Zambi na Karamagi wajitosa ulingoni CCM | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Zambi na Karamagi wajitosa ulingoni CCM

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by armanisankara, Aug 24, 2012.

 1. a

  armanisankara JF-Expert Member

  #1
  Aug 24, 2012
  Joined: Jul 15, 2011
  Messages: 283
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 35
  Geofrey Zambi, Nazir Karamagi ni miongoni mwa vigogo kadhaa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao wameendelea kujitosa kuchukua fomu za kuwania uenyekiti wa mikoa na ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kupitia wilayani.
  Mkoani Kagera wanachama watatu jana walijitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi ya uenyekiti wa mkoa.

  Waliojitokeza ni Costansia Buhiye, ambaye anatetea nafasi hiyo, Edson Mutalemwa kutoka wilayani Missenyi na Alhaj Alid Kahuza kutoka wilayani Muleba, ambaye kabla ya kuwania nafasi hiyo alikuwa mjumbe wa Baraza Kuu la Wazazi Mkoa wa Kagera.

  Kwa mujibu wa Katibu wa CCM mkoa Kagera, Evelen Mushi, wagombea hao walichukua fomu hizo jana.

  Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini na kulazimika kujiuzulu katika serikali ya awamu ya nne kwa kashfa ya Richmond, Karamagi, amechukua fomu ya kutetea nafasi yake ya ujumbe wa NEC kupitia Wilaya ya Bukoba ambayo pia inawaniwa na Prudence Kibuka.

  MBEYA MOTO


  Kinyanganyiro cha uongozi CCM mkoa wa Mbeya kimeanza kupamba moto ambapo wanachama watatu akiwemo Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi, ni miongoni mwa wanachama waliochukua fomu ya kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mbeya.

  Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya, Mangala Sengerema, akizungumza na NIPASHE jana kwa simu kutoka Mbeya, alisema wengine waliochukua fomu za kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa CCM mkoa ni kada wa chama hicho, Brown Mwangomale na Lawrence Mfwango.

  Mwenyekiti wa sasa wa CCM wa mkoa huo, Nawab Mullah, akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, alisema bado hajaamua kuchukua fomu ya kutetea nafasi hiyo.

  Mullah ambaye amekuwa Mwenyekiti wa CCM tangu mwaka 2007, alisema kabla ya Agosti 29, mwaka huu ambayo ni siku ya mwisho ya kuchukua na kurejesha fomu ya uenyekiti wa CCM mkoa atakuwa ameamua kama achukue au la.

  KIGOMA MCHUANO

  Katika mkoa wa Kigoma Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kigoma Mjini, Nashoni Wiliamu Bidyanguze, jana alichukua fomu kugombea uenyekiti wa mkoa kuchuana na mwenyekiti wa sasa, Azim Premji, ambaye naye alichukua fomu jana kutetea nafasi hiyo.

  RUVUMA USHINDANI

  Makada watatu wa CCM mkoani Ruvuma akiwemo Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Songea Mjini, Hemed Dizumba, wamejitokeza kuchukua fomu nafasi mbili tofauti ikiwemo nafasi ya uwenyekiti wa CCM Mkoa.

  Katibu wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Velena Shumbusho, alisema fomu za kugombea nafasi mbalmbali ngazi ya mkoa zimeanza kutolewa na juzi Dizumba alichukua fomu ya kugombea nafasi ya uwenyekiti wa CCM Mkoa Ruvuma.

  Alifafanua zaidi kuwa Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Ruvuma, Cornel Msuwa, ambaye anadaiwa kutaka kutetea nafasi yake mpaka jana alikuwa bado hajachukuwa fomu.

  Dizumba alisema ameamua kugombea uenyekiti wa mkoa kwa sababu ana uwezo mkubwa wa kuimudu nafasi hiyo na kwamba nafasi ya uenyekiti wa wilaya ameamua kuwaachia wengine wagombee.

  Naye Mwanasheria wa CCM Makao Makuu Dodoma, Glorious Luoga, alichukua fomu kugombea ujumbe wa NEC Wilaya ya Songea Vijijini akisema: “Lengo langu la kuchukua fomu ni kuunga mkono jitihada zilizofanywa na wazee wangu na hasa ikizingatiwa wilaya yetu ya Songea Vijijini bado ina changamoto nyingi ambazo utatuzi wake siyo lazima ukasemewe bungeni kwani mkongojo wa wazee hupokelewa na vijana.”

  Kwa upande mwingine alisifia mfumo wa kujivua gamba CCM kuwa una lengo la kukisafisha chama na si kama baadhi ya vyama vya upinzani vinavyodai kuwa kimejaa mafisadi.

  DODOMA NA UFISADI

  Mkoani Dodoma, baadhi ya wagombea wa NEC wameapa kupambana na ufisadi nchini endapo watapata nafasi ya kuwawakilisha wanachama wenzao katika NEC.

  Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukabidhiwa fomu za kuwania nafasi hiyo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CCM Wilaya ya Dodoma Mjini, Christina Masagasi, mgombea wa NEC, Haidary Gulamali, alisema mfumo wa wabunge kutogombea nafasi za NEC wilayani ni ishara ya mapambano ya ufisadi kuanza.

  “Mtu huwezi kujisimamia mwenyewe na kujikosoa mwenyewe, ninamshukuru Rais wetu, kwa kuamua kuwa wabunge wasiwanie ujembe wa NEC kupitia wilayani kwa sababu hii itakipa fursa chama kusimamia vyema serikali,” alisema.

