singidadodoma
JF-Expert Member
- Nov 11, 2013
- 4,394
- 1,536
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeikabidhi Kampuni ya Udalali ya Yono kuwafilisi wateja 24 wanaodaiwa kodi ya Sh bilioni 18.95 baada ya kutorosha makontena ya mizigo yao kwenye Bandari Kavu (ICD) ya Azam mwishoni mwa mwaka jana.
Majina ya wadaiwa hayo yametolewa jana kwenye vyombo mbalimbali vya habari, na Kampuni hiyo ya Udalali ya Yono baada ya TRA kuwakabidhi kazi ya kuwafilisi kutokana na kushindwa kutekeleza wajibu wao baada ya kupewa muda wa kulipa kodi.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Yono Kevela alisema wamepewa amri na TRA ya kisheria ya kukamata mali za wadaiwa na kuwafilisi ili kulipia kodi wanazodaiwa.
Kevela alisema baada ya kupata kazi hiyo, wao wameona busara kuwatangaza kwenye vyombo vya habari na kuwapa siku 14 kulipa kodi wanazodaiwa na kwamba baada ya muda huo kumalizika, hatua za kukamata mali za wadaiwa hao zitaanza na kuwafilisi.
“Tumekabidhiwa wadaiwa 24 na TRA, hawa wamekwepa kodi kwa kutorosha kontena katika Bandari Kavu ya Azam mwishoni mwa mwaka jana, sasa walipewa muda wa kulipa ila wamekaidi, sasa kazi tumepewa sisi na tutawafilisi mali zao zote ili kulipa deni hilo,” alifafanua Kevela.
Majina ya wadaiwa hai na kiasi cha fedha wanachodaiwa kwenye mabano ni Zulea Abas Ali (16,760577.24), Omary Hussein Badawy (21,346,615.40), Libas Fashion (26,593,245.78), Said Ahmed Said (28,249,352.50), Strauss International (45,393,769.95) na Farid Abdallah Salum (52,185, 614.97).
Wengine ni Ally Awes Hamdani (55,485,904.07), Nasir Saleh Mazrui (60,105,873.77), Simbo Yona Kimaro (64,221,009.10), Zuleha Abbas Alli (75,508,551.88), Issa Ali Salim (94,543,161.96), Ally Masoud Dama (102,586,719.22), Juma Kassem Abdul (130,182,395.12), Salum Link Tyres (233,447,913.31), Tybat Trading Co. Ltd (448,690,271.90), IPS Roofing Co. Ltd (966,723,692.10) na Tifo Global Trading Co Ltd (1,573,300,644.58).
Pia wamo Lotai Steel Tanzania Ltd (5,476,475,738.19), Tuff Tyres General Co Ltd (7,435,254,537.03), Swalehe Mohamed Swalehe (34,687,165.00), Rushwheel Tyre General Co Ltd, (1,802,988,679.20), Said Ahmad Hamdan (68,362,558.31), Ahmed Saleh Tawred (59,237,578.40) na Farida Abdullah Salem (75,334,871. 85).
Kevela alisema wadaiwa hao wanapaswa kulipa madeni yao ndani ya siku 14 walizopewa na kwamba iwapo watashindwa kutekeleza amri hiyo, kampuni hiyo itaanza kazi ya kukamata mali zao na kuwafilisi.
Alisema ili kurahisisha kazi hiyo, Kampuni ya Said Salum Bakhresa (SSB) ambayo ndiyo mmiliki wa Bandari Kavu ya Azam pamoja na Kampuni ya Regional Cargo Services wanapaswa kutoa ushirikiano kuhakikisha wadaiwa hao wanalipa kodi walizokwepa.
“Kampuni hizo zinahusishwa na kutoroshwa kwa kontena 329 zilizokuwa Azam ICD, sasa ni vyema watoe ushirikiano ili wadaiwa walipe fedha za serikali,” alifafanua Kevela. Alisema baada ya muda waliotoa kumalizika, wahusika watapaswa kulipa na gharama za ziada ambazo ni pamoja na faini na usumbufu wa kuwatafuta.
Desemba 12, mwaka jana, aliyekuwa Kaimu Kamishna wa TRA, Dk Philip Mpango aliwaambia waandishi wa habari kuwa kampuni 15 kati ya 43 zilizokwepa kodi baada ya kutorosha kontena 329 katika ICD ya Azam, zimelipa.
Dk Mpango alisema Desemba 12, mwaka jana ndiyo ilikuwa siku ya mwisho aliyotoa Rais John Magufuli ya siku saba kwa wakwepa kodi hao 43 kulipa wenyewe kwa hiari, vinginevyo sheria zitachukua mkondo wake. Kutokana na kauli hiyo ya Rais Magufuli, wadaiwa 15 walijitokeza na kulipa na waliobaki hawakujitokeza kulipa.