ALIYEKUWA Mstahiki Meya wa halmashauri ya Jiji la Arusha,Kalisti Lazaro, leo amekabidhi rasmi ofisi kwa mkurugenzi wa halmashauri ya jiji la Arusha Dakta Maulid Madeni,na kuwaaga rasmi watumishi wa halmashauri hiyo na kuwashukuru kwa ushirikiano wao katika kipindi chake cha miaka minne .
Akizungumza wakati wa kuwaaga watumishi kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo, Meya mstaafu Lazaro,amesema ameachia ngazi akiiacha halmashauri ikiwa na mafanikio makubwa ya maendeleo ikiwemo utekelezaji wa miradi mikubwa ,ongezeko la ukusanyaji wa mapato pamoja na jiji kufanya vizuri kielimu.
Amesema kuwa licha ya kuwa yeye ni meya aliyetokana na Chadema, aliweza kukataa maelekezo ya chama chake ya kuahirisha vikao vya baraza la madiwani kwa ajili ya kuendeleza vurugu kwenye jiji yeye alisimamia masilahi ya wananchi na halmashauri.
Meya mstaafu ,Kalisti, amesema ameiacha halmashauri ikiwa juu kwenye Nyanja mbalimbali za maendeleo ikiwemo ukusanyaji mapato kutoka kwenye vyanzo vyake mbalimbali ,pia ameiacha halmashauri ikiwepo kwenye utulivu wa kisiasa na amekuwa ni meya bora tangia mwaka 2016 hadi Novemba 19 mwaka huu alipoachia ngazi na ameweza kutunukiwa tuzo mbalimbali.
Ameyataja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na ujenzi wa hospital ya wilaya inayojrengwa Engutoto, ujenzi wa shule za misingi za maghorofa, pamoja na wenyeviti wapya wa serikali za mitaa waliochaguliwa Novemba 24 mwaka huu kwa asilimia 100 ,
Ameongeza kwamba halmashauri ipo kwenye ubora wa elimu ambapo matokeo ya shule ya msingi mwaka huu imekuwa ni ya kwanza katika mkoa na ya tatu kitaifa .
Amewapongeza madiwani wote wa halmashauri ya jiji la Arusha kwa mshikamano wao na kukataa kugawanywa.
Awali mkurugenzi wa halmashauri ya Jiji ,Dakta Maulid Madeni, amesema meya mstaafu alikuwa ni kiongozi mwenye uwezo na maono na mwelewa sana na amekomaa katika maswala ya siasa.
Amesema meya hakufanya kazi kwa majungu wala msimamo wa Chama chake bali alifanya kazi kwa masilahi ya halmashauri na wananchi wa jiji la Arusha.
Amesema wakati wa uongozi wa Meya mstaafu,mapato ya halmashauri hiyo yaliongezeka kwa kiwango kikubwa na kuifanya halmashauri hiyo kuongoza kitaifa katika ukusanyaji wa mapato.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama cha wafanyakazi serikali za mitaa mkoa wa Arusha, Suleimani Kikingo, amesema kuwa walipokea kwa mshutuko na fedheha kubwa ya Meya kujiuzulu uongozi kwa sababu alikuwa ni kiongozi mahili na kusema kuwa watamkumbuka kwa utendaji wame.