USHIRIKISHWAJI WANANCHI KATIKA KUIBUA MIRADI YA MAENDELEO
Viongozi msikwepe wajibu wenu Rais Kikwete
Na Mwandishi Maalum, Tabora
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa utaratibu wa kuwashirikisha wananchi katika kubuni na kuibua miradi mbali mbali ya maendeleo usitumiwe na viongozi kama kisingizio cha wao kukwepa wajibu wao wa kuwa chachu ya maendeleo katika nafasi zao za uongozi nchini.
Hii tabia ya viongozi kudai kuwa wananchi hawajaibua miradi sasa inatumiwa na sisi viongozi kukwepa majukumu yetu kama wakala wa mageuzi ya maisha ya wananchi nchini, Rais Kikwete amewaambia viongozi wa Wilaya ya Tabora leo, Jumamosi, Oktoba 25, 2008.
Rais ametoa maelekezo hayo kwa viongozi wakati akipokea taarifa ya utendaji ya Wilaya ya Tabora katika siku ya tatu ya ziara yake ya siku nane katika Mkoa wa Tabora wakati alipowasili mjini Tabora akitokea wilaya za Sikonge na Urambo.