Baregu afichua siri nzito Tume ya Katiba

Magazetini

JF-Expert Member
Aug 16, 2014
588
1,698
baregu.jpg

Aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu


Aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu, ametoboa siri kuwa Mwenyekiti wa tume hiyo Jaji Joseph Warioba alikuwa na msimamo wa serikali mbili, kabla ya tume kuja na rasimu yenye muundo wa muungano wa serikali tatu uliotokana na maoni ya wananchi walio wengi.

Baregu alitoboa siri hiyo wakati akizungumza na NIPASHE katika mahojiano maalum yaliyofanyika nyumbani kwake mwanzoni mwa wiki hii. Alikuwa akijibu moja ya maswali aliyoulizwa kuhusiana na namna wao (tume) walivyoondosha tofauti za kimtazamo miongoni mwa wajumbe na kuandaa rasimu iliyokubaliwa na wajumbe wote; tofauti na wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba ambayo walitofautiana sana kuhusiana na suala la muundo wa muungano na mwishowe, wajumbe wengi wa upinzani wakasusia vikao kupitia mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kuwaachia wenzao wanaoundwa na wafuasi wengi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuendelea na kazi hiyo.

Wajumbe wanaounda Ukawa ambao wengi ni kutoka vyama vikuu vya upinzani nchini vya NCCR-Mageuzi, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Wananchi (CUF) walisusia vikao vya Bunge la Katiba kutokana na madai yao kuwa rasimu iliyoandaliwa na tume iliyoongozwa na Warioba kwa kuzingatia maoni ya wananchi ilibadilishwa kwa maslahi ya CCM. Ukawa walikuwa wakitetea rasimu ya Warioba iliyopendekeza muundo wa muungano wa serikali tatu huku wajumbe wengi wa CCM wakisisitiza kuwa na muundo wa muungano wa serikali mbili lakini ulioboreshwa.

Akieleza zaidi, Baregu alisema kuwa kwa ujumla, tume ilijigawa kwenye kamati ndogo tatu wakati wa kuanza kujadili mapendekezo, ambazo ni kamati ya mihimili ya utawala (bunge, serikali na mahakama), kamati ya iliyokuwa ikishughulikia misingi na maadili ya taifa na kamati ya tatu ndiyo iliyokuwa ikishughulikia masuala ya muungano.

"Labda niwaeleze tu, hiyo kamati ya muungano tuliipa jina kama kundi la kifo... na ninalitaja kundi hili kwa masikitiko kwa sababu mmoja wetu, Dk. Mvungi alifariki kweli," alisema.

Prof. Baregu alisema kundi la kifo lilikuwa la watu wenye misimamo kuanzia wa serikali moja, mbili, tatu na wengine waliokuwa na mawazo ya kuwa na muungano wa mkataba.

"Akina nanihii hawa... akina Warioba, akina Butiku, Jaji August... walianza na msimamo wa serikali mbili. Mimi siku nyingi ni mtu wa serikali moja. Wakawapo watu wa serikali tatu, including (akiwamo) Dk. Mvungi. Na kundi la nne la watu wenye msimamo wa serikali ya mkataba," alisema.

Alisema pamoja na minyukano iliyojitokeza kutokana na misimamo hiyo binafsi ya wajumbe, bado waliweza kusimama imara na kuzishinda nafsi zao kutokana na mawazo ya wananchi waliyoyapata wakati wakikusanya maoni katika maeneo mbalimbali nchini, chini ya uongozi wa mwenyekiti wao (Warioba).

Alisema kuwa awali, mwenyekiti wao (Warioba) alitoa nafasi kwa kila mjumbe kwenye suala la muungano kuzungumza na kutoa mchango wake.

"Ninakumbuka kwenye issue hii ya muungano, kila mjumbe ilibidi azungumze. Na mwenyekiti ali-insist kwamba kila mmoja wetu ni lazima achangie, na tukalizungumza kwa karibu wiki nzima," alisema.

Prof. Baregu alisema pamoja na kila mjumbe kuzungumza, pia waliangalia maoni waliyokusanya kutoka kwa wananchi na mwisho wa siku wakaja na maamuzi ya pamoja, ambayo yaliwafanya kuchukua msimamo wa pamoja pia.

