security guard
JF-Expert Member
- Sep 27, 2011
- 799
- 603
SHUJAA
(Dr. Muhammed Seif Khatib)
Watu wenye ujasiri wawezao kuyakabili matatizo, au mateso ya wenzao bila woga au hofu ni adimu kuonekana. Watu hawa huitwa mashujaa. Siyo kuyakabili na kuyabwaga njiani, bali kuyatanzua. Watu kama hao nao ni wachache. Watu wa aina hiyo hufanya mambo makubwa na mazito ambayo huweka alama zisofutika katika jamii zao. Hujijengea heshima iliyotukuka. Shujaa wa kipekee aliyejijengea jina huko Zanzibar ni Abeid Amani Karume. Ametoka katika ukoo wa kimasikini. Alizaliwa Zanzibar, 04.08.1905 huko Mwera, Unguja. Yeye kama walivyo Waafrika wengi wa Unguja na Pemba katika nchi yao walikosa heshima na utu. Fursa ya elimu ndogo aliyoipata, kwa bahati haikumpa manufaa yoyote. Umasikini wake ulimlazimisha kutafuta maisha mjini tokea kijana mbichi. Alikuwa baharia katika meli za mizigo zilizompeleka kutembea nchi kadhaa za Ulaya, Marekani na Bara la Asia. Aliporudi Zanzibar akafanya kazi katika bandari ya Zanzibar. Mbali na shughuli zake za kikazi, Karume alikuwa na silka ya uongozi. Alikuwa kiongozi katika vilabu vya dansi, mabaharia, timu ya mpira na jumuia ya Waafrika. Mwaka 1954, Karume aliteuliwa kuwa diwani. Bila ya shaka huu ulikuwa ndiyo mwanzo wa kujiunga katika siasa waziwazi kwa ajili ya utetezi ya Waafrika wa Zanzibar. Zanzibar ilikuwa nchi ya matabaka, wachache wanacho na wengi hawanacho. Wao wachache wanamiliki njia kuu za uchumi na wengi ndio wazalishaji mali.
Waafrika wa Zanzibar katika nchi yao waliozawadiwa na Mungu, hawana ardhi, huku wageni wachache wanamiliki ardhi yote. Kasir, mahamamu, majengo ya serekali na mabalozi wa nchi za nje zimejengwa kwa mikono na nguvu za Waafrika. Mji Mkongwe wa leo umejengwa kwa mikono na migongo ya Waafrika. Vibarua wenyewe waliishi katika nyumba za matope na makuti huko ng’ambo ya mji. Kazi za wenyeji ni za vibarua, makuli, wachukuzi, maboi, matopasi na mayaya. Huduma za elimu, afya na maji safi kwao ni ndoto. Kuwepo wa Waingereza tokea mwaka 1886 hadi 1963, kulilinda utawala wa Sultan uliodumu kwa zaidi karne. Hali hii ilisababisha Waafrika wa Zanzibar wenye nchi yao kutawaliwa na dola mbili. Dola ya Mwingereza akimhami Sultani na mkururo wa ukoo wa El Busaidy kutoka Omani kuendelea nao kuwatawala wenyeji. Biashara ya kuagiza na kusafirisha nje ilishikwa na jumuia ya Kihindi. Bandari nayo ilishikwa na familia ya kihindi. Mahakimu na Majaji walikuwa jamaa wa Kiarabu na Kizungu. Wakuu wa Polisi walikuwa Wazungu na Waarabu. Skuli chache na serekali zilikuepo lakini nyingi zilikuwa za jamii ya Wahindi. Magazeti mengi yakimilikiwa na Waarabu, Wahindi au jumuia za kikabila. Mfumo mzima wa kiuchumi, kisiasa, kiulinzi, kimahakama na kiutawala uliwanyima Waafrika wa Zanzibar haki zao na uhuru. Waafrika wa Zanzibar walikuwa watumwa, watwana na wajakazi katika ardhi yao waliomegewa na Mungu. Mazingira haya ya kitabaka, unyonge na unyonyaji na uonevu yakandaa mazingira ya kuhitajika shujaa. Mwaka 1957, February 5, Waafrika wa Zanzibar waliogawika kwa hoja ya “Ushirazi” na “Uafrika” wakaamka na kuungana. Ni wakati Chama cha Afrio-Shirazi Party kilipoanzishwa na Abeid Amani Karume akiwa jemadari wake wa kudai uhuru. Safari ya ukombozi inaanzia hapa kwa kujipanga katika uchaguzi wa kusaka dola. Mazingira ya kihistoria ya kutawaliwa inawafanya Afro-Shirazi Party kukosa viongozi wasomi na wenye uzoefu katika siasa. Umasikini wa kipato wa wanachama wao ukilingaisha na uwezo wa kielimu na kipato wa chama kikuu cha upinzani ni mkubwa. Uhusiano wa kidugu na chama cha Waafrika wa Tanganyika TANU unawapa moyo sana Waafrika wa Zanzibar chini ya ASP. Chaguzi nne zinafanyika katika Zanzibar kati ya mwaka 1957 na 1963. Kila uchaguzi Afro-Shirazi inaongoza kwa kura na kwa majimbo lakini Waingereza na Sultan wanawanyima ASP kukabidhiwa dola. Tarehe 10/12/1963 serekali ya mseto wa vyama vya upinzani vya ZNP na ZPPP wanapewa serekali na Waziri Mkuu wake anakuwa Muhamed Shamte. Kitendo hiki kinawaumiza sana viongozi na wanachama wa Afro-Shirazi Party. Ni uonevu. Ni dhuluma.
Usiku wa manane wa siku ya Jumamosi tarehe 11:01:64, Karume anawaongoza viongozi wenzake na umma wa Waafrika wenye hasira, kuipindua serekali ya mseto na Usultan wa El Busaidy uliojikita Zanzibar tokeo mwaka 1830 hadi mwaka 1964. Ujasiri, ujabari na uthubutu wa Karume unawezesha Zanzibar na Waafrika wa Zanzibar kujikomboa na kuwa huru katika ardhi yao. Ni huyu Karume, akaona busara kuungana na Waafrika wenzake wa Tanganyika na kuunda Tanzania. Bila ya shaka ushujaa wa Karume unajengwa katika mambo yafuatayo. Kuamua kusahau tofauti za Waafrika kwa wale waitwao “Washirazi” na waitwao “Waafrika” na kuungana ili kuunda chama imara cha siasa kiitwacho Afro-Shirazi Party. Bila umoja na uimara wa chama cha siasa hiki, hadi leo Zanzibar ingekuwa chini ya Sultan Jamshed bin Abdulla. Uthubutu wa pili, ni kule kukubali na kushiriki katika mapinduzi dhidi ya dola yenye askari na silaha za moto. Na ushiriki huo ukafanikiwa kupindua serekali kwa saa chache na Sultan kutoroka kwa meli. Uthubutu wa tatu, unaoimarisha heshima yake, ni kule kukubali kuunganisha Zanzibar na Tanganyika na kuwa dola kubwa. Shujaa Karume katika maisha yake hakukosa maadui na wasaliti. Tarehe 07:04:72, saa 12 na dakika tano jioni, wahaini wanne wakiongozwa Humoud Barwani walimuuwa kikatili shujaa Karume kwa kumpiga risasi nyingi. Karume hakuwa na silaha Karume alikuwa akicheza dhumuna. Hamoud Barwani na wenzake wanapenda Waafrika wa Zanzibar waendelee kuwa watumwa, watwana na wajakazi katika ardhi yao? Hamoud Barwani na wenzake wanakerwa na hawakutaka “Sultan wao Jamshad El Busaidy” apinduliwe? Hamoud Barwana na wenzake wanakerwa kuona Zanzibar huru inaongozwa na Waafrika kutoka Afro-Shirazi Party? Kuuwawa kwa Karume hakujaondoa ari na shauku ya kuyaenzi na kuendeleza Mapinduzi ya Zanzibar. Karume bado atabaki kuwa shujaa aliyetukuka katika nyoyo za Waafrika wa Zanzibar.