Yatima abakwa kwenye danguro Dar miaka 10

ndiyomkuusana

JF-Expert Member
Aug 2, 2012
666
421
Na Romana Mallya


16th February 2013



Alawitiwa na kuambukizwa virusi vya ukimwi
Polisi naye adaiwa kumbaka akiwa kituoni




Nyumba inayoonekana ni ghorofa inayodaiwa kutumiwa kama danguro iliyopo Mwananyamala Magengeni jijini Dar es Salaam


Msichana yatima, mkazi wa mkoani Manyara, amefungiwa kwenye danguro kwa zaidi ya miaka 10 akinyanyaswa kingono, kuteswa na kuambukizwa Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Msichana huyo aliyeondolewa nyumbani kwao Oysterbay mjini Babat,i alilaghaiwa na mwanamke aliyejifanya kuwa msamaria mwema, akitangaza nia ya kumsaidia kielimu na kimaisha, kufuatia kifo cha mama yake mzazi.

Msichana aliyefikwa na masahibu hayo ni Sara Tarimo (27) ambaye aliangukia mikononi mwa mwanamke mwenye danguro hilo, Abia Lucas (44) anayeishi Mwananyamala Magengeni.

Ilikuwa ni baada ya kifo cha mama yake Magreth Kitinati, aliyekuwa akiishi naye Oysterbay huko Manyara.

Sara anasema mwanamke huyo alimtoa kijijini kwao hadi jijini Dar es Salaam, na kumshinikiza kwenye `utumwa wa ngono' kwa kipindi cha miaka 10 akiwa amefungiwa ndani.

Akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi, mama yake mzazi alifariki, hivyo ujio wa msamaria huyo ulikuwa faraja na tumaini jipya kwa maisha yake. Haikuwa hivyo.

Sara alisema alipoteza bikra yake baada ya kumlazimisha kufanya ngono na mwanamume mtu mzima, aliyembaka na ukawa mwanzo wa kutumiwa kingoni na wanaume wa kila aina.

Sara alisema alifanywa unyanyasaji huo akiwa na miaka 13 na kwamba hilo lilikuwa tukio lake la kwanza kukutana na mwanaume.

Baada ya kufanikiwa kutoroka na kuwataarifu polisi nyendo za mama huyo ambaye sasa anashikiliwa kwa mahojiano, Sara anasimulia kumbukumbu za kusikitisha za miaka aliyoipoteza katika himaya ya danguro la ‘msamaria.'

HISTORIA YAKE


Sara ni mmoja wa watoto watatu katika familia yao. Kaka yake Emmanuel Tarimo (31) na dada yake Neema Tarimo.

Wakati akipochukuliwa na ‘msamaria' alimuacha kaka yake huko Babati akijitafutia riziki kwa kubeba mizigo na dada yake akiendelea na masomo ya shule ya msingi.

Anasikitika kuwa katika maisha yake hakubahatika kumfahamu baba yake, lakini aliwahi kuelezwa na mama yake kuwa ni mwenyeji wa Kilimanjaro.

Mama yake ndiye aliyekuwa anatunza familia yao licha ya kwamba hakuwa na ajira rasmi, wala biashara za kudumu.

Mazingira hayo, yalimlazimisha kukatisha masomo akiwa darasa la tatu katika shule ya Msingi Idangunyii.

Anasema alikuwa na ndoto ya kupata elimu zaidi, lakini kifo cha mama yake kilisababisha ajione kuwa hana bahati.

MAISHA KWENYE DANGURO


Alisimulia kuwa, baada ya ‘msamaria ' kujitokeza na kumwahidi kuwa atamtafutia shule na kugharamia elimu alimsikiliza na kumfuata hadi jijini Dar es Salaam.

Sara alieleza kuwa mwanamke huyo alipofika nyumbani kwao Babat, alieleza kuwa anatafuta wasichana 10 kwa ajili ya kufanya kazi za ndani kwa familia za Dar es Salaam.

"Aliiambia familia yangu kuwa, hata kama wasichana watakaopatikana watakuwa wanasoma wataendelezwa mara baada ya kufika mjini wakati wakiendelea na kazi ,'' anasema na kuongeza:
"Nakumbuka ilikuwa siku ya Ijumaa mwaka 2003, tuliondoka kwa usafiri wa basi tukiwa 10 ingawa sikuwatambua wenzangu kwa sababu alituchukua kutoka katika vijiji tofauti."

Alisimulia kuwa walifika nyumbani kwa mwanamke huyo Mwananyamala Magengeni kwenye ghorofa mbili, ambayo juu linaonyesha ujenzi unaendelea.

Alisema wakiwa nyumbani kwa mama huyo, walibadilishwa mavazi kutoka yale waliyotoka nayo kijijini na kupewa nguo nyingine- sketi fupi, kaptula na blauzi maarufu kama ‘vitop'.
Alikumbuka kuwa baada ya kupewa nguo hizo, walitakiwa kila mmoja akajipumzishe kwenye chumba chake vilivyokuwa ghorofa ya kwanza.

KUBAKWA MARA YA KWANZA


Alieleza kuwa siku hiyo akiwa chumbani kwake mlango uligongwa na alipouliza ni nani, alijibiwa na sauti ya kiume kuwa ni mlinzi.

Alipofungua, mwanaume mtu mzima alimwambia wakati huo sio wa kulala bali ni wa kazi na kumtaka avue nguo huku akimtisha na bisibisi.

Vitisho vilitawala akilazimishwa kufanya ngono kwa nguvu na mwanaume huyo aliyetumia bisibisi kumchoma mdomoni na mkononi karibu na kiwiko.

"Nilipiga kelele za kuomba msaada lakini hakuna aliyekuja kunisaidia hadi yule mzee alipomaliza haja yake na kuniacha nikiwa kwenye maumivu makali."

Anasema hakuamini kilichotokea na kulalamika kwa mwenyeji wake…."Nilimfuata yule mama kumweleza yaliyonitokea cha ajabu aliniambia hiyo ndiyo kazi niliyofuata mjini."

Anasema "baada ya kupewa maneno hayo makali nilipelekwa kwa daktari wa hospitali ya Mwananyamala kwa uchunguzi zaidi."

Anasema aliendelea kuwa mtumwa wa ngono kwa sababu baada ya matibabu akawa anaendelea na kazi hiyo.

Sara anasema katika hospitali hiyo ndiko walikokuwa wanatibiwa na mwanamke huyo alimweleza kuwa huyo ni daktari wao.

Anasema aliwahi kudhalilishwa kingono na wanaume zaidi ya 10 kwa siku moja, wakiwa wa rika, tabia na maumbile tofauti.

"Nakumbuka siku moja alikuja mteja aliyekuwa amelewa, akaniambia amelipa fedha nyingi kwa mama na anachotaka ni kunitumia kinyume cha maumbile."

"Sijawahi kufanya hivyo, nilipokataa alitoa kisu na kunitishia…alinilazimisha nivue nguo na kulala kitandani kabla hajanijeruhi." Anasema.

"Nikiwa kitandani alidondosha kisu tumboni mwangu, akakilalia na kunijeruhi, nikakimbizwa Mwananyamala na kutibiwa na yule daktari wa mwanzo niliyeambiwa ni tabibu wetu ambaye alinishona sehemu nilizojeruhiwa na alikuja nyumbani kunitoa nyuzi," anasema
MALIPO
Sara anasema hakuwahi kulipwa japo wakati wakiendelea na kazi hiyo, mwanamke huyo aliwaeleza kuwa malipo yao ni Sh. 30,000 kwa mwezi na kwamba wangelipwa baada ya kukamilisha alichokitaka.

Akielezea faida waliyomtengenezea mama huyo alisema alikuwa akitoza kati ya Sh. 10,000 hadi 15,000 kwa wateja waliofanya ngono kwa njia ya kawaida na wale waliokuwa wakiwaingilia kinyume cha maumbile ilikuwa aliwalipisha kati ya Sh. 30,000 na 50,000.
Anaeleza kuwa walikuwa wakipatiwa matibabu, chakula na kununuliwa mavazi lakini hawakuruhusiwa kutoka nje ya nyumba hiyo.

"Niliwahi kumhoji mama kwa nini alitudanganya unatuleta mjini kwa ajili ya kufanya kazi za ndani na kutusomesha?"

" Nilimuomba anirudishe nyumbani, lakini alikataa na kuniambia kazi yake itakapokwisha nitarudi sikuyaelewa majibu haya," anasema.
ALIVYOTOROKA
Alisema baada ya kutumikishwa kwa muongo mmoja, Februari 4, 2013, siku aliyofanikiwa kutoroka baada ya mwanaume aliyefanya naye mapenzi siku ya kwanza kufika kwenye danguro hilo akihitaji huduma yake.

"Alilipia na kuja chumbani kwangu na kunieleza kuwa lile embe lililokula kipindi kile lilikuwa bichi, hivyo amekuja kwa mara nyingine likiwa limeiva na baada ya kumaliza haja zake."

"Aliniambia anataka kunipa zawadi hivyo niliporuhusiwa na mama tuliondoka naye, tukipita maeneo tofauti akinielekeza majina ya mitaa na mwishowe tuliingia sokoni Kariakoo," anasimulia.

Waliondoka na gari aina ya Volkswagen hadi Kariakoo na wakati huo alihisi njaa na kumuomba kabla ya kumnunulia zawadi, wanunue kwanza chakula.

Mteja huyo katika mazungumzo yake alimfahamisha kuwa ni mwanasheria anayefanya kazi manispaa japo hakutaja jina.

"Tukiwa njiani alikokuwa amekusudia kunipeleka nilikuwa nikitembea nyuma yake, hapo ndipo nilipotoroka nikikimbia bila kujua ninaelekea wapi, nilizunguka na hatimaye giza liliingia na watu walipungua kwenye eneo nililokuwapo."

"Sijui ilikuwa saa ngapi, lakini niliona gari la polisi niliamua kuwafuata nikamueleza askari wa kike mkasa mzima," alisema.

Anasema walikwenda kituo kikuu cha polisi na kuchukuliwa maelezo lakini pia alimpatia nguo nyingine kwa vile alikuwa amevaa mavazi yasiyo na staha.

"Siku iliyofuata niliambiwa kuna dawati la kushughulikia masuala ya wanawake, lakini kwa wakati huo wahusika hawakupo. Ilipofika Alhamisi nilikabidhiwa kwa askari mwingine anaitwa Happy."

Aliongeza: "tuliondoka naye hadi Oysterbay polisi, huko walitoka askari kadhaa kwenda Mwananyamala nyumbani kwa mama huyo."

Sara alisema walifanya upekuzi kwenye vyumba walivyokuwa wakilala bila mafanikio, walishuka chini na kumuamuru afungue moja ya vyumba vilivyokuwa vimefungwa lakini mwanamke huyo alikataa na polisi walimuagiza aende kituoni kuandika maelezo dhidi ya tuhuma hizo.

Alieleza kuwa wakati mtuhumiwa huyo akiwa mahabusu watoto wake anaoishi nao mmoja mwanaume mwenye miaka 27 na mwingine wa kike walimsihi afute kesi hiyo, lakini alikataa na kuongeza kwa alifungua jalada la uchunguzi lenye kumbukumbu RB/2468/2013 la Februari 7.

VYOMBO VYA HABARI

Alisema amefikisha suala hili kwenye vyombo vya habari akiomba msaada wa nauli ili aweze kurudi kwao pamoja na chakula.
"Kabla sijafika NIPASHE nilitoa taarifa kwenye Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ambacho kimeahidi kulifanyia kazi suala langu," anasema.

AFYA YAKE

Sara analalamikia kuwa na vivimbe mbavuni na sehemu za siri na anahofu kuwa huenda ameambukizwa magonjwa ya ngono na Ukimwi.

Anasema ana wasiwasi kwa vile aliwahi kupata vipele vingi mwilini japo daktari wao alimueleza kuwa vilisababishwa na joto lakini sasa vimekuwa uvimbe mkubwa.

Anasema wakiwa kwenye danguro hilo daktari wao alikuwa anawapa dawa mara kwa mara ambazo hawafahamu zilikusudiwa kutibu nini na zilipomalizika aliendelea kuzileta japo hakuwahi kutumia tiba hiyo.

KONDOMU

Anasema baadhi ya wanaume wenye ndoa walitumia kondomu wakati wa kufanya ngono lakini asilimia kubwa ya wateja wa danguro hilo walikuwa hawatumii mipira hiyo ya kiume.

"Walikuwa wananiambia nina mke ninampenda hivyo natumia kondomu lakini wengine walikuwa hawatumii, chumbani tulikuwa tunawekewa kondomu lakini ukiwaambia wazitumie wanakataa."

KUGUNDULIKA NA VVU
Sara anasema Jumatatu Februari 11, akiwa polisi Oysterbay, aliamriwa kuondoka eneo hilo kwani si sehemu ya kuishi nail kufungua mashtaka.

"Nilikwenda kituo cha mabasi ya mikoani Ubungo lakini usiku nilizidiwa ilipofika asubuhi nilikwenda zahanati ya Mwenge nilikotibiwa na kuelezwa kuwa nimeambukizwa Virusi Vya Ukimwi (VVU) na kutakiwa kuanza kutumia dawa."

KULAWITIWA NA POLISI
Wakati uchunguzi wa tuhuma dhidi ya Abia ukiendelea, inadaiwa kuwa usiku wa Jumatano polisi wa kituo cha Oysterbay alimlawiti Sara eneo lenye migomba kituoni hapo.
Akizungumza na NIPASHE kwenye kituo cha trafiki kilichopo kituo cha mabasi ya mikoani Ubungo, alisema alifanyiwa unyama huo baada ya polisi kumfuata akiwa amelala kwenye maegesho ya magari.

Anasema alikwenda Ubungo kuchukua nguo alizozificha hapo na akiwa huko alikutana na askari huyo ambaye alimueleza matatizo yake, ndipo akamtaka wakale chakula.

"Baada ya chakula wakati tunarudi kituoni, aliniambia nimlipe kwa kumruhusu kunifanyia tendo hilo lakini nilikataa na askari huyo alinishika kwa nguvu na kunilawiti."

Anaongeza kuwa kutokana na kitendo hicho aliondoka kituoni hapo saa 12:00 asubuhi na kufikisha taarifa ITV kwa vile aliona polisi hawakuwa na msaada kwake.

Baada ya kutoa malalamiko yake na kusaidiwa na wafanyakazi wa ITV alijitokeza polisi mwanamke na kumchukua kwa matibabu kwenye zahanati ambayo Sara alisema haifahamu na baadaye kupelekwa kituo cha mabasi Ubungo ili kurudishwa nyumbani kwao Manyara.
Alimweleza Mwandishi Wetu kuwa aliomba simu kutoka mtu aliyekuwa kituoni hapo ili awasiliane naye kabla hajasafirishwa na polisi hao.

Baada ya mwandishi kufika Ubungo na kufanya mahojiano na Sara gari la polisi lenye namba PT 2083 lilifika na kumpeleka polisi Oysterbay na kuandikisha maelezo.
MAELEZO YA POLISI

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, John Mtalimbo, alipofuatwa alisema taarifa zipo kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya Kinondoni (OCD).

Aidha, alisema kwa mujibu wa OCD msichana huyo amekuwa akitangatanga maeneo ya Buguruni na sehemu nyingine ambazo hakuzitaja.

"Naona lengo lake ni kutuchafua, kwa nini asubuhi alikuja ITV na sio kutoa taarifa kwetu kama amelawitiwa na askari wetu, anatuchafua," alisisitiza Kamanda Mtalimbo.
Alikiri kuwa siku mbili zilizopita polisi ilimtafutia tiketi ili kumrudisha kwao lakini haikufanikiwa.

Kamanda alipoulizwa sababu za kumsafirisha Sara wakati amefungua kesi ya kuuzwa kimwili kwenye danguro alisema ni kutokana na kukosa makazi.

Awali, Mwandishi Wetu alinasa mawasiliano ya simu ya Kamanda Mtalimbo na mtu aliyeelezwa kuwa ni OCD akimwelekeza jinsi yakuandika maelezo dhidi ya binti huyo.
Alisikika akisema: "Inabidi tujipange, hapa watakuja waandishi wa habari, (bila kujua kama mwandishi wetu alikuwepo eneo hilo), watataka kujua kinachoendelea na kumshauri andike kuwa walikubaliana kufanya ngono."

Licha ya kusikia kilichozungumzwa juu ya mlalamikaji huyo alipoingia ofisi kwake na kujitambulisha na kuuliza habari za Sara Mtalimbo alimweleza kuwa hana taarifa hizo na kwamba anasubiri zitoke kwa OCD.

Akisoma maelezo ya OCD wa Kinondoni, Mtalimbo alisema Februari 2, mwaka huu Sara aliripoti kituo hapo kuwa alikuwa akiishi Mwananyamala alikokuwa akifanyishwa kazi za kuuza mwili na mtuhumiwa aliyemtaja kwa jina la Abia.

Alisema baada ya polisi kupokea malalamiko hayo walikwenda Mwananyamala kuonyeshwa danguro hilo na polisi walipomkamata Abia mlalamikaji alishindwa kumtambua na kuongeza kuwa walifungua jalada la uchunguzi na kwa sasa mtuhumiwa yuko nje kwa dhamana na Sara aliendelea kubaki kituoni hapo hadi alipoonekana ITV jana asubuhi.

Kamanda alielezwa kuwa katika mahojiano ya Sara na OCD alimfahamisha kuwa Jumatano wiki hii akiwa Ubungo alitongozwa na askari aliyemuahidi kumpatia Sh. 10,000 baada ya kumlawiti.

"Walikwenda kwa makubaliano migombani na baada ya kufanya kitendo hicho, askari alimpa Sh. 20,000 ," alisema na kuhoji sababu za msichana huyo kutofikisha tukio hilo kituoni badala yake alikimbilia ITV.

Hata hivyo alipoulizwa iwapo mlalamikaji amemtambua askari huyo kupitia gwaride la utambuzi na iwapo alichukuliwa hatua alisema bado na kuongeza:"Maelezo niliyokupa ndiyo mambo mengine yatafuata baadaye."
NYUMBANI KWA ABIA

Gazeti hili likafika nyumbani kwa Abia na kukutana na binti alijitambulisha kuwa anafanyakazi za ndani na kueleza kuwa mwenye nyumba hakuwepo na hajui alikokwenda.
Alipoulizwa kuhusu danguro binti huyo mwenye miaka kati ya 13 na 20 alisema hafahamu kinachoendelea kwani mwajiri wake anamkataza kutoka nje kukutana na majirani lakini akadokeza kuwa Jumatatu wiki hii walikuja polisi wakamkamata mama huyo ambaye siku iliyofuata alirudi nyumbani.

KUWEPO MADANGURO
Majirani wa mtuhumiwa walikataa kutoa ushirikiano kwa kuhofia wanazungumza na polisi lakini Mwenyekiti Serikali ya Mtaa Kata ya Makumbusho, Said Muhunzi, alisema uchunguzi uliofanyika umebaini kuwepo kwa danguro hilo.

"Nimebaini wapo wasichana wenye umri mdogo ambao wanaonekana na majirani wakiingizwa hapo kila mara na baadhi ya watu, majirani wamethibitisha hili," alisema.

