Bado tunamkumbuka carlos cardoso

Mtambuzi

Platinum Member
Oct 29, 2008
8,810
15,393
Hii habari nimeona niiweke hapa, ili kuwakumbusha waandishi wetu kuwa kazi ya kufuatilia kashfa ya ufisadi sio kazi nyepesi.
Hebu soma habari hii ya kusikitisha kuhusiana na Mwandishi huyu jasiri alivyouwawa nchini Msumbiji, mwaka 2000.

Ilikuwa ni siku ya jumatano Novemba 22, 2000, Mwandishi mahiri wa habari za kiuchunguzi nchini Msumbiji, Carlos Cardoso aliuwawa katika shambulio la kushitukiza katikati ya viunga vya jiji la Maputo.

Akiwa anaendeshwa na Dereva wake aitwae Carlos Manyate, mara ghafla gari lao likazuiwa kwa mbele na magari mawili na watu wawili wakashuka kwa haraka huku wakiwa na bunduki zao aina ya AK 47 wakalifyatulia gari lao risasi kadhaa na kumuua Carlos Cardoso palepale na kumjeruhi vibaya Dereva wake Carlos Manyate, kisha kutokomea kusikojulikana.

Mauaji hayo ya Cardoso ambae alikuwa ni mzungu raia wa msumbiji mwenye asili ya Ureno yalitafsiriwa na kamati ya kutetea waandishi wa habari nchini msumbiji {Committee to Protect Journalists (CPJ) pamoja na wananchi kwa ujumla kama yalikuwa ni ya kupangwa kwa sababu siku chache zilizopita Cardoso aligeuka kuwa mwiba mchungu kwa mafisadi wa nchini humo ambao wengi wao walikuwa ni wafanyabiashara maarufu pamoja na viongozi waandamizi wa chama tawala cha FRELIMO.

Akiwa ni mmiliki wa kampuni yake binafsi inayomiliki magazeti ya Media Fax na Gazeti lingine linalojulikana kwa jina la "Metical" Linaloandika habari za kibiashara, Cardoso aliibuka na kashfa ya upotevu wa Dola milioni 14 za Kimarekani katika Benki ya biashara ya Msumbiji {Commercial Bank of Mozambique (CBM)} inayomilikiwa na serikali hapo mnamo mwaka 1996.
Miongoni mwa watuhumiwa wakuu katika kashfa hiyo walikuwa ni familia ya wafanyabiashara maarufu nchini humo Abdul Satar.

Tangu kashfa hiyo ilipoanza kuandikwa huku Cardoso akisisitiza kwamba Gazeti lake linaendelea na uchunguzi wa kashfa hiyo, wadau mbalimbali nchini humo waliitaka serikali iwafanyie uchunguzi watu wote waliotajwa katika taarifa hiyo ya Cardoso akiwemo mtoto wa Rais Joaquim Chissano, Nyimpine Chissano ambae alikuwa akiendesha biashara ya Majumba (Real Estate), kampuni ya utalii pamoja na kampuni nyingine ya ushauri wa kifedha inayoendeshwa kwa pamoja na mfanyabiashara mwingine Octavio Muthemba ambayo inasemekana iliingia mkataba usio na faida na benki ya Austral inayoendeshwa na serikali kwa gharama ya dola 3000 za Kimarekani kwa mwezi. Muthemba aliwahi kuwa waziri wa viwanda nchini Msumbiji wakati Fulani.

Mnamo April 2001 Benki ya Austral ilichukuliwa na kuendeshwa na Benki kuu ya Msumbiji.
Ili kuokoa jahazi iliteuliwa bodi ya kuindesha Benki hiyo iliyokuwa chini ya Mkuu wa wasimamizi wa Benki zilizoko chini ya Benki kuu, Antonio Siba-Siba Macuacua.
Hatua ya kwanza kuchukuliwa na Macuacua ni kusitisha mkataba kati ya Benki hiyo na kampuni ya Nyimpine Chissano.
Hatua hiyo ilimgharimu Macuacua maisha yake, kwani mnamo August 11, 2001 Antonio Siba-Siba Macuacua aliuwawa akiwa ofisini katika makao makuu ya Benki hiyo ya Austral jijini Maputo; na muuaji wake hakupata kufahamika.
Lakini Baadhi ya vyombo vya habari vilidai kwamba mmoja waliokuwa walinzi wa Raisi Joaquim Chissano ndie aliyehusika na mauaji hayo.

