Adaiwa kuchinja mwanawe, kumtupa chooni

Bubu Msemaovyo

JF-Expert Member
May 9, 2007
3,832
2,790
Adaiwa kuchinja mwanawe, kumtupa chooni

Na Heckton Chuwa, Moshi

POLISI mkoani Kilimanjaro, inamshikilia mwanamke mkazi wa Dakau, Kibosho, Moshi Vijijini, kwa tuhuma za kumuua mwanawe mchanga kwa kumchinja na kumtumbukiza chooni.

Akithibitisha jana kutokea kwa tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Linus Sinzumwa, alimtaja mwanamke huyo kuwa ni Bi Digna Francis (23).

Kamanda Sinzumwa alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 12 asubuhi na kwamba kichanga hicho cha kike, kiligundulika baada ya majirani kusikia kikilia na kufuatilia.

“Baadhi ya majirani walisikia sauti ya kitoto kichanga kikilia kutokea chooni na kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Dakau,” alisema Kamanda na kuongeza kuwa ndipo ilipogundulika kuwa Digna alikuwa amejifungua.

Alisema wananchi waliofika eneo hilo, walivunja choo na kumtoa mtoto huyo na walipomsafisha waligundua kuwa amekatwa shingoni na kitu chenye ncha kali na alifariki dunia, muda mfupi baada ya kutolewa kwenye shimo hilo.

“Kutokana na hali hiyo, Digna alikamatwa na Polisi kwa uchunguzi zaidi na pamoja na mambo mengine, itabidi akapimwe akili yake kwanza,” alisema.

Kamanda Sinzumwa alisema uchunguzi wa awali wa Polisi ulionesha Bi Digna aliolewa na Bw. James Lelo, mkazi wa Uru Kibosho mwaka 2004 na Februari, mwaka huu, waliachana na mumewe huyo.

“Baada ya kuachana, Digna aliondoka nyumbani kwa mumewe huyo na kurudi kwao akiwa mjamzito na alirudi kwa wazazi wake akiwa na mimba changa,” alisema Kamanda na kuongeza kuwa baadhi ya majirani zake walisema alikuwa akihudhuria kliniki kama kawaida.

Katika hatua nyingine, mtu mmoja amefariki dunia katika ajali ya barabarani iliyotokea Kisangiro, Mwanga, juzi saa moja usiku.

Kamanda Sinzumwa alimtaja marehemu kuwa ni Waziri Hussein (37) ambaye alikuwa abiria katika gari hilo aina ya Peugeot namba T 191 ASQ, lililokuwa likiendeshwa na Bw. Ramadhan Omari (47).

Alisema katika ajali hiyo, watu wawili walijeruhiwa, ambao ni Bibi Mwajuma Hassan (29), mwanafunzi wa Chuo cha Ualimu Korogwe na Bi Rehema Khalifa (25), mkazi wa Unga Limited Arusha, ambaye aliumia mbavu za kushoto. Alisema dereva anashikiliwa na Polisi kwa uchunguzi.


Majira
 
Back
Top Bottom