BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), limekanusha kauli ya Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum ya kukosoa utaratibu wa kazi za Chama Cha Mapinduzi CCM), unaofanywa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.
Hayo yamo katika taarifa ya baraza hilo, iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam. Taarifa hiyo ilitolewa na Mufti wa Tanzania, Issa Shaaban Simba.
"BAKWATA inapenda kuutangazia umma wa Tanzania kuwa haina uhusiano wowote na kauli ya Shehe Alhad Mussa Salum dhidi ya Kinana. Kwa mujibu wa vyombo vya habari, Kinana ameonywa na Shehe Alhad aache tabia ya kuwakatisha tamaa viongozi wa serikali, akiwemo Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu kwa kubeza kauli zake," ilisema taarifa.
Taarifa hiyo ilisisitiza: "Kauli ya Shehe Alhad Mussa Salum imevuka mipaka na taratibu zetu kama BAKWATA kwa kujiingiza katika shughuli za ndani za taasisi nyingine kwa kuwaelekeza namna ya kufanya kazi zao. BAKWATA haijamtuma kufanya hivyo".
Mufti katika taarifa hiyo alisema "BAKWATA, kama ilivyo CCM, kisheria ni taasisi na hapakuwa na sababu ya kumkashifu Mheshimiwa Kinana wakati anafanya kazi za chama chake. Kila taasisi iachwe ifanye kazi zake kufuatana na malengo na taratibu zake ili mradi haihatarishi amani na utulivu wa nchi yetu."
"Kwa niaba ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania, natoa pole kwa Mheshimiwa Kinana na Chama chake cha CCM kwa ujumla kwa kadhia hii", alisema Mufti Simba.
CHANZO: Habari Leo