Hivyo hata mauaji haya ya Cardoso yalikuwa ni mtiririko wa kuficha ukweli na yalitafsiriwa na kamati ya kuwatetea waandishi wa habari nchini msumbiji pamoja na wadau mbalimbali kama ni ujumbe mahsusi kwa waandishi wa habari na wadau wengine kuwa hiyo ndio gharama ya kufuatilia mambo ya wakubwa.

Historia inonyesha kwamba Carlos Cardoso alizaliwa katika mji wa Beira mnamo mwaka 1952.
Elimu yake ya sekondari aliipata nchini Afrika ya Kusini na baadae alijiunga na chuo kikuu cha Witwatersrand nchini humo.
Cardoso alikuwa na historia ya kuwa mwanaharakati tangu akiwa chuo kikuu nchini Afrika ya Kusini. Baaada ya kumaliza masomo yake nchini Afrika ya Kusini alirejea nchini Msumbiji mnamo mwaka 1974, wakati huo Msumbiji ilikuwa ndio imejipatia uhuru wake.

Mnamo mwaka 1976 Cardoso alijiunga na Gazeti la serikali linaliojulukana kwa jina la "Tempo"
Mwaka 1979 alihamishiwa katika kituo cha Redio ya serikali na kupangiwa kuendesha kipindi cha muziki. Alikaa kwa takribani mwaka mmoja katika kituo hicho kabla ya kuhamishiwa katika shirika la habari la msumbiji na kuwa mhariri wa shirika hilo mwaka 1980.
Miaka miwili baadae yaani mwaka 1982 Cardoso alitupwa jela kwa kile kilichosemekana kama maagizo ya Raisi wa wakati huo Hayati Samora Machel, baada ya kutofurahishwa kwake na makala yake aliyoitoa kuhusiana na kukua kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya serikali na waasi wa RENAMO waliokuwa wakiongozwa na Dlakhama.
Hata hivyo Cardoso aliachiwa baada ya kukaa jela kwa siku sita na kurudi katika kazi yake ya uhariri kwenye shirika la habari la nchini humo.
Baadae aliteuliwa na Rais wa wakati huo Hayati Samora Machel kuwa mmojawapo wa washauri wake.
Kutokana na mashinikizo kutoka juu na kile alichokiona kama mazingira magumu ya uandishi wa habari, mnamo mkwaka 1989 Cardoso aliamua kuachana na taaluma hiyo na kuamua kufanya kazi za ufundi rangi.

Miaka mitatu baadae alirudi katika taaluma yake ya uandishi wa habari na kwa kushirikiana na waandishi wenzie wa habari walianzisha shirika lao binafsi la habari lililojulikana kwa jina la Media Coop.
Cardoso hakuridhishwa na muenendo wa ushirika wao hivyo aliamua kujitoa kwa kile alichodai mwenyewe kwamba shirika lao limepoteza muelekeo.

Hivyo mnamo mwaka 1997 alianzisha Kampuni yake mwenyewe iliyokuwa ikimiliki magazeti ya Media Fax gazeti litokalo kila siku pamoja na gazeti lingine alilolipa jina la "Metical", ikiwa na maana ya pesa inayotumika nchini msumbiji ambalo lilikuwa linatoka kila wiki.
Gazeti hilo lilikuwa likiandika habari za kibiashara, ambapo lilikuwa likiwasaidia wafanyabiashara wadogo wadogo ili kuwawezesha kupambana na mabadiliko yaliyoikumba dunia ya soko huria.

