Baba atelekeza watoto 5 alioachiwa

Baba atelekeza watoto 5 alioachiwa

Analogia Malenga

JF-Expert Member
Joined
Feb 24, 2012
Posts
5,286
Reaction score
10,831
Sasa ni kama watoto yatima wanaolelewa na mlezi, lakini wazazi wao wako hai.

Watoto hao watano wa familia moja-- wa kwanza akiwa na umri wa miaka 12 na wa mwisho mwaka mmoja, walitelekezwa na wazazi wao kwenye nyumba iliyobomoka iliyo mtaa wa Kazima, Manispaa ya Mpanda mkoani Rukwa na sasa wanalelewa na ofisa mtendaji.

Watoto hao - Rosemary Lemes (12), Francisco Lemes (8), Selina Lemes (5), Fotunata Lemes (2) na Maria Lemes (1) wametekelezwa katika kipindi ambacho tabia hiyo inakua kwa kasi wilayani Mpanda ambako kumeripotiwa zaidi ya matukio 170 kwa mwaka 2019 pekee.

Mtu wa mwisho kuwakimbia watoto hao ni baba yao mzazi, Lemes Kipeta anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka (40) ambaye aliondoka zaidi ya mwezi mmoja sasa.

Hata hivyo, inaaminika kuwa mama wa watoto hao, Faines Francisco alishaondoka muda mrefu baada ya kutengana na mumewe.

Mmoja wa watoto hao, Rosemary aliiambia Mwananchi kuwa mama yao alitengana na baba yao miezi minne iliyopita wakati wakiishi Kawajense baada ya kutofautiana.

“Siku ambayo mama aliondoka nyumbani aligombana na baba alipokuwa anamuomba hela za kununua chakula, halafu baba akampa Sh20,000, Lakini mama alizikataa kwa sababu alisema ni ndogo hazitoshi,” alisema mtoto huyo.

“Baada ya mama kuzikataa zile hela, baba aliondoka nyumbani na mama naye alipoona baba kaondoka, naye akachukua nguo zake akaweka kwenye mfuko. Tukamuuliza anaenda wapi, akatudanganya anafuata hela kwa baba hakurudi tena.”

Rosemary anasema ilipofika jioni, baba yao alirejea nyumbani na kuwauliza alipo mama yao, wakamjibu hawafahamu.
“Alituchukua akatupeleka kwenye nyumba nyingine tukawa tunakaa huko. Asubuhi akienda kazini alikuwa akirudi usiku huku amelewa chakula chenyewe tulikuwa tunakula mara moja kwa siku na wakati mwingine tunakunywa uji tu. Akawa anatuambia kuna siku nitawaacha peke yenu,” alisema Rosemary.

Baba yao alivyowatelekeza
Mtoto huyo anasema siku ambayo baba yao aliwaacha, alibeba mfuko ambao aliweka nguo zake na walipomuuliza anaenda wapi akawajibu kuwa anaenda kuwatafutia fedha ya chakula.

Rosemary alisema hawajawahi kumuona tena baba yao na msaada mkubwa ulibaki kwa majirani ambao baada ya kubaini kuwa wametelekezwa, wakawa wanawasaidia chakula, siku nyingine walikuwa wakilala njaa.

Mtoto huyo anasema baadaye majirani waliwapeleka ofisi ya serikali ya mtaa kuwaepusha kuendelea kuteseka.
Rosemary, ambaye alitakiwa kuingia darasa la tatu mwaka huu na Francisco darasa la pili katika Shule ya Msingi Makongoro, wameshindwa kuendelea na masomo kutokana na baba yao kushindwa kuwatimizia mahitaji ya shule na tabia ya kuhama makazi mara kwa mara.

Majirani wasimulia
Majirani wa familia hiyo, Happyness Alphonce na mumewe Filberth Mangasini, waliliambia Mwananchi kuwa baba wa watoto hao alikuwa na wake wawili baada ya kuachana na mke mkubwa, aliwachukua watoto na kuwapeleka kwa mke mdogo.

“Mke mdogo ilibainika alikuwa mke wa mtu, baadaye naye aliondoka, baba huyo akaendelea kuishi na watoto wake kwenye nyumba hiyo, ikafikia hatua akaomba akabidhi watoto kwetu tukakataa.

“Siku chache baadae akawa haonekani, watoto wakawa wanashinda na njaa wakaanza kuokota chakula jalalani,” alisema.

“Tukapata hofu wanaweza kufanyiwa vitendo vya kikatili au kuangukiwa na ukuta wa nyumba hiyo, tukaomba barua kwa mjumbe na kuwapeleka kwa Mwenyekiti wa mtaa,” alisimulia Mangasini.

