa ajili ya kuijenga nchi yako na muweze kusimama peke yenu hata kama sitakuwepo. Kama unavyojua mzazi huwa anafarijika sana kuona mtoto wake anafanya vizuri. Ninakuwa na furaha sana na ninapoona unafanya vizuri na mara nyingi sifa zako huwa zinapeperushwa na mawimbi ya maji pamoja na upepo mwanana.

Nimefurahi kusikia kuwa mnataka muungane wewe na ndugu zako kwa ajili ya kunifanyia sherehe ya kutimiza miaka 100 tangu nizaliwe. Mambo ya birthday mimi sijayazoea ila najua nyinyi ni vijana wa kisasa. Kwa hili jambo mimi ninawabariki sana maana nitapata kuona hata watoto wangu ambao nilipotezana nao muda mrefu. Siku hiyo mje wote tule keki pamoja na tuimbe na kucheza kwa pamoja. Haya mambo huwa nayasikia kwa majirani zangu siku hiyo nataka nitambe kuwa mimi ni kidume na nimezaa vidume tupu. Nataka nchi ijue na ulimwengu wote ujue kuwa mimi siyo mgumba nina watoto tena ambao ni vidume kwelikweli.

Ninachokusisitiza waambie na ndugu zako mimi sikuwa na upendeleo katika malezi yenu ninaomba kila mtu awe na amani ya moyo kushiriki jambo hili. Sitaki sherehe yangu iwe chanzo cha migogoro kwenu bali sherehe hii iimarishe upendo na umoja juu yenu, na iwe mfano wa kuigwa hata mabinti wa jirani yangu nao wajifunze kutoka kwenu.Na huwa sipendi mnavyowaita mende wakati mnawataka[emoji23][emoji23].
Mimi macho yangu hayaoni siwezi kuandika nilitamani nikuambie vitu vingi lakini nimeamua nimuombe kijana wangu *Mlimwengu* aniandikie barua hii iweze kukufikia ulipo.
Niliishi na wewe katika vipindi vyote vya furaha na huzuni. Najua kuna wakati ulichoka kula ugali na maharagwe na wakati mwingine ulipata shida sana kuzoea mazingira ya hapa nyumbani. Najua vyoo vilikupa shida sana pamoja na mazingira mazuri ya kusomea lakini mwisho wa yote ulifanikiwa kuondoka salama katika mikono yangu. Nakuomba mwanangu unisaidie kuwasaidia wadogo zako maana sitaki wasome katika mazingira magumu kama uliyopitia, sasahivi kuna magonjwa mengi sipendi kuona wanangu wanateseka wakati ninaamini wewe ukiungana na ndugu zako mnaweza kuwasaidia wadogo zenu. Mimi nguvu yangu imeishia hapa ila naamini wewe una mawazo mapya ya kuwasaidia wadogo zako. Na kama unavyojua mimi sina urithi mwingine wa kuwapa zaidi ya hii elimu.
Naomba niishie hapa nisikuchoshe sana, hivi huwa bado unawasiliana na wale mabinti wa jirani yangu. Maana kipindi kile niligombana sana na wewe kutocheza na wale watoto wa jirani yangu maana sikutaka mkatishe ndoto zenu mapema. Ila sasahivi najua ushakuwa mtu mzima na unaweza kuwasiliana nao pasipokuvunja sheria za nchi hii. Nikutakie maisha mema kama hujaoa Mwenyezimungu akupatie mke mwema na kama umebahatika kuwa na familia basi naomba hata wajukuu wangu waje nao niwalee au wanisalimie wajue baba yenu ninavyoishi. Siku zote nyumbani ni nyumbani ni muhimu wajue chimbuko la baba yao.
Nikutakie kazi njema na usisahau kuwapa ujumbe ndugu zako utakapopata ujumbe wangu.
Mimi wako
*Bwiru Boys Technical secondary School*
Barua hii imeandikwa na
*Mlimwengu*
 
Back
Top Bottom