Pia gazeti hilo lilijikita kwenye maswala ya rushwa kwa upande wa wafanyabiashara wakubwa pamoja na wanasiasa wasio waaminifu, ndipo mwaka 2000 lilipoibuka na kashfa ya benki ya biashara ya msumbiji ambayo ilikuwa ikiwahusisha wafanyabiashara wakubwa pamoja na wanasiasa nchini humo.
Mnamo machi 2001, ikiwa ni takribani miezi minne tangu mauaji ya Carlos Cardoso yatokee, watu sita walikamatwa kwa kuhusika na mauaji hayo.

Watu hao walikuwa si wengine bali Mfanyabiashara maarufu Ayob Abdul Satar na meneja wa zamani wa Benki ya Biashara ya Msumbiji (BCM) ambayo ndiyo iliyohusishwa na kashfa hiyo, Vicente Ramaya.

Wengine walikuwa ni kaka yake Ayob Satar, Momade Assife Abdul Satar ambaye alikuwa akijulikana kwa jina la utani la "Nini" , Carlos Rachid Cassamo, Manuel Fernandes pamoja na Antonio Dos Santos Junior maarufu kwa jina la utani la "Anibalzinho" ambae ndiye aliyekuwa akutuhumiwa kuwa kiongozi wa genge la wauaji na aliyehusika na kumuua Cardoso.

Mnamo Septemba 1, 2002 Anibalzinho alitoroka kutoka katika jela yenye ulinzi mkali ikiwa ni miezi michache kabla ya watuhumiwa kufikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka.
Baadhi ya askari magereza walikiri kwamba mamlaka ya magereza ililazimika kumuachia Anibalzinho atoroke kutokana na shinikizo kutoka ngazi za juu.

Nae mama yake na Anibalzinho, Teresinha Mendonca akiongea na Gazeti la kila siku la la nchi hiyo, "Noticias" alidai kwamba mwanae yuko nchini uingereza kwa ndugu zake, na amekuwa akiwasiliana nae.

Mama Mendonca aliendelea kudai kwamba mwanae huyo yuko tayari kurejea nchini Msumbiji na kusema ukweli wote kuhusiana na mauaji ya Cardoso, ilimradi mamlaka ya Msumbiji imhakikishie usalama wake.

Wahusika wakuu katika kesi hii mtu na kaka yake wanaotoka katika familia moja Ayob na Momade Assife Satar "Nini" pamoja na Vicente Ramaya walikuwa bado wanachunguzwa kuhusiana na ufisadi huo lakini ukweli ni kwamba tuhuma za wahusika wa ufisadi huo hazikuwahi kufikishwa mahakamani na hiyo ilitokana na kile kilichosemekana kama vitendo vya rushwa vilivyokithiri katika ofisi ya mwanasheria wa serikali ya msumbiji ambapo pia Cardoso alikuwa akiichunguza ofisi hiyo.

Ili kukabiliana na tuhuma hizo ilibidi ofisi hiyo itoe hati ya kukamatwa kwa mmoja wa waendesha mashtaka wake aitwae Diamantino Dos Santos ambae ndie aliyekuwa mwendesha mashtaka katika kesi hiyo lakini alitoweka katika mazingira ya kutatanisha na hakujulikana mahali alipo.

Hata hiyo pamoja na Anibalzinho kutoroka, mnamo Novemba 18, 2002 shauri hilo Lilianza kusikilizwa bila ya yeye kuwepo. Kesi hiyo ilisikilizwa nje ya jela waliyohifadhiwa watuhumiwa hao tangu Machi 2001 iliyoko nje ya jiji la Maputo, ambapo kulikuwa kumejengwa turubai kubwa na kuwekwa viti zaidi ya 500 ili kuwawezesha wafuatiliaji wa kesi hiyo kukaa kwa nafasi kwani kesi hiyo ilikuwa imewavutia watu wengi wakiwemo waandishi wa habari wa kimataifa. Pia hali ya usalama katika eneo hilo iliimarishwa kwa kiasi kikubwa.