Serikali ya mtaa
Mwananchi ilizungumza na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kazima, Flaviana Salala anayeishi na watoto hao kwa sasa, alisimulia alipokea taarifa hizo kutoka kwa majirani wa familia hiyo kuwa wametelekezwa na wanaishi kwenye mazingira hatarishi kulingana na umri wao kuwa mdogo.

“Nimewapokea kutoka kwa majirani wakiwa na barua ya mjumbe, sasa kama mzazi ninawasaidia, ninachokula na wao wanakula, nimeripoti polisi wakashauri niwapeleke ustawi wa jamii, najiandaa kufanya hivyo, lakini kitendo hiki hakifai niwashauri wazazi ukizaa uwe tayari kulea,” alisema Flaviana.

Naye mkuu wa wilaya, Lilian Matinga alisema hana taarifa hiyo na kuahidi kufuatilia suala hilo ili ikiwezekana watoto hao wapelekwe kwenye kituo cha kulelea watoto yatima na wale wanaosoma watatafutiwa shule.

“Mwandishi nimepokea taarifa hizi kutoka kwako kwa masikitiko makubwa nitafuatilia kwa kushirikiana na ofisi ya ustawi wa jamii ili wapelekwe sehemu husika na wazazi watatafutwa hadi wakamatwe na vyombo vya dola, nitoe wito wazazi tusikwepe majukumu, viongozi wa dini watusaidie kukemea tabia hii makanisani ili ikome maana imekithiri,” alisema Matinga.

Ofisa Ustawi wa jamii wa mkoa wa Katavi, Bahati Mwailafu alipozungumza na Mwananchi alisema mkoa huo umekuwa na matukio mengi ya kutelekeza watoto.

Alitoa mfano kuwa mwaka 2019, matukio ya wazazi kutelekeza watoto yaliyoripotiwa yalikuwa 179.
“Hii tabia ipo na inasababishwa na uelewa mdogo wa wazazi/walezi kutofahamu wajibu wao na haki za mtoto, matukio yanayoripotiwa ni machache na mengi hayaripotiwi,” alisema.

Chanzo: Mwananchi
 
Duuh noma sana..akija kupata division one utaona wanarudi kama yule msukuma..

Hio roho ngumunya kukimbia hao malaika wanayo mashetani tu.

Ndugu wa karibu inabidi wapambanie damu zao
 
maisha ya katavi buku 20 ndogo, huyu mama alikuwa na mpango wa kusepa ama kutokana na mme kuwa na mke mwingine ama alipata bwana mpya.

hawa watu watafutwe si kwa maana ya kuja kulea familia ila kwa kupelekwa mahakamani na kuhukumiwa angalau miaka 2

NB:Mpanda haipo Rukwa ishatoka sasa ivi ipo katavi, naona mwandishi anasema iko Rukwa badae anakumbuka iko Katavi
 
Mmmh hii ni balaaa. Watoto wote hao na uwezo mdg wa kuwalea unawaleta duniani wa nini?, kuja kuwatesa masikini kama ivyo. Wakikamatwa hao wazazi wapewe adhabu kali. Yani ata huyo mama anadiriki kutoroka wtt wake kweli?
 
Hao jamaa sidhani kama ni watanzania halisi tabia za namna hiyo ziko kwa kina Nkrunzinza
 
Hao jamaa sidhani kama ni watanzania halisi tabia za namna hiyo ziko kwa kina Nkrunzinza
... usishangae lilishavuka ziwa zamani liko ng'ambo ya pili mitaa ya Kalemie huko na linaishi na mwanamke mwingine huko. Yaani kuna mijitu sijui akili zao zikoje.
 
Hii habari imeniumiza sana,haya maisha niliyaishi ni maisha yenye mateso na kubaguliwa kwenye jamii..amna kitu kinaumiza kama kuishi bila wazazi wakati wapo hai...

Mungu asimame mwenyewe kwa kweli!

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Inauma sana ingekuwa uwezekano MUNGU anawanyima uzaz watu wa maisha duni kama mm, ila siku zote mafukara ndo tunaongoza kuzaa watoto wengi hata wa mitaan ni sisi tunasababisha
 
Hatujui hiyo buku 20 ilikuwa ya matumizi gani na kwa muda gani. Unaweza kukuta ni ya mwezi.
Hata kama ni ya mwezi angeipokea, kwa sababu ingeweza hata kumsaidia kufanya nauli au kuanzisha genge la kuuza nyanya akasonga mbele, kwa zama hizi mbona hiyo hela sio bure !!
 
Back
Top Bottom