Na Mwandishi Wetu
Ni skandali nyingine yenye uzani mkubwa kuzunguka Kanisa hususan kwa waumini wenye mlengo wa kilokole, baada ya kuibuka kwa tuhuma kwamba baadhi ya watumishi wa kiroho wanazitumia nafasi zao kupata pumziko la ngono kutoka kwa waumini wao...
Gazeti 5 Star kwa habari za mastaa, Risasi Jumamosi lina data za kiuchunguzi, malalamiko kutoka kwa waathirika pamoja na nukuu za wachungaji wanaothibitisha kuwepo kwa kamchezo hako na kuwanyooshea vidole baadhi ya watumishi wenzao kwamba wanahusika.
Kwa mujibu wa uchunguzi wetu pamoja na kauli za waathirika, baadhi ya watumishi wa kiroho wakiwemo Maaskofu, Wachungaji na Mitume wamekuwa wakiwageuza katuni waumini wao wa kike na kufanya nao mapenzi bila ridhaa yao kwa kuwafanyia ibada maalumu ya kupokea a.k.a Deliverance.
Uchunguzi unabainisha kwamba, watumishi hao huku wakitambua dhima waliyonayo katika kulipa afya neno la Mungu, huingia katika mtego wa dhambi kwa kuwarubuni waumini wao wanaofika mbele yao, madhabahuni wakitaka huduma.
Mmoja wa waumini ambao wamewahi kukumbwa na balaa la Deliverance (delivarensi) aliyejitambulisha kwa jina moja la Sophia, aliliambia gazeti hili hivi karibuni kuwa, alifika kwenye moja ya makanisa yenye mlengo wa kilokole, yaliyopo Wilayani Kinondoni, Dar na kujikuta mikononi mwa mtumishi mmoja maarufu.
Muumini huyo alisema kuwa, alikwenda kanisani hapo kwa lengo la kufanya sala ya toba lakini mchungaji huyo alipokuwa akimfanyia usaili, aliingiwa udenda juu yake, hivyo akamchomekea kuhusu huduma ya delivarensi.
Aliniambia nina dhambi nyingi, kwahiyo roho wa bwana amemwambia nahitaji sala ya kupokea, yaani delivarensi. Nikamwambia mchungaji mimi nipo tayari, akanijibu kama ndivyo basi huduma hiyo lazima ifanyike usiku katika mazingira ambayo sijayazoea.
Nilifikiri angeniambia kanisani lakini haikuwa hivyo, aliniambia nikapange chumba hoteli, halafu nimtaarifu. Nikamjibu sina pesa za kupanga chumba, yeye akaniambia mtumishi wa Mungu yupo, akatoa shilingi 100,000 akanipa, alisema muumini huyo.
Aliendelea kusema: Nilipanga chumba hoteli (jina tunaliminya) kisha nikamtaarifu, akaniambia nioge vizuri ili niwe safi kwa ajili ya kupokea. Akanisisitiza kuwa baada ya kuwa safi nisivae nguo yoyote zaidi ya kanga moja mpya. Nami nikatii.
Saa nne usiku mchungaji alifika hotelini hapo, mwanzoni akawa anaongea kwa kukemea mapepo yaniondoke, baadaye sauti ikawa inashuka, akawa ananisugua mgongo kama ananifanyia masaji, nilipohoji akaniambia hiyo ni sehemu ya ibada ya delivarensi.
Aliendelea kunisugua, akaniondoa kanga nikabaki bila nguo, akanisukumia kitandani. Nilipomuuliza akasema na yeye ni binadamu kama mimi, kwahiyo anaweza kuanguka dhambini lakini atatubu, akaningangania mpaka akatimiza haja zake.
Hata hivyo, jina la mtumishi huyo wa kiroho mwenye taito kubwa na waumini wa kumwaga, linabaki kwenye kuta za Risasi Jumamosi kwa sababu maalum.
Mbali na muumini huyo, gazeti hili lina maelezo ya kondoo mwingine ambaye lawama zake anazielekeza kwa mchungaji huyo huyo kuwa naye alimfanyia spesho delivarensi kwenye gesti moja iliyopo Kinondoni.
Muumini huyo aliliambia gazeti hili kuwa, alikwenda kwenye kanisa la mchungaji huyo akiwa na mchumba wake kwa lengo la kutaka baraka za kiroho kabla ya kuamua kufunga ndoa.
