Ashauri wabunge wafanyiwe tathmini ya walichokifanya

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,322
33,126
headline_bullet.jpg
Pia apinga kuwepo ukomo



Mpyesa%281%29.jpg

Mbunge wa Mbeya Mjini, Benson Mpesya.



Mbunge wa Mbeya Mjini, Benson Mpesya, ametaka kuwepo utaratibu wa kuwafanyia tathmini wabunge ili kuwatambua wale wasiotimiza wajibu wao ipasavyo na kuwaondoa madarakani, badala ya kuweka ukomo wa kushikilia wadhifa huo.
Mpesya aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa mahojiano maalumu na gazeti hili mjini hapa.
Alisema ikiwa itabainika kuna mbunge hatimizi vema wajibu wake kwa wananchi anaweza kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye, akavuliwa madaraka na uchaguzi ukaitishwa upya katika jimbo husika.
"Badala ya kuweka ukomo wa kugombea ubunge, tuweke utaratibu wa kumwita mbunge asiyetimiza wajibu wake na kumpigia kura ya kutokuwa na imani," alisema.
Mpesya alipendekeza kuwa wabunge wanaweza kufanyiwa tathmini ya aina hiyo baada ya miaka miwili tangu alipochaguliwa na kudai kuwa utaratibu kama huo upo katika nchi mbalimbali ikiwemo Marekani na baadhi ya nchi za bara la Ulaya.
Akifafanua zaidi, alisema suala la kuwaletea wananchi maendeleo lazima liwe endelevu, hivyo inapotokea kunakuwa na mabadiliko ya mara kwa mara ya viongozi pia inaweza kuwa na mafanikio hasi.
Alitoa mfano kuwa yeye aliomba jiji la Mbeya liwekewe miundombinu bora ya maji tangu mwaka 2002, lakini utekelezeji wake unafanyika hivi sasa.
"Maendeleo lazima yawe endelevu, mfano ni mimi mwenyewe niliomba maji Mbeya miaka minane iliyopita, utekelezaji wake ndiyo unafanyika leo, kama ningeongoza miaka mitano na kuondoka, inawezekana ombi hili lingewekwa kapuni," alisema.
Aidha, alisema wanaotakiwa kumhukumu mbunge kwa kutowaletea maendeleo ni wananchi waliompigia kura na wala siyo kigezo cha kuwa na umri mkubwa wala kutawala kwa muda mrefu.
Alisema ikiwa kigezo kitakuwa ni ujana wa mgombea, wazee watakuwa hawatendewi haki na kudai kuwa wapo vijana katika Bunge lililopita wamemaliza miaka yote mitano wakiwa ndani ya Bunge bila kutoa hoja madhubuti.
Akizungumzia pendekezo la kuwepo na ukomo wa ubunge kama ilivyo kwa wadhifa wa urais, alisema sio sahihi kufananisha urais na ubunge, kwa sababu urais ni ofisi yenye mamlaka makubwa tofauti na ubunge ambao ni uwakilishi tu wananchi.
"Urais ni ofisi yenye mamlaka makubwa, yenye maamuzi na utendaji, lakini ubunge ni uwakilishi wa wananchi bungeni, tukitambua hilo tunaona kuwa sio sahihi kufananisha urais na ubunge," alisema Mpesya.
Hata hivyo, Mbunge huyo alisema ikiwa wananchi wengi watapendelea kuwepo na ukomo wa kuwania ubunge, yeye hana pingamizi, isipokuwa mabadiliko hayo yanapaswa kuwekwa mapema na sio kusubiri wakati wa uchaguzi.
Ukomo wa kugombea usiwe wa kushtukiza, siyo inapokaribia uchaguzi ndio wanadai ukomo, ukiona hivyo ujue hapo kuna hila, kama wanataka ukomo, tuweke mapema kwenye katiba na ijulikane kwa wote kabla ya uchaguzi," alisema.
Hivi karibuni baadhi ya wazee wa Jimbo la Mtera, walimtaka mbunge wao, Mzee John Samwel Malecela, kutogombea wadhifa huo katika uchaguzi ujao na badala yake astaafu kwa heshima yake na kuwa mshauri wa viongozi watakaofuata.
Hata hivyo Malecela, mwenyewe aliwajibu wazee hao kuwa kazi ya ubunge sio sawa na kubeba zege au kucheza mpira wa miguu, ambazo zinahitaji nguvu na misuli kama walivyo vijana na badala yake akatangaza kuwa ataendelea na mbio zake za kutetea kiti hicho kwenye uchaguzi ujao.



CHANZO: NIPASHE
 
Nakubaliana kabisa na Mh.Mpesya kuwa tuwafanyie tathmini wabunge kila baada ya miaka mitano ili kupima utendaji wao.Tatizo linakuja pale baada ya kujiridhisha kuwa mbunge husika kashindwa lakini bado anatumia takrima kushawishi wajumbe wa chama chake kumpitisha kuendelea kugombea,na kweli wengi wamekuwa wakifanikiwa haswa toka CCM.Hapo ndipo tunapopendekeza ukomo wa vipindi vya mtu kuwa mbunge ili kuondokana na uozo wa aina hii.
 
Huyu Mbunge bogus kabisa, pamoja na wote wanao muunga mkono.

Tayari kuna mchakato unaotakiwa kuangalia ufanisi wa mbunge, mafanikio yake, na kama achaguliwe tena au la.

Huu mchakato unaitwa uchaguzi, wananchi wanatakiwa wawe na uwezo wa kufanya uchambuzi wote huu, kama hawana uwezo huu mbunge anatakiwa kupigania wananchi wake waweze kupata uwezo wa kielimu kufanya hivyo.

Ukitaka kuleta process nyingine yoyote ambayo haihusiani na uchaguzi, utazalisha maswali mengi zaidi ya utakayojibu.Kwa mfano, utawapima wabunge ufanisi wao kivipi? Kwa kipimo gani? Nani atakuwa na jukumu la kupima ufanisi huu? Na kwa sababu kiti cha ubunge ni cha kisiasa, tutajuaje kwamba hakuna msukumo wa kisiasa unaoingia katika mchakato huu?

Ukisikiliza wabunge kama hawa utaona kuna wabunge wanapenda kusema tu ili wasikike, lakini hawaelewi undani wa mambo wanayosema.
 
Back
Top Bottom