Zifahamu Supermarket 20 bora duniani

Damaso

JF-Expert Member
Jul 18, 2018
1,590
2,090
Imekuwa ni suala la kawaida kusikia mijadala ya supermarket ipi ni kubwa kuliko nyingine, na kuhusu supermarket zilizopo hapa nyumbani, ni wazi tumepata kuwa na supermarket kama vile Game supermarket, Nono’s supermarket, TSN supermarket, Nakumat supermarket na kadhalika ila ukienda duniani huko kuna maduka makubwa sana ya supermarket ambayo yanauza mamilioni ya bidhaa kuanzia chakula, vinywaji, bidhaa za ndani, vifaa vya usafi, mavazi, na kadhalika.
Karibu tupate kuona supermarket ishirini bora duniani;
IMG_1680.jpg


1. Metro Cash & Carry
Metro Cash & Carry ni Supermarket kubwa ya Kijerumani ambalo ilianza kazi rasmi mnamo mwaka 1964, yaani miaka 59 kwenye biashara huku makao makuu yakiwa huko huko Ujerumani, ni Supermarket ambayo kwa Ujerumani inashika namba moja kwenye uuzaji wa bidhaa za nyumbani ambazo kitaalamu sio bidhaa za kudumu sana, huku wateja wake wakubwa wakiwa ni wamiliki wa mahoteli, migahawa pamoja na wafanya biashara wadogo wadogo.
IMG_1659.jpg


2. Walmart Inc
Walmart kutoka Marekani ni Supermarket kubwa sana ndani ya Marekani na duniani, huku ikiwa na makao makuu yake pale kwenye jimbo la Arkansas huku ikishika nafasi ya kwanza kwa kuwa mwajiri nambari moja kwa kuajiri watu wengi ndani ya Marekani. Upande wa mapato, Walmart ikiwa imesambaa ndani ya nchi zaidi ya 30 inaongoza kidunia kwa kuwa supermarket nambari moja huku ikiwa na jumla ya maduka makubwa zaidi ya 11600 duniani kote.
IMG_1660.jpg


3. Woolworths Supermarkets
Tutoke Marekani na twende mpaka Australia ambapo tunakutana na Supermarket kubwa ya Woolworths ambayo ni sehemu ya kampuni kubwa ya Woolworths Group iliyoanzishwa mwaka 1924, ukifika kwenye Supermarket za Woolworths basi utakutana na bidhaa nyingi sana kama vile, vipodozi, vyombo vya majumbani, viandikia, bidhaa za watoto na kadhalika, ingawa kwa upana zaidi Woolworths wamelenga kuuza vinywaji baridi na moto. Woolworths wamesambaa kwenye nchi takribani 24 huku wakiwa na maduka makubwa zaidi ya 950 duniani nzima.
IMG_1661.jpg


4. LuLu Group International
Tuondoka taratibu Australia na tusogee juu kwa waarabu na Tukutane na Supermarket za LuLu ambazo makao makuu yake yapo huko kwenye Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE, ingawa biashara hii ni mali ya mhindi tu, lakini makao makuu yapo pale kwenye Jiji la Abu Dhabi. LuLu iliorodheshwa kuwa ni moja kati ya biashara 50 bora zenye Uchumi unaokua kwa kasi zaidi duniani huku ikiwa na maduka makubwa 200 tu duniani kote, LuLu ndo Supermarkets kubwa zaidi kwa upande wa bara la Asia pamoja na mashariki ya Kati.
IMG_1669.jpg


5. Carrefour
Tuwaache waarabu na twende mpaka Ulaya na miguu yetu ifike pale Ufaransa ambapo tunakutana na Supermarket kubwa za Carrefour ambazo zilianza kazi rasmi tokea mwaka 1958, supermarket hizi haziuzi kila kitu na zinauza bidhaa maalumu tu, mfano Carrefour wanauza bidhaa za kubeba na kutunzia fedha pamoja na bidhaa za majumba ya uhifadhi wa vitu, ukiingia Carrefour hakuna chakula Kwa wale mashabiki wa misosi basi tulieni kuna supermarkets nyingine zinakuja mbeleni huko, tulia tu utazifahamu. Carrefour wamekuwa wabunifu sana kiasi kwamba wameanza kutengeneza bidhaa zao ambazo wamekuwa wakiziuza kwa bei nafuu zaidi, mpaka sasa Carrefour anawakimbiza wenzake kwa mwendokasi mkubwa sana.
IMG_1670.jpg



