Zigo la Jairo lazoa vigogo; Luhanjo, CAG Utouh, Ngeleja kuhojiwa

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,796
Wednesday, September 14, 2011Mwandishi Wetu
14 Sep 2011
Toleo na 203
  • ngeleja-jairo.jpg
  • hanjo, CAG Utouh, Ngeleja kuhojiwa
  • Wamo pia vigogo kadhaa serikalini
MOTO wa sakata linalomhusu aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, la uchangishaji fedha za kulainisha wabunge, sasa umesambaa hadi wizara nyingine kutokana na hatua ya Kamati Teule ya Bunge kupanua wigo wa kuhoji vigogo katika wizara hizo, Raia Mwema, imethibitishiwa.

Habari za uhakika zimeeleza wiki hii kwamba mahojiano hayo yalianza juzi Jumatatu na hadi tukienda mitamboni jana Jumanne, Kamati ilikwishakuwahoji watu mbalimbali, wakiwamo baadhi ya viongozi waandamizi serikalini.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili zinabainisha pia ya kuwa wanaotarajiwa kuitwa kwenye kamati hiyo kwa ajili ya kuhojiwa mbali na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, kwenye orodha wamo pia Jairo mwenyewe, Katibu Mkuu Kiongozi Philemon Luhanjo na Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo.

Habari hizo zinasema pia kwamba kwenye orodha hiyo yumo pia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, ambaye ripoti yake ndiyo iliyotumiwa na Luhanjo kumsafisha Jairo katika hatua iliyolikera Bunge na ambayo ndiyo iliyochochea kuundwa kwa Kamati Teule.

Akitumia, na mara kadhaa akinukuu ripoti hiyo ya CAG, Luhanjo alisema CAG hakumkuta Jairo na kosa lolote ambalo lingemlazimisha yeye Luhanjo kuanzisha shauri dhidi ya Jairo, na kwamba kwa ajili hiyo, alikuwa anaamuru Jairo arejee kazini mara moja.

Akizungumza na Raia Mwema wiki hii, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Teule ya Bunge, Mbunge wa Tunduru Kaskazini Mhandisi Ramo Makani, alithibitisha kuanza kwa mahojiano hayo Jumatatu wiki hii na kwamba, viongozi kadhaa wataendelea kuhojiwa kulingana na hadidu rejea za kamati hiyo.

Hata hivyo, Mwenyekiti huyo hakuwa tayari kutaja orodha kamili ya vigogo hao kwa majina, ingawa pia Raia Mwema, limearifiwa baadhi ya majina ya watakaohojiwa.
Kamati hiyo mbali na Magani inaundwa na Mbunge wa Karagwe, Goesbert Blandes; Mbunge wa Karatu, Mchungaji Israel Natse; Mbunge wa Gando, Khalifa Suleiman Khalifa na Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Jachi Umbulla.

Katika mazungumzo hayo na Raia Mwema Makanialieleza kuwa hadi sasa kamati yake haijaweka ukomo wa idadi ya watu watakaohojiwa na kwamba idadi hiyo itaamuliwa kwa kadiri taarifa za kina zinazohitajika zitakavyokuwa zikipatikana kutoka kwa wanaohojiwa.

"Unajua hatuwezi kuweka ukomo wa idadi. Kwa sababu unaweza kupanga kuwahoji watu wanne lakini kwa kadiri mahojiano yanavyokwenda unaweza kuridhika wawili tu wa mwanzo uliowahoji wanatosha au unaweza kuweka idadi hiyo lakini taarifa utakazopata zikakuelekeza kuwa unahitaji kuhoji watu wengine wengi zaidi. Kwa hiyo hatukuweka idadi kamili bali hii itategemea na mwenendo wa mahojiano," alisema Makani na kuongeza;

"Tutawahoji pia watu waliobobea katika taaluma ya utawala. Wapo tutakaowahoji kutokana na ushiriki wao katika suala zima tunalochunguza. Hapa tutakuwa nao pia viongozi wa kada mbalimbali serikalini. Kwa hiyo hatuna idadi kamili lakini tunayo ratiba yetu maalumu."

Kamati hiyo teule ya Bunge iliundwa kutokana na Azimio la Bunge la Agosti 24, mwaka 2011, ambalo lilitaka kuundwa kwa kamati hiyo teule kwa ajili ya kuchunguza uhalali wa utaratibu wa Wizara ya Nishati na Madini, kuchangisha fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti na kubaini kama kitendo cha Katibu Mkuu Kiongozi, kutoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya uchunguzi wa suala la fedha zilizokuwa zikichangishwa na wizara hiyo, kimeingilia na kuathiri madaraka ya Bunge.

Kamati hiyo teule ya Bunge imeundwa kwa mujibu wa kanuni ya 2(2) na 117(4) ya Kanuni za Bunge toleo la mwaka 2007, ikiwa na hadidu rejea mahsusi ambazo ni, kuchunguza utaratibu uliobainika wa kukusanya fedha kwa ajili ya kukamilishwa kwa uwasilishaji wa hotuba za bajeti za wizara bungeni.


Kuchunguza uhalali wa utaratibu huo kisheria na kwa mujibu wa kanuni, iwapo fedha hizo huwa zinakasimiwa katika bajeti husika pamoja na matumizi halisi ya fedha zilizokusanywa.


Kupitia taarifa ya CAG kuhusu uchunguzi alioufanya kuhusiana na agizo la Katibu Mkuu Kiongozi juu ya Jairo, kuchangisha fedha taasisi zilizo chini ya wizara hiyo ili kufanikisha uwasilishaji wa bajeti ya wizara Bungeni.


