Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 20,887
- 30,233
Ukishasikiliza mazungumzo ya Mwalimu Nyerere katika hiyo video hapo juu sasa soma Hotuba yake aliyotoa Bungeni tarehe 10 Desemba, wakati Tanganyika inakua jamuhuri mwaka wa 1962.
Hotuba ya Nyerere ilijikita kwenye matatizo ya upogo kati ya Waislam na Wakristo.
Kwa nini ilikuwa lazima Mwalimu awataje Waislam katika hotuba ile?
Sababu ni jinsi Waislam walivyokuwa mstari wa mbele katika kupambana na ukoloni na namna walivyounda TANU wakamchagua kama kiongozi na kuumuunga mkono toka siku alipochukua uongozi wa TAA katika uchaguzi wa tarehe 17 April, 1953 Ukumbi wa Arnautoglo alipogombea nafasi ya urais dhidi ya Abdul Sykes aliyekuwa Act. President na Secretary wa TAA.
Kwa bahati mbaya sana hii ni historia ambayo ilifunikwa na hakuna yeyote aliyekuwa anaijua hadi nilipoandika kitabu cha Abdul Sykes na kuchapwa mwaka wa 1998.
Mwalimu anasema katika hotuba yake ya Jamhuri ndani ya Bunge la Tanganyika:
''Hakuna njia nyepesi ya kuondoa tafauti baina ya raia wetu Waafrika na wasio Waafrika; hakuna njia nyepesi ya kuondoa tofauti za elimu kati ya Wakristo na Waislam, au baina ya wachache wenye elimu na wengi wa watu wetu wasio kuwa na elimu; hakuna njia nyepesi ambayo Wamasai na Wagogo wanaweza wakalingana na Wahaya na Wachagga na Wanyakyusa.''
Hii ilikuwa kauli ya serikali ya kudhihirisha nia yake njema ya kupigania haki na usawa kwa raia wote wa Tanganyika.
Kauli hii ilikuwa ya kuwapa matumaini na kuwahakikishia Waislam na wale wote walioathirika na dhulma ya wakoloni, kuwa serikali ilikuwa inatambua shida zao na itachukua hatua zifaazo kurekebisha hali hiyo.
Tarehe 5 Novemba, 1985 wakati Mwalimu anastaafu urais, Mwalimu aliwahutubia wazee wa Dar es Salaam.
Hotuba hii ilijaa simanzi, Nyerere akikumbuka jinsi Waislam walivyompokea Dar es Salaam kwa mapenzi makubwa ingawa yeye alikuwa Mkristo.
Katika hotuba hii Nyerere kwa mar ya kwanza hadharani alimtaja Abdul Sykes.
Mwalimu alimtaja na mdogo wake Abdul, Abbas Sykes na Dossa Aziz.
Wazee hawa aliokuwa anawahutubia wengi wao walikuwa wanachama wa zamani wa TANU waliomuunga mkono wakati wa kudai uhuru.
Nyerere aliusifia mchango wa Waislam katika kipindi kile kigumu cha kudai uhuru.
Nyerere alisema neno zito sana kuwa upogo katika elimu uliorithiwa na serikali yake kutoka kwa Waingereza baina ya Waislam na Wakristo yeye ameuondosha katika kipindi cha utawala wake:
''Waislam wametupa nafasi kupitia sera yetu ya elimu, kurekebisha upogo.
Sasa nipo katika hali ya kufarahisha kwa kuwa wakati mwingine sielewi kama Mbunge mpya, Waziri, au Katibu Mkuu katika wizara zetu za serikali, ni Muislam au Mkristo au hana dini labda pale jina lake la kwanza linapotoa utambulisho.
Na hata hivyo hiyo siyo njia ya kuaminika kutoa utambulisho wa dini kwa kuwa tuna Wakristo wenye majina ya Kiislam, na Waislam wenye majina ya Kikristo.
Kuvumiliana huku nyie ndiyo sababu; nilichofanya mimi ni kuzungumzia maadili haya kwa niaba yenu.''
Swali linalokuja hapa ni kuwa ikiwa Mwalimu alisharekebisha upogo huu baina ya Waislam na Wakristo haya malalamiko ya leo kutoka kwa Waislam kuwa wanabaguliwa tunauelezaje?
Waislam hawasemi kweli?
Mgawano wa madaraka ndani ya serikali ya Tanzania baina ya Waislam na Wakristo ni 20:80.
Tumefikaje katika hali hii?
Ni muhimu sana mtu anapotaka kujadili tatizo hili la udini muhimu akaangalia historia hii kwanza kama nilivyoieleza hapo juu kwa kusikiliza mazungumza ya Mwalimu kuhusu udini na kusoma Hotuba yake ya Jamhuri ndani ya Bunge la Tanganyika mwaka wa 1962.
Tatizo hili la udini nimelijadili kwa kirefu sana katika kitabu cha Abdul Sykes.
Tatizo hili si tatizo la kupuuzwa na wala si la leo.
Tatizo hili lilianza mwaka wa 1958 na likasababisha ugomvi mkubwa baina ya Sheikh Suleiman Takadir na Julius Nyerere na Sheikh Suleiman Takadir akafukuzwa TANU.