6. 7-Eleven
Tuondoke Ufaransa na turejee tena Marekani ambapo tunakutana na Supermarkets za 7- Eleven ambazo ni Supermarket zenye ushirikiano baina ya wanahisa kutoka Marekani na Japani, biashara yao ilianza mwaka 1927 na makao makuu yapo pale kwenye Mji wa Dallas katika Jimbo la Texas. 7-Eleven ni supermarket nambari moja kwa supermarkets ambazo zinatoa huduma ndani ya nchi ya Japani. Wao wanajihusisha zaidi na uuzaji wa bidhaa kama mafuta ya diesel na petrol kwa upande wa nje, huku kwa upande wa ndani utakutana na vikapu na makabati mazuri sana yakiwa na pipi, kahawa, bidhaa za maziwa, mikate na kadhalika. 7-Eleven wamesambaa kwenye nchi zaidi ya 20 huku wakiwa wamechukua leseni ya bidhaa zaidi ya elfu saba kwenye nchi hizo.
IMG_1671.jpg



7. FamilyMart
Tubaki huko Japani na tuelekee mpaka kwenye supermarket ya FamilyMart ambayo hii inashika nafasi ya pili nyuma ya supermarket ya 7-Eleven ndani ya Japani. FamilyMart imeweka makao makuu yake ndani ya jiji la Tokyo huku wakianza biashara tokea mwaka 1973, mpaka sasa wana supermarket zaidi 24260 dunia nzima, na lesenei ya bidhaa zaidi ya elfu mbili. FamilyMart wamejidhatiti zaidi katika uuzaji wa vinywaji baridi na moto, magazeti na majarida, vitabu vya hadithi pamoja na bidhaa za ndani. Mpaka sasa FamilyMart ni moja kati ya supermarket bora sana duniani ambazo biashara zake zinazokua kwa kasi sana.
IMG_1672.jpg



8. Lidl
Tuondoke Japani na tuelekee Ujerumani amba[p tunakutana na Supermarkets za Lidl ambazo zilianza kazi rasmi mwaka 1930 na zikaweka makao makuu yake pale Neckarsulm, Ujerumani. Kwa sasa Lidl ina jumla ya ofisi zaidi ya 28500 ndani ya bara la Ulaya pamoja na Marekani tu, ukijumulisha pamoja na zingine maeneo mengine basi hesabu yake itakuwa ni ofisi 30000, na kwa mwenendo wa biashara ya Lidl basi inatosha kumuweka nafasi ya tano ya supermarket kubwa duniani.
IMG_1673.jpg



9. SPAR
Tuondoke Ujerumani na tuelekee huko Uholanzi na Tukutane na supermarket za SPAR ambazo zina makao makuu yake pale kwenye Jiji la Amsterdam ambazo zilianza kazi tokea mwaka 1932. Mpaka sasa zimesambaa kwenye Supermarket zaidi ya 13200 dunia nzima, hawa SPAR wanamiliki Supermarket pamoja na Hypermarkets kwenye nchi tofauti tofauti zaidi ya 28 huku bidhaa zao kubwa ikiwa ni vinywaji pamoja na silaha.
IMG_1674.jpg



10. Tesco
Tutoke Uholanzi na twende Uingereza na kukutana na Tesco ambalo ni kampuni ya Kiingereza iliyoanza kazi tokea mwaka 1919 na makao makuu yakiwa pale Hertfordshire, katika kuangalia mapato na faida za Supermarket duniani basi Tesco ilishika nafasi ya tisa kwa supermarket kubwa, huku ikiwa na maduka makubwa zaidi ya 6900 ndani ya Ulaya pamoja na sehemu kubwa ya bara la Asia.
IMG_1675.jpg



