Na Emakulata Peter
MKAZI wa Kibamba jijini Dar es Salaam, Diana Roman (18) ambaye alikuwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Yusuph Makamba ya jijini Dar es Salaam amejiua kwa kunywa dawa ya Kunguni baada ya kufeli mtihani wa kidato cha nne.
Mama mlezi wa binti huyo, Bibiana Roman alisema mwanafunzi huyo akiwa katika hali mbaya alimweleza kuwa alikuwa amekunywa dawa ya Kunguni ili ajiue baada ya kufeli mtihani huo.
"Baada ya kutoka kusali, Diana aliingia chumbani kwake na kunywa sumu ya Kunguni iliyokuwa juu ya kabati, baada ya muda tulimkuta chumbani akiwa amelala chini,"alisema Bibiana.
Alisema Diana aliwahi kunywa sumu hiyo, lakini alimnyang'anya. "Mara ya kwanza tulimkuta akiwa anakunywa sumu tukamnyang'anya, tulichokosea tuliiweka juu ya Kabati, alienda tena kuichukua na aligombana sana na dada yake mpaka akafanikiwa kuichukua na kuimalizia,"alisema Bibiana.
Alisema baada ya tukio hilo, waliomba maziwa kwa majirani ili waweze kumpatia huduma ya kwanza Diana. "Tulijitajidi, lakini ilishindikana, tulimkimbiza Hospitali ya Tumbi iliyopo Kibaha, lakini alifariki dunia,"alisema.