Alisema hawakumuacha mjumbe yeyote nyuma akiwa bado hajaridhika kwa hoja na maoni waliyokusanya na kwamba, pale ilipotokea hivyo, walianza naye kwenye kikao kilichofuata hadi kuhakikisha kwamba mhusiaka ameridhika.

"Na ndiyo maana sasa hivi ukizungumza na wajumbe wote, sijasikia hata mmoja ambaye amebadilisha mawazo, ama... au amesema kwamba alirubuniwa kwenye tume au labda kwamba Jaji Warioba alifanya maamuzi ya ubabe," alisema.

Alisema kutokana na namna walivyoendesha mambo yao kwa uwazi na kufikia maamuzi ambayo wote waliyaafiki kikamilifu kuwa yamezingatia kwa usahihi matakwa ya wananchi, ndiyo maana bado wana mshikamano mzuri hadi sasa na wameamua kwenda kuitetea rasimu ya tume kwa wananchi.

Amesisitiza kuwa wajumbe wa tume hiyo wamejipanga kuhakikisha wanawaelimisha wananchi kuhusu mapendekezo yaliyokuwa kwenye rasimu hiyo.

Alisema walipokuwa kwenye Tume walifanyakazi kwa bidii, weledi, nidhamu na kujenga maridhiano ndani ya jamii na ndani ya tume.

"Tuliwasikiliza wananchi wanataka nini na kuzingatia maoni ya Watanzania, na lengo la tume lilikuwa ni kupata katiba yenye maoni ya wananchi," alisema.


KATIBA ILIYOPENDEKEZWA
Alisema sasa hivi, kwenye Katiba iliyopendekezwa, kuna mambo mengi ya msingi yamenyofolewa; kama mambo ya maadili, uwajibikaji, kumwajibisha mbunge, ukomo wa ubunge, madaraka ya rais na mawaziri kutokuwa wabunge; mambo ambayo yalipendekezwa na wananchi wengi.

Prof. Baregu alisema njia pekee ya kunusuru mchakato mzima wa katiba ni kukubali kwamba tumekwama na kukubali kusahihisha makosa badala ya kuburuza mchakato huo bila maridhiano.

Katiba iliyopendekezwa ilikabidhiwa juzi mjini Dodoma kwa marais, Jakaya Kikwete wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Dk. Ali Mohamed Shein wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

"Sisi ndani ya Tume tulijenga kwanza maridhiano ndiyo maana tuliweza kutoa rasimu ambayo sote tulikubaliana," alisema
Prof. Baregu alisema: "Kwa hali hii, ilipaswa tuwe na ujasiri wa kupumua kwanza, tukaulizana na tukakubali kwamba tumekwama kwa malengo tuliyokuwa tumejiwekea... sasa hivi ni kama mtu umepotea njia lakini unasema twende tu."

Aliongeza kuwa: "Tulikuwa na lengo, tulikuwa na ramani kwa hiyo kama tungekuwa na ujasiri kama taifa tukasema ngoja tujiulize hapa tufanye nini ili tuweze kutoka hapa, mengi tungeweza kubadilisha." Alisema mchakato umekwama baada ya kutawaliwa na wanasiasa ambao hawawezi kupitisha mapendekezo ambayo yanapingana na maslahi yao.

"Ni vyema kama tungekubali kusema hapa tumekosea, tuunde upya Bunge la Katiba, na kukubali kwamba tumekosea sana... na siyo serikali tu, lakini sote kama taifa."

Alisema. "Nimekuwa nafikiri hivi... ni kama mama mwenye mimba anayepata abortion (mimba kuharibika). Anajisikiaje?" alisema Baregu.

Alisema kwa hali ilivyopelekwa, anahisi kuwa na hali kama hiyo ya mama aliyeharibikiwa na mimba yake, kwamba amekuwa kwenye timu iliyofuatilia watu karibu mwaka mmoja na nusu kutunga katiba, lakini inaishia kusakamwa.

