Ajira za walimu wakuu Nanyumbu shakani | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Ajira za walimu wakuu Nanyumbu shakani

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by kilimasera, Jun 13, 2011.

 1. kilimasera

  kilimasera JF-Expert Member

  #1
  Jun 13, 2011
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 3,073
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  HALMASHAURI ya wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara itawatimua kazini walimu wakuu wa shule sita za msingi wanaokabiliwa na tuhuma za ubadhirifu wa fedha zilizotolewa na halmashauri hiyo kwa ajili ya utengenezaji wa madawati, ujenzi wa vyumba vya madarasa na vyoo katika shule zao.

  Msimamo huo umefikiwa mwishoni mwa wiki na halmashauri hiyo katika kikao cha baraza la madiwani, baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Afya na Maji, Hawa Akwiti kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu.

  Taarifa hiyo ilionesha kuwapo kwa walimu wakuu waliofuja fedha za madawati na ujenzi, vyumba vya madarasa na vyoo.

  Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Dua William akihitimisha hoja za madiwani hao juu ya uamuzi wao wa kutaka hatua kali za kisheria kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa hao, alisema licha ya halmashauri hiyo kukabiliwa na uhaba mkubwa wa walimu, haitakuwa tayari kuendelea kuwakumbatia wabadhirifu, bali kuwafukuza kazi.

  Awali Akwiti akiwasilisha taarifa yake alisema katika kipindi cha 2009/10 halmashauri hiyo ilitoa kiasi cha sh 9,450,000 kwa ajili ya utengenezaji wa madawati kwa shule 21 za wilaya hiyo na kiasi cha sh milioni 4.4 kwa shule Nane kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa chumba kimoja cha darasa na sh milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa matundu 10 ya choo kwa shule tano wilayani hapa.

  Alizitaja shule zinazohusishwa na upotevu wa fedha kuwa ni Nahimba, Nawaje, Mkoromwana, Nakole na Chinyanyila. Diwani wa Kata ya Lumesule, Abdallah Khatau ndiye aliyeibua hoja hiyo kwa kutaka kujua ni hatua zipi zimechukuliwa na halmashauri hiyo dhidi ya walimu hao ambao wanarudisha nyuma maendeleo ya elimu wilayani humo kwa kufuja fedha za maendeleo.

  Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Adoh Mapunda alisema walimu hao wamepewa muda wa miezi mitatu hadi Juni, 30 mwaka huu kuzirejesha fedha hizo, vinginevyo watawafikisha mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria Mapunda alikiri kuwa halmashauri yake kukabiliwa na uhaba mkubwa wa walimua ambapo alibainisha kuwa kwa sasa ina upungufu wa walimu 184, kati ya 600 waliopo ikiwa 452 wanaume na 148 ni wanawake.
   
Loading...