Awali katika maelezo yao Momade Assif Abdul satar na kaka yake Ayob Abdul Satar walikiri kwamba mpango mzima wa kumuua Cardoso ulipangwa katika Hoteli moja maarufu iliyoko katika viunga vya jiji la Maputo na mhusika mkuu katika mpango mzima alikuwa ni Nyimpine Chissano na kwamba wao walikuwa ni watu wa kati tu (Middlemen).

Watuhumiwa hao pia walibainisha kwamba Nyimpine aliwalipa wauaji kwa njia ya hundi ambapo aliandika hundi tofauti tofauti nne ambazo thamani yake haikutajwa pale mahakamani kama malipo ya kumuuwa Cardoso.
Hata hivyo mamlaka zinazohusika zilisita kumuunganisha Nyimpine Chissano katika kesi ile kwa maelezo kwamba tuhuma zilizotolewa dhidi yake wanazifanyia kazi, lakini hata hivyo walimpokonya Nyimpine hati yake ya kusafiria na kumzuia asitoke nje ya Msumbiji mpaka shauri lile litakapokwisha.

Lakini pamoja na Nyimpine kunyang'anywa hati yake ya kusafiria kuna wakati aliripotiwa kuonekana jijini Lisbon nchini Ureno mwezi Disemba mwanka 2002.

Maofisa wa mahakama nchini humo walikiri kumrejeshea Nyimpine hati yake ya kusafiria baada ya kupokea amri kutoka ngazi za juu, bila ya kufafanua kuwa ni ngazi gani ya juu iliyohusika na amri hiyo.

Nae aliyekuwa msemaji wa Rais mstaafu Joaquim Chissano, Antonio Matonse aliwaambia waandishi wa habari kuwa Rais mstaafu (Joaquim Chissano) angependa shauri hilo liendelee kama kawaida na sheria zifuate mkondo wake hata kama mwanae anatajwa kuhusika na mauaji hayo.

Kutokana na Nyimpine kutajwa tajwa Na vyombo mbalimbali vya habari Duniani kwamba Kwa njia moja ama nyingine anahusika Na mauaji ya Cardoso, ilibidi mamlaka ya sheria nchini Msumbiji itoe tamko.

Hivyo mnamo Novemba 3, 2002 mwanasheria wan chi hiyo Joaquim Luis Madeira akinukuliwa na gazeti la Media Fax lililokuwa likimilikiwa Na kampuni ya hayati Cardoso, alisema kwambaNyimpine anachunguzwa kuhusiana na mauaji ya Cardoso.

Lakini alivionya vyombo vya habari kutomtuhumu Nyimpine moja kwa moja kwamba alihusika na mauaji hayo.
Kwa maneno yake mwenyewe Mwanasheria huyo alisema "Mtuhumiwa wa uhalifu hawezi kutiwa hatiani kwa kuhisiwa bali kwa kuthibitishwa, tunachohitaji ni ukweli wa tuhuma hizo kuthibitishwa na mahakama, na kama Nyimpine Chissano alihusika katika mauaji ya Cardoso atahukumiwa kwa mujibu wa sheria , kwani hakuna mtu yeyote aliye juu ya sheria"
Gazeti la Media Fax lilikuwa ni la kwanza kuandika habari hiyo kwa undani katika makala ambayo ilimtuhumu Nyimpine moja kwa moja kwamba hata kama hakuhusika na mauaji ya Cardoso lakini amenufaika nayo.

Baada ya kutoka habari hiyo waandishi waandamizi wa gazeti hilo Marcelo Mosse, Kok Nam na Fernado Lima walipata tishio la kuuwawa kutoka kwa watu wasiojulikana.
Nae Nyimpine alikuja juu kutokana na tuhuma hizo ambazo hata hivyo zilikuwa ahzijathibitishwa mahakamani, hivyo haraka sana Nyimpine alifungua kesi dhidi ya gazeti la Media Fax na baada ya shauri hilo kusikilizwa gazeti hilo lilipatikana hatia na kuamriwa kumlipa Nyimpine Chissano Dola za Kimarekani 70,000, ambapo kutokana na faini hiyo kuwa kubwa ofisi za gazeti hilo zilifungwa kutoakan ana kufilisika.

