Asha Abdala
JF-Expert Member
- Mar 21, 2007
- 1,130
- 44
Vijana CCM wataka Lowassa, Chenge waachie Ubunge
*Pia wamo Karamagi na Dkt. Msabaha
Na Mashaka Mhando,Tanga
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) mkoani Tanga umewataka viongozi wote wanaotuhumiwa kuhusika kwa namna yoyote na vitendo vya ufisadi kuachia mara moja nyadhifa zao za uongozi ndani ya chama ili kukinusuru na chuki dhidi ya umma.
Viongozi hao wametakiwa kukaa na kutafakari kama kweli bado wana uwezo wa kusimama majukwaani na kunadi sera na Ilani ya chama hicho mbele ya umma baada ya kukumbwa na kashfa hizo.
Akitoa tamko la Kamati ya Utekelezaji ya Umoja huo Mkoa wa Tanga kwa waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa UVCCM mkoani hapa, Bw. Emanuel Kiondo, alisema viongozi walioachia nyadhifa zao serikalini hivi karibuni kutokana na kashfa za ufisadi, wameendelea kubaki na madaraka makubwa ndani ya chama hicho jambo ambalo ni hatari katika kujenga imani ya umma.
Bw. Kiondo ambaye pia ni Katibu wa Idara ya Uenezi na Siasa Mkoa wa Tanga, alisema viongozi hao hawana budi kutafakari upya na kupime kama bado wanaheshima ya kusimama mbele ya jamii na kunadi sera bora na Ilani ya CCM na kama hawataaminiwa, wajiondoe haraka.
"Kuachia ofisi za serikali hakutoshi, bado wengine ni wajumbe wa Kamati Kuu, Halmashauri Kuu, wabunge na hata Kamati ya Madili na hizo zote ni ofisi za umma...Kwa kuwa CCM ndicho chama kikongwe na wananchi wengi wanakitegemea kutoa mwongozo na mwelekeo wa Tanzania ya leo na ijayo, tunawaomba wote waliojiuzulu nafasi zao serikalini wafanye hivyo kwenye chama ili kukinusuru kusemwa vibaya," alisema Bw. Kiondo.
Mwenyekiti huyo huku akinukuu mifano mingi kutoka katika vitabu mbalimbali vya marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Dkt. Ibrahim Kaduma, alisema viongozi hao kwa kuziachia nafasi zao za uongozi ndani ya chama kutasaidia kupunguza kilio cha wanachama, wapenzi na mashabiki wa chama hicho.
Alisema wakijiondoa watakuwa wamekubali kujisafisha na kukinusuru chama chao na wakati huo huo kumuenzi Mwalimu Nyerere katika kutoa maamuzi mazito likimwemo la kukubali kukosolewa na kujikosoa.
Miongoni mwa viongozi waliowajibika hivi karibuni kutokana na kashfa mbalimbali ni pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu, Bw. Edward Lowassa aliyeachia wadhifa huo kwa kashfa ya Richmond sambamba na mawaziri wengine wawili, Bw. Mustafa Karamagi aliyekuwa Waziri wa Madini na Nishati na Dkt. Ibrahim Msabaha aliyekuwa Waziri wa Afrika Masharki.
Waziri wa Miundombinu, Bw. Andrew Chenge pia alijizulu kutokana na kashfa ya ununuzi wa rada iliyomhusisha na kutunza mabilioni ya fedha kwenye akaunti yake nje ya nchi.
Katika hatua nyingine, UVCCM Tanga imekitaka Chama cha Wananchi (CUF) kukubali kwenda kwa wananchi kupata maoni yao juu ya kumaliza mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar na kukaa meza moja na CCM kupata ufumbuzi wa tatizo hilo.
"Kitendo cha CUF kukataa kwenda kwa wananchi ili watoe maoni yao si cha kiungwana hata kidogo, wanapingana na jina la chama chenyewe, 'Chama cha Wananchi' halafu wanaogopa kwenda kwa wananchi hao hao," alisema Bw. Kiondo.
Bw. Kiondo alisema UVCCM inapinga kauli ya CUF kutaka Rais Jakaya Kikwete naye ajiuzulu kwa tuhuma za ufisadi na kukariri maneno ya Mwalimu Nyerere kuwa "Kuwajibika kuna ngazi zake, hatuwezi kusema mtendaji akifanya kosa Rais ajiuzulu, hapana aliyetenda kosa likathibitika awajibike mwenyewe."
Aliwataka Watanzania kutambua kwamba CCM ni kama familia kubwa wanamozaliwa watu wenye hekima , waadilifu, vilema, mataahira, majambazi, vichaa na wengine hivyo si busara watu kuisakama familia hiyo kwa kuwepo jambazi moja wakati kuna wengi wenye hekima zao.
Alitetea kuwa CCM imekuwa na viongozi wengi wenye busara na uadilifu mkubwa na kuongeza kuwa chama hicho ni kikubwa ndio maana Rais Kikwete hivi karibuni alikaririwa akisema umefika wakati wa kutenganisha siasa na biashara.
majira
As if they are serious vile! Hawa si ndio waliotoa kauli za kebehi baada ya ufisadi kuibuliwa wakisema kuwa ni uwongo mtupu na hila za upinzani kujitafutia umaarufu? Wakamwambie kwanza boss wao Amos Makala aombe radhi kwa Dr Slaa kwa maneno yake ya dhihaka baada ya list of shame kumwaga hadharani. Na hawa CCM Tanga si ndio waliandamana kabisa? hebu mwenye kumbukumbu azimwage hapa.
Yangu macho, labda wamrudia Allah
Asha