Tulipofika pale Mchungaji
(anamtaja jina) akaniambia mimi nilikuwa na tatizo la ndani ambalo lingesababisha ndoa yangu isidumu. Tukamuuliza cha kufanya akasema ni lazima nipokee sala ya delivarensi.
Akaniambia nipange chumba hoteli, niwe peke yangu halafu yeye atashirikiana na mimi kufanya delivarensi. Sikuwa na pesa yeye akanipa lakini usiku nikiwa chumbani alikuja, akanizuga mpaka tukafanya mapenzi, hiyo ilinikera sana.
Gazeti hili, pia lina eksheni ya mwanamuziki maarufu wa nyimbo za Injili (jina tunalo) ambaye naye aliingizwa mkenge na kufanyiwa delivarensi kwenye gesti moja iliyopo Kwaremi Sinza, jijini Dar es Salaam.
Habari zinasema kuwa, mwanamuziki huyo akiwa anasindikizwa na msaanii mwingine wa nyimbo za Mungu mwenye jina kubwa pia, alikwenda kanisani kwa mchungaji mmoja (naye anahifadhiwa) kwa ajili ya kufanya sala ya toba.
Chanzo chetu kinasema kuwa, baada ya mwanamuziki huyo kuzungumza na mchungaji, walikubaliana kwenda kufanya ibada ya delivarensi kwenye gesti hiyo.
Wakati mchungaji na
(anataja jina la mwanamuziki) wapo chumbani gesti, huyo mwanamuziki mwenzake alikuwa anamsubiria kwa nje, alisema mtoa habari wetu.
Katika moja ya mahubiri yake, Askofu Mkuu wa Full Gospel & Bible Fellowship, Zakaria Kakobe aliwahi kukemea tabia ya baadhi ya watumishi wa Mungu kwenda kuwafanyia maombi waumini kwenye vyumba vya peke yao.
Alisema kuwa, mtindo huo unaondoa utakatifu na kubakiza maswali yenye utata kujibika, akisisitiza kuwa, usafi daima ndiyo unaolinda ukristo.
Aidha, Kakobe aliwahi kusema ifike mahali makanisa ya kilokole yafe na kubaki makanisa yanayohubiri wokovu.
Mchungaji Daniel Rashid Gingo, alisema kuwa, wakristo wengi wamesahau kusoma Biblia na kuwaamini manabii ambao wengi wao ni wa uongo tofauti na mafundisho ya Yesu Kristo.
Wakristo wengi wamesahau Biblia, ndiyo maana wanakumbwa na udanganyifu wa delivarensi na baadhi ya watu wanaojiita watumishi wa Mungu, wengine wanafikia kuuziwa kipande cha sabuni shilingi 10,000 kwa kuambiwa kina upako wakati kipande hicho dukani ni shilingi mia moja, alisema Gingo.
Gingo ambaye pia ni mwandishi wa kitabu cha Wakristo Msidanganyike, aliendelea kusema: Ninachoomba Wakristo wenzangu tukae chini na kusoma Biblia, mimi naamini wewe mwenyewe ukifunga na kuomba kwa Mungu wako basi utapona ili mradi uwe umemkubali Muumba wako, tuachane na utapeli wa manabii waongo.
Wakati Mchungaji huyo akisema hayo, Askofu wa Huduma ya Neno la Upatanisho lililopo Kitunda Bustani ya Edeni (Matembele ya Kwanza Kivule), Nicolaus Suguye naye alikiri kuwa, baadhi ya watumishi wa Mungu wamekuwa wakifanya mambo yasiyompendeza Muumba wao.
Suguye alisema kuwa, leo hii baadhi ya watumishi wamekuwa wakitoa unabii wa uongo kwa kutumia msemo wa Roho wa Bwana amesema na kulaghai waumini wao na kujikuta wanaanguka katika dhambi ya uzinzi.
Mpakwa mafuta huyo wa Mungu aliwaomba watumishi wa kweli kusimama imara na kuwaombea watumishi wanaofanya mambo hayo maeneo ambayo si mazingira ya uwazi la sivyo Tanzania itaingia kwenye janga baya ambalo linaweza kusababisha madhara makubwa katika jamii.