Kesi hiyo ambayo ilikuwa ikisikilizwa na Jaji maarufu nchini Msumbiji Augusto Paulino iliendelea kwa watuhumiwa kutoa utetezi wao.
Akitoa maelezo yake Momade Assife Abdul Satar aliendelea kubainisha pale mahakamani kwamba Nyimpine Chissano alikwenda nyumbani kwake mwanzoni mwa Novemba 2000, kwa ajili ya kukutana na muuaji wa kukodiwa Anibalzinho, ambapo alimlipa kwa hundi ili atekeleze mauaji ya Cardoso ambayo yalikuja kufanyika Novemba 22, 2000.
Mtuhumiwa huyo aliwasilisha hundi nne zilizosainiwa na Nyimpine kama ushahidi kwa Jaji Augusto Paulino.

Watuhumiwa wengine wawili Manuel Fernandes na Carlos Rachid Cassamo walikiri kuhusika na mauaji ya Cardoso lakini walikanusha kutumia bunduki aina ya AK 47, na pia walikiri kuwa mpango huo ulifadhiliwa na Nyimpine Chissano.
Akitoa maelezo yake Manuel Fernandes alidai mahakamani hapo kuwa Anibal Dos Santos Junior (Anibalzinho) alimfundisha namna ya kuuwa kwa kutumia silaha siku hiyo ya mauaji ya Cardoso.
Akimnukuu, Manuel alidai kwamba Anibalzinho alimwambia "Nataka kukutoa kwenye lindi la umasikini, kwani nina kazi ya nzito niliyopewa na mtu mmoja mzito"
Manuel alipomuuliza kuwa ni nani huyo mtu mzito?
Anibalzinho alimjibu kuwa ni Nyimpine Chissano mtoto wa Rais Chissano.

Manuel aliongeza kuwa aliahidiwa kulipwa dola 21,000 za Kimarekani nakuhakikishiwa na Anibalzinho kuwa kila kitu kitakwenda sawa kwani hakuna mtu yeyote atakaewagusa.
Mara baada ya Manuel kukiri kuhusika na mauaji ya Cardoso wakili aliyekuwa akimtetea Simeao Cuamba alitishia kujitoa kumtetea kwa madai kuwa mteja wake ni muongo, lakini Jaji Augusto Paulino alimzuia wakili huyo kujitoa kumtetea Manuel mpaka hapo atakapopatikana wakili mwingine.

Mtuhumiwa mwingine Carlos Rachid Cassamo aliielezea mahakama hiyo kuwa alishuhudia mikutano mitatu kati ya Anibalzinho ambae hakuwepo mahakamani hapo baada ya kutoroka akiwa rumande, na Nyimpine Chissano.

Cassamo aliendelea kudai kwamba mkutano wa kwanza ulifanyika katikati ya jiji la Maputo hapo mnamo septemba 2000 ambapo Chissano alimpa Anibalzinho mfuko wa plastiki ambao ulikuwa na kiasi cha Meticais milioni 100 sawa na dola 4,200 za Kimarekani (Metical ni thamani ya fedha ya Msumbiji)