  Wengine waliochukua fomu kuwania nafasi hiyo kupitia Wilaya ya Dodoma Mjini hadi jana mchana ni aliyekuwa mbunge wa Dodoma Mjini, Epharim Madege, Lucy Rutairwa, Daudui Nyinge na Peter Mang’ati.

  Waliochukua fomu ya kuwania ujumbe wa NEC kupitia Wilaya ya Chamwino ni wanachama watano akiwemo Ofisa Habari wa Chuo cha Mipango, Godrick Ngoli, ambaye anawania ujumbe wa NEC kupitia Wilaya ya Chamwino.

  KILIMANJARO YA KALE YARUDI

  Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoani Kilimanjaro mwaka 1997-2002, Peter David ametangaza nia yake ya kuwania tena nafasi hiyo kwa lengo la kukinusuru chama hicho ambacho huku akijinadi kuwa yeye ni kiyoyozi ndani ya chama.

  Aliyataja mambo ambayo atayafanyia kazi kuwa ni pamoja na kuhakikisha makundi ndani ya chama yanakufa kabisa, kuleta umoja na mshikamano kuanzia ngazi ya shina hadi mkoa, kwa kufanya mikutano na wanachama mara kwa mara na kuwaondoa madalali wote wa waliopo ndani ya chama.

  Alisema sababu kubwa iliyomfanya kuachia ngazi mwka 2002 ni kupisha wengine kuongoza huku akifanya utafiti wa ni sababu gani zinazosababisha chama kuyumba na kwa kutambua hilo na kufahamu njia za kuondoa matatizo yaliyopo ndiyo maana amerudi.

  Alisema wakati akiwa mwenyekiti hakukuwa na chama kikingine kilichokuwa kikifurukuta kwake na alifanikiwa kunyakuwa nafasi mbalimbali za uongozi wa serikali za mitaa kwa asilimia 99.9 na kukomboa majimbo yaliyokuwa upinzani kwa asilimia 75.

  Hadi jana watu watatu akiwemo David walikuwa wamejitokeza kuchukua fomu, inagwa wawili majina yao hayakupatikana. Mwenyekiti anayemaliza muda wake, Vick Swai, alishawahi kusema kuwa hatagombea tena.

  SINGIDA UPINZANI

  Mkoani Singida, Mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo, Joramu Alute, amechukua fomu kutetea wadhifa wake. Alute atapambana na kada wa chama hicho, Aman Raiambaye naye amejitosa kugombea.

  ARUSHA KWEPESI

  Aliyewahi kuwa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Dk. Falash Toure, amechukua fomu za kuwania uenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha.

  Dk. Toure aliwahi kubwagwa na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, kwenye kinyang’anyiro cha kuwania jimbo hilo katika uchaguzi mkuu uliopita, alichukua fomu ya jana.

  Katibu wa Siasa, Itikadi na Uenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Loata Sanare, alisema hadi jana hakuna mwanachama mwingine zaidi ya Dk. Toure ambaye alijitokeza kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya uenyekiti.

  Mwenyekiti wa sasa CCM Mkoa, Onesmo Ole Nangole, hakuwa akipokea simu wakati alipokuwa akipigiwa na NIPASHE ili kueleza msimamo wake.

  “Hakuna wanachama wengine zaidi waliochukua fomu hadi jana jioni,” alisema, na kuongeza: “Kwa kuwa muda bado tunatarajia wengine zaidi watajitokeza kuchukua fomu.”

  Imeandikwa Kibuka Prudence, Bukoba; Joctan Ngelly, Kigoma; Gideon Mwakanosya, Songea; Sharon Sauwa na Jacqueline Massano, Dodoma; Charles Lyimo, Moshi; Thobias Mwanakatwe, Dar; Elisante John, Singida na John Ngunge, Arusha.
  CHANZO: NIPASHE

   
 2. L

  Lua JF-Expert Member

  #2
  Aug 24, 2012
  Joined: May 19, 2011
  Messages: 704
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 0
  ila ninawashauri kipindi hiki wanachochukua fomu za uongozi wa ccm, chama ambacho kinaelekea qibra, angalizo kwangu kisije kikawafia mikononi mwao.
   
 3. kisugujira

  kisugujira JF-Expert Member

  #3
  Aug 24, 2012
  Joined: Aug 13, 2012
  Messages: 769
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 0
  Hee kumbe mzee wa kusaini mikataba yenye utata hotelini huko majuu, Karamagi bado yupo? Anatisha kama Kamongo. Bado anapeta tu ndani ya Chama Cha Magamba! Hawa jamaa ni noma. Hawaoni aibu kabisa kwa mambo waliyolitendea Taifa hili. Kwani ni lazima wawe wanasiasa? Kwa nini wasiwe wachungaji kama mzee wa upako? Mmmm,lakini hata hawa wachungaji wetu wa siku hizi hawaamiki.Usanii umekuwa mwingi. Tumekwisha!
   
 4. U

  Ubungo JF-Expert Member

  #4
  Aug 24, 2012
  Joined: Apr 7, 2012
  Messages: 1,239
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 0
  Waendelee na vita zao ili M4C izidi kushika kasi, wakija kushtuka kazi imeisha.
   
Loading...