Bunge limeelezwa zaidi ya Dola za Marekani 1.25 bilioni sawa na Sh2 trilioni hutoroshwa na kupelekwa nje ya nchi kila mwaka kwa lengo la kukwepa kodi.
Taarifa hiyo imetolewa wakati wingu zito likiwa limegubika uwasilishaji wa ripoti ya kikosi kazi cha Serikali kilichochunguza sakata la Sh315 bilioni zilizofichwa na Watanzania katika mabenki nchini Uswisi.
Takwimu hizo zilitolewa juzi na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe.
Zitto alisema taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwa Tanzania inapoteza kila mwaka mapato hayo ambayo ni sawa na asilimia tano ya Pato la Taifa kupitia uhamishaji huo haramu.
Uhamishaji huu haramu wa fedha kupelekwa nje ya nchi hufanywa kwa lengo la kukwepa kulipa kodi au wahusika kuepuka kukamatwa na fedha walizopata kwa kupokea rushwa, alisema Zitto.
Kamati hiyo imependekeza Bunge kutunga sheria itakayodhibiti uhamishaji haramu au ufichaji wa fedha nje ya kwa lengo la kuogopa kukamatwa na rushwa, kufanya ufisadi na kukwepa kodi.
Zitto alisema hayo ni moja ya maazimio yaliyofikiwa katika mkutano wa 10 wa Jumuiya ya Kamati za Hesabu za Serikali za Mabunge (Sadcopac) ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc).
Alisema katika mkutano huo uliofanyika Septemba 2 hadi 7, mwaka huu Jijini Arusha, wajumbe waliazimia kuhamasisha mabunge ya nchi zao kutunga sheria kudhibiti uhamishaji huo wa fedha.
Wiki iliyopita, mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM), alikaririwa akisema bungeni hapatatosha kama ripoti ya mabilioni ya Uswisi haitawasilishwa katika Bunge hili.
Mpina alisema yeye ni miongoni mwa wabunge waliohojiwa baada ya kutamka bungeni kuwa zaidi ya Sh11.9 trilioni zimetoroshwa kutoka Tanzania kati ya mwaka 1970 na mwaka 2008.
Nilipolisema hilo jambo niliikabidhi Serikali kupitia Bunge taarifa za tafiti mbalimbali ili ifuatilie. Baadaye Zitto akaja na hoja ya bilioni 314
tunataka taarifa hatutanii, alisema.
Ripoti hiyo ilikuwa iwasilishwe Bunge la Aprili lakini Serikali ikaomba muda zaidi na kuahidi kuiwasilisha katika Mkutano wa 14 wa Bunge unaoendelea Mjini Dodoma.
Hata hivyo, Mpina alionyesha shaka kama ripoti hiyo itawasilishwa akisema hata ratiba ya Bunge haionyeshi suala hilo wala katika kikao cha kupeana taarifa cha wabunge suala hilo halikugusiwa.
Mwanasheria Mkuu Jaji Frederick Werema alipoulizwa endapo kikosi kazi anachokiongoza kimekamilisha kazi yake alisema: Bado kazi inaendelea na ni ngumu
tunaendelea na uchunguzi.
Agosti 15 mwaka jana, kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, iliitaka Serikali kuwataja kwa majina viongozi na wafanyabiashara wakubwa walioficha Sh315.5 bilioni katika mabenki nchini Uswisi.
Wakati huo huo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Hesabu za Serikali Kuu na Mashirika ya Umma (PAC), imefichua udanganyifu na mianya mikubwa ya ukwepaji kodi katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema), aliliambia Bunge mwishoni mwa wiki kuwa pamoja na TRA kufikia malengo kwenye makusanyo ya kodi katika mwaka wa fedha wa 2011/12, bado kumekuwapo na udanganyifu na mianya ya ukwepaji wa kulipa kodi katika maeneo kadhaa.
Aliyataja maeneo hayo kuwa ni kusitishwa kwa matumizi ya mita za kupima ujazo wa mafuta yanayoingia nchini kupitia kituo cha kupakulia mafuta cha Kurasini, jijini Dar es Salaam.
Alisema kamati yake imeitaka Serikali kulieleza Bunge sababu za msingi za kusitisha matumizi ya mita hizo na TRA kuainisha athari katika ukusanyaji wa mapato itokanayo na kusitishwa kwa matumizi ya mita hizo.