Kwa mujibu wa Cassamo mkutano wa pili kati ya Nyimpine na Anibalzinho ulifanyika Desemba 2000 mara baada ya mauaji ya Cardoso kando kando ya barabara jirani na ufukwe wa Maputo.
Katika mkutano huo Nyimpine hakutoa fedha, ila Anibalzinho alimwambia yeye Cassamo kuwa " Bosi amesema fedha zitakuja"
Mtuhumiwa huyo alipoulizwa na mahakamni hapo kama aliwahi kukutana usokwa uso na Nyimpine Chissano na kuzungumza nae kuhusiana na njama za kumuua Cardoso, kwa maneno yake mwenyewe Cassamo alijibu "Yule alikuwa ndiye Bosi, mara nyingi nilikuwa natakiwa nijifiche ndani ya gari lakini nilikuwa namuona"
Nae Nyimpine akijibu tuhuma hizo mahakamani hapo ambapo aliitwa kutoa ushahidi kwa upande wa mashitaka, alidai kwamba hakuhusika kabisa na kupanga njama za kumuuwa Carlos Cardoso na hakuwa na biashara yoyote na Familia ya Abdul Satar. Kwa maneno yake mwenyewe Nyimpine alisema "kamwe sijawahi kuwa na biashara yoyote na Satar, huyu mtu ni muongo na anajaribu kuidanganya mahakama"
Akizungumzia kuhusu hundi alizosaini Nyimpine alidai kwamba hundi hizo alisaini kama malipo ya deni alilokopa kwa niaba ya kampuni yake ya kitalii ijulikanayo kwa jina la Expresso Tours kutoka kwa mfanyabiashara mwenzie Bi Candida Cossa ambae pia ni ofisa katika mamlaka ya kodi nchini Msumbiji.
Hata hivyo Nyimpine alishindwa kufafanua kuwa ilikuwaje hundi hizo zikaangukia mikononi mwa Satar.

Baadae mara baada ya shauri hili kwisha Candida aliwaeleza waendesha mashitaka kwamba kulikuwa na shinikizo kutoka kwa Nyimpine kuwa akubalianae na ushahidi wake kuwa zile hundi zilikuwa ni kwa ajili ya kumlipa deni lake kitu ambacho ni kweli lakini hakupata kuziona hizo hundi hapo kabla.

Nyimpine akiendelea kutoa ushahidi wake mahakamani hapo alikanusha kuwafahamu washitakiwa wote isipokuwa Momade Assife Satar.
Lakini Satar alizidi kusisistiza mahakamni hapo kwamba hundi hizo zilikuwa ni malipo kwa ajili ya mauaji ya Cardoso.
Alipoulizwa kama anamfahamu Carlos Rachid Cassamo, Nyimpine kwa dharau alijibu kuwa hamfahamu mtu huyo na wala hajawahi kukutana nae.
Pia Nyimpine alikanusha kuhusu kukutana au kuongea na Anibalzinho.

Alipoulizwa na Jaji Paulino kama hakuhisi kwamba anafuatwa fuatwa kutokana na habari zilizokuwa zikiandikwa na Cardoso kuhusiana kashfa hiyo ya ufisadi ambapo yeye alihusishwa.
Nyimpine hakuficha aliieleza hisia zake za kutofurahishwa na habari zilizokuwa zikiandikwa na magazeti ya Cardoso, kwa maneno yake mwenyewe Nyimpine alisema "Ingawa sikuwa na chuki na gazeti la Metical lakini baadhi ya makala za gazeti hilo ziliathiri ukoo wa Chissano" hata hivyo Nyimpine alikanusha kuwahi kuwa na nia ya kulipiza kisasi.

Mpaka hapo watuhumiwa watatu kati ya sita walikuwa wamekiri kuwa Nyimpine Chissano alihusika na kupanga na kufadhili mauaji ya Muandishi wa habari Carlos Cardoso.

Nae mtuhumiwa mwingine mfanyabiashara Ayob Abdul Satar alikanusha kuhusika na mauaji ya Cardoso na hakuwahi kuwa na uhusiano wowote iwe ni wa kibiashara au kiurafiki na Anibalzinho.
Ayob aliendelea kusema kuwa alianza kusikia habari za kuuwawa kwa Cardoso kupitia Redioni.

Mtuhumiwa mwingine katika kesi hiyo Vicente Ramaya aliielezea mahakama hiyo kuwa mauaji ya Carlos Cardoso hayahusiani na kashfa ya ufisadi ya mwaka 1996 katika Benki aliyokuwa akiisimamia bali yalitokana na sababu nyingine ambayo hata hivyo hakuweza kuibainisha pale mahakamani.

