Baada ya kukatika nchi nzima; umeme warejea!

Wanasiasa wetu wanajua kujieleza na kujinadi zaidi kwa matatizo sio kwa mafanikio. Matatizo ya nishati, maji, elimu, matibabu tunayo tu kama ilivyokuwa mwanzo, sasa na hata milele so long as serikali ni ya CCM.
 
KATUNI%28135%29.jpg

Maoni ya katuni



Kwa takribani miezi miwili sasa kumekuwa na mzozo juu ya mradi wa umeme wa kilovolti 132 unaojengwa kutoka Ubungo kupitia barabara ya Morogoro, Sam Nujoma, New Bagamoyo hadi Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
Mradi huu unaokusudia kuongeza nguvu ya nishati hiyo kwa maeneo ya Kijitonyama, Mikocheni hadi Masaki, umekuwa na mzozo kwa kile kilichoelezwa na Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBFC) kwamba utakuwa na madhara kwa kanisa hilo lililoko barabara ya Sam Nujoma.
Kwa kipindi chote hicho, ujenzi wa mradi huo uliendelea kwenye maeneo mengine yote, isipokuwa kwenye nguzo mbili tu zinazotarajiwa kujengwa mbele ya kanisa hilo.
Kutokana na uamuzi wa kanisa hilo kuupinga mradi huo, Wizara ya Nishati na Madini ikiwa ni wizara mama ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), iliingilia kati kwa kuagiza ufanyike uchunguzi wa kitaalam juu ya madhara yanayoweza kusababishwa na mradi huo kwa kanisa hilo na waumini wake.
Kwa muda wote huo, Wizara hiyo chini ya Waziri wake, William Ngeleja, iliamua kuzuia shughuli yoyote ya undelezaji wa mradi huo mbele ya kanisa hilo kwa kuwa kulikuwa na jambo linabishaniwa, lakini pia hasa baada ya kuonekana kwamba kanisa hilo lilikuwa limeweka waumini wake eneo hilo wakilinda usiku na mchana.
Vyombo vya habari vimeandika kadhia hii kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na mikutano iliyofanyika baina ya vyombo vya serikali na kanisa hilo, pia vimeeleza kwa kina taarifa ya watalaam walioteuliwa kuchunguza kama mradi huo utakuwa na madhara kwa kanisa hilo.
Ni jambo la bahati mbaya kwamba baada ya ripoti ya kitaalam kutolewa, kanisa hilo liliikataa na kuipachika majina mabaya huku likisisitiza kwamba imeandaliwa na watu ambao hata hawakufika eneo la mradi.
Jumamosi iliyopita Waziri Ngeleja mwenyewe alishiriki kikao cha majadiliano na kanisa wizarani kabla ya kuhamia eneo la mradi mbele ya kanisa hilo na kudhihirika kwamba hoja za kanisa zilikuwa zimezingatiwa kuhusu mradi huo, lakini kikubwa zaidi umbali uliokuwa ukibishaniwa kutoka kwenye eneo la kanisa na nguzo pia ulikuwa sahihi kwa upande wa serikali.
Kwanza tungependa kusema wazi kwamba sisi si wasemaji wa serikali na wala hatukusudii kuwa hivyo, ila tunawajibika kusema kitu kwa sababu suala hili lilijitokeza wazi kuigusa jamii ambayo tunaitumikia.
Ni kwa maana hiyo tunafikiria uvumilivu ulioonyeshwa na vyombo vya serikali kwa maana ya Wizara ya Nishati na Madini na Tanesco katika kushughulikia suala hili, licha ya maeneo mengine ambayo mradi huo unapita kutokuwapo kwa vizingiti vyovyote, ni wa hali ya juu na ambao unastahili kuigwa katika kushughulikia migogoro baina ya serikali na raia.
Hadi leo watu wengi wangali wanajiuliza inakuwaje mradi huo uwe na madhara eneo la kanisa hilo tu, lakini kwingine kote unakopita wananchi wenye nyumba zao na biashara kadhaa wasione hofu au kujenga hoja za kuhujumiwa kwa kubuniwa kwa mradi huo?
Tunajua kwamba masuala ya imani ni nyeti sana katika jamii, vurugu za kiimani ni kali na ambazo zinaweza kusababisha madhara makubwa kwa jamii. Kwa bahati nzuri Tanzania ni nchi inayoruhusu uhuru wa kuabudu, kila mtu ana imani yake ambayo inaheshimika na kulindwa isiingiliwe na mtu mwingine.
Ni kwa msingi hiyo kama taifa hatuna budi kuenzi na kulinda uhuru huo usitumike vibaya kama vile kuchochea uvunjaji wa sheria, kuzuia shughuli za maendeleo au hata kuutumia kwa njia ambayo dhahiri inalenga kufarakanisha jamii kwa jambo lolote lile.
Tumeshuhudia uvumilivu wa serikali katika sakata lote hili kuanzia siku ya kwanza na hata pale dalili za uvunjifu wa amani zilipojitokeza kwa baadhi ya watu kutishiwa maisha na wengine kupigwa karibu na kanisa hilo.
Mwisho tumeona serikali kupitia kwa Waziri Ngeleja ikitangaza kuendelea kwa mradi huo eneo la kanisa na kanisa kuafiki ijapokuwa kwa kutoa visingizio vipya; ni dhahiri kama suala hili lingeshughulikiwa kwa pupa lingeweza kabisa kutia doa taifa letu jinsi linavyojenga utamaduni wa kuvumiliana kwa watu wenye imani tofauti.
Kwa hili tunampongeza Waziri Ngeleja kwa kuwa ndiye mwenye dhamana na shughuli yote hiyo kwa kuwa ameonyesha ukomavu mkubwa wa kisiasa katika kutatua jambo hili na sasa mradi unaendelea kwa ajili ya ustawi wa nchi yetu na kanisa linaendelea na shughuli zake.



CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom