Rutashubanyuma
JF-Expert Member
- Sep 24, 2010
- 219,470
- 911,174
Karume: Kanisa halina haki umiliki wa kiwanja
Imeandikwa na Mwandishi Wetu, Zanzibar; Tarehe: 1st January 2011 @ 23:55
MGOGORO wa kiwanja kati ya Kanisa la Anglikana Zanzibar na Fatma Karume, binti wa Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, umechukua sura mpya baada ya Rais huyo mstaafu kudai, kwamba kiwanja hicho ni mali halali ya binti yake.
Mbali ya kueleza hayo, amevilalamikia pia vyombo vya habari, ikiwamo Televisheni ya Taifa Zanzibar (TVZ) kwa upotoshaji, huku akiitaka kuomba radhi na kutishia kuyashitaki baadhi ya magazeti.
Karume aliyemaliza miaka 10 ya urais wa Zanzibar Oktoba mwaka huu, alisema hayo jana
wakati wa mkutano na wanahabari uliofanyika nyumbani kwake Mbweni, mjini hapa.
Katika mkutano huo ambao Karume alitumia muda mwingi kuonesha jinsi Kanisa linavyolazimisha kutaka kutambuliwa kuwa wamiliki wa eneo hilo, alisema:
"Zimekuwapo habari za kupotosha, bahati mbaya waandishi wa habari hawajatupa nafasi ya kujibu suala hilo."
Akiwa na binti yake, Fatma, ambaye yuko katika mgogoro wa kiwanja na Kanisa hilo, Karume alisema Kanisa halina haki na kiwanja hicho.
"Nimekuwa nikilihudumia Kanisa, hata lilipokuwa limetelekezwa miaka iliyopita. Kanisa la Anglikana limekuwa jirani yetu tangu mwaka 1968, na mimi binafsi naliheshimu.
Fatma anamiliki kisheria kiwanja hiki na anaheshimu eneo la makaburi lililopo jirani," alisisitiza Karume aliyewashutumu viongozi wa Kanisa hilo kwa kutoheshimu maadili.
Akifafanua zaidi kwa kutoa ushahidi wa kihistoria kuhusu umiliki wa kiwanja hicho tangu mwaka 1932, Karume alisema viongozi wa Kanisa na waumini wake, walifanya kosa kuvamia kiwanja kufanya maombi kabla ya kuharibu baadhi ya vifaa vya ujenzi vilivyokuwa katika eneo hilo Katika mkutano huo na wanahabari, Fatma ambaye ni mwanasheria kitaaluma, alikuwa miongoni mwa waliohudhuria, kama ilivyokuwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar, Ali Mwinyikai na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Abdallah Mwinyi.
Karume alilazimika kuzungumzia mgogoro huo, baada ya jana baadhi ya vyombo vya habari kuripoti juu ya kundi la waumini wa Kanisa hilo, kuvamia eneo la kiwanja hicho wakidai ni chao na kung'oa vigingi vilivyokuwa vimewekwa katika eneo la ujenzi ili kuonesha hasira zao.
"Tunang'oa na kuharibu vigingi hivi ili kuzuia ujenzi katika kiwanja hiki, kinamilikiwa na Kanisa na tumekuwa tunakimiliki tangu enzi za Wakoloni miaka ya 1920," walisikika wakisema baadhi ya waumini hao mara baada ya kufanya maombi ya dakika 10 yaliyoongozwa na Padri Mathew Mhagama.
Mhagama alipaza sauti akishutumu uvamizi wa kiwanja hicho kinyume cha sheria na uharibifu uliofanywa katika eneo la makaburi wakati wa ujenzi.
"Tumekuwa tukiomba hatimiliki tangu mwaka 1980 kama mbadala wa karatasi tulizokuwa nazo tangu miaka ya 1930," alisisitiza.
Karibu waumini 50 walikusanyika katika Kanisa lao eneo la Mbweni kabla ya kuandamana kwenda eneo hilo la kiwanja lenye ukubwa wa ekari 2.5 ufukweni mwa bahari ya Hindi ambapo walifanya maombi kushutumu kuchukuliwa kwa kiwanja chao ambacho kiko karibu na makazi ya Rais huyo mstaafu