11. Ahold Delhaize
Uingereza hiyo na turejee tena Uholanzi ambapo tunakutana na supermarket yenye kuwahusisha Wabeligiji pamoja na Wadachi ambayo ilianza mwaka 2016, ni Supermarket za Ahold Delhaize ambazo zimesambaa ndani ya Marekani, Ulaya pamoja na Asia. Mpaka sasa Ahold Delhaize ina maduka makubwa zaidi 6700 kwenye nchi zaidi ya 24, maduka haya yamekuwa yakiuzwa bidhaa mbalimbali kama vile,pombe na vilevi vikali pamoja na bidhaa za majumbani, huku pia ikitoa huduma ya duka la mtandaoni.
IMG_1676.jpg



12. Auchan
Tuondoke Uholanzi na twende mpaka Ufaransa ambapo tunakutana na Supermarket za Auchan ambazo zilianza kufanya kazi kuanzia mwaka 1961 huku zikiweka makazi yake pale Croix. Auchan ina maduka makubwa zaidi ya 4084 ambayo yamesambaa ndani ya nchi zaidi ya 11 huku ikishika nafasi ya 35 ya waajiri wakubwa wenye kuongoza kuajiri watu wengi duniani.



13. Costco Wholesale Corporation
Tupande ndege na Tutoke Ufaransa na twende Marekani ambapo tunakutana na Supermarket za Costco ambazo zilianza kufanya kazi tokea mwaka 1976 huku zikiwa zimeweka makao makuu yake pale, Washington. Kwa mujibu wa jarida la Forbes lilitoa ripoti kuwa Costco ni moja kati ya makampuni makubwa ndani ya Marekani, kwa muktadha wa mapato yaliyovunwa. Kwa Marekani Costco imekaa nambari mbili wakati namba moja akiwa ni Walmart, mpaka sasa Costco ana maduka makubwa zaidi ya 800 ambayo yamesambaa kwenye nchi takribani 20 duniani kote.



14. Kaufland
Tuondoke Marekani na turejee Ulaya mpaka Ujerumani ambapo tunakutana na Kaufland ambapo hawa ni wamiliki wa hypermarkets ndani ya bara la Ulaya, huku makao makuu yakiwa huko Neckarsulm sambamba na makao makuu ya Supermarkets za Lidl, huu Kaufland wakiwa mbioni kufungua ofisi zao nyingine huko Australia pamoja na kuongeza maduka mengine ndani ya bara la Asia. Kwa Ulaya tu tayari Kaufland ina maduka makubwa zaidi ya 1250 huku lengo kubwa la Supermarkets za Kaufland likiwa ni kuuza bidhaa kama Vyakula, Vinywaji, bidhaa za majumbani na kadhalika vyote kwa bei ya punguzo zaidi kuliko bei ya wapinzani wake.



15. Netto
Tusalie huko huko Ulaya na tusogee mpaka Denmark ambapo tunakutana na Supermarket za Neto ambazo zilianza kazi tokea mwaka 1981 na kuweka makao makuu yake pale kwenye Jiji la Koge. Neto ni supermarket ambazo zimeajiri wafanyakazi zaidi ya 7200 huku wakijishughulisha na uuzaji wa bidhaa kwa bei ya punguzo, Neto wana maduka makubwa yapatayo 1500 katika nchi zaidi ya 16 duniani walipopata leseni ya kufungua biashara huku Ulaya wakiwa na maduka zaidi ya 1200.



16. Whole Food Market Inc
Tuondoke Denmark na turejee Marekani ambapo tunakutana na Supermarket za Whole Food Market, ambazo zilianzishwa tokea mwaka 1980 na kuwa na makao makuu pale Austin, Texas sawa na ile supermarket ya 7-Eleven. Whole Food Market wamepata kuwa na maduka kwenye nchi za Marekani, Canada pamoja na Uingereza, huku wakijihusisha na uuzaji wa bidhaa zisizo na mafuta pamoja na zile ambazo hazina kemikali za kuongeza rangi wala kemikali za kuongeza ladha. Mpaka sasa Whole Food Market ina maduka makubwa zaidi ya 600 ambazo zimesambaa katika nchi tatu za Marekani, Canada pamoja na Uingereza.