Shahidi mwingine aliyetoa ushahidi ushahidi wake pale mahakamani alikuwa Ni aliyekuwa dereva wa Carlos Cardoso, Carlos Manjate.
Akitoa ushahidi wake Manjate alisema kwamba siku ya tukio mnamo Novemba 22, 2000, wakiwa ndio wanatoka ofisini yeye na Bosi wake Cardoso aliona gari likija kwa kasi na kuwabana kwa wake kisha akasikia milio ya risasi ambapo alipigwa risasi ya kichwa na kupoteza fahamu na hakusikia milio ya risasi zilizomuuwa Bosi wake Cardoso.

Ushahidi wa Manjate ulizua utata kwani ulitofautiana na ushahidi wa watu wengine ambao walidai kwamba kulikuwa na magari mawili yaliyokuwa yakilifukuza gari la Cardoso, wakati Manjate alidai kuwa ni gari moja tu lililohusika na tukio hilo.

Ushahidi mwingine uliotolewa pale mahakamani ni Bunduki ya aina ya AK 47 iliyookotwa na Polisi baada ya kupokea simu kutoka kwa mtu ambae hakujitambulisha, akiwajulisha kuwa ameona silaha kwe nye pipa la taka.
Baada ya uchunguzi ilikuja kubainika kuwa silaha hiyo ndiyo iliyotumika kwenye tukio la kumuuwa Cardoso.

Nae Mtaalama wa silaha kutoka nchini Afrika ya Kusini T J Brits akitoa ushahidi wake mahakamani hapo alisema kwamba watu waliohusika na mauaji ya Cardoso, lazima watakuwa ni watu walio na utaalam wa kutumia bunduku aina ya AK 47.

Ingawa katika maelezo ya mmoja wa watuhumiwa aliyekiri kuhusika na mauaji hayo Carlos Rachid Cassamo alikanusha kutumia bunduki aina AK 47 katika kutekeleza mauaji hayo.
Lakini mtaalam Brits alialiithibitishia mahakama kuwa bunduki aina ya AK 47 ni silaha yenye nguvu sana hivyo si rahisi mtu asiye na utaalam nayo kuweza kuitumia katika mazingira ilivyotumika kumuulia Cardoso.

Hata hivyo Brits alitanabahisha kuwa kuna uwezekana mtumiaji wa silaha hiyo aliitega kwenye Semiautomatic ambapo ilikuwa inamwezesha kufyatua risasi moja baada ya nyingine, hivyo kumezesha mtumiaji asiye na utaalam nayo kuitumia kwa urahisi.

Kesi hiyo iliyodumu Kwa takribani miezi mitatu iliisha mnamo January 23, 2003, Kwa mujibu wa kiongozi wa waendesha mashtaka Mourao Baluce hukumu rasmi ya kesi hiyo itasomwa Januari 31, 2003.

Akihitimisha kesi hiyo Mourao alisema kwamba watuhumiwa wote sita wamepatikana na hatia ya kuhusika na mauaji ya muandishi wa habari Carlos Cardoso hapo mnamo Novemba 22, 2000; na alimuomba Jaji Augusto Paulino atoe adhabu kwa watuhumiwa kifungo cha muda mrefu kisichopungua miaka 24 bila ya uwezekano wa kupewa msamaha wa kifungo cha nje (Parole).

