Baada ya kuilaumu mahakama chadema sasa wawalalamikia na polisi

Marwa_J_Merengo

JF-Expert Member
Aug 6, 2018
4,512
6,856
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimelalamikia hatua ya Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kumshikilia kwa siku mbili mtumishi wao Williard Urassa.

Urassa ambaye ni dereva wa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alikamatwa jana nje ya chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Taarifa iliyotolewa leo, Novemba 24, 2018 na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene imeeleza tangu Urassa alipokamatwa na polisi, jeshi hilo limekataa kumpatia dhamana huku likizuia mtu yeyote kuonana naye.

Hii ndio Taarifa kamili:

Kwa siku ya pili leo Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia Ndugu Williard Urassa, ambaye ni mtumishi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Makao Makuu, bila kueleza sababu za kumshikilia, huku pia akinyimwa haki zake za msingi, kinyume cha sheria za nchi.

Ndugu Urassa ambaye ni Dereva wa Mwenyekiti wa Chadema Taifa, alikamatwa jana nje ya chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akiwa mmoja wa wananchi waliokuwa wakisikiliza kesi na. 112/2018 inayowakabili baadhi ya Viongozi Wakuu wa Chama na wabunge saba wa Chadema.

Tangu alipokamatwa na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, jeshi hilo limekataa kumpatia dhamana huku pia likizuia mtu yeyote kuonana naye, wakiwemo wanasheria waliofika kwa ajili ya kumpatia msaada wa kisheria, hali ambayo inaibua maswali mengi na sintofahamu kubwa kuhusu hali yake baada ya kukamatwa.

Tunalaani na kukemea vikali kitendo hicho cha Jeshi la Polisi ambacho ni mwendelezo wa tabia inayopaswa kuachwa mara moja ya jeshi hilo kujipatia mamlaka lisilokuwa nayo, hasa kuwakamata na kuwashikilia chini ya ulinzi kinyume cha sheria.

Ni vyema jeshi hilo likatambua kuwa halina mamlaka ya kumshikilia mtu yeyote kwa namna hiyo, hivyo tunalitaka lieleze kwanini linamshikilia dereva huyo, apewe haki zake za msingi ikiwemo kuonana na ndugu na wanasheria na pia kuachiwa huru kwa dhamana.

Imetolewa leo Jumamosi, Novemba 24, 2018 na;

Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA
 
Wewe huwezi kulitaka jeshi kutoa maelezo isipokuwa, unaweza fungua shauri mahakamani, ili mahakama ilitake jeshi kutoa maelezo.
 
Back
Top Bottom