17. Mercator
Tuondoke Marekani na twende mpaka Slovenia ambapo tunakutana na supermarket za Mercator ambazo zimesambaa katika nchi nyingi ndani ya bara la Ulaya, huku zikiwa na makao makuu yake pale Ljubljana, wao Mercator wana jumla ya maduka makubwa zaidi ya 1200 ambayo yanafanya biashara ndani ya nchi Slovenia na Mashariki na kati ya bara la Ulaya, huku ikiwa ni supermarket kubwa ndani ya Slovenia.



18. Lotte Mart
Tutoke Slovenia na twende mpaka Korea Kusini ambapo tunakutana na Supermarket za Lotte Mart ambazo zilianza kazi tokea mwaka 1998, katika Jiji la Seoul, Lotte Mart wana maduka mengine makubwa katika nchi zingine za bara la Asia huku wakiwa na jumla ya maduka 200. Wao wanajihusisha na uuzaji wa vinywaji, wanasesere, midori, nguo pamoja na vifaa vya umeme huku wakiwa wanatoa na ofa za manunuzi katika mfumo wa vocha na zawadi.



19. Billa
Tuondoke Asia na twende mpaka bara la Ulaya na tubishe hodi Austria pale mbele ya supermarket kubwa za Billa ambazo zilianza kazi mnamo mwaka 1953, Billa ni maarufu sana ndani ya Austria na nchi jirani huku wakiwa na maduka makubwa ndani ya nchi za Ulaya. Mpaka sasa kuna maduka makubwa zaidi ya 200 kwenye nchi za Ujerumani, Uingereza, Ureno, Uhispania pamoja na Austria huku baadhi ya maduka yasiyozidi 50 yakiuzwa kwenda kwenye makampuni ya SPAR pamoja na Carrefour.



20. Aeon
Tukwee tena pipa na twende Asia mpaka Japani tukamilishe orodha yetu ambapo tunakutana na Aeon ambao ni sehemu ya kampuni kubwa ya kampuni ya Aeon Industry, kampuni kongwe haswa kwani ilianza kufanya kazi tokea mwaka 1758, takribani miaka 265 sasa wakiwa kwenye biashara huku wakiwa na makao makuu yao pale Chiba ndani ya nchi ya Japani. Kampuni ya Aeon inamiliki maduka makubwa, maduka ya kati pamoja na majumba ya mauzo huku wakiuza bidhaa zao ndani ya nchi zaidi ya nne ndani ya bara la Asia.


Mpaka sasa biashara ya supermarket imekuwa biashara kubwa sana huku mwaka jana kukiwa na mapato ya zaidi ya $14.78 trillion fedha za kimarekani. Kwa Tanzania tuna; Sifamart, Shoppers, Shrijees Supermarkets, Village, Viva Marche, Mr Price, SafeWay Food Stores, pamoja na Shoprite. Je kwanini hawa wakubwa hawatokei kuwekeza huku nyumbani?
 

Attachments

  • IMG_1662.jpg
    IMG_1662.jpg
    45.5 KB · Views: 13
  • IMG_1663.jpg
    IMG_1663.jpg
    29.1 KB · Views: 10
  • IMG_1679.jpg
    IMG_1679.jpg
    55.4 KB · Views: 11
  • IMG_1664.jpg
    IMG_1664.jpg
    49.1 KB · Views: 12
  • IMG_1665.jpg
    IMG_1665.jpg
    53.7 KB · Views: 12
  • IMG_1666.jpg
    IMG_1666.jpg
    46.8 KB · Views: 12
  • IMG_1667.jpg
    IMG_1667.jpg
    51.1 KB · Views: 13
  • IMG_1668.jpg
    IMG_1668.jpg
    59.6 KB · Views: 11
  • IMG_1677.jpg
    IMG_1677.jpg
    66.8 KB · Views: 9
  • IMG_1678.jpg
    IMG_1678.jpg
    63 KB · Views: 12
Back
Top Bottom