Kwa mujibu wa Mourao mauaji ya Cardoso yalipangwa katika vikao kadhaa vilivyofanyika katika hotel tangu mwanzoni mwa Julai 2000.
Na watuhumiwa wote sita walishiriki katika vikao hivyo iwe ni baadhi ya vikao au vikao vyote, na lengo la watuhumiwa ilikuwa ni kumuuwa Cardoso kutokana na ujasiri wake wa kuandika habari za kashfa ya ufisadi iliyotokea mwaka 1996 katika Benki ya Biashara ya Msumbiji (BCM) ambapo Dola za Kimarekani milioni 14 zilifujwa pasipo maelezo ya kutosha.
Mnamo Januari 31 2003, washitakiwa wote sita akiwepo Anibalzinho aliyetoroka walihukumiwa vifungo vya muda mrefu jela.
Anibalzinho alihukumiwa kifungo cha miaka 28 jela pamoja na kwamba hakuwepo mahakamani na wenzie Ayob Abdul Satar, Momade Assife Abdul Satar, Vincente Ramaya , Carlos Rachid Cassamo na Manuel Fernandes walihukumiwa kifungo cha miaka 24 kila mmoja.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutoa hukumu hiyo Jaji Augusto Paulino alikiri kuwa wakati anaendesha kesi hiyo kulikuwa na shinikizo kutoka katika jamii na kwenye vyombo vya habari nchini kote wote wakitaka kujua kwamba ni kitu gani kinaendelea.
Wakati hukumu hiyo inatolewa Anibalzinho alikuwa amekamatwa nchini Afrika ya kusini na na juhudi zilifanyika akarejeshwa nchini Msumbiji na kutumikia kifungo chake.

Hata hivyo mnamo May 9, 2004 Anibalzinho alitoroka tena katika jela ilyokuwa na ulinzi mkali.
Habari zisizothibitishwa zilidai kwamba alitoroshwa Kwa ushirikiano wa Polisi na askari magereza ili kuficha ukweli katika kesi nyingine ya ufisadi katika benki ya biashara ya msumbiji (BCM) iliyokuwa ianze wakati wowote ambapo muhusika mkuu alikuwa ni Nyimpine Chissano pamoja na wenzie 15.

Safari hii Anibalzinho alikimbilia nchini Canada ambapo aliomba hifadhi ya kisiasa. Ombi lake lilikataliwa na kwa kushirikiana na Interpol, Serikali ya msumbiji ilifanikiwa kumrejesha Anibalzinho nchini humo na kuendelea na kifungo chake.

Anibalzinho hakuishia hapo kwani alifanya jaribio lingine la kutoroka lakini lilishindikana baada ya kugunduliwana askari mmoja mgeni aliyehamishiwa katika gereza hilo akitokea makao makuu ya magereza.
Tukio hilo lilitokea wakati ambapo Nyimpine alikuwa ndio amefunguliwa mashitaka ya kuhusika na mauaji ya muandishi wa habari Carlos Cardoso, mapoja na makosa mengine ya uahujumu uchumi ambapo aliunganishwa na watuhumiwa wengine 15.
Mwanasheria wa jiji la Maputo Bi Virginia Maria aliliambaia gazeti la kila siku la Zambezi la nchini humo kuwa mwendesha mashitaka Fernando Canana alikuwa ametoa hati ya kuakamatwa kwa Nyimpine Chissano lakini utekelezaji wa hati hiyo ulisitishwa baada ya wazazi wa Nyimpine kuingilia kati.

Hata hivyo Bi Virginia alibaianisha kuwa Rais mstaafu Joaquim Chissano pamoja na mkewe Bi Marcelina walikwenda ofisini kwake na kuzungumza nae , ingawa hakuweka mazungumzo yao bayana.

Wakati Nyimpine akifunguliwa mashitaka hali yake kiafya ilikuwa si ya kuridhisha hivyo iliamuliwa asubirie kuanza kwa kesi iliyokuwa ikimkabili akiwa nyumbani badala ya jela.
Lakini mnamo Novemba 20, 2007 zilitangazwa habari za kusikitisha kwamba Nyimpine Joaquim Chissano amefariki dunia jana yake akiwa nyumbani kwake katika katika jiji la Maputo akiwa na umri wa miaka 37.
Habari za kuaminika zilidai kwamba Nyimpine amefariki kutokana na tatizo la shinikizo la damu.
 
Back
Top Bottom