Ajinyonga dukani kwa kuchoshwa na maisha


kilimasera

kilimasera

JF-Expert Member
Joined
Dec 2, 2009
Messages
3,073
Likes
23
Points
135
Age
42
kilimasera

kilimasera

JF-Expert Member
Joined Dec 2, 2009
3,073 23 135
MUUZA duka John Vincent (16), mkazi wa Mchikichini Bondeni, Ilala, Dar es Salaam amejinyonga kwa kutumia shuka alilokuwa amelitundika kwenye nondo ya dirisha ndani ya duka hilo kwa madai ya kuchoshwa na maisha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 1.30 asubuhi katika duka hilo mali ya Priscus Felix (24), mkazi wa Mchikichini Bondeni.

Shilogile alisema sababu za kijana huyo kujinyonga hazijafahamika ingawa kabla ya tukio hilo, alimwandikia ujumbe kaka yake (Priscus) ambaye yupo safarini mkoani Kilimanjaro.

Ujumbe huo unadaiwa ulisomeka, “Kwa heri kaka, mimi siwezi kujitesa usiku mwema.” Pia katika daftari yalikutwa maandishi yenye neno “kwa heri.”

Kamanda Shilogile alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Amana huku polisi wakiendelea na uchunguzi zaidi.

Katika tukio jingine, kijana aliyetambuliwa kwa jina moja la Ally anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 20, amekufa baada ya kugongwa na gari wakati akiliongoza kuingia katika eneo la kuoshea magari.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 10.30 jioni katika Barabara ya Morogoro eneo la OilCom Kagera na kuhusisha gari lenye namba za usajili T967 AUC aina ya Toyota Spacio likiendeshwa na dereva asiyefahamika.

Alisema gari hilo likiwa linapandishwa katika ngazi ya chuma kwa ajili ya kuoshwa, lilipitiliza na kumgonga kijana huyo aliyekuwa akimuongoza kutokana na vizuizi kuwa vifupi.

Kamanda Kenyela alisema Ally alikufa papo hapo na maiti yake kupelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mwananyamala, na polisi wakiendelea kumsaka dereva wa gari hilo aliyekimbia baada ya tukio hilo.

Wakati huo huo, mkazi wa Mbagala, Ugumu Mkomwa (65), amekufa papo hapo baada ya kugongwa na pikipiki wakati akivuka Barabara ya Kilwa eneo la Mbagala Kipati.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, David Msime, tukio hilo lilitokea juzi saa 4.40 usiku na kuhusisha pikipiki yenye namba T377 BZE aina ya Yamaha ikiendeshwa na Maftaha Hussein (40), mkazi wa Mbagala akitokea Mbagala Sabasaba kwenda Mbagala Kizuiani.
 

Forum statistics

Threads 1,237,565
Members 475,562
Posts 29,293,830