Alisema tume imefanya kazi kwa uadilifu, weledi, tena usiku na mchana, siku saba kwa wiki, saa 24 kwa zaidi ya mwaka, lakini kazi waliyofanya kwa uadilifu na umakini mkubwa ni kama imekuwa bure tu.


UCHAMBUZI WA KINA
Baregu alisema kuwa baada ya uchambuzi wa kina na tafiti na taarifa za tume mbalimbali, wajumbe walibaini kwamba Muungano ni yatima na hauonekani kwa kuwa hakuna mamlaka inayosimamia maslahi ya Muungano.

Alisema ili kuondoa kero za Muungano, njia pekee ni kuweka mamlaka mahsusi ili kuuimarisha Muungano.

Alisema inashangaza kuona kwamba wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba (BMK), waliishia kuzungumzia gharama za serikali tatu badala ya kueleza ubaya au udhaifu wa serikali hizo na uzuri wa serikali mbili kwa kina.

"Mimi utabiri wangu, huko tunakokwenda, ama tutaendelea kutumia nguvu zaidi kuwaweka Zanzibar kwenye Muungano ama vinginevyo Muungano utavunjika."

Alisema wananchi wa pande zote za Muungano walitoa mapendekezo yao ambayo tume iliyachambua kwa kina na kutoa fursa kwa wajumbe wote kuchangia jambo hilo.

Akizungumzia tuhuma nyingi walizorushiwa na wajumbe wa bunge maalumu la katiba kuwa rasimu waliyotoa siyo maoni ya wananchi, bali maoni ya kina Warioba, alisema: "Kwa hili, mimi nasema wasitoe tuhuma za kitoto. Kama wana ushahidi, tuundiwe tume ya kimahakama ichunguze mwenendo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kimaadili, kiweledi, kiuadilifu na kwa kila aina."

Alisema kama tume hiyo itakuja na majibu kwamba tume ilifanya kazi yake chini ya kiwango, basi wao wawajibishwe na pia rasimu inaweza kubadilishwa.

Alisema siyo busara kuendelea kukosoa kazi ya tume na badala yake, kama ikionekana kwamba haikuwa na uaminifu wala uadilifu; ni vyema jambo hilo likachunguzwa ili kubaini kama ilifanya kazi kinyume cha sheria na pia kinyume cha hadidu za rejea.

Alikikosoa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kuvuruga mchakato wa Katiba na kueleza kuwa Katiba ni suala la maridhiano zaidi na siyo wingi au uchache kwa kuwa hata wananchi walio wachache, wanapaswa kusikilizwa.

*Usikose kusoma mahojiano zaidi na Profesa Baregu Jumatatu.

CHANZO: NIPASHE
 
Mmegonga mihuri mizuri mioyoni mwetu hatutakata tamaa ya kuamini kuwa ipo siku mambo mazuri tunayohitaji kwa taifa hili yatapatikana, kwakuwa bado mpo watetezi wa wanyonge na wapenda haki. Mungu awaepushe na kila ovu kutoka kwa wapinga ukweli na walafi wa madaraka. R.I.P DR. MVUNGI.
 
Duh!!! Dr. Mvungi(R.I.P) muumini wa serikali tatu na CCM waumini wa Serikali mbili(2) ili kushinda ameuliwa kwa kuwa tu alikuwa muumini wa Serikali 3, tutakukumbuka daima Dr. Pumzika kwa amani waliokutoa roho akiwepo na KOVA na sinema zake ipo siku watakukuta kwenye ufalme wa mbinguni na wao wakiingia motoni.
 
Inashangaza kazi iliyofanywa kwa weledi mkubwa na kutumia rasilimali kubwa za walipa kodi wa nchi hii, kazi hiyo njema kwa mustabali wa Taifa, mwishoni inakuja kuonekana 'takataka' na wahafidhina wa CCM, ambao ndiyo wanajiona kama ndiyo wamekabidhiwa hati miliki na Mungu wetu, ya kutawala nchi yetu hadi mwisho wa dunia!
 
