Hatimae Mahakama ya Mkoa Wete imemuhukumu kwenda kutumikia chuo cha mafunzo kwa muda wa miaka kumi (10) pamoja na kulipa fidia ya shilingi laki mbili mshitakiwa Khalifa Khalfan Mwaveso mwenye umri wa miaka 25 mkaazi wa Micheweni Pemba, aliepatikana na kosa la kumbaka msichana mwenye umri wa miaka 17.
Baada ya mahakama kufanya uchambuzi wa Sheria juu ya ushahidi uliwasilishwa na upande wa mashitaka, mahakama imeweza kuthibitisha kosa pasi na chembe ya shaka ya maana.
Ndipo hakimu wa mahakama hiyo Abdalla Yahya Shamhun alipotoa hukumu hiyo chini ya kifungu cha 210 cha Sheria nambari 7 ya mwaka 2018, baada ya kumkuta na hatia mshitakiwa huyo
Hakimu Shamhuni alimuamuru mshitakiwa huyo kwenda kutumikia chuo cha mafunzo kwa muda wa miaka kumi (10) pamoja na kulipa fidia ya shilingi laki mbili ndani ya siku 14
Kabla ya hukumu hiyo, mwendesha mashitaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa mashitaka Pemba, Juma Mussa Omar alidai kuwa, hawana kumbu kumbu za awali kwa mshitakiwa huyo, ingawa aliiomba mahakama kutoa adhabu kali, ili iwe fundisho kwa wengine.
“Muheshimiwa hakimu kutokana na kosa hili mtuhumiwa apewe adhabu kali na kumlipa fidia muathiriwa chini ya kigungu cha 109 (1) cha Sheria nambari ya mwaka 2018, Sheria ya Zanzibar, ili iwe funzo kwa wengine wenye tabia kama hiyo”, alidai mwendesha mashitaka huyo.
Kwa upande wake mshitakiwa huyo aliiomba mahakama impunguzie adhabu angalau, impatie adhabu ya kwenda kuitumikia jamii.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, mtuhumiwa huyo alitenda kosa siku na tarehe isiyojukana mwezi Octoba mwaka 2019 saa 3:00 usiku huko Pandani Masipa Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba. Ilidaiwa kuwa, bila ya halali alimbaka msichana mwenye umri wa miaka 17, jambo ambalo ni kosa kisheria.
Kufanya hivyo ni kosa kinyume na kifungu cha 108 (1) (2) (e) na kifungu cha 109 (1) vya Sheria namba 6 ya mwaka 2018 Sheria ya Zanzibar.
Kesi hiyo yenye namba RM 04/2020 kwa mara ya kwanza ilianza kusikilizwa katika Mahakama ya Mkoa Wete Januari 1 mwaka huu.