MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya tatu mfululizo, Yanga, wameanza kufanya balaa kwa fujo baada ya kukubaliana na kiungo mwenye uwezo wa kukaba na kushambulia ‘box to box midfilder’ wa Kagera Sugar, Babu Ally Seif na leo anaweza kumwaga wino.
Ally ambaye aliisaidia Kagera kumaliza msimu uliopita nafasi ya tatu, anapewa nafasi kubwa kutibu tatizo la kiungo mkabaji la timu hiyo ambayo ilishindwa kuzibwa na Juma Said Makapu na Justin Zulu ‘Mkata Umeme’ tangu waondoke wachezaji, Frank Domayo na Athuman Idd ‘Chuji’.
Akizungumza na bingwa jana, Ally alisema mazungumzo baina yake na Yanga yamekwenda vizuri na kesho (leo) anaweza kusaini mkataba wa kuichezea timu hiyo.
“Mambo yanakwenda vizuri na kesho (leo) nakutana tena na viongozi wa Yanga kwa ajili kufanya mazungumzo, ambayo bila shaka yataambatana na kumwaga wino,” alisema Ally.
Kiungo huyo tayari ameshakubaliana kila kitu na viongozi wa Yanga likiwemo suala la masilahi na dau lake la usajili na kusema: “Kuhusu masilahi tumekwishamalizana, hivyo hilo sina wasiwasi nalo, sasa akili zangu ziko kwenye kuvaa uzi huo wa Yanga na kupiga kazi.”
Ukiachana na kiungo huyo, pia Yanga iko mbioni kumnasa mshambuliaji wa Mbao FC, Habib Haji ambaye ana uwezo wa kucheza nafasi hiyo ya ushambuliaji pamoja na winga beki.
Lakini Yanga watakuwa na kazi nzito ya kukamilisha usajili wa nyota huyo kutokana na masharti aliyowapa pamoja na dau lake ili atie saini ya kuichezea klabu hiyo ya Jangwani.
Akizungumza na bingwa jana, Habib alisema bado yupo katika mazungumzo na mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania ili aweze kusaini mkataba wa kuichezea timu hiyo.
“Ni kweli nipo katika mazungumzo na Yanga na nimewapa masharti yangu. Kwanza wanipatie sehemu ya kuishi na dau la Sh milioni 30,” alisema Haji.
Haji ambaye yuko kwenye mazungumzo na Yanga, pia anafukuziwa na klabu za Azam FC na Simba na zote zinataka saini yake.
Akizungumzia kufukuziwa na klabu hizo, Haji alisema: “Klabu yoyote inayonitaka tukikubaliana na kunipa fedha ninayotaka mimi nitasaini.”