Duh!!! Dr. Mvungi(R.I.P) muumini wa serikali tatu na CCM waumini wa Serikali mbili(2) ili kushinda ameuliwa kwa kuwa tu alikuwa muumini wa Serikali 3, tutakukumbuka daima Dr. Pumzika kwa amani waliokutoa roho akiwepo na KOVA na sinema zake ipo siku watakukuta kwenye ufalme wa mbinguni na wao wakiingia motoni.
Hii post imenigusa sana !
 
bora muungano kuvunjika kuliko kua na muungano geresha kama tume ilivyopendekeza. ingekua kupoteza muda na kuwapa urahisi maadui wa muungano. jambo muhimu ni kwamba wasiotaka muungano ni wachache, kwa nini kuwapa jukwaa kufanikisha azma yao?
 
Daima tutasonga mbele kurudi nyuma mwiko, tupo pamoja wazee wetu kwa kazi nzuri mlioifanya.R.I.P Dr Mvungi.
 
Unajua mishahara ya viongozi wengi hasa wanaofanya maamuzi (wanasiasa) haikatwi kodi na wananchi ndio walipa kodi wakuu. Hata pale kodi zinapopungua kutokana na matumizi ya anasa zilizopindukia za serikali yetu basi wanakopa kwa wafadhili ili wajilipe posho na mahitaji mengine lakini walipa deni wakubwa ni wananchi. Na hawa ndio wazalishaji wakuu.

Sasa kwenye suala hili katiba inasema wazi kuwa madaraka ya nchi yanatoka kwa wananchi.
Cha ajabu wananchi wametoa maoni ya jinsi wanayotaka nchi yao iendeshwe lakini hawa watu wachache wanaotunzwa na wananchi wanasema kuwa wao ndio wenye mawazo sahihi na sio wananchi.

Jaji Warioba kakubali kuachana na misimamo yake na kuwasikiliza wananchi wanachotaka lakini Sitta/Chenge na JK wanasema watasikilizana kama viongozi wenye jeshi, dola na hata theruthi mbili isipopatikana ITATOSHELEZWA.

Ninachoona sasa ni kuwa idadi ya Watanzania tusioelewa jinsi nchi inavyoendeshwa itakuwa imeelewa kwa mchakato huu.
 
Duh!!! Dr. Mvungi(R.I.P) muumini wa serikali tatu na CCM waumini wa Serikali mbili(2) ili kushinda ameuliwa kwa kuwa tu alikuwa muumini wa Serikali 3, tutakukumbuka daima Dr. Pumzika kwa amani waliokutoa roho akiwepo na KOVA na sinema zake ipo siku watakukuta kwenye ufalme wa mbinguni na wao wakiingia motoni.

Natamani kujua binti wa Dr Mvungi ambaye alikuwa Mbunge wa BMK alipiga kura ya Ndio au Hapana....sidhani kama alipiga Hapana.
 
Kwa hakika majina yenu yameandikwa kwa wino wa dhahabu mmeonyesha nn maana ya uzalendo na maslahi mapana ya nchi yetu kwa ujumla.mungu atawalipa ktk kila jema mliloitendea tz na watu wake
 
watunga katiba ni akina Hawa Ghasia, Hawa Ghasia anaponda elimu, alipendekeza wanaogombea nafasi ya uongozi si lazima wawe na elimu zaidi ya kujua kusoma na kuandika, hapo kuna katiba kweli?
 
Mh, hii ni hatari sana, Mtu unakuwa kwenye
"kundi la kifo" then unauwawa kweli!! Watu hatari sana hawa

Hivi Limit ya taifa letu kukaa na siri hatari kama hizi ni miaka mingapi? Ninaham ya kujua kwanini walimuua Mvungi? (rip)

BACK TANGANYIKA
 
Natamani kujua binti wa Dr Mvungi ambaye alikuwa Mbunge wa BMK alipiga kura ya Ndio au Hapana....sidhani kama alipiga Hapana.

Mara nyingi hawa watoto uwekwa katika mazingira ya kusahau walichofanyiwa wazazi wao, mifano hai ni kwa Adam malima, Godfrey Mgimwa kwani hawakumbuki kabisa kuwa vifo vya wazazi wao vimefanywa na hao hao wanaoonyesha kuwa kwa sasa wananwapenda sana.
 
Back
Top Bottom