Aliongeza kuwa, Jumatano iliyopita kikundi chake cha ulinzi shirikishi, kilifika kwenye nyumba hiyo saa 7:00 usiku na kumkuta mtuhumiwa Abia na watu wengine wakiwa nje na kuwataka waingie ndani kwa kwani haukuwa muda wa kukaa nje.

"Ijumaa iliyopita niliwaambia walinzi waende tena saa 8:00 usiku kuangalia kama watawakuta nje, waliona watu watano wakinywa pombe nje," alisema na kuongeza:
Aliongeza kuwa watu hao ni Abia, Salome, mtoto wa marehemu mumewe na wanaume watatu na kuongeza kuwa kijana mmoja anayeitwa Juma alifahamika baada ya wenzake kumtaja kutokana na kuwatishia walinzi hao kwa bastola.

Muhunzi alisema Salome anatumiwa na Abia kutafuta mabinti kwa ajili ya danguro hilo na kwamba kufuatia tukio hilo la walinzi kutishiwa walifungua kesi tatu katika kituo cha polisi Minazini alizozitaja kuwa ni kukutwa nje wakinywa pombe usiku,kutishia kuua na kuzuia ulinzi usifanyike

Alisema walifungua jalada lenye kumbukumbua RB/118/2013 na kesi hiyo ilifikishwa kituo cha polisi Oysterbay na kukuabidhiwa kwa mpelelezi aliyemtaja kwa jina moja la Mwesiga
Katika hatua nyingine mwenyekiti huyo, alisema eneo lake moja ya changamoto zilizopo ni kuibuka kwa madanguro na baadhi ya wasichana wenye umri mdogo kujiuza kwenye baa nyakati za usiku.

Alitaja baadhi ya baa (majina tunayo ) kuwa zinaongoza kwa kuwa na wasichana wengi wanaojiuza na kwamba wanatoa elimu kupitia kamati ya Ukimwi na kufanya msako lakini tatizo ni kubwa.

Alitaja danguro maarufu liitwalo ‘kwa wahaya' lililopo Minazini na kusema kuwa ofisi yake inawajua watuhumiwa kwa majina.

Habari zilizozifikia gazeti hili jana asubuhi, Sara alikuwa amewekwa mahabusu kituoni hapo.




CHANZO: NIPASHE
 
uyu msichana mbona story yake anaonekana ni mjanja? na pia hii habari inaacha maswali mengi....mfano kuficha nguo ubungo,????
 
Unaweza kuficha nguo ubungo sehemu gani? Anaona watu kuwa ni wajinga . Pole zake lakini
 
Kweli Tanzania imeisha! Kina mama wamegeuka kuwa wanyama yaani unatoka kukusanya watoto wa wenzio kuwauza? Siku ya kufa kwako utamwambia Mwenyezi Mungu ulikuwa mama au mbwa? Hawa polisi nao hivi ni lazima kumdhalilisha kingono kila wanayemkuta? Maadili ya kazi ya polisi ni yapi? Na kama hali ndiyo hii tutasalia wangapi hapa duniani? Mungu turehemu yaani nimeumizwa sana na story ya huyu dada!
 
Asingalipata HIV asingetoka kwa Boss! na alipofikisha umri wa miaka 18 au 19 alipaswa kutoroka. Sasa anasubiri ukimwi umtoe Dar na kashaa kula pesa za kutosha.
 
Najua hy family inayotuumiwa kufanya human trafficking I can't believe it kama Kweli but its very sad.
 
Sasa huyo afande aliyemlawiti Sara, si amenunua UKIMWI kwa kujitakia!
Ndiyo hivyo tena ukipenda vya bei rahisi ndo madhara yake hayo. Mungu alishasema kila mwanaume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe. Ukiacha maelekezo ya Mungu hakika utaumia kama huyo afande; lakini huenda naye tayari ni victim huwezi jua
 
Back
Top Bottom