Alisema mpaka sasa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) baada ya kusitishwa kwa matumizi ya mita hizo inatumia vijiti vya kupimia ambavyo vipimo huchukuliwa wakati mafuta yako kwenye meli na baada ya kuwekwa kwenye matangi ya wafanyabiashara walioyaingiza mafuta hayo.
Alisema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika taarifa yake ya 2010/11 alihoji kuhusu sababu za kusitisha matumizi ya mita kupima ujazo wa mafuta katika bandari za Tanga na Dar es Salaam na hivyo kusababisha hasara kwa Serikali kwa kufanya manunuzi yasiyo na tija.
Alifafanua kuwa kamati yake iliwahoji maofisa masuuli wa TPA aliyeeleza kuwa mita hizo zilinunuliwa mwaka 2004 na TPA na kufungwa katika kituo cha kupakulia mafuta cha Kurasini (KOJ) mwaka 2004 na kuanza kutumia mwaka 2005 kwa lengo la kupima kiwango cha mafuta yanayoingizwa nchini kupitia Bandari za Tanga na Dar es Salaam.
Hata hivyo, alisema ilipofika Februari 2011, Wakala wa Vipimo nchini (WMA), iliyoridhia awali matumizi ya mita hizo, iliwaandikia TPA kusitisha matumizi ya mita hizo kwa sababu zimethibitika kutoa vipimo visivyo sahihi hivyo kusababisha walipa kodi kulalamika.
Zitto alisema wakati TPA ikisema mita hizo hazina matatizo yo yote na zinaweza kuendelea kutumika, WMA wanasisitiza kuwa mita hizo hazitoi vipimo sahihi vya ujazo wa mafuta na kusababisha malalamiko mengi kutoka kwa TRA na wafanyabiashara ambao wamekuwa wakilipa kodi kubwa kutokana na vipimo visivyo sahihi vya ujazo wa mafuta vinavyosomwa na mita hizo.
Hata hivyo, alisema TRA walishindwa kuieleza Kamati jinsi ambavyo usitishaji wa matumizi ya mita hizo umeathiri upatikanaji wa mapato yatokanayo na kodi ya kuingiza mafuta nchini.
Maeneo mengine yenye udanganyifu ni mkataba wenye utata wa leseni za udereva, ambapo mkataba wa utengenezaji wa leseni za udereva uliingiwa kati ya TRA na kampuni ya M/s Track Innovations Ltd (OIT) ya Israel.
Alisema kamati ilibaini kasoro kadhaa katika baadhi ya vipengele vya masharti ya mkataba ambazo zinaiweka Serikali katika hatari ya kupoteza mapato makubwa.
Alisema mkataba huo ulihusu kubuni na kutengeneza mfumo wa kielektroniki wa utengenezaji wa leseni za udereva na makubaliano yalikuwa ni kutengeneza leseni za udereva 800,000 na tayari hadi kamati inakagua Machi, mwaka huu, leseni 681,850 zilikuwa zimetengenezwa na mkataba ulitegemewa kukamilika mwezi uliopita.
Alisema eneo lingine la upotevu wa kodi ni katika sekta ya mawasiliano kama TRA kukokotoa Kodi ya Ongezeko la Thamani na ushuru wa bidhaa kwa kutumia taarifa zinazotolewa na kampuni za simu pekee bila kuoanisha na taarifa za Mamlaka ya Usimamizi wa Mawasiliano (TCRA).
Alisema kwa mfano, katika mwaka wa fedha 2011/12, Kampuni ya Airtel ilikuwa na trafiki ya dakika 4,847,642,069 zinazoweza kutozwa Vat na ushuru wa bidhaa, lakini kampuni ilionyesha dakika 4,233,637,174 tu ambayo ni tofauti na dakika 614,004,885.
Alisema TRA imekiri kutoshirikiana katika kutafuta taarifa zilizosahihi kwa ajili ya ukokotoaji wa kodi lakini TCRA waliiarifu Kamati kuwa wamenunua mtambo utakaotumiwa na TCRA na TRA katika kutambua aina, kiasi halisi na thamani ya miamala inayofanywa na kampuni za simu.
Kwa hisani ya Mwananchi na Nipashe.