Maofisa wa Ikulu Kenya wapata kikombe cha Babu Send to a friend Sunday, 17 April 2011 11:16
Mussa Juma, Samunge
MAJAJI wanane wa Mahakama Kuu na Rufani wa Tanzania, Maofisa wa Ikulu wa Serikali ya Kenya, jana walifika Samunge kupata dawa ya magonjwa sugu inayotolewa na Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la KKKT, Ambilikile Mwasapila.
Maofisa wa Ikulu ya Kenya waliofika Samunge kupata kikombe cha dawa waliongozana na wanasiasa kadhaa mashuhuri wa nchi hiyo waliofika huko pamoja na wapiga kura wao.
Vigogo hao wa serikali za Kenya na Tanzania, walifika Samunge mchana wakiwa wanasindikizwa na askari polisi ambapo walienda moja kwa moja kwa Mchungaji Mwasapila kujitambulisha na kupata kikombe.
Kundi la kwanza kufika kijijini hapo lilikuwa la maofisa wa Ikulu ya Kenya na walinzi wa Rais Mwai Kibaki.
Vigogo hao walikuwa wameongozwa kwenye msafara huo na Chifu John Saitoti aliyekuwa amevalia sare za jeshi akiwa na mke wake na maofisa wengine sita.
Mmoja wa maofisa hao, alikuwa ni Chifu Daniel Kaka anayetoka Ikulu ya Rais Mwai Kibaki.
Wakati kundi hilo likipata kikombe, aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Narok Kusini, Steven Ndutu ambaye anagombea useneta wa jimbo hilo, alipata kikombe hicho akiwa na kundi la wapigakura wake.
Akizungumza na Mwananchi Jumapili, Ndutu alisema ameamua kufika Samunge na baadhi ya wapiga kura wake, ambao ni wagonjwa.Ofisa wa Ikulu ya Kenya, Chifu Saitoti ambaye alijitambulisha kwa maofisa Usalama wa Tanzania na Polisi waliopo Samunge, alisema amekuja kumleta mke wake, Lenini Saitoti, anayesumbuliwa na ugonjwa wa moyo.
"Nimetoka Nairobi, nimemleta mke wangu kunywa dawa baada ya kupata taarifa za mchungaji huyu kupitia vyombo vya habari," alisema Saitoti.
Majaji wa Tanzania
Majaji wanane wa Rufani na Mahakama Kuu Tanzania jana walitinga Samunge kupata kikombe cha Mchungaji Mwasapila wakiwa wameongozana na maofisa kadhaa wa Serikali.Baada ya kuwasili Loliondo majaji hao waliripoti Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro na baadaye kuelekea Samunge.Jaji Fredrica Mgaya kabla ya kupata kikombe, alikwenda kujitambulisha kwa Mchungaji Mwasapila na kusalimiana naye.
Mbali na majaji hao, Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba, naye alipata kikombe cha cha dawa ya Babu kwenye majira ya saa saba mchana jana.
Wageni waongezeka
Mbali na ujio wa vigogo hao, watu kutoka nje ya nchi wanaofika Samunge wameongezeka maradufu.
Kwa mujibu wa taarifa za maofisa uhamiaji waliyopo Samunge, hadi jana Wakenya walioandikishwa walikuwa 2,596.
Ofisa Uhamiaji aliyepo Samunge, Hussein Hamis aliliambia gazeti hili kuwa miongoni mwa wageni waliofika kijijini hapo walikuwapo Waganda wanne, Wanyarwanda wawili na Walebanon watatu.Kwa mujibu wa Ofisa Uhamiaji huyo wageni wengine ni Wamarekani wawili, Wazimbabwe wanne, Mdenmark mmoja na Waingereza wawili.
"Kuna baadhi hatukupata taarifa zao kutokana na kutojitambulisha, hivyo idadi ya wageni ni kubwa zaidi ya hii tuliyonayo," alisema Hamis.
Ajali yaua wawili
Watu wawili walifariki dunia jana na wengine zaidi ya saba kujeruhiwa vibaya, baada ya gari aina ya Land Rover walilokuwa wanasafiria wakati wanatoka kwa Mchungaji Mwasapila kupata dawa kuacha njia na kuanguka.
Gari hilo lilianguka baada ya kuteleza kwenye changarawe katika eneo la Sale, kilometa chache kutoka Kijiji cha Samunge.
Dereva wa gari linalobeba watu kutoka Arusha kwenda Samunge, Amani Mshana, alisema wakati wakiwatoa majeruhi wa ajali hiyo ambao walikuwa wamenasa kwenye gari hilo, kuwa chanzo cha ajali ni ubovu wa barabara.
"Tulikuwa tunafuatana na hili gari ila lilivutwa na changarawe na kuanguka ...hapa tayari kuna miili ya watu wawili waliofariki na wengine ni majeruhi," alisema Mshana.
Foleni yaongezeka
Katika hatua nyingine, maelfu ya watu wamefurika Samunge na sasa foleni ya magari imefika zaidi ya kilomita 10 kutoka kijijini hapo.
Idadi hiyo ya watu haijawahi tokea tangu Serikali iweke utararibu wa kusimamia magari yanayokwenda Samunge.
Ongezeko hilo sasa limeanza kusababisha watu kukaa zaidi ya siku mbili kusubiri kupata kikombe na kama lisipodhibitiwa, huenda vifo vikaanza kujirudia.
Baadhi ya wenye magari wamefunga barabara ya kutoka Samunge na hivyo kuzuia gari la kubeba wagonjwa kwenda kusaidia wagonjwa mahututi.
Shirika la PSI latinga Samunge
Maofisa wa Shirika la Kimataifa la PSI, wamejitokeza Samunge na kuanza kuhamasisha jamii kujikinga na magonjwa ya mlipuko na Malaria na Ukimwi.
Ofisa wa Uhamasishaji wa PSI maeneo ya vijijini mikoa ya Arusha na Manyara, Erasmus Majura, alisema wameamua kuweka kambi Samunge kutokana na ongezeko la watu katika eneo hilo ili kulinda afya.
"Tunatoa elimu ya matumizi ya maji safi na kutoa dawa, tunatoa elimu ya Ukimwi na Malaria na pia tunaonyesha sinema usiku" alisema Majura.