Daniel Mbega
JF-Expert Member
- Mar 20, 2013
- 338
- 180
KUNA uwezekano mkubwa kwa mabingwa wa Tanzania Bara, kupangwa kundi moja na mabingwa watetezi wa Kombe la Shirikisho, Etoile Sportive du Sahel ya Tunisia katika hatua ya makundi.
Ingawa upangaji wa makundi unategemea zaidi upigaji wa kura, lakini uwezekano uliopo ni kwamba, Yanga inaweza kuwa kwenye kundi la Etoile na wala siyo kundi litakaloongozwa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kanuni za mashindano ya Kombe la Shirikisho la CAF zinaeleza kwamba, timu mbili ambazo zimefanya vizuri kwenye mashindano ya klabu ya CAF kwa miaka mitano iliyopita, ndizo ambazo zinakuwa vinara wa makundi wakati timu nyingine sita zilizosalia zitaungana nazo kwa njia ya kura (draw).
Kigezo kingine kinachoangaliwa ni ubora wa klabu husika katika viwango vya CAF, ambao TP Mazembe na Etoile bado ziko juu kuliko timu zote zilizofuzu kwa hatua ya makundi ya kombe hilo.
TP Mazembe, ambayo imeweza kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, imefanya vizuri katika miaka iliyopita ikiwa ni pamoja na kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika ambalo imelitema mwaka huu.
Timu tano kutoka ukanda wa Afrika Kaskazini (Maghreb), zikiwemo mbili kutoka Morocco, zimefuzu kwenye hatua ya makundi ambazo ni mabingwa watetezi Etoile du Sahel (Tunisia), FUS Rabat (Morocco), Kawkab Marrakech (Morocco), MO Bejaia (Algeria), na Al Ahly Tripoli (Libya).
Yanga, TP Mazembe na Medeama ya Ghana ndizo timu pekee kutoka nje ya ‘Uarabuni’ kufuzu kwenye hatua hiyo, ambapo zitachanganywa na ‘Waarabu hao wa Afrika’ katika mseto ambao unaonyesha dhahiri kwamba, mashindano hayo yametawaliwa na timu za Kaskazini mwa Afrika.
Yanga, licha ya kufungwa bao 1-0 na Sagrada Esperanca katika mechi ya marudiano mjini Dundo, Angola jana, lakini imefuzu kufuatia ushindi wake wa mabao 2-0 ilioupata Mei 7 jijini Dar es Salaam.
Kwa upande mwingine, TP Mazembe na Medeama zimefuzu kwa sharia ya bao la ugenini baada ya matokeo ya jumla kulingana.
TP Mazembe awali ilishinda bao 1-0 dhidi ya Stade Gabesien ya Tunisia, lakini jana ilifungwa 2-1 ugenini na kusonga mbele, wakati Medeama jana ilishinda nyumbani kwa mabao 2-0 dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na kufanya matokeo ya jumla kuwa 3-3, hivyo kusonga mbele ya bao la ugenini baada ya kufungwa 3-1 katika mechi ya kwanza.
FUS Rabat imesonga mbele kwa ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Stade Malien ya Mali, ambayo katika mechi ya kwanza zilitoka suluhu mjini Bamako.
Al-Merreikh ya Sudan, wawakilishi wengine wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), wameyaaga mashindano hayo baada ya kufungwa jumla ya mabao 2-1 na Kawkab Marrakech ya Morocco licha ya kushinda mechi ya kwanza 1-0. Mechi ya pili walifungwa 2-0.
Misr Elmaqasah, timu pekee ya Misri iliyokuwa imesalia kwenye mashindano hayo – tena ikiingia baada ya kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa – imeng’olewa kwa faida ya bao la ugenini baada ya kutoka sare nyumbani ya 1-1 na Al Ahly Tripoli ya Libya. Katika mechi ya kwanza mjini Tripoli, timu hizo zilitoka suluhu.
MO Bejaia ya Algeria nayo ilitoka sare ya bao 1-1 Esperance jijini Tunis, hivyo kusonga mbele kwa faida ya bao la ugenini baada ya kutoka suluhu katika mechi ya kwanza.
Mabingwa watetezi, Etoile Sahel wamesonga mbele kwa ushindi wa jumla ya mabao 2-1 dhidi ya CF Mounana ya Gabon. Timu hiyo licha ya kufungwa 1-0 ugenini jijini Libreville jana, lakini ushindi wake wa mabao 2-0 katika mechi ya kwanza ulikuwa mkubwa kuiwezesha kutetea kwa muda taji lake.
Novemba 29, 2015 ilitwaa taji hilo baada ya kuifunga Orlando Pirates ya Afrika Kusini bao 1-0 kupitia kwa Ammar Jemal, hivyo kupata ushindi wa jumla ya mabao 2-1. Katika mechi ya kwanza Novemba 21, timu hizo zilifungana 1-1 mjini Johannesburg.
Utawala wa Kaskazini
Kombe la Shirikisho lina timu tano kutoka Afrika Kaskazini wakati kwenye Ligi ya Mabingwa ziko nne, hatua inayoonyesha dhahiri kwamba, msimu huu vikombe hivyo vinaweza kuzama Maghreb baada ya kushindikana mwaka 2015.
TP Mazembe ilivunja utawala wa timu za huko baada ya kuichapa USM Alger ya Algeria jumla ya mabao 4-1, kwanza ikishinda 2-1 na baadaye 2-0, huku Mtanzania Mbwana Samatta akiibuka shujaa kwa kufunga mabao muhimu ya ushindi.
Katika Ligi ya Mabingwa mwaka huu, kuna timu za Al Ahly na Zamalek za Misri, Wydad Casablanca ya Morocco na Entente Sportif de Setif ya Algeria.
Timu ambazo hazitoki Kaskazini ni Enyimba ya Nigeria, ASEC Mimosas ya Ivory Coast, ZESCO United ya Zambia na AS Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.