Kuchunguza mfumo wa Serikali kujibu hoja zinazotolewa bungeni na taratibu za kuarifu Bunge matokeo ya utekelezaji wa hoja hizo.


Hadidu nyingine ni kuchunguzwa kwa usahihi wa utaratibu uliotumiwa na Katibu
Mkuu Kiongozi kwa suala la Jairo na kubaini iwapo utaratibu huo umeathiri dhana ya haki na madaraka ya Bunge. Kuangalia nafasi ya Mamlaka ya Uteuzi kwa ngazi za Makatibu Wakuu katika kushughulikia masuala ya nidhamu ya anaowateua. Nyingine ni kuangalia mambo mengine yoyote yenye uhusiano na uchunguzi huo.


Wakati akitangaza wajumbe wa kamati hiyo pamoja na hadidu rejea Agosti 26, mwaka huu, muda mfupi kabla ya kuahirishwa kwa mkutano wa nane wa Bunge la 10, mjini Dodoma, Spika Anne Makinda, alisema; "Ni imani yangu na ya wabunge wote na Watanzania wote kwa ujumla kwamba ninyi niliowateua mtafanya kazi hii kwa umakini, busara na uaminifu mkubwa mkiongozwa na Katiba ya nchi, sheria na kanuni zetu na vilevile mtatoa haki kwa watu wote watakaohusika na suala hili."


Kabla ya kuundwa kwa kamati hiyo, suala la Jairo lilikuwa likipata sura tofauti kila baada ya siku chache, na kati ya matukio hayo ni pamoja na Rais Jakaya Kikwete kutengua uamuzi wa Katibu Mkuu Kiongozi, Luhanjo, kumrejesha kazini Jairo ambaye awali ndiye aliyemsimamisha kazi kupitisha uchunguzi ambao Luhanjo, alimteua Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuchunguza ukusanyaji fedha.


Katika uchunguzi wa awali uliofanywa na CAG, ambao ulitangazwa na Luhanjo, Jairo hakupatikana na hatia na hivyo kutakiwa kurudi kazini kuanzia.


Hatua hiyo ilipingwa na wabunge akiwamo Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka, aliyeomba Bunge liunde kamati teule kuchunguza suala hilo.


Katika uchunguzi huo Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo naye aliingia mtegoni baada ya kuutangazia umma kile alichokiita uchunguzi ambao ulimsafisha Jairo na kuamua kumrudisha kazini kabla ya Rais Jakaya Kikwete kutengua uamuzi, huku Bunge likiunda Kamati Teule baada ya kukerwa na hatua hiyo.


Taarifa nyingine zilizopatikana jana Jumanne zikikariri gazeti la Mwananchi, zinasema kwamba kabla ya sakata hilo la Jairo, Serikali ilikwishakutoa waraka wa kuzuia utaratibu wa wizara kuchangisha taasisi zake.


Kwa mujibu wa uchunguzi wa gazeti hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Ramadhani Khijjah, alitoa waraka maalumu kwa makatibu wakuu wa wizara zote unaowazuia kuchangisha au kupokea fedha kutoka taasisi zilizo chini yake kwa sababu yeyote ile.


Kwa mujibu wa Mwananchi waraka huo ni namba 3 wa Machi 7, mwaka huu, wenye kumbukumbu namba TYC/A/400/620/18, unaonyesha kuwa hatua hiyo ilifikiwa baada ya kuonekana kwamba baadhi ya mashirika na taasisi za umma zinatoa ruzuku au mikopo kwa wizara, bila kuzingatia taratibu na sheria.


Kwa mujibu wa waraka huo, makatibu wakuu wa wizara, wakuu wa mashirika na taasisi za umma ambao wangeshindwa kuzingatia agizo hilo, wangechukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa kanuni na taratibu zilizowekwa.


"Kwa kuzingatia misingi hiyo, wizara haipaswi kupewa fedha za ziada kupitia mashirika na taasisi zilizo chini yake," unaeleza waraka huo ambao Mwananchi limesema limeuona.


Kwa mujibu wa Mwananchi waraka huo unaeleza zaidi: "Endapo kutatokea mahitaji yatakayolazimu wizara kuzichangisha fedha taasisi zilizo chini yake, mashirika au taasisi za umma, lazima ipate kibali cha Waziri wa Fedha baada ya kushauriwa na Mlipaji Mkuu wa Serikali (PMG) na Msajili wa Hazina kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2008."


Mbali na kutumwa kwenye wizara mbalimbali, waraka huo ulitumwa pia kwa Katibu Mkuu Kiongozi Ikulu, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).


Kamati hiyo teule ya Bunge ni ya kwanza katika Bunge hili la 10, ikiwa imetanguliwa na Kamati teule pekee iliyoundwa katika Bunge la tisa, iliyosababisha kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, Februari 7, mwaka 2008.


Mbali na Lowassa, mawaziri wengine wawili walijiuzulu hao ni waliopata kuongoza Wizara ya Nishati na Madini, kwa nyakati tofauti; Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi walioguswa katika kashfa ya utoaji zabuni ya kufua umeme kwa kampuni ya Richmond.


Kamati hiyo teule iliongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe, ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri wa Ujenzi.


 
At least natamani ije na style kama ile ya Richmond vile, ila wa kujiuzulu awe JK
 
Mimi sioni haja ya hii kamati ni kupoteza muda na fedha za walipa kodi bure.
 
dah! sasa kama kunawaraka ulitolewa kuzuia kuchangisha michango kutoka kwenye taasisi zilizo chini ya wizara husika kwanini waweka kamati?
hapo kulikuwa hakuna haja ya kamati ni hukumu tu basi!
 
Kuhojia na kuzolewa ni kitu kimoja? Heading na habari haviendani kabisa
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom